Friday, February 10, 2012

ZAMBIA YATOA UBANI KWA WENZAO.

TIMU ya taifa ya Zambia imejiandaa na fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa kwenda kwenye ufukwe na kuimba nyimbo pamoja na kuweka mashada ya maua kuwakumbuka wachezaji wenzao ambao walikufa katika ajali ya ndege karibu miongo miwili iliyopita. Wachezaji hao walitembea katika mchanga ufukweni jijini Libreville karibu na mahali ambapo ndege ya kijeshi ya Zambia ilianguka baharini mara baada ya kuruka muda mfupi mwaka 1993 na kuua wachezaji 25 na maofisa wa timu hiyo pamoja na wahudumu watano wa ndege hiyo. Tukio hilo la kuhuzunisha liliiondolea Zambia kikosi bora kabisa kuwahi kutokea katika nchi hiyo ambao walikuwa wakitajwa kama moja ya nchi ambazo zingenyakuwa Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka uliofuata. Kikosi hicho kilitembea kimyakimya huku kila mchezaji akiwa ameshika maua na baadae kuanza kuimba na kulaza maua pembeni mwa ufukwe huo huku wakiomba kwa wenzao ambao walipoteza maisha eneo hilo. Jumapili kikosi hicho kitaingia uwanjani kupambana na timu inayopewa nafasi kubwa kunyakuwa kombe hilo ya Ivory Coast ambayo inashika nafasi ya kwanza katika orodha za ubora Afrika na duniani nafasi ya 18.

No comments:

Post a Comment