Wednesday, July 18, 2012

TIKETI LAKI TANO ZADODA OLIMPIKI.

WAANDAAJI wa michuano ya Olimpiki wanapunguza ukubwa wa baadhi ya viwanja ambavyo vitatumika katika mechi za soka baada ya kushindwa kuuza tiketi zote walizotengeneza kwa ajili ya michuano hiyo. Waandaaji wa michuano hiyo ambayo itafanyika jijini London, wamesema kuwa tiketi za soka zipatazo 250,000 bado ziko sokoni hivi sasa huku zingine 50,000 zikiwa zimebakia kwa ajili ya michezo mingine. Tiketi zaidi ya 200,000 za soka na tiketi zingine 200,000 kwa ajili ya michezo mingine zinatarajiwa kwenda sokoni mara baada ya kurudishwa na Kamati ya Olimpiki ya Taifa huku tiketi zingine 150,000 zikitarajiwa kugawiwa kwa watoto wa shule. Kiongozi wa kamati ya maandalizi ya michuano hiyo Sebastian Coe amesema kuwa siku zote tiketi za mpira wa miguu ndio huwa zinasuasua lakini kuelekea michuano hiyo tiketi zilizouzwa zaidi ni za soka kuliko za michezo mingine. Zaidi ya tiketi milioni moja bado hazijauzwa lakini waandaaji walipunguza idadi hiyo kwa kupunguza idadi ya viwanja na kubakia na tiketi 500,000 ambazo hazijauzwa. Mechi za soka zitachezwa katika viwanja tofauti ambavyo ni Uwanja wa Saint James Park uliopo jijini Newcastle, Old Trafford uliopo jijini Manchester, Hampden Park jijini Glasgow, City of Coventry uliopo jijini Coventry, Uwanja wa Millenium jijini Cardiff na Wembley uliopo jijini London. Fainali ya soka ya wanaume na wanawake zinatarajiwa kuchezwa katika Uwanja wa Wembley.

No comments:

Post a Comment