Wednesday, February 8, 2012

FIFA YATOA RAMBIRAMBI MISRI.

SHIRIKISHO la Soka la Dunia-FIFA limetoa kiasi cha dola 250,000 kama rambirambi kwa familia zilizopoteza ndugu zao katika vurugu zilizotokea uwanjani nchini Misri. Katika taarifa yake FIFA imesema kuwa itatoa fedha hizo kupitia akaunti iliyofungiliwa na klabu ya Al Ahly ya kusaidia wahanga wa tukio hilo. Mashabiki wa klabu hiyo yenye maskani yake jijini Cairo ndio wengi waliopoteza maisha katika tukio hilo lililochukua roho za watu wapatao 70 katika mchezo wa Ligi Kuu nchini humo kati ya Al Masry na Al Ahly jijini Port Said. Katika taarifa hiyo rais wa FIFA Sepp Blatter amesema kuwa wahanga wengi katika tukio hilo walikuwa ni vijana wadogo na pia walipata msaada mkubwa kutoka katika familia zao ambao sasa nao wanahitaji msaada. Polisi wanatuhumiwa kushindwa kuwalinda mashabiki wa Al Ahly ambao walikuwa wakiandamana mwaka uliopita na kumuondoa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Hosni Mubarak.

No comments:

Post a Comment