MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Italia, Ciro Immobile amemtaka kocha Cesare Prandelli kumchezesha sambamba na Mario Balotelli katika mchezo wao wa ufunguzi wa Kombe la Dunia dhidi ya Uingereza utakaochezwa Jumamosi. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 alifunga mabao matatu na kutengeneza mengine mawili katika ushindi wa mabao 5-3 iliyopata Italia dhidi ya klabu ya Fluminense ya Brazil ukiwa ni mchezo wa kujipima nguvu kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia. Immobile ambaye kwasasa amejiunga na Borussia Dortmund baada ya kumaliza msimu akiongoza kwa ufungaji mabao akiwa na Torino katika Ligi Kuu ya Italia, anategemea kiwango chake hicho kitampa nafasi ya kuanza katika mchezo wao wa kwanza wa kundi D. Nyota huyo amesema anajua maamuzi ya mwisho anayo kocha na ataheshimu chochote atakachoamua lakini yeye anadhani akicheza sambamba na Balotelli wataweza kufanya maajabu. Italia itacheza mechi yao ya ufunguzi Jumamosi dhidi ya Uingereza huko Manaus kabla ya kupambana na Costa Rica na Uruguay katika mechi zingine za kundi lao.

No comments:
Post a Comment