MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Real Madrid, Gareth Bale ameonyesha furaha yake ya kucheza fainali ya kwanza ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati timu yake ikijiandaa kupambana na Atletico Madrid. Nyota huyo wa kimataifa wa Wales amekuwa na msimu mzuri na timu hiyo baada ya kuwa mmoja wapo ya wachezaji muhimu katika safari hiyo ya kwenda Lisbon kufuatia uhamisho wake wa euro milioni 100 kutoka Tottenham Hotspurs. Bale amesema ana hamu kubwa na mchezo huo dhidi ya mahasimu wao wa jiji na mabingwa wa La Liga Atletico na kuongeza kuwa amependa mambo yalivyokwenda katika msimu wake wa kwanza na timu hiyo. Nyota huyo pia alikuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Madrid kwenye mchezo wa mwisho wa La Liga dhidi ya Espanyol baada ya kufunga bao katika ushindi wa mabao 3-1 waliopata kwenye mchezo huo.
No comments:
Post a Comment