Saturday, September 8, 2012
MESSI AWASHUKURU MASHABIKI WA ARGENTINA.
NAHODHA wa kikosi cha timu ya taifa ya Argentina Lionel Messi ameonyesha kufurahishwa kwake na ushindi waliopata katika mchezo wa kufuzu michuano ya Kombe la Dunia dhidi ya Paraguay na kuwashukuru mashabiki kwa kushangilia katika mchezo huo. Nyota huyo anayecheza katika klabu ya Barcelona mashuti yake yaligonga mwamba mara mbili wakati timu yake ilipoibuka na ushindi wa mabao 3-1 katika Uwanja wa Mario Kempes uliopo jijini Cordoba lakini alifanikiwa kuzifumania nyavu katika kipindi cha pili kwa mpira mzuri wa adhabu aliopiga. Mabao mengine ya timu hiyo yalifungwa na Angel Di Maria na Gonzalo Higuain na kuipaisha Argentina mpaka kileleni mwa msimamo wa timu zitakazofuzu michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014. Akihojiwa Messi amesema kuwa anajisikia furaha pindi anapoona mashabiki wanawashangilia kwani kunawaongeza nguvu ya kufanya vizuri zaidi. Mshambuliaji huyo mpaka sasa ameshafunga mabao tisa katika mechi tano alizoichezea timu hiyo kwa mwaka huu ambapo katika michezo yote aliyofunga timu yake iliibuka na ushindi.

No comments:
Post a Comment