MWANA Mfalme wa Jordan Ali Bin Al Hussein, rafiki wa karibu wa rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya Michel Platini, ametangaza mipango yake ya kugombea uongozi katika uchaguzi ujao wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA. Al Hussein ambaye ndiye makamu wa rais wa FIFA na kiongozi wa Shirikisho la Soka la Jordan na Asia Magharibi, amesema amevutiwa kugombea nafasi hiyo ili kumaliza tuhuma za rushwa zinaoliandama shirikisho hilo. Mwana Mfalme huyo mwenye umri wa miaka 39 ambaye amepata elimu yake nchini Uingereza na Marekani anaungana na Jermone Champagne katika kinyang’anyiro hicho cha kutaka kumuangusha rais wa sasa Sepp Blatter ambaye naye ametangaza kugombea kwa kipindi kingine. Al Hussein amesema anaitaka nafasi hiyo kwani ameona wakati umefika wa kubadili fikra na muonekano wa shirikisho hilo ambalo limegubikwa na kashfa mbalimbali za ufisadi. Uchaguzi wa Shirikisho hilo unatarajiwa kufanyika Mei mwaka huu jijini Zurich, Switzerland.

No comments:
Post a Comment