Friday, July 19, 2013
CAS YAZIFUNGULIA FENERBAHCE NA BESIKTAS.
KLABU za Fenerbahce na Besiktas zinatarajiwa kuwepo katika upangaji ratiba wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na Europa League baada ya adhabu zao kutenguliwa kwa muda. Klabu hizo za Uturuki zilikuwa zimepewa adhabu ya kufungiwa kushiriki michuano ya vilabu ya Ulaya Juni mwaka huu kutokana na kuhusishwa na tuhuma za upangaji matokeo katika mechi zao za ligi. Lakini adhabu hizo zilitenguliwa na Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo-CAS baada ya timu hizo kuwasilisha rufani zao huko. Kutokana na hilo klabu hizo zitajumuishwa katika ratiba za awali za michuano hiyo lakini bado wanaweza kufungiwa kuingia katika hatua ya makundi wakati CAS itakapotoa uamuzi wake wa mwisho. CAS itatangaza uamuzi wake kwa Fenerbahce Agosti 28 siku moja kabla ya kupangwa ratiba ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya huku hatma ya Besiktas ikijulikana Agosti 30 nayo ikiwa ni siku moja kabla ya upangaji ratiba ya makundi ya Europa League.
No comments:
Post a Comment