MENEJA wa klabu ya Juventus, Antonio Conte ambaye amiongoza timu hiyo kushinda mataji matatu mfululizo ya Ligi Kuu nchini Italia maarufu kama Serie A amejiuzulu wadhifa huo ikiwa imepita miezi miwili toka asaini mkataba mpya. Conte ambaye amewahi kuwa mchezaji Juventus kwa miaka 13 na baadae kuchukua mikoba ya kuinoa klabu hiyo mwaka 2011 alikuwa akitaka uwekezaji mkubwa ili aweze kupambana na changamoto katika michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya. Kikosi cha Juventus kilifanikiwa kumaliza msimu wa Serie A wakiwa mabingwa kwa tofauti ya alama 17 na AS Roma alioshika nafasi ya pili na kuwa klabu ya kwanza nchini humo kumaliza kwa zaidi ya alama 100. Pamoja na kwamba taarifa hizo zimekuwa za ghafla sana, lakini Juventus wameshajipanga kuziba nafasi hiyo ambapo kocha Massimiliano Allegri anaonekana kupewa nafasi kubwa. Allegri amekuwa hana kibarua toka alipotimuliwa na AC Milan Januari mwaka huu na Juventus itakuwa changamoto nzuri kwake kumrudisha katika ramani.

No comments:
Post a Comment