MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amebainisha Alexis Sanchez anaweza kurejea katika mchezo wa Jumapili hii dhidi ya Stoke City lakini nyota huyo wa kimataifa wa Chile atafanyiwa vipimo kabla ya uamuzi wa kumtumia kutolewa. Mara ya mwisho Sanchez mwenye umri wa miaka 27 kuonekana uwanjani ilikuwa katika sare ya bao 1-1 dhidi ya Norwich City Novemba 29 mwaka jana na toka wakati huo amekuwa nje akijiuguzi majeruhi ya msuli wa paja. Arsenal ilikuwa na matumaini ya nyota huyo kurejea kabla ya mwaka mpya lakini majeruhi hayo yalimkwamisha na kumfanya kuongeza wiki zingine tatu. Akihojiwa Wenger amesema atakuwa na tahadhari ingawa ana nafasi ya kuwepo katika kikosi cha Jumapili hii. Wenger aliendelea kudai kuwa pamoja na hayo atafanyiwa vipimo Ijumaa na Jumamosi ili kujiridhisha kama wanaweza kumtumia kwa ajili ya mchezo huo.

No comments:
Post a Comment