KOCHA wa timu ya taifa ya Brazil, Luiz Felipe Scolari amedai kuwa mshambuliaji wake nyota Neymar alikuwa akilia kuwa hana hisia katika miguu yake baada ya kuchezewa na faulo na beki wa Colombia Juan Zuniga. Scolari amesema timu nzima ilichanganyikiwa baada ya faulo hiyo na Marcelo ndiye mchezaji wa kwanza kufika eneo la tukio na kumuuliza Neymar anavyojisikia na kujibiwa kuwa hana hisia katika miguu yake. Mara baada ya kupewa jibu hilo Marcelo aliogopa na kuanza kupaza sauti akimuta daktari lakini ilishindikana kuingia uwanjani kwa wakati kwasababu ya kutopata ruhusa kutoka kwa mwamuzi. Kocha aliendelea kudai kuwa wamempoteza mchezaji mmoja ambaye walikuwa hawataki kumkosa kuelekea katika mchezo wao wa nusu fainali na fainali. Wakati huo huo, daktari wa timu hiyo Jose Luiz Runco, amezima tetesi kuwa kuna uwezekano wa Neymar kuwepo katika mchezo wa fainali ya michuano ya Kombe la Dunia kama timu hiyo ikifanikiwa kufika huko. Vyombo vya habari nchini Brazil vimeripoti kuwa mshambuliaji huyo anaweza kupata matibabu maalumu ambayo yanaweza kumuwezesha kuwa fiti katika mchezo wa fainali lakini Runco alikanusha hilo na kudai kuwa ni jambo lisilowezekana.
No comments:
Post a Comment