Tuesday, July 31, 2012

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

MECHI YA NGORONGORO HEROES YAINGIZA MIL 12/-
Mechi ya kwanza ya raundi ya pili kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 20 kati ya Tanzania (Ngorongoro Heroes) na Nigeria (Flying Eagles) iliyochezwa juzi (Julai 29 mwaka huu) imeingiza sh. 12,901,000. Fedha hizo zimepatikana kutokana na watazamaji 3,377 waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo lililochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Sehemu iliyoingiza watazamaji wengi ilikuwa viti vya bluu na kijani ambapo 2,697 walikata tiketi kwa kiingilio cha sh. 3,000 kila mmoja. Viingilio vingine katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C na B, na sh. 15,000 kwa VIP A iliyoingiza watazamaji 21. Mgawanyo wa mapato hayo ni kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ilikuwa sh. 1,967,949.15, gharama ya kuchapa tiketi sh. 2,250,000, gharama za waamuzi na kamishna wa mechi hiyo sh. 760,000 na ulinzi na usafi kwa Uwanja wa Taifa sh. 2,350,000. Malipo kwa Wachina (Beijing Construction) sh. 2,000,000, asilimia 20 ya gharama za mchezo ni sh. 714,610.17, asilimia 10 ya uwanja sh. 357,305.08, asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 178,652.54 na asilimia 65 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 2,322,483.05. Mechi ya marudiano ya michuano hiyo ambayo fainali zake zitafanyika mwakani nchini Algeria itachezwa Agosti 12 mwaka mjini Ilorin, Jimbo la Kwara, Nigeria.

PONGEZI KWA UONGOZI MPYA SIREFA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Singida (DOREFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Julai 28 mwaka huu. Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa SIREFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani Singida. TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya SIREFA chini ya uenyekiti wa Baltazar Kimario ambaye amechaguliwa kwa mara ya kwanza. Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu mkoani Singida kwa kuzingatia katiba ya SIREFA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake. Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya SIREFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF. Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo uliofanyika Chuo Cha Maendeleo ya Jamii Singida ni Baltazar Kimario (Mwenyekiti), Hussein Mwamba (Katibu Mkuu), Gabriel Gunda (Katibu Msaidizi), Gabriel Mwanga (Mhazini), Hamisi Kitila (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF), Omari Salum (Mwakilishi wa Klabu TFF), Yagi Kiaratu na Dafi Dafi (wajumbe wa Kamati ya Utendaji). Nafasi za Makamu Mwenyekiti, Mhazini Msaidizi na wajumbe wawili wa Kamati ya Utendaji zitajazwa katika uchaguzi mdogo utakaofanyika baadaye.

MICHELSEN AITA 22 KAMBI YA COCA-COLA
Kocha wa timu za Taifa za vijana za Tanzania, Jakob Michelsen ameita wachezaji 22 kwa ajili ya michuano ya kimataifa ya Coca-Cola itakayofanyika baadaye mwaka huu nchini Afrika Kusini. Baadaye watachujwa na kubaki 16 ambao ndiyo watakaokwenda kwenye michuano ya Afrika Kusini. Wachezaji waliochaguliwa wametokana na michuano ya Copa Coca-Cola iliyofanyika jijini Dar es Salaam na mkoani Pwani kuanzia Juni 24- Julai 2 mwaka huu. Wachezaji walioitwa ni Abdulrahman Mandawanga (Dodoma), Abraham Mohamed (Mjini Magharibi), Ayoub Alfan (Dodoma), Bakari Masoud (Tanga), Daniel Justin (Dodoma), Denis Dionis (Ilala), Edward Songo (Ruvuma), Fikiri Bakari (Tanga), Hassan Kabunda (Temeke), Joseph Chidyalo (Dodoma), Mutalemwa Katunzi (Morogoro) na Mwarami Maundu (Lindi). Wengine ni Nankoveka Mohamed (Ilala), Nelson Peter (Morogoro), Omari Saleh (Singida), Rajab Rajab (Mwanza), Said Said (Kagera), Shiza Kichuya (Morogoro), Shukuru Msuvi (Temeke), Tanganyika Suleiman (Kigoma), Tumaini Baraka (Kilimanjaro) na William John (Ruvuma). Pia Michelsen ameongeza wachezaji saba kwenye kikosi cha Serengeti Boys ambacho Septemba mwaka huu kitacheza na Kenya kuwania tiketi ya fainali za vijana wenye umri chini ya miaka 17 za Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Morocco. Wachezaji walioongezwa kwenye kikosi hicho ambao pia wametoka kwenye Copa Coca-Cola ni Abdallah Baker (Mjini Magharibi), Abdallah Kheri (Mjini Magharibi), Calvin Manyika (Rukwa), Dickson Ambunda (Mwanza), Hassan Mganga (Morogoro), Miza Abdallah (Kinondoni) na Mzamiru Said (Morogoro).

OLIMPIKI 2012: YE SHIWEN AKANA KUTUMIA DAWA ZA KUONGEZA NGUVU.

Ye Shiwen.
MUOGELEAJI kutoka China aliyeshinda medali ya dhahabu katika michuano ya Olimpiki, Ye Shiwen amekanusha taarifa kuwa alikuwa ametumia madawa ya kuongeza nguvu katika mashindano hayo. Kocha wa timu ya waogeleaji kutoka Marekani awali alikaririwa akisema kuwa Shiwen ambaye alivunja rekodi katika mashindano ya uogeleaji ya mita 400 alikuwa ametumia kitu cha ziada kutokana na kasi aliyoionyesha katika mzunguko wa mwisho uliopelekea kuvunja rekodi hiyo. Kwa upande mwingine polisi jijini London walimkamata kijana mmoja kutokana na tuhuma za kutuma ujumbe wa kuudhi katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii twitter kwenda kwa mpiga mbizi wa Uingereza Tom Daley. Kikosi cha timu taifa ya Uingereza kinatarajiwa kutupa karata yake ya kwanza baadae leo kuwania medali katika michezo ya canoeing, sarakasi, kupiga mbizi, na kukimbiza farasi.

Monday, July 30, 2012

FIRST LADY MICHELLE OBAMA HUGS ENTIRE U.S. BASKETBALL TEAM AFTER WIN OVER FRANCE.







HISPANIA WAAGA MAPEMA MICHUANO YA OLIMPIKI.

TIMU ya taifa ya vijana chini ya miaka 23 ya Hispania imeenguliwa mapema katika michuano ya Olimpiki inayofanyika jijini London baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Honduras ikiwa ni kipigo cha pili mfululizo kufuatia kile walichopata kutoka kwa Japan kwa idadi kama hiyo ya mabao. Honduras ambao walishinda bao la mapema kupitia kwa mshambuliaji wake Jerry Bengtson wamefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali pamoja na Japan ambao waliwafunga Morocco bao 1-0 katika kundi D. Katika michezo ya kundi C Brazil ilifanikiwa kusonga mbele baada ya kuifunga Belarus mabao 3-1 wakati Misri ilitoa sare ya bao 1-1 na New Zealand hivyo itabidi washinde mchezo wao wa mwisho dhidi ya Belarus ili waweze kusonga mbele. Mexico ilifanikiwa kushinda mabao 2-0 dhidi ya Gabon katika kundi B wakati Korea Kusini walifanikiwa kushinda mabao 2-1 hivyo kupelekea timu hizo kuwa na alama sawa katika kundi hilo.

HAMILTON AIBUKA KINARA WA MBIO ZA LANGALANGA ZA HUNGARY GRAND PRIX.

DEREVA wa magari yaendayo kasi ya Langalanga kutoka timu ya McLaren, Lewis Hamilton amefanikiwa kushinda mbio za Hungary Grand Prix jana. Hamilton ambaye ni raia wa Uingereza alimaliza mbio hizo kwa kasi zaidi ya wenzake ambao aliwaacha kwa sekunde 0.413 na kufuatiwa na dereva wa timu ya Lotus, Romain Grosjean aliyeshika nafasi ya pili katika mbio hizo. Sebastian Vettel wa timu ya Red Bull alimaliza katika nafasi ya tatu akifutiwa na Jenson Button ambaye ni muingereza kutoka timu ya McLaren pia alimaliza katika nafasi ya nne. Wengine ni Kimi Raikkonen aliyemaliza katika nafasi ya tano akifuatiwa na Fernando Alonso wa timu ya Ferrari katika nafasi ya sita wakati mkali mwingine wa mbio hizo Mark Webber alimaliza katika ya 11. Magari ya Ferrari ambayo yalitamba kipindi cha mvua katika michuano ya Ujerumani katika mbio hizo za majira ya kiangazi yameshindwa na kusababisha kupunguza pengo la alama ambazo Alonso alikuwa akiongoza katika orodha ya madereva bora duniani.

WILSHERE KUREJEA UWANJANI OCTOBA.

Jack Wilshere.
MENEJA wa klabu ya Arsenal Arsenal Wenger amesema kuwa kiungo nyota wa klabu hiyo Jack Wilshere hata kuwa sehemu ya kikosi chake katika michezo ya mwanzo wa Ligi Kuu nchini Uingereza kutokana na majeraha yanamsumbua. Wilshere ambaye ana miaka 20 alishindwa kucheza msimu uliopita kutokana na kufanyiwa upasuaji wa goti aliofanyiwa Mei mwaka jana. Wenger ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kukamilisha ziara ya bara la Asia jijini Hong Kong amesema kuwa anatarajia mchezaji huyo kurejea dimbani mwezi Octoba. Wakati akiuguza goti lake Wilshere alilitonesha tena wakati akifanya mazoezi ili arejee uwanjani na hivyo kumfanya mchezaji kukosa michuano ya Ulaya iliyomalizika Julai mosi mwaka huu ambapo anatarajiwa kuanza mazoezi mepesi Agosti na akitarajia kurejea uwanjani Octoba.

Arsenal vs Kitchee FC 2-2 Pre Season Hong Kong