Friday, March 15, 2013

UJERUMANI KUWANIA NAFASI YA KUANDAA NUSU FAINALI NA FAINALI YA EURO 2020.

CHAMA cha Soka cha Ujerumani-DFB kimesema kuwa kinaweza kugombea kuandaa michuano ya Ulaya 2020 hatua ya nusu fainali na fainali kama jiji la Istanbul litapewa jukumu la kuandaa michuano ya olimpiki 2020. Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA limesema kuwa linataka michuano ya 2020 kufanyika katika miji 13 kuzunguka bara hilo badala ya nchi moja moja kwasababu ya matatizo ya kifedha na kusheherekea miaka 60 toka kuanzishwa michuano hiyo. UEFA imedai kuwa miji 12 itapewa nafasi ya kuandaa mechi tatu za makundi na mchezo mmoja wa hatua ya mtoano ya timu 16 bora au robo fainali. Mji mwingine uliobakia ndio utapewa uenyeji wa kuandaa hatua muhimu ambazo ni mechi mbili za nusu fainali na fainali lengo kubwa likiwa kujaribu kupunguza gharama kubwa ambazo nchi moja imekuwa ikipata wakati wa kuandaa michuano hiyo. Rais wa DFB Wolfgang Niersbach amesema bado hawajaamua kama wagombee nafasi ya kuandaa michezo mine mpaka robo fainali au michezo ya nusu fainali na fainali mpaka uchaguzi wa mji utakaoandaa michuano ya olimpiki 2020 utakapofanyika ambapo Istanbul ni mojawapo ya miji inayotafuta nafasi hiyo. 


No comments:

Post a Comment