RAIS wa Shirikisho la Soka nchini Ukraine Anatoliy Konkov amesema wachezaji wa timu ya taifa ya nchi hiyo hawatasafiri kwenda Cyprus kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Marekani utakaochezwa kesho lakini Chama Cha Soka cha Marekani kinaamini mchezo huo utakachezwa kama ulivyopangwa. Mchezo huo mara ya kwanza ulitakiwa kuchezwa jijini Kharkiv lakini ulihamishwa na kupelekwa Cyprus kwasababu ya matatizo ya kisiasa na baada ya Marekani kuomba hivyo. Konkov amesema kwasasa hawawezi kucheza mashindano ya kitaifa kwasababu hawaruhusiwi kucheza katika ardhi yao ya nyumbani hivyo haoni umuhimu wa kwenda Cyprus katika kipindi hiki ambacho nchi yao iko katika matatizo. Rais huyo aliendelea kudai kuwa wanacheza soka kwa ajili ya watu wao na nchi yao hivyo timu yao haitasafiri kwenda Cyprus badala yake itabakia nyumbani. Wakati Konkov akitoa kauli hiyo Shirikisho la Soka la Marekani liliandika katika mtandao wake wa twitter kuwa mechi hiyo itachezwa kama ilivyopangwa kwakuwa shirikisho la Ukraine lilithibitisha timu yao kusafiri kwenda Cyprus. Mvutano huo umekuja kufuatia rais wa Urusi Vladimir Putin kupata kibali kutika katika bunge la nchi hiyo kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Ukraine katika rasi ya Crimea hatua ambayo inapingwa na Marekani na mataifa mengine barani Ulaya.
No comments:
Post a Comment