Thursday, July 18, 2013

BLATTER APANGA KUBADILISHA MICHUANO YA KOMBE LA DUNIA 2022.

RAIS wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Sepp Blatter amesema michuano ya Kombe la Dunia 2022 inatakiwa kubadilishwa na kuchezwa katika kipindi cha baridi kwasababu ya joto katika majira ya kiangazi nchini Qatar. Blatter amekiri kuwa anatakiwa apokee baadhi ya lawama kwa kutoliangalia tatizo la joto kali kwa karibu wakati walipoipa nchi ya Qatar haki ya kuandaa michuano hiyo mwaka 2010. Akihojiwa na waandishi wa habari jijini Kitzbuehel, Austria Blatter amesema michuao ya Kombe la Dunia huwa ni sherehe kwa mashabiki hivyo haiwezi kuchezwa katika kipindi cha kiangazi. Blatter aliendelea kusema kuwa inawezekana kuweka vipoza hewa uwanjani lakini huwezi kuweka vipoza hewa nchi nzima na wachezaji wanatakiwa kucheza kwenye hali ya hewa nzuri ili waweze waonyeshe soka safi. Mapema Machi mwaka huu Blatter alidai kuwa Kombe la Dunia ni michuano ambayo inatakiwa kuchezwa Juni na Julai na kusema kuwa mabadiliko yoyote ya michuano hiyo mwaka 2022 watapendekeza waandaaji wenyewe. Lakini baada ya ziara yake huko Mashariki ya Kati na kujionea hali ilivyo katika kipindi cha kiangazi katika nchi zenye majangwa Blatter ameonekana kubadili msimamo wake na kuamua kuanzisha mjadala kujadili suala hilo na kamati ya utendaji ya shirikisho hilo itakayokutana Octoba mwaka huu.

No comments:

Post a Comment