MCHEZAJI tenisi namba moja wa zamani kwa upande wa wanawake, Martina Hingis amepata ushindi wake wa kwanza toka aliporejea tena uwanjani baada ya kushinda mechi ya mzunguko wa kwanza ya wawili wawili katika michuano ya wazi California. Hingis mwenye umri wa miaka 32 raia wa Switzerland alistaafu mchezo huo mwaka 2007 lakini alikubali mwaliko wa kucheza pamoja na Daniela Hantuchova wa Slovakia. Wawili hao walitumia muda wa dakika 51 pekee kuwagaragaza Julia Goerges na Darija Jurak kwa seti 2-0 zenye alama za 6-1 6-1 na kusonga mbele katika hatua ya pili ya michuano hiyo. Hingis ambaye ji raia wa Switzerland amesema anajisikia vyema kushinda mchezo huo na kumpongeza mwenzake kwamba alifanya mchezo huo uwe rahisi kwao kutokana na uwezo mkubwa alionao. Maumivu ya kifundo cha mguu yalimlazimisha Hingis kustaafu mchezo huo kwa mara ya kwanza mwaka 2003 akiwa na umri wa miaka 22 lakini alirejea miaka mitatu baadae na kushinda taji lake la 43 la WTA kabla ya kushindwa vipimo vya dawa za kuongeza vilivyopelekea kufungiwa kwa miaka miwili.
No comments:
Post a Comment