Wednesday, March 5, 2014

SIOGOPI KUACHWA KOMBE LA DUNIA - PODOLSKI.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Ujerumani, Lukas Podolski amesisitiza kuwa haogopi kuachwa katika kikosi cha nchi hiyo kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia lakini ana uhakika atachaguliwa. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 28 alipata majeruhi ya kuchanika msuli mwishoni mwa Agosti mwaka jana hatua ambayo ilipelekea kumuweka nje mpaka mwishoni mwa jana huku akifanikiwa kuanza katika mechi tano pekee katika klabu yake ya Arsenal msimu huu. Wakati ikiwa imebaki miezi mitatu kabla ya kuanza michuano ya Kombe la Dunia nchini Brazil, Podolski anajua anahitaji muda zaidi ili kuonyesha kuwa anastahili nafasi katika kikosi hicho kinachonolewa na Joachim Low lakini nyota huyo amesema ana uhakika na nafasi yake. Akihojiwa kabla ta mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Chile baadae leo Podolski amesema hana hofu juu ya nafasi yake katika kikosi cha Ujerumani kwasababu ana uzoefu wa muda mrefu kwa kucheza mechi na mashindano mengi. Podolski amesema baada ya kukaa nje kwa kipindi kirefu hivi sasa yuko fiti na tayari ameshazungumza na makocha wote wawili wa klabu na timu yake ya taifa. Ujerumani imepangwa kundi moja na timu za Ureno, Ghana na Marekani katika michuano ya Kombe la Dunia inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Juni 12.

No comments:

Post a Comment