Friday, August 30, 2013

BESIKTAS YAENGULIA EUROPA LEAGUE BAADA KUSHINDWA RUFANI YAO.

KLABU ya Besiktas ya Uturuki imeshindwa rufani yao waliyokata kupinga kufungiwa na Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA kwa kujihusisha na upangaji matokeo ya baadhi ya mechi za ligi. Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo-CAS ilitangaza uamuzi wake wa kutupilia mbali rufani iliyokatwa na klabu hiyo hivyo kuendelea na kifungo chao cha mwaka mmoja walichopewa na UEFA na kufanya klabu hiyo kuenguliwa katika michuano ya Europa League msimu huu. Nafasi yake katika hatua ya makundi itachukuliwa na klabu ya Tromso ya Norway pamoja na kuwafunga katika mechi ya mtoano iliyochezwa jana. Klabu ya Fenerbahce nayo nafasi yake itachukuliwa na klabu ya APOEL ya Cyprus baada ya wao pia kushindwa katika rufani yao waliyopeleka CAS. 


ARSENAL YAPANGWA KUNDI LA KIFO CHAMPIONS LEAGUE.

KLABU ya Arsenal huenda ikakabiliwa na kibarua kigumu katika mechi za kutafuta nafasi ya kuingia hatua ya mtoano ya michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya. Katika mechi za makundi ya michuano hiyo Arsenal imepangwa kundi moja na timu za Borussia Dortmund ya Ujerumani, Olympique Marseille ya Ufaransa na Napoli ya Italia. Arsenal ilifuzu hatua ya makundi baada ya kuifunga Fenerbahce ya Uturuki kwa jumla ya mabao 5-0 katika mechi za mikondo miwili. Timu nyingine ya Uingereza itakayo kuwa na wakati mgumu katika mechi hizo za makundi ni Celtic ya Scotland kwani imepangwa kucheza na wababe wa soka Barcelona, AC Milan ya Italy na Ajax ya Uholanzi. Manchester City wao wamepangwa kundi moja na timu za Bayern Munich ya Ujerumani ambao ni mabingwa watetezi wa michuano hiyo, CSKA Moscow na Viktoria Plzen huku mahasimu wao Manchester United wakipangwa na Shakhtar Donetskya Ukraine, Bayer Leverkusen ya Ujerumani na Real Sociedad ya Hispania. Chelsea wenyewe wamepata kundi jepesi miongoni mwa timu za Uingereza ambapo watachuana na timu za Schalke ya ujerumani, FC Basel na Steaua Bucharest.

KAKA ATAKA KUONDOKA MADRID.

KIUNGO mahiri wa kimataifa wa Brazil, Kaka amebainisha kuwa anataka kuondoka Real Madrid ikiwa imebakia wiki moja kabla ya kipindi cha usajili majira ya kiangazi kumalizika. Kaka mwenye umri wa miaka 31 amekuwa akipambana kukuza kiwango chake chini ya kocha wa zamani Jose Mourinho na haonekana kuwa katika mipango ya kocha mpya Carlo Ancelotti baada ya kukaa benchi katika mechi mbili za La Liga msimu huu. Bali na hivyo pia ujio wa Gareth Bale kutoka Tottenham Hotspurs nao unaonyesha kumlazimisha nyota huyo kuondoka baada ya kuona atakuwa hana nafasi tena kwenye kikosi hicho. Kaka amesema anadhani wakati wake wa kuondoka umefika na tayari ameshazungumza na Ancelotti pamoja na viongozi juu ya azma yake. Kaka alitua Madrid akitokea AC Milan mwaka 2009 na toka kipindi hicho amecheza mechi 85 pekee baada ya kusumbuliwa na majeruhi ya mara kwa mara yaliyochangai kwa kiasi kikubwa kushusha kiwango chake.

NADAL AZIDI KUCHANJA MBUGA US OPEN.

MCHEZAJI nyota wa tenisi, Rafael Nadal ameendeleza ubabe katika michuano ya wazi ya Marekani kwa kumgaragaza Rogerio Dutra Silva wa Brazil na kutinga mzunguko wa tatu wa michuano hiyo inayofanyika jijini New York. Nadal anayeshika namba mbili katika orodha za ubora duniani kwa upande wanaume alifanikiwa kumfunga Dutra Silva kwa 6-2 6-1 6-0 kwa kutumia dakika 92 pekee. Kwa upande mwingine bingwa mtetezi kwa upande wa wanawake Serena Williams, bingwa mara tano wa michuano hiyo Roger Federer na Victoria Azarenka wote walifanikiwa kutinga mzunguko wa tatu wa michuano hiyo baada ya kushinda mechi zao. Williams alitinga hatu hiyo baada ya kumfunga Galina Voskoboeva kwa 6-3 6-0 wakati Federer alisonga mbele baada ya kumfunga Carlos Berlocq 6-3 6-2 6-1 huku Azarenka akimgaragaza Aleksandra Wozniak kwa 6-3 6-1.

BOLT ASHINDA MBIO ZA DIAMOND LEAGUE ZA ZURICH.

MWANARIADHA nyota wa mbio fupi, Usain Bolt wa Jamaica amefanikiwa kushinda mbio za mita 100 katika mashindano ya Diamond League yaliyofanyika jijini Zurich pamoja na kuanza taratibu. Bolt mwenye umri wa miaka 27 alishinda mbio hizo kwa kutumia muda wa sekunde 9.90 na kumshinda Mjamaica mwenzake Nickel Ashmeade aliyeshika nafasi ya pili kwa sekunde 9.94 huku Jastin Gatlin wa Marekani akishika nafasi ya tatu kwa kutumia sekunde 9.96. Akihojiwa mara baada yam bio hizo, Bolt ambaye mapema kabla alitamba kukimbia chini ya sekunde 9.80, alikiri kuanza taratibu sana katika mbio hizo ndio maana akatumia muda huo. Bolt amesema alikuwa akidhani yuko vyema lakini hakuwa katika kiwango chake alichokuwa akitaka kama ilivyokuwa mwanzoni mwa msimu.

Thursday, August 29, 2013

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

MECHI YA YANGA, COASTAL YAINGIZA MIL 152/-
Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Yanga na Coastal Union iliyochezwa jana (Agosti 28 mwaka huu) katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 152,296,000. Watazamaji 26,137 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo namba 14 ya VPL msimu wa 2013/2014 iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1. Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 36,947,427.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 23,231,593.22. Mgawo mwingine ni asilimia 15 ya uwanja sh. 18,786,827.52, tiketi sh. 3,818,890, gharama za mechi sh. 11,272,096.51, Kamati ya Ligi sh. 11,272,096.51, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 5,636,048.26 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 4,383,593.09.



COPA COCA-COLA KANDA KUANZA SEPT 2
Michuano ya Copa Coca-Cola kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 inayoshirikisha mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani inaanza kutimua vumbi Septemba 2 mwaka huu katika vituo sita tofauti. Kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa leo (Agosti 29 mwaka huu), kituo cha Mwanza mechi zake zitachezwa katika viwanja vya Alliance ambapo timu zitakazofungua dimba ni Kagera vs Kigoma, Mara vs Tabora, Simiyu vs Geita na Mwanza vs Shinyanga. Kituo cha Mbeya ambapo mechi zitachezwa viwanja vya Iyunga ni Katavi vs Njombe, na Ruvuma vs Mbeya. Kituo cha Pwani ni Ilala vs Kaskazini Unguja, na Lindi vs Pwani. Ufunguzi katika kituo cha Arusha ambapo mechi zake zitachezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta AMri Abeid ni Manyara vs Kilimanjaro, na Arusha vs Singida. Uwanja wa Jamhuri ambapo utatumika kwa mechi za kituo cha Morogoro, Tanga itacheza na Dodoma wakati Morogoro itaumana na Temeke. Mjini Zanibar kwenye Uwanja wa Chuo cha Amaan ni kati ya Kaskazini Pemba na Mjini Magharibi, na Kusini Pemba dhidi ya Kusini Unguja.



USAILI WAGOMBEA TFF, TPL BOARD KUANZA KESHO
Usaili kwa wanaoomba kuteuliwa kuwa wagombea uongozi katika uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na ule wa Bodi wa Ligi Kuu (TPL Board) unaanza kesho (Agosti 30 mwaka huu). Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Agosti 30 mwaka huu ni usaili kwa waombaji uongozi wote katika Bodi ya Ligi Kuu pamoja na waombaji uongozi wa TFF kwa kanda namba 11 (Morogoro na Pwani), kanda namba 12 (Kilimanjaro na Tanga) na kanda namba 13 (Dar es Salaam). Agosti 31 mwaka huu ni kanda namba sita (Rukwa na Katavi), kanda namba saba (Mbeya na Iringa), kanda namba nane (Njombe na Ruvuma), kanda namba tisa (Lindi na Mtwara) na kanda namba kumi (Dodoma na Singida). Usaili kwa kanda namba moja (Geita na Kagera), kanda namba mbili (Mara na Mwanza), kanda namba tatu (Simiyu na Shinyanga), kanda namba nne (Arusha na Manyara) kanda namba tano (Kigoma na Tabora), na nafasi za Rais na Makamu wa Rais wa TFF utafanyika Septemba Mosi mwaka huu. Waombaji wote wamepangiwa muda wao wa usaili. Kwa mujibu wa ratiba usaili ufanyika kuanzia saa 3 kamili asubuhi hadi saa 2 usiku. Wasailiwa wote wanatakiwa kuzingatia muda waliopangiwa.

ARSENAL YAMPA FLAMINI MKATABA WA MIAKA MIWILI.

KIUNGO Mathieu Flamini amekuwa mchezaji wa klabu ya Arsenal kwa mara ya pili baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo jana. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa alifikia makubaliano na klabu jana ambapo anatarajiwa kulipwa kiasi cha paundi 50,000 kwa wiki huku kukiwa na uwezekano wa kuongezwa mwaka mwingine wa tatu katika mkataba wake. Arsenal inatarajiwa kumtangaza rasmi nyota huyo baada ya kupata ruhusa kutoka kwa viongozi wa Ligi Kuu. Huo unakuwa usajili wa pili kwa Wenger baada ya Yaya Sanogo ambapo wachezaji wote hao walikuwa huru kutokana na kushindwa kuongeza mikataba katika klabu walizokuwepo.

CHELSEA YAAMUA KUMCHUKUA ETO'O BAADA YA KUCHEMKA KWA ROONEY.

KLABU ya Chelsea inatarajia kumsajili Samuel Eto’o kwa mkataba utakaomuwezesha kukucha kitita cha paundi milioni saba kwa mwaka baada ya kukiri kushindwa kumngo’a Wayne Rooney Manchester United. Eto’o mwenye umri wa miaka 32 atapunguza kiasi kikubwa cha mshahara wake wa paundi milioni 17 kwa mwaka ambao ulikuwa unamfanya kuwa mchezaji anayelipwa zaidi duniani akiwa na klabu ya Anzhi Makhachkala ya Urusi. Hata hivyo kuna ripoti kuwa Anzhi wamemlipa mamilioni ya fedha Eto’o ili kukatisha naye mkataba baada ya klabu hiyo kuamua kupunguza gharama za matumizi na kujaribu kuvuna wachezaji kutoka katika shule yao ya michezo badala ya kununua. Eto’o alitua jijini London kwa treni jana usiku ambapo alipigwa picha akiwa na wakala maarufu Pini Zahavi na anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya katika uwanja wa mazoezi wa Chelsea kabla ya kumaliza mazungumzo ya mwisho na klabu hiyo.

MURRAY AANZA VYEMA KUTETEA TAJI LAKE LA US OPEN.

BINGWA mtetezi wa michuano ya wazi ya Marekani, Andy Murray wa Uingereza amefanikiwa kutinga mzunguko wa pili wa michuano kwa kumchapa bila huruma Michael Llodra wa Ufaransa. Murray mwenye umri wa miaka 26 alifanikiwa kushinda kwa 6-2 6-4 6-3 ambapo sasa anatarajiwa kukwaana na Leonardo Mayer wa Argentina katika mzunguko wa pili wa michuano hiyo. Hatua ya kubadilisha mechi ya Murray kuwa mojawapo ya mechi zilizochezwa usiku, hazikuwafurahisha baadhi ya watu ambao wanadhani inaweza kuwa kikwazo kwake huko mbele ukilinganisha na wapinzani wake. Akihojiwa mara baada ya mechi hiyo ambayo ilichezwa jana usiku Murray hakuonyesha kujali muda aliopangiwa kwasababu kuna mechi nyingine pia zilizopangwa muda huo. Kwa upande wa wanawake, mwanadada Venus Williams alijikuta akiiaga michuano hiyo mapema baada ya kukubali kipigo kutoka kwa Zheng Jie wa China kwa 6-3 2-6 7-6. Pamoja na kipigo hicho Williams mwenye umri wa miaka 33 raia wa Marekani alikataa uwezekano wa kustaafu mchezo huo na kudai kuwa bado ataendelea kupambana mpaka dakika za mwisho.

MARTINO AMZAWADIA VILANOVA TAJI LA SUPERCUP.

MENEJA wa klabu Barcelona, Gerardo Martino amelitoa taji la Supercup walilopata jana kwa kocha wa zamani wa timu hiyo Tito Vilanova ambaye alilazimika kubwaga manyanga kutokana na kusumbuliwa na saratani ya koo. Barcelona walilazimishwa sare ya bila ya kufungana nyumbani dhidi ya Atletico jana hivyo kutawadhwa mabingwa wa Supercup baada ya kushinda kwa bao la ugenini walilopata katika sare ya bao 1-1 waliyopata katika mechi ya mkondo wa kwanza. Akizungumza na waandishi wa habari, Martino amesema fainali hiyo ilikwenda vyema kutokana na kazi nzuri iliyofanywa msimu uliopita hivyi wamekuwa mabingwa kwasababu ya wacheza, Vilanova na benchi lake lote la ufundi. Katika mechi hiyo Lionel Messi na Neymar walioanza katika kikosi cha kwanza cha Barcelona kwa mara ya kwanza na Martino anaamini kuwa wawili hao wataelewana vizuri zaidi katika siku za usoni. Martino alikiri wawili hao kutoelewana vizuri katika mechi hiyo lakini hana shaka kwamba katika siku zijazo watacheza vyema kwa pamoja na kutengeneza safu hatari ya ushambuliaji.

BOLT ATAMBA KUSHINDA ZURICH.

MWANARIADHA nyota wa mbio fupi, Usain Bolt wa Jamaica amesema amepumzika na yuko tayari kukimbia muda mwingine wa haraka wakati atakaposhindana katika mashindano ya Diamond League jijini Zurich, Switzerland. Bolt alishinda medali tatu katika mashindano ya Dunia yaliyofanyika jijini Moscow mapema mwezi huu huku akishinda mbio za mita 100 kwa kutumia muda wa sekunde 9.77. Akihojiwa kabla ya mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika kesho, Bolt amedai kupata mapumziko ya kutosha hivyo anaamini anaweza kukimbia chini ya sekunde 9.80 katika Uwanja wa Letzigrund. Bolt ambaye alishinda mbio za mita 200 kwa kutumia sekunde 19.66 katika uwanj huohuo mwaka jana, atachuana na Justin Gatlin wa Marekani na Mjamaica mwezake Nesta Carter ambao walishinda medali za fedha na shaba katika mashinano ya dunia.

Wednesday, August 28, 2013

CAS YATUPILIA MBALI RUFANI YA FENERBAHCE.

MAHAKAMA ya Usuluhishi ya Michezo-CAS imetupilia mbali rufani ya klabu ya Fenerbahce ya kufungiwa miaka miwili na Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA kwa kosa la kupanga matokeo. Katika taarifa yake CAS ilidai wameamua kutupilia mbali rufani hiyo kwa kukosa ushahidi hivyo adhabu waliyopewa na UEFA itaendelea kama kawaida. Kwa taarifa hiyo Fenerbahce ambao ilikuwa washiriki michuano ya Europa League msimu huu baada ya kuenguliwa na Arsenal katika mechi za kufuzu Ligi ya Mabingwa wataondolewa katika ratiba ya michuano hiyo ambayo inatarajiwa kupangwa Agosti 30. Fenerbahce walifungiwa na UEFA Juni mwaka huu baada ya maofisa wake kusaidia kupanga matokeo na kushinda taji la Ligi Kuu nchini Uturuki mwaka 2011.

GUARDIOLA NI BORA KULIKO MOURINHO - HOENESS.

RAIS wa klabu ya Bayern Munich, Uli Hoeness anadhani kuwa Pep Guardiola ameonyesha kwamba yeye ni kocha bora kuliko meneja wa Chelsea Jose Mourinho katika kipindi chake wakati akiwa Barcelona. Guardiola amekuwa na uhusiano wa mashaka na Mourinho wakati wote wakiwa nchini Hispania na maneno baina ya wawili hao yameibuka tena wiki hii wakati Mourinho alipohoji uwezo wa Guardiola kabla ya mchezo wao wa Super Cup kuashiria msimu mpya wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hata hivyo, Hoeness anaamini kuwa uamuzi wa kumteua Guardiola kuwa mbadala wa Jupp Heynckes unaonyesha wazi kuwa nani ni kocha bora. Hoeness amesema makocha hao wawili wamekuwa wakipambana kuonyeshana nani mbabe nchini Hispania kwa msimu kadhaa ambayo wamekuwa huko na Guardiola ameongoza kwa mbali. Bayern Munich ambao ni mabingwa wa Ulaya watakwaana na Chelsea ambao ni mabingwa wa Europa League katika mchezo utakaochezwa Ijumaa jijini Prague.

WAWEKA PINGAMIZI WAGONGA MWAMBA TFF.

KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeshindwa kusikiliza pingamizi mbili zilizowasilishwa mbele yake dhidi ya waombaji uongozi wawili baada ya kukosa sifa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za TFF. Kwa mujibu wa Ibara ya 11 (3) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF, pingamizi ni lazima iwekwe na mwanachama wa TFF (vyama vya mpira wa miguu vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu) au kiongozi wa kuchaguliwa wa TFF. Pia pingamizi yoyote ni lazima iwe kwa maandishi ikieleza wazi sababu za pingamizi pamoja ushahidi wa kuunga mkono pingamizi hilo, jina kamili, anuani ya kudumu na kusainiwa na mweka pingamizi au Mwenyekiti/Katibu wa mwanachama husika. Pingamizi hizo ziliwasilishwa na Shamsi Rashid Kazumari na Samwel Nyalla dhidi ya Wallace John Karia anayeomba kuwania nafasi ya Makamu wa Rais wa TFF na Vedastus Kalwizira Lufano anayeomba kuwania ujumbe wa Kamati ya Utendaji kupitia Kanda Namba Mbili ya mikoa ya Mara na Mwanza. Kwa upande wa Kazumari ambaye alikiri hata kutowahi kuiona Katiba ya TFF pamoja na Kanuni za Uchaguzi, pingamizi lake halikusikilizwa kwa vile si mwanachama wa TFF wala kiongozi wa kuchaguliwa wa TFF. Wakati pingamizi la Nyalla halikusikilizwa kwa vile hakukuwa na ushahidi wowote uliowasilishwa, hivyo kushindwa kukidhi matakwa ya Ibara ya 11(3) ya kanuni husika.

MCHEZAJI AFARIKI UWANJANI ARGENTINA.

MCHEZA soka wa Ligi Daraja la Tatu nchini Argentina amefariki kwa shinikizo la damu wakati mechi. Klabu ya Deportivo Laferrere imesema kuwa mchezaji huyo aitwaye Hector Sanabria alianguka katika dakika ya 29 ya mchezo dhidi ya General Lamadrid jana ikiwa ni siku moja kabla ya kutimiza miaka 28 ya kuzaliwa kwake. Mwamuzi wa mchezo huo Hernan Mastrangelo ambaye aliahirisha mchezo huo alidai kuwa Sanabria hakuwa amegongana wala kuwa karibu na mchezaji yoyote wakati anaanguka. Shirikisho la Soka nchini Argentina limesema mechi zote za ligi za mwishoni mwa wiki zitatanguliwa na kusimama kwa dakika moja kwa ajili ya kutoa heshima kwa Sanabria.

MALAWI WAMSHITAKI KESHI KWA UBAGUZI.

KOCHA wa timu ya taifa ya Malawi, Tom Saintfiet amesema Shirikisho la Soka la nchi hiyo limemshitaki FIFA kocha wa timu ya taifa ya Nigeria Steven Keshi. Hata ya Shirikisho hilo imekuja kufuatia Keshi kumwambia Saintfiet kwamba ni mtu mweupe anayepaswa kurejea nchini kwao Ubelgiji. Hatua ya makocha hao kurushiana maneno imekuja kufuatia Saintfiet kuonyesha wasiwasi wa usalama katika mji wa Calabar uliopo kusini mwa Nigeria ambao utatumika kwa ajili ya mechi za kufuzu Kombe la Dunia baina ya nchi hizo mbili. Keshi akihojiwa katika kipindi cha Afrikan TV amesema anafikiri kocha huyo wa Malawi ni mpuuzi na sio mwafrika hivyo anapaswa kurejea nchini kwao, kauli ambayo imechukuliwa na Saintfiet kama ni ubaguzi.

DJOKOVIC, FEDERER WASONGA MBELE US OPEN.

MICHUANO ya wazi ya Marekani imeendelea kupamba moto ambapo Sam Stosur wa Australia amekuwa mchezaji wa kwanza wa viwango vya juu kuenguliwa mapema katika michuano hiyo baada ya kukubali kipigo kutoka kwa mchezaji kinda Voctoria Duval. Stosur anayeshika namba 11 katika orodha za ubora duniani kwa upande wa wanawake , ambae ni bingwa wa michuano hiyo mwaka 2011 alijikuta akipoteza mchezo huo wa kwanza kwa Duval mwenye umri wa miaka 17 kwa 5-7 6-4 6-4. Kwa upande mwingine nyota anayeshika namba moja katika orodha za ubora duniani kwa upande wanaume Novak Djokovic alifanikiwa kutinga mzunguko wa pili wa michuano hiyo kwa kumtandika Ricardas Berankis kwa 6-1 6-2 6-2. Bingwa mara tano wa michuano hiyo Roger Federer wa Switzerland naye alifanikiwa kusonga mbele kwa kumchapa Grega Zemlja wa Slovakia kwa 6-3 6-2 7-5.

PODOLSKI AINGIA KATIKA ORODHA YA MAJERUHI ARSENAL.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amesema kuwa Lukas Podolski atakaa nje ya dimba kwa kipindi cha wiki tatu baada ya mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani kuumia msuli katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Fenerbahce jana usiku. Podolski alitolewa kwa machela mapema katika kipindi cha pili ambapo Arsenal ilishinda kwa mabao 2-0 katika Uwanja wa Emirates na kufanikiwa kutinga katika hatua ya makundi ya michuano hiyo kwa jumla ya mabao 5-0 katika mechi za mikondo miwili walizokutana. Wenger pia alishuhudia kiungo Aaron Ramsey ambaye alifunga mabao yote mawili naye akitolewa kutokana na kuumia kigimbi wakati Jack Wilshere alipata tatizo la kifundo cha mguu katika dakika za mwisho wa mchezo huo. Wenger amesema Wilshere anaonekana hakuumia sana lakini Podolski ana uhakika kuwa atakosekana kwa siku 21 huku Ramsey akitegemewa kufanyiwa uchunguzi zaidi kutokana na tatizo alilopata.

Tuesday, August 27, 2013

MBIA ATIMKIA SEVILLA KWA MKOPO.

KIUNGO mahiri wa klabu ya Queen Park Rangers-QPR, Stephane Mbia, amejiunga na klabu ya Sevilla kwa mkopo. Mchezaji huyo wa kimataifa kutoka Cameroon, mwenye umri wa miaka 27, sasa ataichezea klabu hiyo ya Hispania msimu huu wote. Mbia alijiunga na QPR, kutoka klabu ya Marseille mwaka uliopita, kwa mkataba wa miaka miwili, naye Joey Barton akajiunga na Marseille msimu huo kwa mkopo. Aliicheza QPR mechi 32, wakati klabu hiyo iliposhushwa daraja msimu uliopita. Mbia ni mchezaji wa Saba kuihama klabu hiyo kwa mkopo au kwa mkataba wa kudumu tangu waliposhushwa daraja. Katika miezi ya hivi karibuni, klabu hiyo imepoteza wachezaji wake Christopher Samba, Djibril Cisse, Jose Bosingwa, Loic Remy, Esteban Granero na Park Ji-sung. Mchezaji huyo kutoka Cameroon, alipigwa faini na QPR mwezi Mei mwaka uliopita, wakati alipotuma ujumbe kwenye ukurasa wake wa Twitter akiashiria kuwa anataka kurejea Hispania na kuichezea klabu yake ya zamani

MAJERUHI YAMSTAAFISHA DECO.

KIUNGO mahii wa kimataifa wa zamani wa Ureno, Deco ametangaza rasmi kustaafu soka akiwa na umri wa miaka 35 baada ya kupata majeraha ya msuli kwa mara ya nne toka msimu wa Ligi Kuu nchini Brazil uanze Februari mwaka huu. Deco ambaye ni mzaliwa wa Brazil alikuwa akicheza katika klabu ya Fluminense kwa miaka zaidi ya mitatu na kuiwezesha timu hiyo yenye maskani yake jijini Rio de Janeiro kushinda mataji mawili ya ligi mwaka 2010 na 2012. Katika taarifa yake Deco alidai kuwa angependelea kuendelea kuisadia Fluminense zaidi lakini anaona mwili wake unakataa kutokana na umri alionao na kuwashukuru wote waliokuwa pamoja naye katika kipindi chote ambacho amekuwa akicheza soka. Kiungo huyo ambaye jina lake halisi anaitwa Anderson Luis de Souza anakabiliwa na tuhuma za kutumia madawa yaliyokatazwa michezoni mapema mwaka huu, kesi ambayo bado inashughulikiwa na mahakama ya juu wa michezo ya Brazil. Deco alianza soka lake katika klabu ya Corinthians ya Sao Paulo mwaka 1996 na baadae kwenda timu ya CSA de Alogoas kabla ya kutimkia Ureno ambako alicheza katika vilabu vya Alverca, Salgueiros na Porto ambako alishinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya pamoja na Kombe la Mabara mwaka 2004.



Baada ya kutoka Porto alihamia Barcelona na kucheza kuanzia mwaka 2004 mpaka 2008 ambapo katika kipindi hicho alifanikiwa kushinda mataji mawili ya La Liga na Kombe la Mfalme mwaka 2005 na 2006 pamoja na taji la Ligi ya Mabingwa mwaka 2006.

HIGUAIN APATA AJALI YA BOTI ITALIA.

VYOMBO vya habari nchini Italia vimeripoti kuwa mshambuliaji mpya wa klabu ya Napoli, Gonzalo Higuain ameshonwa nyuzi 10 usoni baada ya kupata ajali ya boti Jumatatu. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Argentina ameripotiwa kupata na ajali na kujigonga usoni katika boti aliyokuwa akitumia katika kisiwa cha Capri kilichopo kusini mwa pwani ya nchi hiyo. Nyota alitibiwa kusiwani humo na baadae kuruhusiwa ambapo klabu yake ambayo inakabiliwa na mechi dhidi ya Chievo Jumamosi haikuzungumzia lolote kuhusiana na tukio hilo. Higuain alijunga na Napoli akitokea Real Madrid JUlai mwaka huu na alicheza mechi ya kwanza ya Serie A dhidi ya Bologna ambapo timu yake ilishinda mabao 3-0.

INTER YAONGEZA MKATABA NA NIKE.

KLABU ya Inter Milan ya Italia imetangaza kuongeza mkataba wa udhamini na kampuni ya Nike kwa miaka 10 zaidi na kupelekea ushirikiano na kampuni hiyo kufikia miaka 25. Mara ya kwanza Inter kuingia ubia na kampuni hiyo ya Marekani ilikuwa ni mwaka 1998, ambapo Nike bado inafaidi mikataba kama hiyo na vilabu vingine vikubwa duniani kama Manchester United na Barcelona. Pamoja na Inter kushindwa kufanya vizuri msimu uliopita ambapo walimaliza katika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu nchini Italia, mkataba huo utawasaidia kujiimarisha ili kurejesha makali yao kama ilivyokuwa zamani. Inter ambayo kwasasa inanolewa na kocha mpya Walter Mazzarri, ilianza msimu mpya wa ligi kwa kupata ushindi wa mabao 2-0 nyumbani dhidi ya Genoa Jumapili iliyopita.

WILLIAMS, NADAL WAPETA US OPEN.

MICHUANO ya wazi ya Marekani imeanza kutimua vumbi rasmi jijini New York jana kwa viwanja mbalimbali vya mji huo kuwaka moto. Bingwa mtetezi wa michuano hiyo kwa upande wa wanawake Serena Williams alianza kwa kishindo kwa kutinga mzunguko wa pili kirahisi baada ya kumgaragaza Francesca Schiavone wa Italia kwa 6-0 6-1. Williams aliyetumia muda wa saa moja pekee katika mchezo huo, amesema alikuwa akijitahidi kuwa mwangalifu kwasababu alikuwa akicheza na Schiavone ambaye ni bingwa wa zamani wa michuano ya wazi ya Ufaransa hivyo lolote lingeweza kutokea. Kwa upande wa wanaume Rafael Nadal wa Hispania ambaye aliwahi kuwa bingwa wa michuano hiyo mwaka 2010 naye alitinga mzunguko wa pili kwa kumgaragza Ryan Harrison wa Marekani kwa 6-4 6-2 6-2. Nadal ambaye alikosa kucheza michuano hiyo mwaka uliopita kutokana na kuwa majeruhi, mechi hiyo inakuwa ya kwanza kwake toka alipofungwa na Novak Djokovic katika fainali mwaka 2011.

MOURINHO AMPA ROONEY SAA 48 ZA KUCHAGUA.

MENEJA wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho amempa Wayne Rooney saa 48 kuchagua kama anataka kuondoka Manchester United na kwenda Stamford Bridge. United imekuwa ikisisitiza kuwa hawana mpango wa kumuuza nyota wake huyo ambaye alionyesha mchezo wa hali ya juu katika mechi baina ya timu hizo iliyoisha kwa sare ya bila kufungana jana. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo Mourinho amesema mtu aliyeanzisha habari hiyo ndio anatakiwa kumaliza na muda wa kufanya hilo umefika. Mourinho amesema Rooney anatakiwa kutamka kwa kinywa chake kama anataka kuondoka au kubakia Old Traford kwa msimu mwingine.

Monday, August 26, 2013

ZUBIZARRETA AMUUNGA MKONO MARTINO KUMPUMZISHA NEYMAR.

MKURUGENZI wa michezo wa klabu ya Barcelona, Andoni Zubizarreta anamuunga Gerardo Martino jinsi anavyolishughulikia suala la Neymar ambapo kocha huyo amekuwa akitumia muda mwingi kumpumzisha mchezaji huyo. Kwa mara nyingine Neymar alipangwa kama mchezaji wa akiba katika ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Malaga pamoja na kuumia kwa Lionel Messi ambaye hakucheza katika mechi hiyo ya jana. Pamoja na Messi kuumia Zubizarreta anaamini kuwa Martino alichukua uamuzi sahihi kutomuanzisha katika mechi hiyo kwasababu bado hajakuwa fiti kucheza dakika zote tisini kutokana na kutopumzika kwa muda wa kutosha. Zubizarreta amesema nyota huyo atakuwepo hapo kwa kipindi kirefu hivyo mashabiki watapata nafasi ya kumuona akicheza dakika 90 wakati akiwa fiti kwa asilimia 100. Neymar ambaye amejiunga na Barcelona akitokea Santos kwa ada ya euro milioni 57 mapema masimu huu, aligundulika na tatizo la upungufu wa damu kabla ya kupoteza uzito wa kilo saba baada ya kufanyiwa upasuaji wa koo wa maandalizi ya msimu mpya.

PELLEGRINI ALAUMU SAFU YAKE YA ULINZI KWA KUKOSA UMAKINI.

MENEJA wa klabu ya Manchester City, Manuel Pellegrini amelaumu uwezo wa safu yake ya ulinzi kushindwa kuzuia mipira miwili ya kona na kupelekea timu yake kupata kipigo cha kushangaza cha mabao 3-2 kutoka kwa timu iliyopanda daraja msimu huu ya Cardiff City. Pellegrin amesema kitu kibaya zaidi walitangulia kuondoza naa baada ya kushinda bao hilo alitegemea mambo kuwa rahisi kwao lakini mipira miwili ya kona kutoka kwa wapinzani wao iliamua matokeo hayo. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa hakutegemea kufungwa katika mchezo huo lakini kwa jinsi wapinzani wao walivyokuwa wakijilinda iliwawia vigumu kwao kutengeneza nafasi za kufunga. Lakini kocha huyo amesema pamoja na kipigo hicho walichopata hawatakiwi kukata tamaa kwani ligi bado ndefu na taratibu watajaribu kurejesha makali yao ili waweze kufanya vyema katika mechi ijayo dhidi ya Hull City.

CAF YAZIRUHUSU ZAMALEK NA AL AHLI KUCHEZA MECHI ZAO NYUMBANI PAMOJA NA MACHAFUKO.

SHIRIKISHO la Soka barani Afrika-CAF limedai kuwa mechi mbili za Ligi ya Mabingwa ya Afrika zitafanyika nchini Misri kama zilivyopangwa pamoja na machafuko yanayoendelea ambayo yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 1,000 toka jeshi litwae madaraka mwezi uliopita. Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa katika mtandao wa CAF mabingwa watetezi wa michuano hiyo Al Ahli itacheza na AC Leopards ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo-DRC katika Uwanja wa El Gouna na kufuatiwa na mechi kati ya Zamalek na Orlando Pirates ya Afrika Kusini mechi zote zitachezwa mwishoni mwa wiki ijayo. Klabu hizo mbili maarufu nchini Misri ambazo zimekuwa zikitawala soka la Afrika katika kipindi cha karibuni zote zimepangwa katika kundi A ambalo Pirates ndio wanaoongoza wakiwa na alama saba. Ahli wanafuatia katika nafasi ya pili wakiwa na alama nne sawa na Leopards waliopo nafasi ya tatu huku Zamalek wakishika mkia katika kundi hilo wakiwa na alama moja. Mechi zote mbili zitachezwa bila mashabiki baada ya mamlaka husika kuepuka mikusanyiko ambayo inaweza kuzua machafuko zaidi.

TOTTENHAM WAKUBALI KUMWACHIA BALE KWA PAUNDI MILIONI 86.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Wales, Gareth Bale yuko huru kujiunga na Real Madrid baada ya Tottenham Hotspurs kukubali uhamisho wa rekodi wa paundi milioni 86 Jana usiku. Usajili huo wa Bale kwenda Madrid utavunja rekodi ya duniani ya usajili wa paundi milioni 80 ambao klabu hiyo iliipa Manchester United kwa ajili ya Cristiano Ronaldo mwaka 2009. Inaaminika kuwa safari ya mwenyekiti wa Spurs Daniel Levy kwenda Madrid kukutana na Perez ilikuwa ni moja ya mbinu za kiongozi huyo ili aweze kumuuza nyota huyo kwa bei ghali zaidi. Mbali na Spurs kufaidika kwa kumuuza Bale ambaye walimnunua kwa paundi milioni saba kutoka Southampton miaka sita iliyopita pia mchezaji huyo anatarajiwa kukunja kitita cha paundi 300,000 kwa wiki katika mkataba wa miaka sita anaotarajiwa kusaini.

Sunday, August 25, 2013

CHELSEA YATHIBITISHA KUFIKIA MAKUBALIANO NA WILLIAN PAMOJA NA ANZHI KUHUSU UHAMISHO WA KIUNGO HUYO.

KLABU ya Chelsea imebainisha kufikia makubaliano na klabu ya Anzhi Makhachkala ya Urusi pamoja na kiungo Willian kwa ajili ya uhamisho wa kutua Stamford Bridge. Kiungo huyo wa kimataifa wa Brazil mwenye umri wa miaka 25 alionekana atasajili Tottenham Hotspurs baada ya kufanyiwa vipimo vya afya Alhamisi iliyopita lakini Chelsea waliwapiga bao baada ya kuongeza dau. Willian alisafiri kwenda Uingereza wiki iliyopita akitegemewa kusajili Spurs ili kuziba nafasi ya Gareth Bale baada ya mchezaji huyo pia kufanya mazungumzo na Liverpool. Pamoja na kufanyiwa vipimo vya afya katika uwanja wa mazoezi wa Spurs lakini nyota huyo alidai kuwa alikuwa akitafuta timu inayoshiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa ndio maana haikuwa ngumu kwake kubadili mawazo Chelsea walipomfuata na dau kubwa.


NEYMAR KUANZA KWA MARA YA KWANZA KATIKA KIKOSI CHA BARCELONA.

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Barcelona, Neymar anatarajiwa kwa mara ya kwanza kupangwa katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo kitakachocheza na Malaga wakati Lionel Messi akikosa mchezo huo kutokana na majeruhi aliyopata katika mechi ya Super Cup dhidi ya Atletico Madrid Alhamisi iliyopita. Neymar ambaye alisajili kwa euro milioni 57 mapema katika kipindi hiki cha usajili wa majira ya kiangazi akitokea Santos alipoteza kilo saba kufuatia upasuaji wa kuondoa mafindofindo baada ya michuano ya Kombe la Shirikisho Juni mwaka huu na amekuwa akipambana ili kurejea katika kiwango chake toka wakati huo. Neymar ambaye alianzia katika benchi la wachezaji wa akiba katika ushindi wa mabao 7-0 katika mechi ya La Liga dhidi ya Levante na kufunga bao lake kwanza akiwa na timu hiyo wakati alipoisawazishia katika sare ya bao 1-1 waliyopata dhidi ya Atletico. Meneja wa Barcelona, Gerard Martino alidai wiki iliyopita hawataki kumuwekea shinikizo lolote nyota wao huyo kwani wanataka azoee kucheza na wenzake kidogo kidogo.

DJOKOVIC, MURRAY WAMUHOFIA NADAL US OPEN.

MCHEZAJI nyota wa tenisi wa Serbia, Novak Djokovic amedai kuwa kiwango bora alichokuwa nacho Rafael Nadal katika kipindi hiki kinamfanya kuwa mgumu kufungika katika michuano ya wazi ya Marekani inayotarajiwa kuanza kesho. Nadal ambaye ni raia wa Hispania ameweka rekodi ya kushinda mechi 15 katika viwanja vigumu kwa mwaka huu na pia kushinda mataji ya Masters katika michuano ya Indian Wells, Montreal na Cincinnati. Djokovic alimsifu Nadal kwa kurejea katika kiwango chake baada ya kukaa nje ya uwanja kwa kipindi miezi saba akiuguza majeraha na kudai kuwa anadhani ndio mchezaji bora kwa mwaka huu na hilo halina ubishi. Mbali na Djokovic kumgwaya Nadal lakini pia Andy Murray wa Uingereza naye alionyesha kumhofia nyota huyo na kudai kuwa atakuwa moto wa kuotea mbali katika michuano hiyo itakayofanyika jijini New York.

BALE ATUA HISPANIA KUMALIZIA UHAMISHO WAKE KWENDA MADRID.

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Tottenham Hotspurs, Gareth Bale ametua nchini Hispania kujiandaa kuweka saini Real Madrid lakini klabu hizo mbili bado zinavutana kuhusiana na rekodi ya usajili kwenye uhamisho huo. Nyota huyo wa kimataifa wa Wales mwenye umri wa miaka 24 alitua Malaga kwa ndege binasfi na kwenda kwa teksi hadi Marbella, ambako anatarajiwa kukaa kwa ajili ya kukamilisha majadiliano ya dakika za mwisho kabla ya kufungwa kwa pazia la usajili. Inafahamika kuwa Madrid imetenga kitita cha euro milioni 100 sawa na paundi milioni 86 ikijumuisha na malipo kadhaa ndani ya miaka mitatu au minne, baada ya paundi milioni 70 kulipwa taslimu.  Real Madrid inacheza na Granada Jumatatu usiku katika La Liga na kama kutambulishwa kwa Bale itakuwa Jumanne. Bale, ambaye alijiunga na Spurs kwa dau la paundi milioni 10 kutoka Southampton mwaka 2007, alishinda tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Chama cha Wachezaji wa Kulipwa na Waandishi wa Soka msimu uliopita, ameifungia mabao 26 Spurs.

MECHI YA YANGA, ASHANTI YAINGIZA MIL 102/-.

MECHI ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Yanga na Ashanti United iliyochezwa jana (Agosti 24 mwaka huu) katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 102,856,000. Watazamaji 17,744 walikata tiketi kushuhudia mecchi hiyo namba moja ya VPL msimu wa 2013/2014 iliyomalizika kwa mabingwa watetezi Yanga kuibuka na ushindi mnono wa mabao 5-1. Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 24,400,102.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 15,689,898.31. Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 12,406,831.75, tiketi sh. 4,453,890, gharama za mechi sh. 7,444,099.05, Kamati ya Ligi sh. 7,444,099.05, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 3,722,049.53 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 2,894,927.41.

TYSON AKIRI KUZIDIWA NA MADAWA NA POMBE.

BINGWA wa zamani wa ngumi za uzito wa juu, Mike Tyson wa Marekani amedai kuwa anakaribia kufa kutokana na matatizo ya kutumia madawa na pombe nyingi. Tyson mwenye umri wa miaka 47 alikiri kuwa amekuwa akinywa pombe kupita kiasi lakini ana mategemeo ya hali yake kutengemaa baada ya kuanza matibabu. Akihojiwa na luninga ya ESPN, Tyson amesema anataka kuishi maisha ya bila kutumia kilevi chochote kwasababu hataki kufa. Mwaka 1987 akiwa na umri wa miaka 20 Tyson aliweka rekodi ya kuwa bingwa wa ngumi mdogo zaidi kushikilia mikanda ya uzito wa juu ya WBC, WBA na IBF. Lakini miaka mitano baadae Tyson alikamatwa kwa kosa la kumbaka mrembo Desiree Washington na kufungwa miaka sita jela na baadae kurejea tena ulingoni lakini aliamua kustaafu mwaka 2006 na sasa anafanya shughuli za upromota.

Saturday, August 24, 2013

USAJILI WA WACHEZAJI 37 WAKWAMA VPL.

KAMATI ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imezuia usajili wa wachezaji 37 wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kutokana na usajili wao kuwa na kasoro. Klabu husika zimetakiwa kurekebisha kasoro hizo kabla ya kuanza kuwatumia wachezaji hao kwenye mechi za VPL ambazo zinaanza leo (Agosti 24 mwaka huu) katika viwanja mbalimbali nchini. JKT Ruvu Stars inatakiwa kuwafanyia uhamisho (transfer) wachezaji Salum Machaku Salum aliyekuwa Polisi Morogoro na Emmanuel Leonard Swita (Toto Africans). Mgambo Shooting inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji Mohamed Hussein Neto (Toto Africans), Kulwa Said Manzi (Polisi Morogoro) na Mohamed Ally Samata (African Lyon). Pia Salum Aziz Gilla anaonekana bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Coastal Union huku kukiwa hakuna vielelezo vyovyote kutoka kwa mchezaji mwenyewe, Coastal Union au Mgambo Shooting kama ulivunjwa au umenunulia na klabu anayotaka kuchezea msimu huu. Tanzania Prisons inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji James Mjinja Magafu kutoka Toto Africans na Six Ally Mwasekaga (Majimaji). Nayo Coastal Union inatakiwa kumfanyia uhamisho mchezaji Kenneth Abeid Masumbuko kutoka Polisi Morogoro. Kagera Sugar inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji Suleiman Kibuta Rajab (Toto Africans), Godfrey Innocent Wambura (Abajalo), Eric Mulera Muliro (Toto Africans), Adam Juma Kingwande (African Lyon) na Peter Gideon Mutabuzi (Toto Africans). Pia Kagera Sugar imepata Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa ajili ya mchezaji Kitagenda Hamis Bukenya, lakini bado hana kibali cha kufanyia kazi nchini (work permit). Kwa upande wa Ruvu Shooting inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji Abdul Juma Seif (African Lyon), Lambele Jerome Reuben (Ashanti United), Juma Seif Dion (African Lyon) na Cosmas Ader Lewis (African Lyon). Oljoro JKT inatakiwa kumfanyia uhamisho mchezaji Tizzo Charles Chomba kutoka Polisi Morogoro, lakini imekataliwa kumsajili mchezaji Damas Mussa Kugesha wa Mlale JKT kwa kigezo kuwa ni askari na amehamishiwa Arusha kwa ajili ya mafunzo ya kijeshi. Kama Oljoro JKT inamtaka mchezaji huyo ni lazima ifuate taratibu za usajili kwa kumfanyia uhamisho kutoka Mlale JKT. Nayo Mtibwa Sugar inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji Ally Shomari Sharrif (Polisi Morogoro), Salim Hassan Mbonde (Oljoro JKT U20) na Hassan Salum Mbande iliyemsajili kwenye kikosi chake cha U20 akitokea Oljoro JKT U20. Ashanti United haiwezi kumtumia Said Maulid Kalikula aliyekuwa akicheza Angola kwa vile hajapata ITC. Nayo Rhino Rangers inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji Ally Ahmad Mwanyiro (Mwadui FC), Laban David Kambole (Toto Africans) na Musa Boaz Chibwabwa (Villa Squad). Klabu ya Simba inatakiwa kumfanyia uhamisho Betram Arcadi Mwombeki kutoka Pamba SC wakati wachezaji Gilbert John Kaze na Amisi Tambwe bado hawajapata ITC kutoka Burundi na hawana vibali vya kufanya kazi nchini. Mchezaji Joseph Owino tayari ITC imepatikana lakini hana kibali cha kufanya kazi nchini. Pia kipa Abel right Dhaila hana kibali cha kufanya kazi nchini. Vilevile Simba inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji wawili iliyowasajili katika kikosi chake cha U20. Wachezaji hao ni Twaha Shekue Ibrahim kutoka Coastal Union 20 na Adeyun Saleh Seif (Oljoro JKT U20). Nayo Yanga inatakiwa kumfanyia uhamisho mchezaji Rajabu Zahir Mohamed kutoka Mtibwa Sugar U20 wakati Hussein Omari Javu bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Mtibwa Sugar huku kukiwa hakuna vielelezo vyovyote kutoka kwa mchezaji mwenyewe, Mtibwa Sugar au Yanga kama mkataba huo ulivunjwa au umenunulia na klabu anayotaka kuchezea msimu huu. Wachezaji waliosajiliwa kutoka nje ambao ITC zimefika na pia wana vibali vya kufanya kazi nchini ni Crispine Odula Wadenya kutoka Bandari ya Kenya na Yayo Wasajja Fred Lutimba kutoka URA ya Uganda waliojiunga na timu ya Coastal Union. Pia Mtanzania Hamis Thabit Nyige aliyejiunga na Yanga kutoka Ureno naye tayari na ITC. Kwa mujibu wa kanuni, wachezaji wote wa ridhaa (wa madaraja ya chini ikiwemo Daraja la Kwanza) wanatakiwa kufanyiwa uhamisho (transfer) kwa klabu husika kujaza fomu za uhamisho na kulipia ada Chama cha Mpira wa Miguu cha Wilaya, Chama cha Mpira wa Miguu cha Mkoa na TFF. Pia TFF inakumbusha kuwa wachezaji wanaotajwa kuwa wamesajiliwa kama wachezaji huru (free agent) ni lazima waoneshwe kama huko walipokuwa mikataba imekwisha au la.

MAJINA YA WAOMBAJI UONGOZI TFF, TPL BOARD YAWEKWA WAZI.

KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imebandika rasmi kwenye ubao wa matangazo majina ya waombaji uongozi kwenye uchaguzi wa TFF na Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board) ili kutoa fursa kwa pingamizi. Kipindi cha pingamizi kinaanza kesho (Agosti 24 mwaka huu) hadi sas 10 kamili jioni ya Agosti 26 mwaka huu ambapo waweka pingamizi wanaruhusiwa kupitia taarifa za wale wanaokusudia kuwawekea pingamizi kabla ya kuwasilisha pingamizi husika. Kwa mujibu wa tangazo la uchaguzi, Agosti 27 hadi 29 mwaka huu ni wawekaji pingamizi na wawekewa pingamizi kufika mbele ya Kamati ya Uchaguzi kwa ajili ya kusikiliza pingamizi. Waombaji kuwania uongozi katika TFF ambao majina yao yamebandikwa ni Athuman Jumanne Nyamlani, Jamal Emil Malinzi, Omari Mussa Nkwarulo na Richard J. Rukambura (urais). Nafasi ya Makamu wa Rais ni Imani Omari Madega, Ramadhan Omari Nassib na Walace John Karia. Walioomba nafasi za ujumbe kuwakilisha kanda ni Kanda Namba Moja (Kagera na Geita) ni Abdallah Hussein Mussa na Kaliro Samson. Kanda Namba Mbili (Mara na Mwanza) ni Jumbe Odessa Magati, Mugisha Mujwahuzi Galibona, Samwel Nyalla na Vedastus Kalwizira Lufano. Kanda Namba Tatu (Shinyanga na Simiyu) ni Epaphra Amana Swai, Mbasha Matutu Mong’ateko na Stanslaus Haroon Nyongo. Kanda Namba Nne (Arusha na Manyara) ni Ally Mtumwa, Elley Simon Mbise na Omari Walii Ali. Kanda Namba Tano (Kigoma na Tabora) ni Ahmed Idd Mgoyi na Yusuf Hamisi Kitumbo. Kanda Namba Sita (Katavi na Rukwa) ni Ayoub Nyaulingo, Blassy Mghube Kiondo, Nazarius A.M. Kilungeja. Kanda Namba Saba (Iringa na Mbeya) ni Ayoub Shaibu Nyenzi, Cyprian Charles Kuyava, David Samson Lugenge, Elias Lusekelo Mwanjala, Eliud Peter Mvella na John Mwachendang’ombe Kiteve. Waombaji wa Kanda Namba Nane (Njombe na Ruvuma) ni James Patrick Mhagama, Kamwanga Rajabu Tambwe na Stanley William Lugenge. Kanda Namba Tisa (Lindi na Mtwara) ni Athuman Kingome Kambi, Francis Kumba Ndulane na Zafarani Mzee Damoder. Kanda Namba Kumi (Dodoma na Singida) ni Charles Komba, Hussein Zuberi Mwamba na Stewart Ernest Masima. Kanda Namba 11 (Morogoro na Pwani) ni Farid Salum Mbarak, Geoffrey Irick Nyange, Juma Abbas Pinto, Riziki Juma Majala na Twahil Twaha Njoki. Wanaowania kuteuliwa kugombea kupitia Kanda Namba 12 (Kilimanjaro na Tanga) ni Davis Elisa Mosha na Khalid Abdallah Mohamed wakati Kanda Namba 13 (Dar es Salaam) ni Alex Chrispine Kamuzelya, Muhsin Balhabou, Omar Isack Abdulkadir, Shaffih Dauda Kajuna na Wilfred Mzigama Kidao. Kwa upande wa TPL Board waliotangazwa kuomba kuwania uongozi wa juu ni Hamad Yahya Juma (Mwenyekiti) na Said Muhammad Said Abeid (Makamu Mwenyekiti). Wajumbe wa Kamati ya Uendeshaji ni Kazimoto Miraji Muzo, Michael Njunwensi Kaijage, Omari Khatibu Mwindadi, Salum Seif Rupia na Silas Masui Magunguma.

CASILLAS ANAPASWA KUFIKIRIA KWENDA BARCELONA - CANIZARES.

GOLIKIPA wa zamani wa klabu ya Real Madrid, Santiago Canizares amedai kuwa Iker Casillas anapaswa kufikiria kuondoka katika klabu hiyo na kwenda Barcelona. Casillas ambaye ni nahodha wa Madrid alijikuta akipoteza nafasi ya kipa namba moja kwa Diego Lopez msimu uliopita wakati Jose Mourinho akiwa hapo na pia ameonekana kubakia kuwa chaguo la pili hata chini ya kocha mpya Carlo Ancelotti. Kutokana na suala hilo Canizares haoni sababu ya Casillas kushindwa kwenda Barcelona ambako anaweza kujihakikishia kucheza katika kikosi cha kwanza. Canizares amesema kwa jinsi mambo yanavyokwenda hapo Madrid ni wazi kwamba Casillas atakuwa hana chake hivyo huu ni wakati wa kufikiria kwenda kuanza kwingine. Casillas kwasasa ana mkataba na Madrid ambao unamalizika mwaka 2017.

SINA UHAKIKA WA KIKOSI CHA KWANZA - TERRY.

NAHODHA wa klabu ya Chelsea, John Terry amesisitiza kuwa hajahakikishiwa nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo na Jose Mourinho msimu huu. Terry alijikuta mara kwa mara akikosa namba katika kikosi cha Chelsea kilichokuwa kikinolewa na Rafael Benitez kutokana na kuandamwa na majeruhi ya mara kwa mara msimu uliopita. Lakini Mourinho amempa nafasi beki huyo mkongwe kucheza dakika zote 90 katika mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu nchini Uingereza lakini Terry mwenyewe anajua kuwa bado ana kazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha anapata nafasi ya kidumu kwenye kikosi cha kwanza. Terry amesema hata kama ukiwa nahodha haimaanishi kuwa ndio utakuwa na nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza na Mourinho mwenyewe aliweka wazi toka siku ya kwanza aliyotua Stamford Bridge kwa mara ya pili. Chelsea inatarajiwa kuchuana na Manchester United Jumatatu usiku, klabu ambazo zinapewa nafasi ya kuchuana katika kugombea taji la ligi la nchi hiyo msimu huu.

WACHEZAJI WATATU WA MALAWI WAFARIKI KWA AJALI.

SOKA nchini Malawi limekumbwa na simanzi kubwa baada ya wachezaji watatu wa timu ya Mafco kufariki katika ajali ya gari iliyotokea Ijumaa asubuhi katika mji wa Nkhotakota. Wachezaji hao Sadani Magwere, Gift Mphonde na Chifundo Phiri walifariki katika eneo la tukio baada ya gari la jeshi walilokuwa wakisafiria kutoka katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Carlsberg kupata ajali. Polisi walithibitisha kuwa wachezaji wengine watatu Sailesi Phiri, Jimmy Mzunga na Gift Soko wamelazwa hospitalini wakiuguza majeraha ya ajali hiyo. Katika taarifa yake Mwenyekiti wa Mafco, Chitumbo Charamba aliwaambia wanahabari kuwa mwili wa Phiri unatarajiwa kuzikwa wilaya ya Kasungu wakati wengine wawili wao wazikwa katika mji mkuu wa zamani wa Zomba leo.

MADRID KUFANYA ZIARA ALGERIA MWAKANI.

KLABU ya Real Madrid ya Hispania, imethibitisha kufanya ziara nchini Algeria mwakani ambapo watacheza mechi ya kirafiki na mojawapo ya vilabu vya huko. Awali ziara ya Madrid chini humo ilitakiwa kufanyika mwishoni mwa msimu huu lakini ilishindakana kwasababu ya kuingiliana na mwezi mtukufu wa Ramadan hivyo baadhi ya maandalizi ya mwiho kushindwa kukamilika. Kwa mujibu wa waratibu wa ziara hiyo kampuni za Mobilis na Mediapro za huko, mkataba wa makubaliano tayari umesainiwa na tarehe kwa ajili ya tukio hilo inatarajiwa kutajwa wakati wowote. Waratibu hao wamesema klabu ambayo itacheza na Madrid wakati wa ziara hiyo nchini Algeria itachaguliwa na mashabiki watakaopiga kura katika mtandao.

Friday, August 23, 2013

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

VPL KUANZA KUTIMUA VUMBI JUMAMOSI
Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu wa 2013/2014 inaanza kutimua vumbi kesho (Agosti 24 mwaka huu) katika viwanja saba tofauti huku mabingwa watetezi Yanga wakianza kutetea ubingwa wao kwa kuikaribisha Ashanti United kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Azam ya Dar es Salaam na wenyeji Mtibwa Sugar. Oljoro JKT itaikaribisha Coastal Union kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha. Mgambo Shooting itaoneshana kazi na JKT Ruvu ambayo hivi sasa iko chini ya Kocha Mbwana Makata. Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga wakati Rhino Rangers itakwaruzana na Simba katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora. Mbeya City iliyopanda VPL msimu huu itapimana ubavu na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya huku Ruvu Shooting ikiialika Mabatini, Mlandizi timu ya Tanzania Prisons kutoka Mbeya. Mzunguko wa pili wa ligi hiyo utachezwa Agosti 28 mwaka huu. Baada ya hapo ligi itasimama kupitisha mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Gambia na Tanzania (Taifa Stars) itakayochezwa Septemba 7 mwaka huu jijini Banjul. VPL itaingia mzunguko wa tatu Septemba 14 mwaka huu.



TIKETI ZA ELEKTRONIKI KUANZA MZUNGUKO WA NNE
Tiketi za elektroniki zitaanza kutumika katika mzunguko wa nne wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) utakaoanza Septemba 18 mwaka huu. Tayari benki ya CRDB ambayo ndiyo ilishinda tenda hiyo imeshakamilisha ufungaji wa vifaa kwa ajili ya matumizi ya tiketi hizo katika viwanja vyote. Hivi sasa Serikali ambayo ndiyo inamiliki Uwanja wa Taifa, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) pamoja na CRDB zinashughulikia mfumo wa tiketi hizo kwenye uwanja huo ambao ndiyo ulikuwa haujakamilika kwa matumizi katika upande huo. Mfumo (system) iliyoko kwenye uwanja huo inapishana na ule utakaotumiwa na CRDB, hivyo pande husika zinashughulikia suala hilo ili mifumo hiyo iweze kuingilia. Pia mashine za kuchapia (printer) kwa ajili ya tiketi ambazo CRDB wameziagiza kutoka nje ya nchi zinatarajiwa kuwasili mwishoni mwa mwezi huu. Hivi sasa CRDB inashughulikia ufungaji wa vifaa vya matumizi ya tiketi za elektroniki iwemo turnstiles kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi ambao mwanzoni hakuwemo kwenye mpango huo kutokana na Mkoa wa Tabora kutokuwa na timu ya Ligi Kuu.

MADRID YAMTENGEA BALE JEZI NAMBA 11.

KWA mujibu wa vyombo vya habari nchini Hispania, klabu ya Real Madrid imeweka fulana zenye jina la winga mahiri wa kimataifa wa Wales Gareth Bale sokoni baada ya mazungumzo ya uhamisho utakaoweka rekodi ya dunia na Tottenham Hotspurs kufikia mahali pazuri. Mazungumzo kati ya Madrid na Spurs kuhusiana na na suala la Bale yanaonekana kufikia sehemu nzuri lakini nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 bado hajaondoka kwenda Bernabeu kukamilisha mazungumzo binafsi. Gazeti moja la michezo jijini Madrid lilichapisha picha katika mtandao wake unaoonyesha fulana ya Bale iliyopewa namba 11 ikiwa katika duka la vifaa vya michezo vya klabu hiyo kongwe nchini humo. Usajili wa mchezaji huyo ambaye amekuwa roho ya Spurs msimu uliopita umezua gumzo kubwa barani Ulaya kwasababu ya kutaka kuvunja rekodi ya usajili ya paundi milioni 80 iliyokuwa ikishikiliwa na Cristiano Ronaldo wakati alipohamia Madrid akitokea Manchester United mwaka 2009.

BARCELONA YAMNASA SUAREZ.

KLABU ya Barcelona ya Hispania imetangaza kumnasa kinda Denis Suarez kutoka klabu ya Manchester City kwa ada ambayo haikuwekwa wazi. Mchezaji huyo mwenye miaka 19 alikuwa akitabiriwa kurejea Hispania kwa kipindi kirefu na sasa amesaini mkataba wa miaka na Barcelona ambapo ataanzia katika kikosi B cha timu hiyo. Suarez ambaye ni mchezaji wa nafasi ya kiungo aliibukia katika shule ya Celta Vigo lakini aliondoka na kutimkia City katika kipindi cha usajili wa majira ya kiangazi mwaka 2011. Hata hivyo alishindwa kuitwa katika kikosi cha kwanza cha City pamoja na kuteuliwa kuwa mchezaji bora anayechipukia mwaka 2012 hivyo kuamua kujaribu kwingine.

WENGER AJIPANGA KUMSAJILI TENA FLAMINI.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger anajipanga kufanya usajili wake mkubwa katika kipindi hiki cha usajili kwa kumrudisha kiungo wake wa zamani Mathieu Flamini. Flamini mwenye umri wa miaka 29 amekuwa akifanya mazoezi na Arsenal katika kipindi cha wiki mbili baada ya klabu yake ya AC Milan kushindwa kumuongeza mkataba mwishoni mwa msimu uliopita. Flamini aliondoka Arsenal na kujiunga na Milan miaka mitano iliyopita kama mchezaji huru lakini anaonekana kutaka kurejea katika klabu yake hiyo ya zamani kama mchezaji huru tena. Kwa mujibu wa mtandao wa Daily Mail wa Uingereza, Wenger ameonyeshwa kuridhishwa na juhudi za Flamini katika mazoezi na kufikiria kumpa mkataba ili kujaribu kuimarisha kikosi chake ambacho kimekuwa kikisumbuliwa na majeruhi katika siku za karibuni. Viungo wa klabu hiyo Mikel Arteta, Abou Diaby na Alex Oxlade-Chamberlain wote ni majeruhi hivyo kumfanya Wenger kukiri kuwa anahitaji kusajili mchezaji wa kiungo ili kujaribu kuziba nafasi hiyo katika kipindi hiki.
0000

Thursday, August 22, 2013

58 WAJITOSA UCHAGUZI TFF, BODI YA LIGI.

JUMLA ya wanamichezo 58 wamerusha fomu kuomba kuteuliwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na ule wa Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board) utakaofanyika Oktoba mwaka huu. Kwa upande wa TFF waliorejesha fomu kwa upande wa urais ni Athuman Jumanne Nyamlani,Jamal Emil Malinzi, Omari Mussa Nkwarulo na Richard Rukambura. Nafasi ya Makamu wa Rais wamejitokeza Imani Omari Madega, Nasib Ramadhan na Walace Karia. Walioomba nafasi za ujumbe kuwakilisha kanda mbalimbali ni Abdallah Hussein Mussa, Kaliro Samson, Jumbe Odessa Magati, Mugisha Mujwahuzi Galibona, Vedastus Kalwizira Lufano, Samwel Nyalla, Epaphra Amana Swai, Mbasha Matutu Mong’ateko, Stanslaus Haroon Nyongo, Ally Mtumwa, Elley Simon Mbise na Omari Walii. Ahmed Msafiri Mgoyi, Yusuf Hamisi Kitumbo, Ayoub Nyaulingo, Blassy Kiondo, Nazarius Kilungeja, Ayoub Shaib Nyenzi, Cyprian Charles Kuyava, David Lugenge, Elias Mwanjala, Eliud Peter Mvela, John Mwachendang’ombe Kiteve, James Patrick Mhagama, Kamwanga Rajabu Tambwe na Stanley William Lugenge. Athuman Kambi, Francis Kumba Ndulane, Zafarani Damoder, Charles Komba, Hussein Mwamba, Stewart Ernest Masima, Farid Salum Nahdi, Geoffrey Nyange, Riziki Majala, Twahil Twaha Njoki, Davis Elisa Mosha na Khalid Abdallah Mohamed. Wengine ni Alex Chrispine Kamuzelya, Juma Abbas Pinto, Muhsin Balhabou, Omar Isack Abdulkadir, Shaffih Dauda Kajuna na Wilfred Mzigama Kidao. Kwa upande wa uchaguzi wa TFF mwombaji ambaye hakurudisha fomu ni Venance Mwamoto pekee. Kwa upande wa TPL Board waliojitokeza kuwania uongozi wa juu ni wawili tu; Hamad Yahya Juma (Mwenyekiti) na Said Muhamad Said (Makamu Mwenyekiti). Walioomba nafasi za ujumbe wa TPL Board ni Kazimoto Miraji Muzo, Michael Njunwensi Kaijage, Omari Khatibu Mwindadi, Salum Seif Rupia na Silas Masui Magunguma.

KOCHA WA DINAMO ZAGREB ATIMULIWA BAADA YA KIPIGO.

RAIS wa klabu ya Dinamo Zagreb ya Croatia, Zdravko Mamic ametangaza kumtimua kocha wake Krunoslav Jurcic baada ya kipigo cha mabao 2-0 iliyopata timu hiyo kutoka kwa Vienna ya Austria katika mechi ya mkondo wa kwanza hatua ya mtoano ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Jurcic aliiongoza Zagreb kuweka rekodi ya kushinda taji la nne mfululizo la Ligi Kuu ya nchi hiyo April mwaka huu huku wakiongoza msimamo wa ligi hiyo baada ya kucheza mechi sita lakini amejikuta akitimuliwa baada ya kipigo hicho walichopata jana usiku. Katika taarifa yake iliyotumwa katika mtandao wa klabu hiyo, Mamic alimshukuru kocha huyo kwa alichokifanya katika kipindi cha miaka mitatu waliyokuwa nayo lakini ameamua kumuachia aondoke kwasababu ya kipigo walichopata kutoka kwa Vienna. Taarifa hiyo iliongeza kuwa msaidizi wa kocha huyo Damir Krznar ndiye atashika nafasi hiyo kwa muda mpaka hapo watakapopata mbadala mwingine katika siku chache zijazo.

VALCKE AZIWEKEA NGUMU NCHI ZITAKAZOOMBA UENYEJI WA KOMBE LA DUNIA.

KATIBU mkuu wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Jerome Valcke amedai kuwa nchi zitakazoomba kuandaa michuano ya Kombe la Dunia miaka ijayo zitatakiwa kwanza zipate kibali kutoka katika mabunge yao. Kauli hiyo ya Valcke imekuja kufuatia misuguano iliyojitokeza kati ya FIFA na serikali ya Brazil kuhusiana na maandalizi ya michuano hiyo mwakani. Valcke amesema wanatakiwa kujifunza kitu fulani kutokana na matatizo waliyopata nchini Brazil ndio maana ameona kuna haja ya nchi kupata ridhaa ya mabunge yao kwanza kabla ya kutafuta nafasi ya kuwa wenyeji wa michuano hiyo. Serikali ya Brazil na FIFA zimejikuta katika msuguano katika mambo kadhaa ikiwemo suala la kuuza pombe viwanjani kitu ambacho kilifungiwa nchini humo lakini imebidi waruhusu kwasababu mojawapo ya wadhamini wa FIFA ni kampuni za pombe.

FIFA YAPATA MAOMBI ZAIDI MILIONI 2.3 YA TIKETI KATIKA SAA 24 ZA KWANZA TOKA ZIINGIE SOKONI.

SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA limedai kuwa zaidi tiketi milioni 2.3 zimeombwa na mashabiki kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia 2014 katika saa 24 za kwanza toka ziwekwe sokoni katika mtandao. Katika taarifa iliyotumwa katika mtandao wake FIFA imesema toka tiketi hizo ziingie sokoni kwa mara ya kwanza zaidi ya mashabiki 400,000 wametuma maombi ya zaidi ya tiketi milioni 2.3. FIFA imesema maombi mengi ya tiketi hizo yametoka katika nchi za Brazil ambao ndio wenyeji wa michuano hiyo, Argentina, Marekani, Chile na Colombia. Kuna maombi ya tiketi zaidi ya 372,000 kwa ajili ya mechi ya ufunguzi itakayofanyika jijini Sao Paulo Juni 12 na zaidi ya maombi 344,000 kwa tiketi za mchezo wa fainali utakaofanyika katika Uwanja wa Maracana jijini Rio de Janeiro Julai 13 mwakani. Tiketi hizo zilianza kuingia sokoni Jumanne na mashabiki watatakiwa kutuma maombi yao mpaka kufikia Octoba 10 mwaka huu.