Tuesday, March 18, 2014

FA YAMSHIKIA BANGO ANELKA MPAKA FIFA.

CHAMA cha Soka nchini Uingereza kimekwenda mbali zaidi kuhakikisha kuwa Nicolas Anelka anaitumia adhabu ya mechi tano alizofungiwa kwa kuonyesha ishara ya kibaguzi. Anelka aliyekuwa akicheza West Bromwich Albion alitimuliwa na klabu hiyo Ijumaa iliyopita baada ya kutandikwa adhabu na FA kwa ishara yake hiyo aliyoionyesha wakati akishangilia bao dhidi ya West Ham United Desemba mwaka jana. FA inataka kuwa na uhakika kuwa Mfaransa huyo bado atatumikia adhabu hiyo pamoja na uwezekano wa klabu yake nyingine ikawa nje ya Uingereza ndio maana wameamua kulipeleka suala hilo Shirikisho la Soka Duniani-FIFA. Msemaji wa FIFA alithibitisha kuwasiliana na FA kuhusiana na suala hilo na kuomba adhabu hiyo ifanye kazi popote duniani ambapo mchezaji huyo atakwenda. FIFA kwasasa inaliangalia suala hilo kwa mapana kabla ya kulitolea majibu.

No comments:

Post a Comment