Thursday, March 17, 2016

HODGSON AMUITA DRINKWATER KATIKA KIKOSI CHAKE.

KOCHA wa timu ya taifa ya Uingereza, Roy Hodgson amemuita kwa mara ya kwanza kiungo wa Leicester City Danny Drinkwater katika kikosi cha nchi hiyo kwa ajili ya mechi mbili za kirafiki dhidi ya Ujerumani na Uholanzi. Nyota huyo amekuwa katika kiwango bora msimu huu huku klabu hiyo ikiongoza Ligi Kuu kwa tofauti ya alama tano wakiwa wamebaki na mechi nane kabla ya msimu kumalizika. Kutokana na juhudi za kiungo huyo mwenye umri wa miaka 26ambaye alianza soka lake Manchester United, Hodgson ameamua kumuita kwa mara ya kwanza kuitumikia Uingereza. Wengine waliojumuishwa katika kikosi hicho ni pamoja na nyota wa Tottenham Hotspurs Danny Rose, Dele Alli, Eric Dier na Harry Kane. Nahodha wa Uingereza Wayne Rooney amekosekana kutokana na majeruhi lakini Daniel Sturridge amerejea na ataungana na Jamie Vardy, Theo Walcott na danny Welbeck kuunda safu ya ushambuliaji.

No comments:

Post a Comment