KIUNGO mahiri wa kimataifa wa Ivory Coast Yaya Toure ana nafasi ya kuwa mchezaji wa kwanza kushinda tuzo ya mchezaji bora wa Afrika kwa mara ya tano mfululizo wakati mshindi atakapotangazwa kesho jijini Lagos. Tuzo hizo ambazo hupigiwa kura na manahodha na makocha wa timu za taifa, Toure anagombani sambamba na golikipa wa Nigeria Vincent Enyeama na mshambuliaji nyota wa Gabon Pierre-Emerick Aubameyang. Pamoja na Ivory Coast kushindwa kufanya vyema katika Kombe la Dunia mwaka jana, Toure amefanikiwa kupata nafasi hiyo kutokana na kiwango pamoja na mafanikio aliyopata katika klabu yake ya Manchester City. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 31 ndiye aliyefunga bao la ushindi katika mchezo wa fainali wa Kombe la Ligi dhidi ya Sunderland Machi mwaka jana na kufunga mabao 20 katika mbio zao za taji la Ligi Kuu. Kwa upande wa Aubameyang mwenye umri wa miaka 25, yeye amekuwa katika kiwango cha juu katika klabu ya Borussia Dortmund pamoja na kuwa msimu wake wa kwanza katika timu hiyo huku Enyeama yeye akiisaidia Nigeria kutinga mzunguko wa pili katika Kombe la Dunia mwaka jana. Nyota hao wawili Aubameyang na Enyeama wote wanaingia katika orodha hizo kwa mara ya kwanza.

No comments:
Post a Comment