Monday, September 3, 2012

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

KLABU KUTETEA PINGAMIZI ZA WACHEZAJI
Klabu zote zilizowekewa pingamizi za wachezaji kwenye usajili na zile zilizoweka pingamizi zinatakiwa kufika kwenye kikao cha Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kitakachofanyika kesho (Septemba 4 mwaka huu). Kikao hicho kitafanyika kwenye ofisi za TFF kuanzia saa 6 kamili mchana, na kitakuwa chini ya uenyekiti wa Alex Mgongolwa. Klabu ambazo zimewekewa/ kuweka pingamizi na zitakiwa kuwepo kwenye kikao zilikiwa na nyaraka zote kuthibitisha madai yao ni Azam, African Lyon, Flamingo, JKT Ruvu, Kagera Sugar, Oljoro JKT, Polisi Mara, Rollingstone Multipurpose Ateclass Foundation, Simba, Super Falcon, Toto Africans, Villa Squad na Yanga.

PONGEZI KWA UONGOZI MPYA KRFA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Kigoma (KRFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika juzi (Septemba 1 mwaka huu). Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa KRFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani Kigoma. TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya KRFA chini ya uenyekiti wa Omari Saleh Mkwarulo ambaye amechaguliwa kwa kipindi cha kwanza. Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu mkoani Kigoma kwa kuzingatia katiba ya KRFA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake. Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya KRFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF. Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Omari Saleh Mkwarulo (Mwenyekiti), Issa Bukuku (Katibu), Ahmed Msafiri Mgoyi (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF) na Mohamed Nassoro (Mwakilishi wa Klabu TFF). Nafasi za Makamu Mwenyekiti na Katibu Msaidizi zitajazwa kwenye uchaguzi mdogo utakaofanyika baadaye baada ya waliogombea ambao hawakuwa na wapinzani kushindwa kupata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa.

DEREVA WA LANGALANGA AFUNGIWA KUTOZWA FAINI KWA KUSABABISHA AJALI.

DEREVA wa magari ya kwenda kasi ya Langalanga wa timu ya Lotus, Romain Grosjean amefungiwa mara moja kushiriki mashindano ya magari hayo baada ya kusababisha ajali katika kona ya kwanza ya michuano ya Grand Prix nchini Ubelgiji. Grosjean raia wa Ufaransa mwenye miaka 26 ambaye amehusika katika ajali saba za mzunguko wa kwanza katika mashindano 12 msimu huu pia ametozwa faini ya paundi 40,000 kwa tukio hilo. Dereva huyo alimchomekea dereva wa MacLaren, Lewis Hamilton mwanzoni mwa mashindano hayo na kusababisha magari hayo kugongana na kuharibika vibaya ingawa kahuna mtu aliyejeruhiwa kwenye tukio hilo. Grosjean ambaye ni dereva wa kwanza kufungiwa kushiriki shindano moja toka Michael Schumacher alipopewa adhabu kama hiyo mwaka 1994 amesema kuwa alitazama vibaya umbali uliokuwepo kati yake na Hamilton akidhani kuwa alikuwa tayari amempita dereva huyo lakini haikuwa hivyo. Dereva huyo aliomba radhi kwa tukio hilo lililosababisha ajali mbaya lakini cha muhimu anashukuru hakuna aliyeumia kati yao.

MCHEZAJI SWEDEN AANGUKA NA KUFA UWANJANI.

Victor Brannstrom.
MCHEZAJI mmoja wa soka nchini Sweden ameanguka na kufariki kwa kile kinachodaiwa moyo wake kusimama kufanya kazi ikiwa ni dakika moja baada ya kuifungia timu yake bao la ushindi katika mchezo wa ligi uliochezwa Jumapili. Mchezaji huyo anayeitwa Victor Brannstrom mwenye umri wa miaka 29, aliifungia bao timu yake ya Pitea ambayo ilikuwa ikicheza na Umedalen dakika nne baada ya mchezo kuanza jana wakati alipokaa chini ghafla na kuanza kugalagala kwa mujibu ya walioshuhudia tukio hilo. Watu wa huduma ya kwanza waliingia uwanjani kujaribu kumsadia mchezaji huyo kwa kumpa huduma ya kwanza kabla ya magari matatu ya wagonjwa kuwasili na kumbeba kumuwahisha Brannstron hospitali ambapo alitangazwa kufariki muda mfupi baadae. Mchezaji huyo ambaye alikuwa akicheza katika klabu ya Helsingborg ambayo inashiriki Ligi Kuu nchini humo, alistaafu soka Januari mwaka huu kufuatia tatizo hilohilo la kuanguka lakini alirejea tena dimbani baada ya vipimo kuonyesha kuwa hakuwa na tatizo kubwa la moyo. Taarifa za awali kutoka hospitali ya Pitea ambako alipelekwa mchezaji huyo zinasema kuwa moyo wake ulisimama kufanya kazi lakini watatoa taarifa zaidi pindi mwili wake utakapofanyiwa uchunguzi wa kitu kilichopelekea kifo chake.

BRAZIL KUTUMIA JINA LA "BRAZUCA" KATIKA MIPIRA ITAKAYOTUMIKA KWENYE KOMBE LA DUNIA 2014.

SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA limesema kuwa nchi ya Brazil imeamua kuupa jina la Brazuca mpira utakaotumika kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia 2014 jina ambalo hutumika mara chache kuonyesha fahari ya taifa hilo lililopo Amerika ya Kusini. FIFA wamesema kuwa watu zaidi ya milioni moja walipiga kuchagua majina mbalimbali huku asilimia 70 ya watu hao walichagua jina hilo. Katika taarifa yake FIFA imesema kuwa jina hilo ni ishara ya hisia, fahari na ukarimu kwa wote nchi hiyo ikiwa kama kioo katika mchezo wa soka. Kampuni ya Ujerumani ya Adidas ambao ndio wasambazaji rasmi wa mipira ya Kombe la Dunia toka mwaka 1970, wamesema kuwa majina mengine mawili ambayo ni Bossa Nova na Carnavalesca ndio yalikuwa majina ya mwisho kupigiwa kura katika kinyang’anyiro hicho. FIFA waliendelea kusema kuwa hiyo ni mara ya kwanza mashabiki kushirikishwa moja kwa moja kutaja majina mpira utakaotumika kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia, ambayo bado inatengenezwa na kujaribiwa na vilabu na vyama mbalimbali vya soka duniani kote.

CAF CHAMPIONS LEAGUE: MAZEMBE WAIZIDI MAARIFA AL AHLY NA KUIPIGA 2-0, SAMATTA ANG'ARA.

MABINGWA mara nne wa michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika, TP Mazembe wamefanikiwa kukata tiketi ya kucheza nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kuifunga mabao 2-0 Al Ahly ya Misri katika mchezo uliochezwa jijini Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo-DRC. Matokeo hayo ya jana yanamaanisha timu ya Berekum Chelsea ya Ghana imeenguliwa katika michuano hiyo ya ngazi ya juu kwa vilabu barani Afrika baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Zamalek. Mabao ya Mazembe yalifungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta na Deo Kanda katika kipindi cha pili na kuendeleza uteja kwa Al Ahly ambao wameshindwa kutamba kwao katika mara zote walizokutana. Timu zote mbili zimefikisha alama 10 hivyo kuongoza katika kundi B huku nafasi ya tatu ikishikiliwa na Berekum Chelsea wenye alama tano huku wakiwa wamebakisha mchezo mmoja wa mwisho. Katika mchezo wa mwisho Al Ahly italazimika kushinda mchezo wake wa mwisho dhidi ya mahasimu wao Zamalek na kuomba TP Mazembe wapoteze mchezo wao dhidi ya Berekum Chelsea ili waweze kusonga mbele kama vinara wa kundi lao ili kuepuka kukutana na Esperance ambao wanaongoza kundi A katika nusu fainali ya michuano hiyo.

Inter vs Roma 1-3 All Highlights and Goals 2-9-2012

Udinese vs Juventus [1-4] Serie A Highlights, 02 September 2012