Saturday, September 8, 2012
US OPEN: SERENA ATINGA FAINALI, SASA KUKUTANA NA AZARENKA.
MCHEZAJI tenisi nyota kutoka Marekani, Serena Williams amefanikiwa kutinga hatua ya fainali ya michuano ya wazi ya Marekani baada ya kumsambaratisha Sara Erran kutoka Italia kwa 6-1 6-2. Williams mwenye mataji makubwa 14 ambaye alishinda medali ya dhahabu katika michuano ya Olimpiki mwaka huu alimfunga Errani ambaye anashika namba 10 katika orodha za ubora wa mchezo huo kwa upande wa wanawake kwa kutumia muda wa dakika 64 kujihakikishia nafasi yake ya kucheza fainali. Mwanadada huyo amepoteza mchezo mmoja kati ya 26 aliyocheza toka alipolewa katika mzunguko wa kwanza kwenye michuano ya wazi ya Ufaransa Mei 29 mwaka huu. Sasa atapambana na mwanadada Victoria Azarenka ambaye anashika namba moja katika orodha za ubora ili kujaribu kushinda taji lake la nne la michuano hiyo katika fainali itakayofanyika kesho jijini New York. Azarenka ambaye ni raia wa Belarus alitinga katika hatua hiyo baada ya kumfunga Maria Sharapova kutoka Urusi katika nusu fainali iliyochezwa jana.

No comments:
Post a Comment