MWANARIADHA nyota wa mbio fupi kutoka Jamaica, Usain Bolt amepanga kuibuka na ushindi katika mashindano ya dunia ya mbio za mita 100 baada ya kupoteza medali hiyo mwaka 2011 jijini Daegu. Bolt ambaye ni bingwa mara sita wa medali za dhahabu katika michuano olimpiki, alienguliwa katika mashindano ya jijini Daegu kwa kuanza kukimbia kabla ya kuruhusiwa hatua ambayo ilipelekea Mjamaica mwenzake Yohane Blake kushinda mbio hizo baada ya kurudiwa. Toka wakati huo Bolt anaonekana kusahau kipindi hicho kigumu na kuingia jijini Moscow akiwa mwanariadha anayepewa nafasi kubwa ya kushinda baada ya Blake kujitoa kutokana na majeruhi na wengine kama Tyson Gay wa Marekani na Asafa Powell wa Jaimaica wao wakijitoa baada ya kushindwa vipimo vya dawa za kuongeza nguvu. Akihojiwa mara baada ya kushinda mbio za mita 100 za Diamond League zilizofanyika jijini London wiki iliyopita, Bolt amesema kocha wake amekuwa akimkumbusha juu ya tatizo lake kwenye kuanza lakini akamtaka kuacha kukumbuka yaliyotokea nyuma.
No comments:
Post a Comment