MSHAMBULIAJI wa Everton, Romelu Lukaku amesema ni hatua ya kujivunia kufunga bao la 50 kwa klabu lakini amesikitishwa kutoweza kuihakikishia timu yake alama tatu katika mchezo dhidi ya Crystal Palace Jumatatu iliyopita. Lukaku mwenye umri wa miaka 22, alikuwa akicheza mechi yake ya 100 akiwa na Everton na kusheherekea mafanikio hayo kwa kufunga bao la 50 katika mashindano yote. Pia huo unakuwa mchezo wa tano mfululizo wa Ligi Kuu kwa mashambuliaji huyo kufunga bao akizidiwa michezo na Jamie Vardy wa Leicester City aliyeweka rekodi mpya ya kufunga katika michezo 11 mfululizo. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1, Lukaku amesema anadhani walistahili kuondoka na alama zote tatu kwani walitengeneza nafasi nyingi za kufunga. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa anajivunia hatua aliyofikia lakini akiwa kama mchezaji anataka kupata ushindi katika mechi.

No comments:
Post a Comment