Wednesday, July 18, 2012

URA, SIMBA ZATINGA ROBO FAINALI KAGAME.


MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, timu ya Simba imefanikiwa kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Ports ya Djibout katika mchezo wao wa pili wa hatua ya makundi wa michuano ya Afrika Mashariki na Kati inayojulikana kama Kombe la Kagame. Katika mchezo huo mshambuliaji mpya kutoka Ruvu Shooting ya Pwani, Abdallah Juma aliyeingia kuchukua nafasi ya Amri Kiemba mwanzoni mwa kipindi cha pili ndiye alikuwa shujaa wa mchezo huo baada ya kufunga mabao mawili dakika za 60 na 73 na Felix Sunzu kumalizia msumari wa mwisho katika jeneza la Ports kwa kufunga kwa penalti dakika ya 64. Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika bila nyavu za Ports kutikisika, na katika kipindi hicho Sunzu, mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia, alipoteza nafasi tatu za wazi mno, za kufunga mabao akiwa amebaki yeye na kipa, Kalid Ali Moursal. Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mserbia, Milovan Cirkovick kipindi cha pili kuwaingiza Juma Nyosso kuchukua nafasi ya Haruna Shamte, Abdallah Juma aliyechukua nafasi ya Kiemba na baadaye Uhuru Suleiman kuchukua nafasi ya Haruna Moshi ‘Boban’ yaliisaidia Simba. Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha alama tatu baada ya kucheza mechi mbili na sasa inashika nafasi ya tatu kwenye Kundi A, nyuma ya URA ambayo imeshaingia hatua ya robo fainali kwa kuwa na alama sita baada ya kuibuka kidedea kwa mabao 3-1 dhidi ya AS Vita. Simba itamaliza na AS Vita ya DRC, mechi ambayo itakuwa kali kwa sababu timu zote zina alama sawa.

No comments:

Post a Comment