MENEJA wa zamani wa Chelsea, Jose Mourinho amesema mafanikio ya Barcelona yanatokana na juhudi zao za kucheza kitimu na sio uwezo wa Lionel Messi pekee. Barcelona walipata nafasi ya kucheza robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuiondosha Arsenal kwa jumla ya mabao 5-1 huku Messi akifunga bao katika mchezo wa Camp Nou jana. Messi mwenye umri wa miaka 28 ndio anaonekana nyota katika kikosi cha Barcelona baada ya kufunga mabao 37 na kusaidia mengine 15 katika mechi 37 alizocheza msimu huu. Akihojiwa kuhusiana na hilo Mourinho amesema pamoja na Barcelona kuwa na vipaji vya mchezaji mmoja mmoja akiwemo na Messi lakini pia hucheza kitimu jambo ambalo huwafanya mambo yao mengi kuonekana rahisi. Hata hivyo, Mourinho aliongeza kuwa hakuna meneja asiyemtaka mchezaji kama Messi kuwepo katika kikosi chake.
No comments:
Post a Comment