SHIRIKISHO la Soka la Italia, FIGC limetangaza kumfungia nahodha wa klabu ya Lazio Stefano Mauri kwa miezi sita baada ya kushindwa kutoa taarifa ya shughuli za upangaji matokeo katika mechi. Mbali na Mauri wachezaji wengine walioadhibiwa ni pamoja na Mario Cassano, Stefano Ferrario, Carlo Gervasoni na Alessandro Zamperini kutokana na sakata hilo. Wachezaji watano walikuwa katika uchunguzi kufuatia tuhuma za upangaji matokeo wa mechi za Lazio dhidi ya timu za Genoa na Lecce katika msimu wa Serie A 2010-2011 na sasa wamekutwa na hatia na kamati ya nidhamu ya FIGC. Katika taarifa ya FIGC iliyotumwa katika mtandao wake imedai kuwa katika tukio lililohusha mchezo kati ya Lazio na Genoa, Gervasoni amefungiwa miezi miwili, Cassano amefungiwa miezi minne, Ferrario na Mauri wamefungiwa miezi sita na Zamperini amefungiwa miaka miwili. Kwa kuongezea timu ya Lecce ilitozwa faini ya euro 20,000 na Lazio euro 40,000 baada ya timu hizo nazo kukutwa na hatia ya upangaji matokeo.
No comments:
Post a Comment