KLABU ya Esperance ya Tunisia hatimaye imefanikiwa kupata ushindi wake wa kwanza katika hatua ya makundi baada ya kuwafunga mahasimu wao wa Tunisia CS Sfaxien jana kwa mabao 2-1. Mabao yaliyofungwa na Oussama Darragi katika dakika ya 65 na lingine la Idriss Mhirssi alilofunga dakika moja baadae yalitosha kuwapa ushindi waliohitaji mabingwa hao wa michuano hiyo mwaka 2011. Pamoja na ushindi huo Esperance imeendelea kubakia mkiani mwa kundi B baada ya mwezi uliopita kufungwa na Entente Setif ya Algeria na baadae kufungwa tena na Al Ahli Benghazi ya Libya. Kwa upande wa mechi nyingine ya kundi B Entente Setif nao walilazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani na Al Ahli Benghazi. Kwa upande wa kundi A TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC nayo ilifanikiwa kuichapa Zamalek ya Misri kwa bao 1-0 katika mchezo uliochezwa jijini Lubumbashi. Bao pekee lililofungwa na Rainford Kalaba lilitosha kuipa Mazembe ushindi ambao umewaweka kileleni mwa kundi lao wakiwa na alama sita. Kwa upande wa wenzao wa DRC klabu ya AS Vita wao wako katika nafasi ya pili katika kundi hilo wakitofautiana kwa alama mbili baada ya kutoa sare ya bao 1-1 na Al Hilal ya Sudan katika mchezo uliochezwa Ijumaa iliyopita.

No comments:
Post a Comment