Wednesday, June 4, 2014

RONALDO BADO GONJWA.

TIMU ya taifa ya Ureno imeingiwa na mchecheto katika kambi waliyoweka huko New Jersey, Marekani kutokana afya ya mshambuliaji wao nyota Cristiano Ronaldo. Wakati michuano ya Kombe la Dunia ikikaribia, Ronaldo ambaye ni mchezaji bora wa dunia wa mwaka amekuwa na habari mbaya kuhusu maumivu aliyonayo. Chama cha Soka cha nchi hiyo kimetoa taarifa kuwa Ronaldo amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya msuli wa nyuma ya mguu wake wa kushoto pamoja na goti katika mguu huo huo. Mbali na Ronaldo wachezaji wengine wa timu hiyo akiwemo Meireles, Pepe na Beto nayo wamekuwa wakisumbuliwa na majeraha na wote wamekuwa wakifanya mazoezi katika kituo cha mazoezi cha New York Jet ili kuwaweka fiti kabla ya michuano ya Kombe la Dunia inayotarajiwa kuanza Juni 12. Wakati Ureno wakiwa wameshazungumzia mara kwa mara juu ya majeraha ya msuli yanayomsumbua Ronaldo hii ni mara ya kwanza kuripoti juu ya maumivu ya goti kwa mchezaji huyo. Ureno imepangwa katika kundi G na watafungua dimba kwa kuikabili Ujerumani Juni 16 huko Salvador kabla ya kuivaa Marekani wiki moja baadae huko Manaus na baadae kumaliza na Ghana katika mechi zake za makundi Juni 26 jijini Brasilia.

No comments:

Post a Comment