Friday, March 4, 2016

RONALDO ATAKA KUFUNGA BAO LA KIHISTORIA.

MSHAMBULIAJI nyota wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo amebainisha kuwa na hamu kubwa ya kufunga bao kipekee kwa kuwapiga chenga wachezaji wote 11 wa upinzani, wakati wakielekea katika mchezo wao wa La Liga dhidi ya Celta Vigo. Nyota huyo wa kimataifa wa Ureno mwenye umri wa miaka 31, ameshafunga mabao 500 kwa klabu na nchi yake wakati kipindi chote hiki lakini bado ana matamanio ya kufunga mengine zaidi ya kumbukumbu. Ronaldo amekiri bao analofikiria kufunga hivi sasa inaweza isiwezekane kwa uhalisia kutokana na ugumu wake lakini amesema atajaribu kufanya hivyo siku moja. Ronaldo amesema amefunga mabao mengi mazuri lakini bao analotaka katika ndoto zake hivi sasa ni lile la kuwapiga chenga wapinzani wake wote 11 kama vile ilivyo katika michezo ya video. Nyota huyo amewahi kunyakuwa tuzo ya bao bora la mwaka inayojulikana kama FIFA Puskas kufuatia bao lake la mkwaju wake wa mbali aliopiga katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya FC Porto mwaka 2009.

No comments:

Post a Comment