Tuesday, September 17, 2013

TIMU YA MADAKTARI WA FIFA YASHAURI KOMBE LA DUNIA 2022 NCHINI QATAR LIFANYIKE MAJIRA YA BARIDI.

MWENYEKITI wa kamati ya afya ya Shirikisho la Soka Duniani-FIFA Michel D’Hooghe ameshauri kuwa michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika nchini Qatar 2022 ni lazima ichezwe katika majira ya baridi. D’Hooghe amesema anajua Qatar wana uwezo wa kuandaa michuano hiyo katika majira ya kiangazi ambapo timu zinaweza kufanya mazoezi na kucheza katika hali ya hewa inayokubalika lakini tatizo linabaki kwa mashabiki watakaokwenda kushuhudia michuano hiyo. Amesema mashabiki watahitaji kusafiri kutoka uwanja mmoja kwenda mwingine na anafikiri itakuwa sio vyema kwao kufanya hivyo katika sehemu yenye joto linalozidi nyuzi joto 47 au zaidi. Tayari rais wa FIFA Sepp Blatter amekubaliana na mpango wa kuangalia uwezekano wa kubadilisha michuano hiyo kutoka katika majira ya kiangazi kama ilivyozoeleka kwenda majira ya baridi. Lakini mpango huo wa kuhamisha michuano hiyo kati ya Novemba na Desemba 2022 unapingwa vikali na Uingereza ambao wanalalamika utavuruga ratiba ya ligi yao.

No comments:

Post a Comment