MWAMUZI aliyeshindwa kuona tukio la Luis Suarez akimng’ata Giorgio Chiellini wakati wa Kombe la Dunia amechaguliwa kuchezesha mchezo wa nusu fainali utakaowakutanisha wenyeji Brazil na Ujerumani hapo kesho. Shirikisho la Soka Duniani-FIFA lilithibitisha kuwa mwamuzi huyo Marco Rodriguez ambaye ni raia wa Mexico ndiye atakayechezesha mechi hiyo itakayopigwa huko Belo Horizonte. Huo unakuwa mchezo wa pili kwa Rodriguez kuchezesha katika michuano hiyo ukiwemo mchezo kati ya Uruguay na Italia katika hatua ya makundi ambao ulishuhudia Uruguay wakisonga mbele kwa ushindi mwembamba wa bao 1-0. Mapema katika mchezo huo Rodriguez alimpa kadi nyekundu Claudio Marchisio wa Italia kwa kucheza faulo mbaya lakini alishindwa kuona tukio la Suarez kumng’ata Chiellini ambalo lilipelekea FIFA kuingilia kati na kumfungia mshambuliaji huyo miezi minne. FIFA pia imethibitisha kuwa mwamuzi wa Mark Geiger wa Marekani ndiye atakayekuwa msimamizi wa mchezo huo wa kesho.
No comments:
Post a Comment