BEKI wa Barcelona, Dani Alves ameitwa katika dakika za mwisho katika kikosi cha timu ya taifa ya Brazil kea ajili ya michuano ya Copa Amerika ambayo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi leo. Alves mwenye umri wa miaka 32 anachukua nafasi ya beki wa kulia wa Real Madrid Danilo ambaye alipata majeruhi Jumapili iliyopita katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Mexico. Nyota huyo ambaye alisaini mkataba wa miaka miwili na Barcelona Jumanne, alikuwa hajajumuishwa katika kikosi cha Brazil toka ilipotandikwa mabao 7-1 katika mchezo wa nusu fainali wa Kombe la Dunia dhidi ya Ujerumani mwaka jana. Alves aliachwa na kocha Luiz Felipe Scolari katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo na toka wakati huo hajapata tena nafasi toka ujio wa kocha mpya Dunga. Danilo anakuwa mchezaji wa nne kuondolewa katika kikosi cha Brazil kutokana na majeruhi baada ya Luis Gustavo, Diego Alves na Marcelo nao kuachwa.

No comments:
Post a Comment