MENEJA wa timu ya taifa ya Uingereza, Roy Hodgson ametuma wajumbe wake maalumu kukagua sehemu ya kuchezea ya uwanja watakaotumia Jumamosi kwa ajili mechi yao ya ufunguzi dhidi ya Italia huku mkuu anayehusika na kutengeneza nyasi za uwanja huo akikiri kuwa ziko katika hali mbaya. Katika picha zilizopigwa katika sehemu mbalimbali za uwanja huo wa Amazonia zimeonyesha sehemu kubwa ya nyasi zikiwa zimekauka na kubadili rangi na kuwa ya kahawia. Carlos Botelli ambaye ndiyo msimamizi wa uwanja huo amesema uwanja huo uko katika hali mbaya kutokana na kutofanyiwa ukarabati wa kutosha. Botella aliongeza kuwa mji Manaus uliopo uwanja huo hauna barabara hivyo vifaa vingi viwkimo mashine na mahitaji mengine yalilazimika kuletwa kwa meli ndio maana mambo mengi yamechelewa. Uwanja huo wenye uwezo kuingiza mashabiki 39,118 ulijengwa mwaka jana na unatarajiwa kutumika kwa ajili ya michezo minne ukiwemo mchezo wa kundi G kati ya Marekani na Ureno utakaochezwa Juni 22. Lakini pamoja na hayo Shirikisho la Soka Duniani-FIFA limedai kuwa nyasi za uwanja huo kukauka na kubadili rangi kumetokana na matumizi makubwa ya mbolea na tatizo hilo limeshughulikiwa na hakuna shaka kwamba mchezo wa kundi D utachezwa hapo. Baada ya kucheza mechi yao ya ufunguzi ya kundi D Jumamosi, Uingereza wanatarajiwa kupambana na Uruguay katika mchezo utakaochezwa huko jijini sao Paulo Juni 19 kabla ya kuivaa Costa Rica huko Belo Horizonte siku tano baadae.

No comments:
Post a Comment