Friday, August 28, 2015

EUROPA LEAGUE DRAW: LIVERPOOL KUANZA NA RUBIN KAZAN, SPURS KUPIGA MASAFA MPAKA AZERBAIJAN.

KLABU ya Liverpool, inatarajiwa kusafiri kwenda Urusi baada ya kupangwa kundi moja na Rubin Kazan katika michuano ya Europa League. Liverpool iliyo chini ya meneja Brendan Rodgers pia wanatarajiwa kupambana na Bordeaux ya Ufaransa na FC Sion ya Uswisi katika kundi lao. Kwa wa Tottenham Hotspurs wao wanakabiliwa na safari ndefu ya kuifuata Qarabag ya Azerbaijan huku pia wakipangwa kucheza na Anderlecht ya Ubelgiji na Monaco ya Ufaransa. 
Celtic ambao waling’olewa katika hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, wao watavaana na Ajax Amsterdam ya Uholanzi, Fenerbahce ya Uturuki na Molde ya Norway katika kundi lao. Kila inatarajiwa kucheza mechi sita katika makundi yao huku mechi za kwanza zikitarajiwa kuchezwa Septemba 17 mwaka huu.

MESSI AMPIGA BAO RONALDO TUZO YA UEFA.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Argentina, Lionel Messi ameongeza tuzo nyingine katika orodha ndefu ya tuzo alizonazo jana baada ya kupigiwa kura kuwa mchezaji bora wa Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA msimu uliopita. Nyota huyo wa Barcelona alimshinda mchzaji mwenzake Luis Suarez na nyota wa Real Madrid Cristiano Ronaldo katika tuzo hiyo ambayo ilipigiwa kura na wanahabari za michezo barani Ulaya. Msimu uliopita Messi alifanikiwa kufunga mabao 58 na kutengeneza mengine 31 hivyo kuisaidia Barcelona kushinda taji la La Liga, Kombe la Mfalme na Ligi ya Mabingwa Ulaya. Messi ndio wa kwanza kushinda tuzo hilo mara mbili baada ya kushinda pia msimu wa 2010-2011 huku hasimu wake Ronaldo akishinda tuzo hiyo msimu uliopita.

CITY IMEJIPANGA KUMPA MSHAHARA MNONO DE BRUYNE.

MKURUGENZI wa michezo wa Wolfsburg ya Ujerumani Klaus Allofs amedai kuwa Manchester City imejipanga kumpa ofa ya mshahara mkubwa winga wao Keniv de Bruyne. De Bruyne mwenye umri wa miaka 24, ameachwa katika kikosi cha Wolfsburg kitakachopambana na Schalke baadae leo kutokana na kuendelea kwa mazungumzo yake ya kwenda City. Allofs amesema mara ya kwanza walikuwa hawataki kumuuza De Bruyne lakini sasa wameamua kuanza mazungumzo na City ingawa hakuna lililoafikiwa mpaka sasa. City hawajatoa kauli yeyote juu ya taarifa za kukubali kwao kutoa kitita cha paundi milioni 58 kwa ajili ya kumnyakuwa nyota huyo wa kimataifa wa Ubelgiji.

SCHMEICHEL AMSIHI DE GEA ABAKI UNITED.

GOLIKIPA wa zamani wa Manchester United, Peter Schmeichel amemtaka David de Gea kusaini mkataba na klabu hiyo, kutokana na uwezekano wake kuhamian Real Madrid kuwa mdogo. Suala la De Gea linatarajiwa kwenda mpaka siku ya mwisho ya usajili wa kiangazi kutokana na United na Madrid kuonekana kuendelea kuvutana kufikia muafaka wa usajili wa kipa huyo ambye mpaka sasa hajajumuishwa katika kikosi cha Louis van Gaal msimu huu. Van Gaal amesisitiza De Gea hatauzwa mpaka dirisha la usajili litakapofungwa pamoja na mkataba wa nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 kukaribia kumalizika mwishoni mwa msimu huu. Schmeichel anaonekana kuchoshwa na suala hilo na anataka De Gea kuendelea kuitumikia United msimu huu. Schmeichel aliendelea kudai kuwa De Gea amekuwa katika kiwango kizuri katika msimu miwili iliyopita hivyo angefurahi kama angesaini mkataba mwingine wa miaka mitano Old Trafford.

WENGER AMKINGIA KIFUA COQUELIN.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amemkingia kifua kiungo wake Francis Coquelin akidai kuwa amekuwa akifanya kazi kubwa akiwa kama chaguo namba moja katika nafasi ya kiungo mkabaji. Beki wa zamani wa Manchester United ambaye kwasasa ni mchambuzi Gary Neville aliponda nafasi ya kiungo ya Arsenal haswa Coquelin lakini Wenger anaonekana kuwa na imani na nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 24. Wenger aliuambia mtandao wa klabu hiyo kuwa Coquelin ana rekodi nzuri katika nafasi ya ulinzi na amekuwa akifanya kazi nzuri toka kuanza kwa msimu huu. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 65 aliendelea kudai kuwa kama watu watakuwa wanatizama soka kama anavyotizama yeye anadhani wataona kazi nzuri anayofanya.

RUFANI YA PIQUE YATUPILIWA MBALI.

BEKI wa Barcelona, Gerard Pique anatarajiwa kukosa safari ya kwenda kuifuata Atletico Madrid mwezi ujao baada ya rufani yake kupinga adhabu ya kufungiwa mechi nne kutupiliwa mbali jana. Pique alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kwa kumtolea maneno ya matusi mwamuzi msaidizi wakati Barcelona walipotandikwa kwa jumla ya mabao 5-1 katika mchezo wa Super Cup dhidi ya Athletic Bilbao wiki iliyopita. Nyota huyo wa kimataifa wa Hispania alikuwekwa kando wakati mabingwa hao wa Ulaya walipolipa kisasi kwa Bilbao kwa kuitandika bao 1-0 katika mchezo wao wa kwanza wa La Liga mwishoni mwa wiki iliyopita. Hata hivyo, Pique sasa anatarajiwa kukosa mchezo dhidi ya Malaga utakaochezwa kesho na Levante utakaochezwa Septemba 20 sambamba na ule wa Atletico Septemba 12.

WILFRIED BONY MAJANGA.

MSHAMBULIAJI wa Manchester City, Wilfried Bony anaweza kukaa nje ya uwanja kwa kipindi kirefu zaidi baada ya kutuma picha katika mtandao akiwa na magongo huku mguu wake ikiwa umefungwa bandeji gumu. Bony hajacheza katika mechi yeyote kati ya tatu za Ligi Kuu ambazo City wamecheza msimu huu na sasa anatarajiwa kukosekana kwa muda mrefu zaidi kutokana na picha hiyo aliyotuma. Bony alitua City akitokea Swansea City kwa kitita cha paundi milioni 28 katika kipindi cha usajili wa dirisha dogo Januari mwaka huu. Nyota huyo wa kimataifa wa Ivory Coast kwa ujumla amecheza mechi 30 za Ligi Kuu msimu uliopita na kufunga mabao 11.

SON AMWAGA WINO SPURS.

KLABU ya Tottenham Hotspurs imefanikiwa kukamilisha usajili wa mshambuliaji Son Heung-min kutoka klabu ya Bayer Leverkusen ya Ujerumani. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 23 ana rekodi ya kufunga mabao 29 katika mechi 87 alizoichezea Leverkusen toka ajiunge akitokea Hamburg mwaka 2013. Spurs inaripotiwa kutoa kitita cha paundi milioni 22 kwa ajili ya kunasa saini ya nyota huyo huku wakimpa mkataba wa mpaka mwaka 2020. Klabu hiyo pia imeshuhudia ofa zake mbili kwa ajili ya kumuwania Saido Berahino zikitupiliwa mbali na West Bromwich Albion ambao wamedai hawana mpango wa kumuuza nyota huyo mwenye umri wa miaka 22. Kukataliwa huko kumsajili Berahino ndio kunatajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa Spurs kumgeukia Son.

Thursday, August 27, 2015

BOLT ADHIHIRISHA UFALME WAKE BEIJING.

MWANARIADHA nyota wa mbio fupi wa Jamaica, Usain Bolt amefanikiwa tena kutetea ubingwa wake dunia kwa kunyakuwa medali ya dhahabu katika mbio za 200 zilizofanyika leo. Bolt ambaye pia alifanikiwa kutetea ubingwa wake katika mbio za mita 100 Jumapili iliyopita alifanikiwa kushinda mbio hizo za leo akitumia muda wa sekunde 19.55 ukiwa ni muda bora mwaka huu. Mpinzani wake wa karibu ambaye alikuwa akipewa nafasi kubwa ya kushinda Bolt, Justin Gatlin wa Marekani alishika nafasi ya pili na kupata medali ya fedha akitumia muda wa sekunde 19.74. Nyota kutoka Afrika Kusini Anaso Jobodwana alishika nafasi ya tatu katika mbio hizo.

BAYERN YAMUONGEZA MKATABA THIAGO.

KLABU ya Bayern Munich imethibitisha kiungo wao Thiago Alcantara ameongeza mkataba mwingine mpya ambao utamalizika mwaka 2019. Kiungo huyo alijiunga na Bayern akitokea Barcelona mwaka 2013 ambapo aliungana na kocha Pep Guardiola waliyekuwa naye Camp Nou. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 amekuwa akisumbuliwa na majeruhi kwa kipindi kirefu alichokuwa Ujerumani lakini alionyesha kiwango bora pindi alipokuwa fiti jambo ambalo limemfanya kupewa mkataba mwingine. Ofisa mkuu wa Bayern, Karl-Heinz Rummenigge amesema amefurahishwa na taarifa hizo kwani Thiago bado ni mchezaji mdogo hivyo atakuwa hazina nzuri kwa timu hiyo ziku za baadae. Thiago amecheza mechi 25 pekee za Bundesliga toka atue Bayern huku akifunga mabao mawili.

SPURS YAMUWANIA NYOTA WA KOREA KUSINI.

KLABU ya Tottenham Hotspurs iko katika mazungumzo ya kuwania kumsajili mshambuliaji wa Bayer Leverkusen Son Heung-min. Nyota huyo wa kimataifa wa Korea Kusini mwenye umri wa miaka 23, amefunga mabao 21 kati ya mechi 62 za Bundesliga alizocheza toka ajiunge na Leverkusen akitokea Hamburg mwaka 2013. Inaaminika kuwa Spurs wamepanga kutoa kitita cha paundi milioni 22 kwa ajili ya kunasa saini ya Son. Spurs wanafanya hivyo kufuatia ofa yao ya pili kwa mshambuliaji wa West Bromwich Albion Saido Berahino kukataliwa.

WENGER AKIRI USAJILI UNAMNYIMA USINGIZI.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amethibitisha kuwa wanafanya kazi saa 24 kuangalia uwezekano wa kufanya usajili kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili la kipindi hiki cha kiangazi. Klabu hiyo imefanikiwa kumsajili Petr Cech pekee kutoka Chelsea kipindi hiki huku wachezaji wengine waliokuwa wakiwaania Karim Benzema na Grzegorz Krychowiak wakithibitisha kubakia katika vilabu vya Real Madrid na Sevilla. Pamoja na kushindwa kuongeza wachezaji katika nafasi ya kiungo na ushambuliaji, Wenger amedokeza kuwa timu yake ya usajili inahaha kutafuta wachezaji mahali popote watakaofaa. Wenger amesema wamekuwa wkifanya kazi saa 24 kuhakikisha wanapata wachezaji sahihi watakaofaa ili kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya msimu huu.

ROONEY AANZA KUCHONGA BAADA YA KUPIGA HAT-TRICK.

NAHODHA wa Manchester United, Wayne Rooney amesema ana uzoefu wa kutosha wa kukabiliana na wanaomkosoa baada ya kumaliza ukame wa kutofunga bao katika mechi 10 alizoichezea timu hiyo. Mshambuliaji huyo anaonekana kurejesha makali yake baada ya kuanza msimu kwa kusuasua, akifunga mabao matatu hat-trick katika ushindi wa mabao 4-0 waliopata United dhidi ya Club Brugge katika mechi ya kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo uliochezwa jana usiku, Rooney amesema kama asingekuwa imara jambo hilo lingeweza kumuathiri lakini anafahamu uwezo wake. Ushindi unaifanya United kujihakikishia nafasi ya kuwepo katika ratiba ya makundi ya michuano hiyo baada ya kukosa kushiriki msimu uliopita.

BALOTELLI AKIRI KUACHA MAMBO YA KITOTO.

MSHAMBULIAJI nyota Mario Balotelli amesema hawezi kufanya makosa zaidi hivi sasa baada ya kurejea AC Milan kwa mkopo. Nyota huyo wa kimataifa wa Italia, mwenye umri wa miaka 25 amereje Milan akitokea Liverpool alipocheza kwa msimu mmoja pekee. Akihojiwa Balotelli amekiri kupoteza nafasi nyingi alizopata kutokana na mambo yasiyokuwa na umuhimu jambo ambalo limemrudisha nyuma kwa kiasi fulani. Nyota huyo amesema hajasahau kucheza soka na kwasasa amepevuka na sio mtoto tena hivyo ana uhakika wa kurejea katika ubora wake. Balotelli alifanikiwa kufunga bao moja pekee katika Ligi Kuu akiwa Liverpool baada ya kusajiliwa kwa kitita cha paundi milioni 16 kutoka Milan Agosti mwaka 2014.

OZIL ATAKA SCHWEINSTEIGER APEWE MUDA ILI KUONYESHA MAKALI YAKE.

KIUNGO wa Arsenal, Mesut Ozil anaamini Mjerumani mwenzake Bastian Schweinsteiger anakosolewa visivyo kufuatia uhamisho wake kwenda Manchester United. Kumekuwa na mijadala ya aidha mwili wa Schweinsteiger mwenye umri wa miaka 31 kama utaweza kukabiliana na mikikimikiki ya Ligi Kuu baada ya kuondoka Bayern Munich Julai mwaka huu. Mpaka sasa kiungo huyo hajapata nafasi ya kucheza dakika zote tisini kwani amekuwa aidha akianza na kutolewa katikati au kuingia baada ya muda wa mapumziko katika mechi kadhaa za United zilizopita. Akihojiwa Ozil amesema hana shaka kabisa kuwa Schweinsteiger atawanyamazisha wale wote wanaomkosoa kwa kuonyesha kiwango bora pindi wakati utakapowadia. Ozil aliendelea kudai kuwa kwasasa ni mapema mno kukosoa kiwango chake kwani anamfahamu vyema uwezo wake.

Wednesday, August 26, 2015

ARSENAL WAPANGIWA MAHASIMU WAO TOTTENHAM HOTSPURS KOMBE LA LIGI.

KLABU ya Tottenham Hotspurs itakuwa wenyeji wa mahasimu wao wa kaskazini ya London Arsenal katika mchezo wa mzunguko wa tatu wa Kombe la Ligi. Mabingwa Chelsea wao wataanza kutetea taji lao kwa kusafiri kuifuata Walsall inayoshiriki ligi daraja la kwanza wakati Aston Villa wao wamepangwa na mahasimu wao Birmingham City. Katika mechi zingine, Manchester United na Liverpool zimepewa mechi za nyumbani dhidi ya Ipswich Town na Carlisle. Hatua hiyo itakuwa na mechi zingine tatu zitakazohusisha timu za Ligi kuu ambapo Sunderland wao watakuwa wenyeji wa Manchester City, Norwich watachuana na West Bromwich Albion na Leicester City wakiivaa West Ham United.

BALOTELLI APIGWA MKWARA MZITO AC MILAN.

MSHAMBULIAJI mahiri wa kimataifa wa Italia, Mario Balotelli amewekewa sheria kali katika mkataba wake wa mkopo na klabu ya AC Milan, akizuiwa kunyoa na kuvaa nguo za kiajabuajabu na pia akitakiwa kuishi maisha bora. Vyombo vya habari nchini Italia vimedai kuwa Ofisa Mkuu wa klabu hiyo Andriano Galliani amemuwekea sheria hizo ambazo mara nyingi hutumika kwa watu wanatumikia jeshi la nchi hiyo. Balotelli mwenye umri wa miaka 25 ambaye mara kadhaa amekuwa akikosolewa kwa kushindwa kujituma anatarajiwa kuanza kuitumikia Milan tena ikiwa ni mwaka mmoja toka aondoke kwenda Liverpool ambako nako alishindw akung’aa. Inadaiwa kuwa mbali na kuzuiwa kuvaa na kunyoa kiajabuajabu Balotelli pia hatatakiwa kuvuta sigara, kufanya starehe katika vilabu vya usiku kupiliza pamoja na unywaji pombe.

VALENCIA AITUHUMU WEST HAM KUMTENGA.

MSHAMBULIAJI wa West Ham United, Enner Valencia amekasirishwa na klabu yake hiyo, akiamini kuwa imemtelekeza toka apate majeruhi. Nyota huyo wa kimataifa wa Ecuador aliumia mguu wakati wa mchezo wa Europa League dhidi ya Astra Giurgiu Agosti 2 mwaka huu na sasa anatakiwa kukaa nje ya uwanja kwa miezi mitatu. Hata hivyo, Valencia ambaye alifunga mabao manne katika Ligi Kuu msimu uliopita, amedai amekuwa akiwekwa gizani kuhusu maendeleo yake na kuituhumu klabu hiyo kumzuia kwenda kujitafutia matibabu yake mwenyewe. Akihojiwa Valencia amesema West Ham wanaonekana wamemsahau kama ameumia kwani hawataki kumruhusu kuzungumza na madaktari wengine na hajui kwanini madaktari wa timu hiyo wanamfanyia hivyo.

VIDAL ADAI WACHEZAJI SASA WANALIPWA SANA KULIKO VIWANGO VYAO.

KIUNGO wa Bayern Munich, Arturo Vidal amesema ada zinazolipwa na klabu kwa ajili ya kusajili wachezaji ni kubwa sana, na kudai kuwa baadhi yao wanapaswa kufunga walau mabao matatu au manne ili kufikia thamani hiyo. Vidal mwenyewe alitua Bayern akitokea Juventus kwa kitita kikubwa kilichofikia euro milioni 40 Julai mwaka huu. Akihojiwa Vidal amekiri kuwa wachezaji wachache sana ndio wanastahili kununuliwa kwa thamani hiyo katika soka hili la kisasa. Vidal aliendelea kudai kuwa kwa mtazamo wake gharama hizo zilipaswa kushuka ili kupunguza shinikizo kwa baadhi ya wachezaji.

MASCHERANO AUTAKA UKOCHA AKISTAFU.

KIUNGO wa Barcelona, Javier Mascherano amebainisha kuwa anataka kuwa kocha wakati atapoamua kutundika daruga zake. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 31 ana miaka mitano Barcelona toka ahamie akitokea Liverpool mwaka 2010 baada pia ya kuzitumikia West Ham United, Corinthians na River Plate. Akihojiwa Mascherano ambaye kwasasa ni nahodha msaidizi wa Barcelona amesema anataka kuwa kocha pindi atakapostaafu soka ingawa anafahamu haitakuwa kazi rahisi. Nyota aliendelea kudai kuwa ukiwa mchezaji mambo huwa sio magumu sana lakini huwa yanabadilika unapohamia upande wa pili lakini anafahamu anaweza kukabiliana na changamoto zozote kutokana na uzoefu wake.

HISPANIA YAWA NCHI YA KWANZA KUINGIZA TIMU TANO CHAMPIONS LEAGUE.

HISPANIA imekuwa nchi ya kwanza kupata timu tano zilizofuzu hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kufuatia Valencia kufanikiwa kuichapa Monaco katika mechi ya mtoano. Valencia waliowahi kuwa washindi wa pili wa michuano hiyo mwaka 2001, ambao wana beki wa zamani wa Manchester United katika benchi lao ufundi, wanaungana na Real Madrid, Barcelona na Atletico Madrid. Sevilla wao pia watakuwepo katika ratiba hiyo ya makundi wakifuzu kama mabingwa wa michuano ya Europa League msimu uliopita. Ratiba ya makundi ya michuano hiyo inatarajiwa kupangwa rasmi kesho. Huu ni msimu wa kwanza kuwepo uwezekano wan chi moja kuwa na timu tano kati ya timu 32 zitakazokuwepo katika hatua ya makundi toka Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA kutangaza kuwa mshindi wa Europa League pia atapata nafasi ya moja kwa moja kucheza Ligi ya Mabingwa msimu unaofuata.

Tuesday, August 25, 2015

HABARI PICHA: MAN UNITED WAIFUATA BRUGGE.




HABARI PICHA: RONALDO ANUNUA BONGE LA APARTMENT LENYE THAMANI YA ZAIDI YA DOLA MILIONI 18 KATIKA JENGO LA DONALD TRUMP.






BALOTELLI ADAI KUFURAHIA KUREJEA SERIE A.

MSHAMBULIAJI nyota wa Liverpool, Mario Balotelli amesema anajisikia furaha kurejea Serie A baada ya kukamilisha vipimo vya afya tayari kwa uhamisho wake wa mkopo kwenda AC Milan. Nyota huyo wa kimataifa wa Italia alitua Milan mapema leo ili kukamilisha hatua za mwisho za mkopo wake huo. Akizungumza na wanabahari mara baada ya kufanyiwa vipimo vya afya Balotelli amesema amefurahi kurejea na yuko fiti anachosubiri sasa ni kuanza mazoezi na wenzake. Nyota huyo mwenye maneno na vibwanga vingi ndani na nje ya uwanja safari hii amesema hataki kuongea sana bali kufanya kazi iliyomleta hapo. Balotelli ambaye amefunga bao moja pekee katika mechi 16 za Ligi Kuu alizocheza msimu uliopita, alikuwa ameondolewa katika mipango ya meneja Brendan Rodgers.

BARCELONA YAIZODOA MAN UNITED KWA NEYMAR.

RAIS wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu amepuuza tetesi zinazomuhusisha Neymar na klabu ya Manchester United na kubainisha kuwa wanataka nyota huyo wa kimataifa wa Brazil astaafu akiwa Camp Nou. Kumekuwa tetesi hivi karibuni zikidai kuwa United wanajipanga kuvunja rekodi kwa kuwania kumsajili Neymar kabla dirisha la usajili halijafungwa huku baadhi ya vyombo vya habari vikidai pia nyota huyo mwenye umri wa miaka 23 yuko tayari kutua Old Trafford. Hata hivyo, Bartomeu amekanusha taarifa hizo akidai kuwa Barcelona hawana mpango wowote wa kuuza mmmoja kati ya wachezaji muhimu na kufafanua kuwa wana matumaini mazuri ya hivi karibuni kusaini naye mkataba mwingine mrefu zaidi. Bartomeu amesema hawataki Neymar aondoke kwani bado mdogo na wanataka astaafu akiwa hapo. Rais huyo aliendelea kudai kuwa wataanza mazungumzo naye ya mkataba mpya katika kipindi cha miezi michache ijayo kwa ajili ya kumuongeza mkataba mrefu zaidi.

NYOTA SENEGAL AINGIA MATATANI UINGEREZA KWA KUTISHIA KUUA.

MCHEZAJI nyota wa kimataifa wa Senegal na klabu ya West Ham United, Diafra Sakho amekamatwa na polisi kufuatia tuhuma za kutishia kuua hadharani. Msemaji wa polisi alithibitisha kukamatwa kwa mshambuliaji huyo kwa tuhuma hizo na baadae kutolewa kwa dhamana. Naye msemaji wa nyota huyo alithibitisha taarifa hizo akidai kuwa Sakho amekanusha tuhuma hizo na wanasubiri uchunguzi wa polisi kabla ya kurejea tena polisi mapema mwezi Octoba. Sakho amekuwa akiandamwa na matukio ya nje ya uwanja katika siku za karibuni kwani mwezi uliopita alihojiwa na polisi kufuatia kuhisiwa kunyanyapaa. Sakho alijiunga na West Ham akitokea klabu ya Metz ya Ufaransa msimu uliopita na kufunga mabao 12 katika msimu wake wa kwanza Upton Park.

BEKI WA ZAMANI LA MADRID AMKINGIA KIFUA BENITEZ.

KIUNGO wa zamani wa Real Madrid, Ruben de la Red anaamini ni mapema mno kuhoji uwezo wa Rafael Benitez wa kuwa meneja wa klabu hiyo. Kufuatia matokeo mchanganyiko wakati wa maandalizi, Madrid wameanza rasmi mechi zake za mashindano chini ya Benitez aliyechukua nafasi ya Carlo Ancelotti kwa sare ya bila kufungana na Sportinh Gijon mwishoni mwa wiki iliyopita. Hata hivyo, De La Red amesema mashabiki wa Madrid wanapaswa kuwa wavumilivu na kocha huyo wa zamani wa Liverpool wakati huu akiwaongoza kwenda kunyakuwa taji lao kwanza la La Liga toka mwak 2012. De La Red aliendelea kudai kuwa Benitez anapaswa kupewa muda kwani kocha yeyote mpya hupitia katika kipindi hiki cha mpito katika kuwaelewesha wachezaji wake waweze kuzoea mbinu zake.

CITY WAPIGWA CHANGA LA MACHO KWA DE BRUYNE.

KIUNGO Kevin De Bruyne amefanya mazoezi na klabu yake ya Wolfsburg mchana wa leo pamoja na taarifa kuwa alitakiwa kusafiri kwenda nchini Uingereza kwa ajili ya kukamilisha uhamisho wake wenda Manchester City. Nyota huyo wa kimataifa wa Ubelgiji ni mmoja kati ya wachezaji City inaowaania na wiki iliyopita kuna taarifa zilizagaa zikidai kuwa City walikuwa tayari kuvunja rekodi ya usajili ili kumnasa kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili. Taarifa zilizozagaa nchini Uingereza leo ni kuwa De Bruyne alitarajiwa kusafiri kwenda jijini Manchester kumalizia uhamisho wake lakini kocha wa Wolfsburg Dieter Hecking alithibitisha kuwa nyota huyo atakuwepo mazoezini leo mchana. De Bruyne alijiunga na Wolfsburg Januari mwaka 2014 baada ya kushindw akung’aa katika klabu ya Chelsea chini ya Jose Mourinho.

HAMBURG WAMLILIA DJOUROU.

NAHODHA wa Hamburg SV Johan Djourou anatarajiwa kukosekana uwanjani kwa muda usijulikana baada ya kupata majeruhi ya paja katika mchezo wa Bundesliga dhidi ya VfB Stuttgart ambao walishinda mabao 3-2 Jumamosi iliyopita. Beki huyo wa kimataifa wa Uswisi mwenye umri wa miaka 28, alifunga bao katika dakika ya 89 ya kuisaidia timu yake kuibuka na ushindi huo wa kwanza dhidi ya Stuttgart. Klabu hiyo ilithibitisha kuumia kwa Djourou na kudai kuwa ni pigo kubwa kumkosa nahodha wao huyo tegemeo. Hamburg ambao wamelazimika kucheza hatua ya matoano kwa miaka miwili ili wabaki Bundesliga, Jumamosi hii wanapambana na Cologne.

Thursday, August 20, 2015

BAADA YA KUPIGWA BAO KWA PEDRO MAN UNITED SASA WAMGEUKIA MSENEGAL.

KLABU ya Southampton imekiri kuwa Manchester United wanamuwania winga wao wa kimataifa wa Senegal Sadio Mane. Wiki iliyopita Southampton walikanusha taarifa za kupokea ofa yeyote kwa ajili ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 23. Mshambuliaji wa Barcelona Pedro amekuwa akihisiwa kujiunga na United lakini kwa sasa yupo katika hatua za mwisho za kijiunga na Chelsea kwa dau la pauni milioni 21. Hivyo kufuatia hilo United wameamua kuongeza nguvu zao katika kumsajili mane kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili wa kiangazi. Mane amefunga mabao 10 katika mechi 32 alizocheza msimu uliopita baada ya kujiunga na klabu yake ya sasa akitokea Red Bull Salzburg ya Austria na yumo pia katika orodha ya wachezaji waliowahi kufunga magoli matatu -hat-trick kwa muda mfupi zaidi.


PEDRO ATUA RASMI CHELSEA.

KLABU ya Chelsea imemsajili rasmi mshambuliaji wa Barcelona Pedro kwa kitita cha paundi milioni 21. Nyota huyo wa kimataifa wa Hispania katika siku za karibuni alionekana kama ataenda Manchester United lakini kushindwa kwao kufikia dau la euro milioni 30 lililotakiwa na Barcelona kumefanya mshambuliaji huyo kupata chaguo lingine. Mapema asubuhi Barcelona walithibitisha kuwa Pedro alikosa mazoezi ya klabu hiyo kwasababu ya kupewa ruhusa ya kwenda kukamilisha taratibu za uhamisho wake. Pedro ameitumikia Barcelona mechi 300 toka alipoibuka katika kikosi cha kwanza msimu wa 2007-2008, lakini ujio wa nyota wengine kama Neymar na Luis Suarez umemfanya mshambuliaji huyo kukosa nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza. Pedro amekuwa mchezaji wa nne kusajiliwa na Chelsea baada ya Asmir Begovic, Radamel Falcao na Baba Rahman.

Wednesday, August 19, 2015

CHELSEA YAIPIGA BAO MAN UNITED KWA PEDRO.

VYOMBO vya habari nchini Hispania vimetoa taarifa kuwa klabu ya Chelsea imefanikiwa kuwazidi maarifa mahasimu wao Manchester United katika usajili wa mshambuliaji wa kimataifa wa Hispania Pedro kutoka Barcelona. Kwa mujibu wa taaifa zilizochapishwa na gazeti la Marca, zimedai kuwa taratibu zote za pedro kujiunga na Chelsea zimeshakamilika baada ya vilabu hivyo kuafikiana uhamisho wa euro milioni 28 huku kukiwa na nyongeza ya euro milioni mbili itakayolipwa baadae. Taarifa hizo ziliendelea kudai kuwa Pedro tayari ameshatua jijini London kufanyiwa vipimo vya afya baada ya kupewa ruhusa na Barcelona. United walikuwa wakitajwa kwa wiki kadhaa kumuwania mshambuliaji huyo kwa kutoa ofa ya euro milioni 25.

PIQUE ALIMWA ADHABU YA MECHI NNE PAMOJA NA KUOMBA RADHI.

BEKI wa Barcelona, Gerard Pique ameomba radhi kufuatia kutolewa kwake katika mchezo wa maruadiano wa Super Cup dhidi ya Athletic Bilbao lakini amekanusha kumtukana mwamuzi msaidizi. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 28, alimavaa mwamuzi msaidizi na kumzonga wakati wa mchezo wao dhidi Bilbao ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 katika Uwanja wa Camp Nou. Pique aliandika katika ukurasa wake wa mtandao kijamii wa twitter akiomba radhi kwa tukio hilo lakini alikanusha kumtukana mwamuzi huyo kama ilivyofikiriowa na wengi. Hata hivyo pamoja na Pique kuomba radhi, Shirikisho la Soka la Hispania limemlima adhabu ya kutocheza mechi nne beki huyo leo. Barcelona wanatarajiwa kuanza kutupa karata yao ya kwanza ya kutetea taji lao la La Liga kwa kuvaana tena na Bilbao Jumapili hii.

LIVERPOOL ITALIPA KISASI DHIDI YA ARSENAL - LALLANA.

KIUNGO wa Liverpool, Adam Lallana amesema timu hiyo imesuka mipango kabambe ya kuibuka na ushindi ugenini wakati watakapokwenda kuchuana na Arsenal katika Uwanja wa Emirates Jumatatu ijayo. Liverpool wameshinda mechi zao zote mbili za Ligi Kuu msimu huu na Lallana amesema meneja wao Brendan Rodgers amepanga kupata alama zote tatu kutoka kwa mahasimu wao hao. Lallana mwenye umri wa miaka 27 aliendelea kudai kuwa Rodgers amewapanga kwenda kupata matokeo katika mchezo huo. Arsenal waliichapa Liverpool mabao 4-1 msimu uliopita lakini Lallana anaamini matokeo hayo hayataweza kujirudia tena safari hii.

Monday, August 17, 2015

BENITEZ AMTAKA BENZEMA KUFUNGA MABAO 25 MSIMU HUU.

MENEJA wa Real Madrid, Rafa Benitez anataka mshambuliaji wake Karim Benzema kufunga walau mabao 20 msimu huu. Nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa, amekuwa akihusishwa na tetesi za kwenda Arsenal katika wiki za karibuni huku meneja wa timu hiyo Arsenal Wenger akiwa na matumaini ya kumsajili kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili wa kiangazi mwishoni mwa mwezi huu. Benzema amefunga mabao 22 katika mashindano yote msimu uliopita lakini benitez anadhani nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 anaweza kufanya zaidi katika msimu huu wa 2015-2016. Akihojiwa Benitez amesema Benzema ni mchezaji mkubwa na moja ya malengo aliyonayo juu yake ni kumtaka ajitahidi kufunga mabao zaidi kati ya 20 mpaka 25 ana uhakika hilo liko ndani uwezo wake.

CHUNG MONG-JOON ATANGAZA RASMI KUGOMBEA URAIS FIFA.

MFANYABIASHARA na mwanasiasa maarufu nchini Korea Kusini Chung Mong-joon ametangaza rasmi nia yake ya kugombea nafasi ya urais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA katika uchaguzi utakaofanyika mwakani. Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Februari 26 baada ya rais wa sasa Sepp Blatter kutangaza nia yake ya kuachia ngazi Juni mwaka huu kufuatia kashfa ya ufisadi iliyolikumba shirikisho hilo. Blatter alichaguliwa tena kuongoza muhula wa tano wakati kashfa hiyo ilipoibuka lakini baadae alithibitisha rasi mpya atachaguliwa katika mkutano mkuu usio wa kawaida utakaofanyika Februari. Akizungumza na wana habari jijini Paris kutangaza nia yake hiyo, Chung ambaye pia ni makamu wa rais wa heshima wa FIFA, amesema FIFA inahitaji kiongozi ambaye ataleta uaminifu, uwazi na uwajibikaji. Chung mwenye umri wa miaka 61 aliendelea kudai kuwa ili shirikisho lifanikiwa kupiga teke ufisadi ni lazima liweze kupata mabadiliko ya mara kwa mara katika uongozi. Mbali na Chung, wengine waliotangaza nia ya kugombea nafasi hiyo mpaka sasa ni pamoja na rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA Michel Platini, nguli wa soka wa zamani wa Brazil, Zico na rais wa Shirikisho la Soka la Liberia Musa Bility.

PELLEGRINI AANZA KUCHONGA, ADAI WACHEZAJI WAKE WANA HASIRA NA NJAA YA USHINDI.

MENEJA wa Manchester City, Manuel Pellegrini amesema wachezaji wake wana njaa na kiu baada ya kulikosa taji la Ligi Kuu msimu uliopita. City walimaliza katika nafasi ya pili msimu uliopita nyuma ya mabingwa Chelsea wakitofautiana kwa alama nane. Akihojiwa mara baada ya kikosi chake kuichapa Chelsea kwa mabao 3-0 jana, Pellegrini amesema pengine kilichotokea msimu uliopita kilikuwa ni uzoefu tosha kwao. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa wachezaji wake hivi sasa wana njaa na kiu ndio maana wanataka kushinda katika kila mchezo. Mabao ya City katika mchezo huo yalifungwa na Sergio Aguero, nahodha Vincent Kompany na Fernandinho.

MOURINHO ATETEA UAMUZI WAKE WA KUMTOA TERRY.

MENEJA wa Chelsea, Jose Mourinho ametetea uamuzi wake wa kumuondoa nahodha John Terry wakati wa mapumziko kufuatia kipigo cha mabao 3-0 walichopata kutoka kwa Manchester City jana. Beki huyo mkongwe mwenye umri wa miaka 34 alibadilishwa na nafasi yake kuchukuliwa na Kurt Zouma huku City wakiwa tayari wanaongoza kwa bao 1-0 katika kipindi cha kwanza. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo, Mourinho alithibitisha kuwa Terry hakuumia katika mchezo huo na kumtoa kwake ilikuwa sehemu ya mipango yake. Mourinho amesema ilikuwa wazi kwake kuwa Zouma alitakiwa kucheza katika mechi hiyo. Terry ameshinda mataji manne ya Ligi Kuu, matano ya Kombe la FA, moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya na moja la Europa League katika kipindi cha miaka 17 ambayo ameitumikia Chelsea.

RAMOS AKUBALI KUSAINI MKATABA MPYA.

HATIMAYE beki mahiri Sergio Ramos aliyekuwa akiwaniwa na klabu ya Manchester United, amekubalia kusaini mkataba mpya wa miaka mitano na timu yake ya Real Madrid. United walituma ofa ya paundi milioni 28.6 kwa ajili ya beki huyo mwenye umri wa miaka 29 mapema kiangazi hiki wakati mazungumzo ya mkataba wake yalipokuwa yakisuasua. Hata hivyo, nyota huyo wa kimataifa wa Hispania sasa atabakia Madrid baada ya kuonekana akiwa sambamba na rais Florentino Perez katika shughuli za kusaini mkataba huo. Mkataba mpya wa Ramos utamfanya kuendelea kuwepo Santiago Bernabeu mpaka mwaka 2020. Akihojiwa mara baada ya kusaini mkataba huo Ramos amesema fedha sio sababu iliyomfanya kuongeza mkataba mwingine katika timu hiyo. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa angeweza kupata fedha nyingi zaidi kama angeamua kuondoka kwenda kwingine lakini kunatokana na mapenzi aliyonayo kwa Madrid asingeweza kufanya hivyo.

Manchester City vs Chelsea 3-0 2015 HIGHLIGHTS Premier league 16 -08-2015

Crystal Palace vs Arsenal 1-2 2015 Highlights Premier League 16 -08-2015

Monday, August 10, 2015

BAYERN INAPSWA KUIMARIKA ZAIDI - LAHM.

NAHODHA wa Bayern Munich Philipp Lahm amesisitiza kuwa kikosi chao kinapaswa kuimarika zaidi pamoja na ushindi mzuri wa mabao 3-1 waliopata dhidi ya Nottingen katika mchezo wa Kombe la Ujerumani jana. Mabao yaliyofungwa na Arturo Vidal, Mario Gotze na Robert Lewandowaski yalitosha kuwapa mabingwa ushindi dhidi ya timu hiyo ya daraja la chini. Hata hivyo, Lahm amesema bado wana safari ndefu ya kuimarika kwani hawakucheza kwa kiwango chao bora katika mchezo huo. Nahodha huyo aliongeza kuwa jambo la muhimu wamesonga mbele katika hatua inayofuata na hakuna mchezaji yeyote aliyeumia lakini ni wazi watalazimika kucheza vyema zaidi katika michezo mingine. Bayern watafungua pazia la Bundesliga kwa kucheza dhidi ya Hamburg Ijumaa hii.

CHELSEA HAIJUTII KUMKOSA PETR CECH - MOURINHO.

MENEJA wa Chelsea, Jose Mourinho amesema timu hiyo haijutii kumkosa golikipa Petr Cech na ana uhakika kikosi chake kitaendelea vyema pamoja na kumkosa Thibaut Courtois anayetumikia adhabu wakati watakapokuwa wageni wa Manchester City Jumapili ijao. Mourinho hakufurahishwa sana Cech mwenye umri wa miaka 33 kujiunga na mahasimu wao Arsenal baada ya kuwatumikia mabingwa hao kwa misimu 11 yenye mafanikio lakini meneja huyo amesisitiza ana furahia aina ya makipa aliobakiwa nao katika kikosi chake. Akihojiwa Mourinho amesema ana magolikipa wawili wazuri hivyo haoni kama kuna tatizo lolote kumkosa Cech. Cech aliamua kuhamia Arsenal baada ya kujikuta akikosa namba katika kikosi cha kwanza na kuchukuliwa na Courtois ambaye aliitwa na Chelsea kutoka Atletico Madrid alikokuwa kwa mkopo.

WENGER ADAI HATAKURUPUKA KUSAJILI.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amedai kuwa hatakurupuka kukimbilia sokoni kutafuta wachezaji wapya kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili wa kiangazi baada ya kipigo cha kushtusha kutoka kwa West Ham United jana. Golikipa Petr Cech ndio sura mpya pekee iliyotua Emirates katika kipindi hiki cha usajili na ameonekana kuanza vibaya kibarua chake hicho toka atoke Chelsea. Kuna tetesi kuwa Wenger ameshatenga fungu kwa ajili ya kumuwania mshambuliaji wa Real Madrid, Karim Benzema. Lakini meneja huyo amesema hatakurupuka kusajili kwasababu ya kupoteza mchezo wao kwanza katika ligi kwani jambo la msingi ni kuangalia walipokosea na kurekebisha.

NITAITENDEA HAKI JEZI NAMBA SABA - DEPAY,

MSHAMBULIAJI mpya wa Manchester United, Memphis Depay ana uhakika kuwa ataweza kuitendea haki jezi namba namba aliyopewa na klabu hiyo kama nyota wengine waliowahi kuivaa. Depay alipewa namba hiyo mashuhuri baada ya Angel Di Maria kuondoka kwenda Paris saint-Germain na kufuatia nyayo za nyota wengine waliowahi kuvaa jezi kama Cristiano Ronaldo, David Beckham, Eric Cantona na George Best. Nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa amesema yuko tayari kuitendea haki jezi hiyo kama ilivyokuwa kwa nyota wengine na kutamba kuwa atafanikiwa akiwa Old Trafford. Depay aliendelea kudai kuwa anafahamu changamoto yake na historia lakini ana uhakika ataendelea kuimarika zaidi na kupata mafanikio kama ilivyokuwa kwa wengine.