MENEJA wa Manchester United, Louis van Gaal amethibitisha winga Jesse Lingard alipata majeruhi katika mchezo wa Ligi Kuu waliofungwa mabao 2-1 na Bournemouth juzi. Lingard alitolewa nje katika kipindi cha kwanza kufuatia kupata majeruhi ya msuli wa paja na Van Gaal amesema winga huyo mwenye umri wa miaka 22 atachunguzwa kuangalia ukubwa wa tatizo lake. Kuumia kwa Lingard kunaongeza orodha ndefu ya majeruhi kwa United hivyo kumpa wakati mgumu Van Gaal kupata kikosi bora katika kipindi hiki. Van Gaal aliwakosa wachezaji saba wa kikosi cha kwanza katika mchezo dhidi ya Bournemouth akiwemo nahodha Wayne Rooney, mabeki Chris Smalling, Matteo Darmian, Marcos Rojo na Luke Shaw huku viungo wakiwa Antonio Valencia na Ander Herrera. Kiungo Bastian Scheinsteiger alikosa mchezo wa juzi kutokana na kutumikia adhabu na pia atakosa mechi zingine mbili za United dhidi ya Norwich City na Stoke City.

No comments:
Post a Comment