Wednesday, January 7, 2015

PEARSON AWAONYA WACHEZAJI WANAOKWENDA KWENYE AFCON.

MENEJA wa klabu ya Leicester City, Nigel Pearson amewaonya wachezaji wake wanaokwenda kushiriki michuano ya Mataifa ya Afrika-Afcon mwezi huu kujichunga na kuhakikisha wanarejea wakiwa katika kiwango chao cha juu. Nyota hao Riyadh Mahrez ataiwakilisha Algeria na Jeffrey Schlupp ataiwakilisha Ghana katika michuano hiyo itakayofanyika huko Guinea ya Ikweta kuanzia Januari 17 mpaka Februari 8 mwaka huu. Pearson amesema wachezaji hao wanapaswa kujichunga na kuwa tayari kwa mapambano ya kujiokoa na balaa la kushuka daraja pindi watakaporejea katika majukumu yao ya kimataifa. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa wachezaji wengi wanaokwenda kushiriki michuano hiyo hurejea viwango vyao vikiwa vimeshuka kutokana na kubadili hali ya hewa na staili ya uchezaji. Pearson alifafanua kuwa Ligi Kuu ina kasi sana kulinganisha na michuano ya Afcon hivyo mara nyingi wachezaji wakitoka huko lazima wapambane kurejesha kasi yao kama ilivyokuwa awali.

No comments:

Post a Comment