NIGERIA imepigwa marufuku ya kushiriki mashindano yeyote ya soka yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA. Hatua hiyo imefikiwa baada ya maofisa wa serikali kufukuza viongozi wote wa kamati ya utendaji ya Shirikisho la Soka nchini humo-NFF. Hatua hiyo ya FIFA inamaanisha kuwa hakuna klabu yeyoye ya soka wala timu ya taifa itakayoruhusiwa kushiriki mashindano yoyote ya kimataifa. Kabla ya kuchukua hatua hiyo FIFA iliionya Nigeria kuwa ingeichukulia hatua ifikiapo Jumanne iliyopita kama viongozi wa NFF hawatarejeshwa lakini Serikali ikapuuza onyo hilo. FIFA katika taarifa yake imedai kuwa wataifungulia nchi hiyo kushiriki michuano ya kimataifa mara watakapowarejesha madarakani viongozi waliowatimua. Hatua hiyo itaiathiri timu ya taifa ya soka ya wasichana walio na umri wa chini ya miaka 20 ambayo inapaswa kushiriki mchuano wa Kombe la Dunia endapo kifungo hicho hakitaondolewa mpaka Julai 15.

No comments:
Post a Comment