MKURUGENZI wa michezo wa klabu ya Feyenoord, Martin van Geel amekiri kuwa wako tayari kumuuza Stefan de Vrij kama watapata ofa nzuri katika kipindi hiki cha usajili wa kiangazi. Beki huyo kinda ni mmoja ya wachezaji waliong’ara katika michuano ya Kombe la Dunia na amekuwa akifuatiliwa kwa karibu na timu ya Lazio kabla ya kuanza kwa msimu wa 2014-2015, wakati Manchester United nao pia wameonyesha kumuwinda ili kuendelea kuimarisha kikosi chao. Kutokana na mkataba wa De Vriji kubakia mwaka mmoja, Feyenoord wanaonekana wako tayari kuanza mazungumzo ya kumuuza kama wataletewa ofa nzuri. Van Geel amesema beki huyo ametoka katika akademi yao na amecheza katika kikosi cha kwanza kwa kipindi cha miaka mitano hivyo kama timu yoyote wataleta ofa nzuri wanaweza kumuuza. De Vrij mwenye umri wa miaka 22 amecheza mechi zaidi 150 akiwa na Feyenoord toka alipoanza kuchezea kikosi cha kwanza mwaka 2009-2010 huku akiitumikia timu yake ya taifa ya Uholanzi mechi 19 na kufunga bao moja.

No comments:
Post a Comment