Tuesday, January 6, 2015

TETESI ZA USAJILI ULAYA: UNITED KUMUUZA HERNANDEZ KIANGAZI, CHELSEA YAWAZIDI MAARIFA ARSENA NA LIVERPOOL KWA KINDA LA SAINT ETIENNE, INTER YAMNASA SHAQIRI.

KATIKA habari za tetesi za usajili zilizopamba vichwa vya habari vya mitandao na magazeti mbalimbali barani Ulaya ni pamoja na klabu ya Manchester United kupanga kumuuza Javier Hernandez mwishoni mwa msimu huu pindi atakapomaliza mkopo wake Real Madrid. Kwa upande mwingine Chelsea wanaonekana kupigwa bao na Leicester City baada ya mshambuliaji wa kimataifa wa Croatia Andrej Kramaric mwenye umri wa miaka 23 kuchagua kujiunga na timu hiyo badala ya Chelsea. Pamoja na habari hizo Chelsea nao wanaonekana kuwazidi maarifa Arsenal na Liverpool katika mbio za kulinasa kinda la Saint Etienne kiungo Rayan Souici mwenye umri wa miaka 16 ambaye amepewa jina utani la Paul Pogba mpya. Naye Wilfried Bony amewapasha Swansea City kuwa nataka kuhamia klabu inayoshioriki Ligi ya Mabingwa Ulaya mwezi huu. Nyota huyo wa kimataifa wa Ivory Coast ambaye atakuwa sehemu ya kikosi cha nchi hiyo kitakachoshiriki michuano ya Mataifa ya Afrika, amekuwa akiwindwa na mabingwa Ligi Kuu Mancherster City. City nao wanaweza kumpoteza Micah Richards ambaye anaweza kwenda Chelsea katika majira ya kiangazi. Beki huyo mwenye umri wa miaka 26 yuko kwa mkopo katika klabu ya Fiorentina lakini mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu. Habari nyingine kubwa ni klabu ya Inter Milan imefanikiwa kuipiga bao Liverpool kwa kumsajili winga wa klabu ya Bayern Munich Xherdan Shaqiri mwenye umri wa miaka 23. Naye meneja wa klabu ya Juventus, massimiliano Allegri amethibitisha kuwa timu hiyo ina nia ya kumsajili kiungo wa klabu ya Galatasaray Wesley Sneijder mwenye umri wa miaka 30. Kwa upande mwingine klabu ya Leeds United imempa ofa ya mkataba mwingine kiungo chipukizi Lewis Cook mwenye umri wa miaka 17 hivyo kuzikata maini klabu za Liverpool, Manchester United, Arsenal na Tottenham Hotspurs zilizokuwa zikimmezea mate.

No comments:

Post a Comment