Wednesday, December 9, 2015

RONALDO AVINJA REKODI YAKE MWENYEWE YA MABAO CHAMPIONS LEAGUE.

MSHAMBULIAJI nyota wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo amefunga mabao manne na kuweka rekodi mpya ya mabao katika hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kufuatia kuigaragaza Malmo ya Sweden kwa mabao 8-0 jana. Mshambuliaji nyota wa kimataifa wa Ufaransa, Karim Benzema pia alifunga hat-trick yake ya kwanza katika kipindi cha miaka mitano katika mchezo huo uliokuwa wa upande mmoja. Ronaldo anakuwa amefikisha jumla ya mabao 11 aliyofunga katika hatua ya makundi na kuipita rekodi ya mabao tisa aliyoweka mwenyewe msimu wa 2013-2014 na Luiz Adriano wa Shakhtar Donetsk msimu uliopita. Akihojiwa Ronaldo amesema amefurai kujiwekea rekodi nyingine lakini pia aliwapongeza wachezaji wenzake kwa kuonyesha dalili za kuimarika huku wakijenga hali ya kujiamini zaidi. Madrid pia wamefanikiwa kufikia rekodi ya ushindi mkubwa zaidi katika michuano hiyo ambayo iliwekwa na Liverpool walioichapa Besiktas kwa mabao 8-0 Novemba mwaka 2007, kipindi hicho pia wakinolewa na Rafa Benitez.

No comments:

Post a Comment