MSHAMBULIAJI wa Bayern Munich, Mario Mandzukic amethibitisha kuwa ataondoka katika timu hiyo ikiwa ni matokeo ya kushindwa kwenda sawa na mipango ya kocha Pep Guardiola. Mandzukic amekuwa akihusishwa kuhamia katika vilabu vya Ligi Kuu nchini Uingereza ikiwemo Chelsea baada ya mustakabali wake katika timu hiyo kwenda mrama kutokana na usajili mshambuliaji wa Borussia Dortmund Robert Lewandowski. Nyota huyo wa kimataifa wa Croatia ambaye alikuwa akipata namba katika kikosi cha kocha wa zamani wa Bayern Jupp Heynckes amekuwa hana namba ya kudumu katika kikosi cha Guardiola msimu huu. Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28 hatimaye amethibitisha kuondoka Bayern huku tatizo kubwa akilitaja kushindwa kuendana na falsafa za Guardiola. Mandzukic pia amebainisha kuwa alikutana na Karl-Heinz Rummenigge mapema mwezi jana na kumtaarifu ofisa huyo nia yake ya kuondoka.

No comments:
Post a Comment