Wednesday, August 3, 2016

DRAXLER ABAINISHA KUTAKA KUONDOKA WOLFSBURG.

KIUNGO wa kimataifa wa Ujerumani, Julian Draxler amebainisha kuwa anataka kuondoka VfL Wolfsburg kwenda klabu kubwa kiangazi hiki na kuongeza tayari alishaweka wazi nia yake hiyo wakati wa michuano ya Ulaya. Draxler mwenye umri wa miaka 22 alitoa kauli hiyo wakati akifanyiwa mahojiano na jarida la Bild, akijibu madai ya meneja Dieter Hecking aliyedai kuwa kiungo huyo hawezi kuondoka klabuni kiangazi hiki. Akihojiwa Hecking alidai kuwa hawezi kujibu tetesi zote lakini anachofahamu yeye ni kuwa Draxler ataendelea kubaki nao kwa ajili ya msimu ujao. Hata hivyo, Draxler ambaye alijiunga na Wolfsbuef akitokea Schalke kwa euro milioni 34 mwaka 2014 na kusaini mkataba wa miaka mitano, amekanusha madai hayo akidai walipaswa kuzungumza naye kwanza kabla ya kutoa kauli hiyo hadharani. Draxler amecheza mechi 35 za mashindano yote msimu uliopita na kufunga mabao tisa na kusaidia mengine nane.

No comments:

Post a Comment