Friday, February 28, 2014

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

MALINZI AUNDA KAMATI YA MIAKA 50 FIFA
RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameunda kamati ya watu tisa kuratibu maadhimisho ya miaka 50 tangu TFF ilipojiunga na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA). TFF ilipata uanachama wa shirikisho hilo la kimataifa Oktoba 8, 1964 ambapo itaadhimisha miaka hiyo 50 kwa kufanya shughuli mbalimbali za mpira wa miguu. Kamati hiyo itaongozwa na Mhariri Mtendaji wa kampuni ya magazeti ya Serikali, Gabriel Nderumaki wakati Katibu atakuwa Lina Kessy ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake (TWFA). Wajumbe ni Ahmed Mgoyi, Hoyce Temu, Teddy Mapunda, Ruge Mutahaba, Richard Kasesela, Boniface Wambura na Meneja Biashara wa TFF anayetarajiwa kuajiriwa hivi karibuni. Kamati itafanya kikao chake cha kwanza Jumatatu (Machi 3 mwaka huu) kwenye hoteli ya Courtyard iliyopo Upanda Seaview saa 7 mchana.



KILA LA KHERI YANGA MECHI YA LIGI YA MABINGWA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaitakia kila la kheri yake kwenye mechi yake ya kwanza ya raundi ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly kutoka Misri. Mechi hiyo inachezwa kesho (Machi 1 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia 10 kamili jioni. Timu hizo zitarudiana Machi 9 mwaka huu jijini Cairo, Misri. Maandalizi ya mechi hiyo yamekamilika ambapo kamishna Abbas Sendyowa kutoka Uganda na waamuzi wanne kutoka Burundi tayari wapo nchini kwa ajili ya mechi hiyo inayotarajiwa kuvuta maelfu ya washabiki. Milango yote katika uwanja huo itakuwa wazi, ukiwemo ule wa upande wa Uwanja wa Ndani (Indoor Stadium) wakati Barabara ya Taifa (Taifa Road) itafungwa kuanzia chuo cha DUCE hadi msikitini kuanzia saa 4 asubuhi. Magari maalumu yenye sticker pekee ndiyo yatakayoruhusiwa kuingia uwanjani. Vilevile washabiki wanakumbushwa kuwa hawaruhusiwi kuingia uwanjani wakiwa na silaha au vifaa vyovyote vya chuma.



MAREKEBISHO YA MECHI VPL, FDL
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imefanya marekebisho madogo ya ratiba kwa mechi mbili za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na moja ya Ligi Daraja la Kwanza (VPL). Mechi namba 143 kati ya Tanzania Prisons na Simba iliyokuwa ichezwe Machi 8 mwaka huu sasa imesogezwa kwa siku moja hadi Machi 9 mwaka huu, kwa vile Machi 8 mwaka huu Mbeya City itautumia uwanja huo kwa mechi nyingine ya VPL. Nayo Mgambo Shooting iliyokuwa icheze na Kagera Sugar, Aprili 12 mwaka huu Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga sasa imesogezwa hadi Aprili 13 mwaka huu kwa vile Kituo cha Tanga kitakuwa na mechi mbili. Kwa upande wa FDL, mechi ya Mkamba Rangers na Kimondo SC sasa itachezwa Machi 3 mwaka huu badala ya Machi 9 mwaka huu mjini Ifakara. Mechi hiyo imerudishwa nyuma ili kuipunguzia gharama Kimondo SC kwani Machi 1 mwaka huu itacheza na Burkina Faso mjini Morogoro.


MAKALA: DROGBA KUTOA KITABU CHA VIKARAGOSI.

MSHAMBULIAJI nyota wa Ivory Coast alianza kutembea wakati ana miezi sita, akaondoka nyumbani akiwa na umri wa miaka mitano na kutumbukia katika dimbwi la mapenzi kwa mwanamke aliyekuja kuwa mke wake katika umri wa miaka 17.

Hizo ni baadhi ya dondoo za matukio ya maisha ya nyota huyo ambayo yatachapishwa rasmi katika mfumo wa vikaragosi nchini Ufaransa.

Pia kutakuwa na matoleo ya Uingereza ambapo Drogba bado anakubalika na mashabiki wa klabu yake ya zamani ya Chelsea, Brazil ambapo atakwenda kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia baadae mwaka huu na Uturuki ambapo sasa anacheza katika klabu ya Galatasaray.

Matukio hayo yatakuwa yakifuatilia safari ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 35 kutoka alipoanzia jijini Abidjan mpaka mafanikio aliyopata katika soka duniani.

Drogba alizaliwa Machi 11 mwaka 1978 ambapo alienda nchini Ufaransa akiwa na umri wa miaka mitano kuishi na mjomba wake Michel Goba ambaye naye alikuwa mcheza soka ambapo wazazi wake waliamini kuwa hatua itampa nafasi ya kuwa na maisha bora.

Ni mara chache nyota huyo amekuwa akizungumzia maisha magumu aliyopitia akiwa mdogo, muda mrefu aliotengana na wazazi wake na maisha ya kuzunguka kutokana na mjomba wake kubadilisha timu kila mara.

Wazazi wake waliungana naye Ufaransa wakati akiwa na miaka 13 na wakaweka makazi yao jijini Paris ambapo Drogba ndipo alipoanza safari yake ya soka katika timu ya Levallois SC.

Akihojiwa kuhusiana na kitabu hicho Drogba amesema kitakuwa na maelezo mengi juu ya mambo aliyopitia ili kuwaonyesha watoto kuwa wakipita mahali alipopita basi wanaweza kufanikisha malengo yao.

Sehemu ya mauzo ya kitabu hicho yatakwenda katika mfuko wa hisani uitwao Didier Drogba ambao husaidia mipango ya Afya na Elimu barani Afrika.

MAPUMZIKO YAMEMUWEKA FITI OZIL - WENGER.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger anaamini mapumziko aliyompa Mesut Ozil yatamsaidia kumrejesha katika kiwango chake na ana uhakika anaweza kuhimili msukumo anaopewa katika timu hiyo. Nyota huyo wa zamani wa Real Madrid alipumzishwa katika mchezo wa ligi dhidi ya Sunderland wiki iliyopita baada ya kukosa penati katika mchezo dhidi ya Bayern Munich kwenye Ligi ya Mabingwa barani Ulaya. Akihojiwa Wenger amesema huwa hampi msukumo wowote mchezaji huyo kama watu wanavyodai kwasababu huwa anaamini ushindi wa timu unatoka kwa ushirikiano wa wachezaji wote na sio mmoja. Wenger kikubwa anachopenda yeye ni wachezaji wake kufurahia mchezo na kucheza vyema kwa kuelelewana hivyo hana shaka na Ozil kwasababu anapitia kipindi kigumu na kila mtu hupitia huko.

NASRI, ABIDAL WAACHWA UFARANSA.

BEKI wa kati Eric Abidal na kiungo Samir Nasri wameachwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa wakati kocha Didier Deschamp alipotaja majina ya wachezaji 24 watakaoiwakilisha nchi hiyo katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Uholanzi utakaochezwa wiki ijayo. Mshambuliaji Antoine Griezmann ni mmoja ya wachezaji walioitwa kwa mara ya kwanza katika kikosi hicho sambamba na beki wa kushoto Lucas Digne ambaye anaziba nafasi ya Gael Clichy wa Manchester City. Griezmann mwenye umri wa miaka 22 anayekipiga Real Sociedad ya Hispania amefunga mabao 19 katika mechi 38 alizochezea timu yake msimu huu. Akihojiwa kama wachezaji hao wameshapoteza namba zao katika kikosi chake Deschamp amesema asingependa kuzungumzia suala hilo lakini anachojua yeye mchezaji muhimu ndio atakayekuwepo katika kikosi chake kitakachokwenda Brazil.

EUROPA LEAGUE YAFIKIA PATAMU.

KLABU za Sevilla na Real Betis zote za Hispania zinatarajiwa kukutana katika hatua ya timu 16 bora katika michuano ya Europa League baada ya kufanikiwa kusonga mbele jana. Baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 katika mechi ya kwanza dhidi ya NK Maribor, Sevilla walihakikisha wanatumia vyema uwanja wao wa nyumbani katika mchezo wa pili na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 hivyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao 4-3. Betis wao walisonga mbele baada ya kuigandamiza Rubin Kazan ya Urusi kwa mabao 2-0 hivyo kuwafanya kusinga mbele kwa jumla ya mabao 3-1 kutokana na sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kwanza. Kocha wa Napoli Rafael Benitez ambaye alishinda taji hilo akiwa na Chelsea msimu uliopita naye alifanikiwa kusonga mbele baada ya kuiengua Swansea City na ataendelea kutetea taji hilo dhidi ya Porto ambao waliwatoa Wajerumani Eitracht Frankfurt. Tottenham Hotspurs ya Uingereza wao watakwaanza na Benfica ya Ureno katika mzunguko unaofuata huku mabingwa wa Italia Juventus wao wakikwaana na wenzao Fiorentina.

MAYWEATHER AMENIOGOPA - KHAN.

BINGWA wa zamani wa dunia wa ngumi kutoka Uingereza, Amir Khan amemtuhumu Floyd Mayweather kwa kuchukua chagua rahisi baada ya bondia huyo kukubali kupigana na Marcos Maidana Mei 3 mwaka huu. Khan alishinda kura za katika mtandao baada ya Mayweather mwenye umri wa miaka 36 kuwataka mashabiki wake kuamua bondia wa kupigana naye lakini Mmarekani huyo aliamua kumchagua Maidana raia wa Argentina ambaye ni bingwa wa WBA. Akihojiwa Khan mwenye umri wa miaka 27 amesema anadhani Mayweather amechagua njia rahisi ya kutetea taji lake. Khan amesema ni jambo lililomhuzunisha kwasababu alifuta pambano lake na Devon Alexander lililokuwa lichezwe Desemba mwaka jana kwasababu alikuwa akijua atapigana na Mayweather kwa asilimia 100. Bondia huyo aliendelea kulalama kuwa tayari alishapeleka mkataba na ukasainiwa juu ya pambano lake hivyo akadhani wanaweza kutangaza pambano hilo Desemba, Januari au Februari lakini matokeo yake Mayweather akataka mashabiki kuamua kwa kura. Jambo la kushangaza Khan alishinda katika kura hizo kwa asilimia 57 lakini Mayweather akaamua kupigana na Maidana aliyepata kura chache.

Thursday, February 27, 2014

BOWE AWAOMBA RADHI MASHABIKI WA LIVERPOOL KWA KAULI YAKE...

BINGWA wa zamani wa masumbwi wa uzito wa juu duniani, Riddick Bowe amewaomba radhi mashabiki wa Liverpool baada ya kuandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kuwa angependa mashabiki wote wa Liverpool wafe. Bowe raia wa Marekani mwenye umri wa miaka 46, alisukumwa kutuma ujumbe huo baada ya kusumbuliwa na watu wakimtaka kufafanua kwanini ameamua kuwa mshabiki wa Everton. 
Ujumbe huo ulizusha hasira kali kutoka kwa mashabiki wa Liverpool huku wale wa Everton wakimshauri kuwaomba radhi mahasimu wao hao. Bowe aliamua kuandika ujumbe mwingine wa kuomba radhi akidai kuwa amefanya hivyo baada ya kushauri na mashabiki wenzake wa Everton kwakuwa wao ni kitu kimoja.

BENCHI LAMDATISHA XAVI.

KIUNGO mahiri wa klabu ya Barcelona, Xavi Hernandez ameonyesha kuchanganyikiwa kwa kupunguziwa muda wa kucheza chini ya kocha mpya Gerardo Martino msimu huu lakini amesisitiza kuwa hatasababisha matatizo yoyote kutokana na mabadiliko hayo. Xavi mwenye umri wa miaka 34 alicheza dakika zote tisini katika mechi tisa kati ya 25 za ligi alizocheza msimu huu huku akishindwa kuchomoza katika kikosi cha kwanza, amekiri kuwa sio rahisi kupambana na hali hiyo mpya. Akihojiwa nyota huyo amesema ni jambo linalomchanganya wakati anapokosa muda wa kucheza lakini siku zote anaheshimu maamuzi ya kocha ambaye ndo mwenye uamuzi wa mwisho. Xavi aliendelea kusema kuwa katika kikosi cha Barcelona wachezaji wote wanajua hakuna aliyekuwa juu ya kocha.

OZIL FITI KUIKABILI STOKE CITY.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amebainisha kuwa Mesut Ozil anatarajia kurejea katika kikosi cha timu hiyo wakati watakapoifuata Stoke City katika mchezo wa Ligi Kuu utakaochezwa Jumamosi. Nyota huyo wa kimataifa wa Ujerumani aliachwa katika kikosi kilichoshinda mabao 4-1 dhidi ya Sunderland kufuatia kiwango kibovu alichocheza katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich ambao ulishuhudia akikosa penati dakika za mwanzoni. Wenger alipuuza taarifa kuwa alimuacha Ozil kutokana na kushuka kiwango na kusisitiza kuwa alimuacha kiungo huyo apumzike kutokana na mchezo mgumu dhidi ya Bayern na sasa mchezaji huyo sambamba na Thomas Vermaelen watarejea kwenye mchezo dhidi ya Stoke. Kocha huyo amesema mchezo dhidi ya Bayern ulikuwa mgumu hivyo ni muhimu kumpa mchezaji mapumziko haswa anapokuwa katika shinikizo.

TFF, POULSEN WAKUBALIANA KUVUNJA MKATABA.

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen wamekubaliana kuvunja mkataba katika makubaliano ambayo ni siri kwa pande zote mbili. Uamuzi huo umetangazwa leo (Februari 27 mwaka huu) jijini Dar es Salaam kwa pamoja na Rais wa TFF, Jamal Malinzi na Kocha Poulsen mbele ya waandishi wa habari. Rais Malinzi kwa niaba ya TFF ametoa shukrani za dhati kwa Kocha Poulsen kwa ushirikiano na mchango ambao ameutoa kwa Tanzania kuanzia kwenye mpira wa miguu wa vijana. Naye Kim amewashukuru Watanzania kwa ushirikiano waliompatia kwa kipindi cha miaka mitatu alichokaa nchini kuanzia Mei 2011 alipoteuliwa kuwa kocha wa timu za Taifa za vijana, na baadaye Taifa Stars. Akizungumzia benchi jipya la ufundi la Taifa Stars, Rais Malinzi amesema linatarajiwa kutangazwa hivi karibuni likiongozwa na kocha kutoka nje ya Tanzania. Amesema kwa upande wa mechi dhidi ya Namibia itakayochezwa Machi 5 mwaka huu jijini Windhoek, Stars itaongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi, Salum Madadi akisaidiwa na kocha Hafidh Badru kutoka Zanzibar. Katika hatua nyingine, Kocha Madadi amewaondoa wachezaji watano wa Yanga katika kikosi kilichotajwa awali ili wapate fursa ya kuitumikia timu yao kwenye mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al-Ahly ya Misri. Wachezaji hao ni Athuman Idd, David Luhende, Deogratius Munishi, Frank Domayo, Kelvin Yondani na Mrisho Ngasa. Pia kipa Ivo Mapunda ameondolewa katika kikosi hicho baada ya kupata msiba. Nafasi zao zimezibwa na wachezaji Abdi Banda (Coastal Union), Himid Mao (Azam), Juma Luizio (Mtibwa Sugar), Said Moradi (Azam) na Shabani Kado (Coastal Union). Taifa Stars itaingia kambini keshokutwa (Machi 1 mwaka huu) jioni kwenye hoteli ya Accomondia jijini Dar es Salaam, na itaondoka Machi 3 mwaka huu alfajiri kwa ndege ya South African Airways na kurejea nchini Machi 7 mwaka huu saa 8.15 mchana.



TWIGA STARS IMEWIVA, SHEPOLOPOLO YATUA
Wakati Zambia (Shepolopolo) imewasili leo mchana (Februari 27 mwaka huu), Twiga Stars imesema mazoezi yamewaingia barabara tayari kwa mechi dhidi ya Wazambia hao itakayochezwa kesho (Februari 28 mwaka huu). Mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya kwanza ya michuano ya Afrika kwa Wanawake (AWC) itafanyika Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi kuanzia saa 10 kamili jioni, na hakutakuwa na kiingilio. Wakizungumzia mechi hiyo, Kocha wa Twiga Stars, Rogasian Kaijage na nahodha wa timu hiyo Sophia Mwasikili wamesema kikosi chao kimewiva kwa ajili ya mpambano huo baada ya kufanyia kazi upungufu uliojitokeza katika mechi ya kwanza. Twiga Stars ilipoteza mechi ya kwanza iliyochezwa Februari 14 mwaka huu jijini Lusaka kwa mabao 2-1, na inahitaji ushindi ili iweze kusonga mbele kwenye michuano hiyo ambayo fainali zake zitafanyika Oktoba mwaka huu nchini Namibia. Iwapo Twiga Stars itafanikiwa kuitoa Zambia katika mechi hiyo itakayooneshwa moja kwa moja na Azam Tv itacheza raundi ya mwisho na Zimbabwe. Msafara wa Shepolopolo una watu 26 ambapo wachezaji ni Anita Mulenga, Annie Kibanji, Carol Howes, Debora Chisanga, Emelda Musonda, Esther Mukwasa, Grace Zulu, Hazel Nali, Hellen Mubanga, Lweendo Chisamu, Meya Banda, Mirriam Katamanda, Misozi Zulu, Mupopo Kabange, Noria Sosala, Rachel Lungu na Susan Banda.





Viongozi ni Maclean Daka, Charles Bwale, Kaluba Kangwa, Enala Phiri, Cornelia Chazura, James Nyimbili, Besa Chibwe, Dorothy Sampan a Kabungo Katongo.

WAAMUZI WA ITALIA NDIO BORA DUNIANI - CONTE.

MENEJA wa klabu ya Juventus ya Italia, Antonio Conte anafikiri waamuzi wa soka wa Italia ndio bora duniani na wanastahili kuheshimiwa. Kauli ya kocha huyo mwenye umri wa miaka 44 inakinzana na ile aliyotoa msimu uliopita wakati alipomshukia mwamuzi Marco Guida aliyechezesha mchezo kati ya Juventus na Genoa ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1. Hata hivyo, Conte amesisitiza kuwa amebadili mtazamo wake juu ya waamuzi wan chi hiyo. Akihojiwa Conte amesema hakupenda kilichotokea mwaka jana wakati alipotoa maneno makali kwa mwamuzi katika mchezo huo kwasababu kwa mawazo yake alidhani walistahili penati katika dakika za majeruhi lakini hawakupewa. Conte amesema alifanya makosa kufanya alivyofanya na tayari ameomba msamaha na kubadilisha mtazamo wake juu ya waamuzi kwani anadhani wanapaswa kuheshimiwa kwa kazi kubwa wanayofanya. Juventus inajiandaa na mchezo wake wa mkondo wa pili wa Europa League dhidi ya Trabzonspor utakaochezwa baadae leo huku wakiwa na akiba ya mabao 2-0 waliyopata katika mchezo wa kwanza waliocheza nyumbani.

MURRAY ATINGA ROBO FAINALI ACAPULCO.

MCHEZAJI nyota wa Uingereza, Andy Murray amefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya michuano wazi ya Mexico kwa ushindi wa 6-3 6-4 dhidi ya Joao Sousa waa Ureno katika mchezo uliochezwa jijini Acapulco. Murray ambaye kama akishinda mchezo wake wa robo fainali atakuweza kucheza nusu fainali yake ya kwanza kwa mwaka huu anatarajiw akupambana na Gilles Simon wa Ufaransa. Katika mechi zingine zilizochezwa David Ferrer alifanikiwa kumtandika Mhispania mwenzake Feliciano Lopez kwa 7-6 6-2 huku Grigor Dimitrov akimuondosha Marcos Baghdatis kwa 6-1 6-4. Murray atapambana na Sousa anayeshika nafasi ya 23 huku akiwa na rekodi nzuri ya kushinda mechi 11-1 walipokutana kipindi cha nyuma.

MOURINHO AMZUSHIA BALAA ETO'O KUHUSU UMRI WAKE.

SUALA la umri mkubwa kwa mshambuliaji wa Chelsea, Cameroon Samuel Eto'o limechukua sura mpya baada ya mpenzi wa zamani kujitokeza na kushindilia msumari mwingine. Meneja wa Chelsea Jose Mourinho alikaririwa na moja ya vyombo vya habari vya nchini Ufaransa akisema tatizo la timu yake ni safu ya washambuliaji ambao wamekuwa butu kwakuwa wana umri tofauti na ule unaofahamika. Mourinho alimtolea mfano Eto’o akidai kuwa ana miaka 32 lakini inawezekana ana miaka mitatu zaidi ya hiyo ambayo inatajwa ingawa baadae alipinga kauli yake hiyo na kudai alizungumza kiutani na mtu ambaye hajui mpira huku wakicheka lakini akashangaa kupelekwa kwenye vyombo vya habari. Sasa kama hiyo haitoshi mpenzi wake wa zamani na mama wa mtoto wake wa kwanza Anna Barranca mwenye umri wa miaka 43 amesema ana ushahidi kuwa mshambuliaji huyo ana miaka zaidi ya aliyotaja wakati anaingia barani Ulaya na anadhani hana miaka 35 ana miaka zaidi ya 39. Mwanamama huyo amesema Eto’o amezaliwa mwaka 1974 ambayo inamfanya awe ana miaka 39 kwasasa lakini hati yake ya kusafiria inaonesha kuwa ana miaka 32. Akiulizwa kuhusiana na suala la umri wake Eto’o mwenyewe hakutaka kulizungumzia na kudai kuwa siku zote amekuwa mkweli kwa timu anazocheza na kitu pekee anachotaka ni kuisaidia Chelsea kushinda mataji.

MOYES ATAMBA KUWA WALISTAHILI KUSHINDA.

MENEJA wa klabu ya Galatasaray, Roberto Mancini anafikiri kuwa Chelsea walistahili kufungwa na timu yake katika mchezo wao wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabibgwa barani Ulaya hatua ya timu 16 bora uliochezwa jana. Juhudi za Chelsea kuanza mchezo huo kwa kasi zilizaa matunda baada ya kupata bao la mapema la dakika ya tisa kupitia kwa Fernando Torres lakini Galatasaray walionyesha kutawala mchezo huo kwa kipindi kirefu. Wenyeji Galatasaray walifanikiwa kurudisha bao hilo mapema katika kipindi cha pili kupitia kwa Aurelien Chedjou na kupelekea mchezo huo uliochezwa katika Uwanja wa Turk Telekom Arena kumalizika kwa sare ya bao 1-1. Akihojiwa Mancini amesema hakuridhishwa na matokeo hayo kwasababu anadhani kipindi cha pili walistahili kupata bao lingine zaidi ambao lingewafanya kuibuka na ushindi. Chelsea wanatarajiwa kuikaribisha Galatasaray katika mchezo wa mkondo wa pili utakaochezwa Machi 18 mwaka huu.

FARAH, BOLT, RONALDO, NADAL, VETTEL KUSHINDANIA TUZO YA MWANAMICHEZO BORA WA MWAKA.

MWANARIADHA nyota wa Uingereza Mo Farah ambaye ni bingwa wa mashindano ya dunia katika mbio za mita 5,000 na 10,000 yaliyofanyika jijini Moscow, Urusi mwaka jana, ametajwa katika orodha ya wanamichezo watakaogombea tuzo ya dunia ya mwanamichezo bora wa mwaka. Mbali na Farah wanamichezo wengine waliopo katika orodha hiyo ni pamoja na bingwa wa dunia wa mashindano ya langalanga Sebastian Vettel, nyota wa tenisi Rafael Nadal, mwanasoka Cristiano Ronaldo na nyota wa mpira wa kikapu wa Marekani LeBron James. Mwanariadha nyota wa mbio fupi kutoka Jamaica, Usain Bolt ambaye amewahi kushinda tuzo hiyo mara tatu naye pia ameteuliwa katika orodha hiyo kwa mara nyingine. Sherehe za utoaji wa tuzo zinatarajiwa kufanyika jijini Kuala Lumpur, Malysia Machi 26 mwaka huu.

Wednesday, February 26, 2014

NGULI WA ZAMANI WA BENFICA NA NAHODHA URENO KUFANYIWA MAZISHI YA KITAIFA MSUMBIJI.

MSUMBIJI inatarajia kumfanyia mazishi ya kitaifa mchezaji wa zamani wa Benfica na nahodha wa Ureno Mario Coluna ambaye amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 78. Coluna aliisaidia Benfica kushinda taji la Ulaya mara mbili huku akiiongoza Ureno akiwa nahodha kushika nafasi ya tatu katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1966. Mwishoni mwa maisha ya uchezaji, Coluna alirejea Msumbiji ambako alizaliwa na akaifundisha timu ya taifa ya nchi hiyo kwa muda. Coluna pia aliwahi kuliongoza Shirikisho la Soka la Msumbiji na pia waziri wa michezo wan chi hiyo. Rais wa klabu ya Benfica, Luis Felipe Vieira alituma salamu zake za rambirambi kwa msiba wa nguli huyo. Coluna alizaliwa Msumbiji mwaka 1935 na kuanza kucheza soka jijini Maputo kabla ya kusaini Benfica mwaka 1954 na kuifungia mabao 150 katika mechi 677 alizocheza.

ZLATAN NI MMOJA YA WACHEZAJI WATATU BORA DUNIANI - BECKHAM.


NGULI wa soka David Beckham amemtaja mshambuliaji wa Paris Saint-Germain Zlatan Ibrahimovic kama mmoja ya wachezaji ambao amepata kucheza nao na kumuweka katika orodha ya wachezaji watatu bora duniani. Beckham ambaye ni nahodha wa zamani wa Uingereza alimalizia soka lake PSG msimu uliopita na kukisaidia kikosi hicho kilichokuwa kikinolewa na Carlo Ancelotti wakati huo kunyakuwa taji la Ligi Kuu nchini Ufaransa baada ya kusaini kuitumikia klabu hiyo Januari. Beckham ambaye amecheza na nyota wengine kama Zinedine Zidane na Ronaldo wakati wa enzi zake anaamini Msweden huyo ni mmoja wa wachezaji bora katika soka kwasasa. Akihojiwa Beckham amesema kucheza timu moja Ibrahimovic ilikuwa ni jambo la kipekee kwasababu ni mmoja ya wachezaji wenye vipaji aliopata kuwaona wakati akicheza soka. Ibrahimovic amefunga jumla ya mabao 37 katika mashinano yote msimu huu.

ZAMBIA WATUA KUIKABILI TWIGA STARS

TIMU ya Taifa ya Zambia (Shepolopolo) inatua nchini kesho mchana (Februari 27 mwaka huu) kwa ajili ya mechi ya marudiano ya michuano ya Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Tanzania (Twiga Stars) itakayochezwa keshokutwa (Februari 28 mwaka huu). Shepolopolo yenye msafara wa watu 29 itawasili kwa ndege ya Fastjet ikitokea Lusaka na itafikia kwenye hoteli ya Accomondia kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi kuanzia saa 10 kamili jioni. Waamuzi wa mechi hiyo kutoka Burundi wakiongozwa na Ines Niyosaba wamewasili nchini leo asubuhi wakati Kamishna Fran Hilton-Smith kutoka Afrika Kusini atawasili kesho (Februari 27 mwaka huu) saa 8 kamili mchana kwa ndege ya South African Airways.

SYMBION KUSAIDIA PROGRAMU ZA VIJANA TFF.

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania, TFF na Symbion Power Tanzania Limited zimesaini makubaliano ambapo kampuni hiyo itasaidia kwenye maeneo matatu ya mpira wa miguu wa vijana. Katika taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura imedai kuwa makubaliano hayo yamefikiwa na kutiwa saini leo katika ofisi za shirikisho hilo mbele rais wake Jamal Malinzi na mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo Peter Gathercoles.Maeneo ambayo Symbion itasaidia ni ujenzi wa vituo viwili vya kuendeleza vipaji vitakavyojengwa Kidongo Chekundu na Kinondoni mkoani Dar es Salaam, mashindano ya Taifa ya wachezaji wenye umri wa chini ya miaka 12 yatakayofanyika mwaka huu na kuisaidia timu ya vijana chini ya miaka 17 Serengeti Boys. Kampuni hiyo imetoa jumla ya shilingo milioni 176 kwa ajili ya mashindano ya vijana chini ya umri wa miaka 12 na pia maandalizi ya Serengeti Boys kwa ajili ya mchezo wao wa mchujo kuwania tiketi ya michuano ya Mataifa ya Afrika dhidi ya Afrika Kusini utakaochezwa Julai mwaka huu. Malinzi aliishukuru kampuni hiyo kwa kukubali kushirikiana na TFF katika mpira wa miguu wa vijana, lakini vilevile amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kwani ndiye chachu ya kampuni hiyo kuamua kujishirikisha na mpira wa miguu wa vijana.

CAMPBELL APANIA KUREJEA ARSENAL.


MCHEZAJI chipukizi anayecheza kwa mkopo katika timu ya Olympiakos, Joel Campbell amesisitiza kuwa anataka kuonyesha thamani kwa Arsene Wenger na kupambana ili aweze kurejea katika timu yake ya Arsenal msimu ujao. Kinda huyo wa kimataifa wa Costa Rica alisaini mkataba wa miaka mitatu na Arsenal lakini ametumia muda wake mwingi katika mkataba huo akicheza kwa mkopo huku pia akikosa kibali kitakachomuwezesha kusakata kabumbu Uingereza. Campbell mwenye umri wa miaka 21 ameonyesha kiwango kizuri msimu huu akiwa na Olympiakos huku akifunga moja ya mabao katika ushindi wa mabao 2-0 waliopata dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu Manchester United katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo Campbell amesema Arsenal walipomfuata hakusita kujiunga nao na anaamini hivi sasa tayari ameiva kuichezea klabu hiyo msimu ujao.

CARLOS ATAMANI KUINOA MADRID.

BEKI nguli wa zamani wa klabu ya Real Madrid, Roberto Carlos amekiri kuwa angependa kuinoa klabu hiyo ndani ya miaka kumi ijayo. Nyota huyo wa kimataifa wa Brazil ametumia miaka 11 Santiago Bernabeu akiwa kama mchezaji na kuisaidia timu hiyo kushinda mataji manne ya La Liga na matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Carlos mwenye umri wa miaka 40 kwasasa ni kocha wa timu ya Sivasspor ya Uturuki. Carlos alikaririwa na gazeti la Marca la Hispania akidai kuwa kuinoa Madrid ndani ya kipindi cha miaka 10 ijayo ni moja ya ndoto zake kwa hivi sasa.

MASHABIKI WA CHELSEA WARIPOTIWA KUSHAMBULIWA ISTANBUL.

WAKATI imebaki saa chache kabla ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Galatasaray na Chelsea kumekuwa na ripoti kuwa baadhi ya mashabiki wa timu hiyo ya Uingereza wameshambuliwa jijini Istanbul. Shabiki mmoja ameripotiwa kuchomwa kisu mguuni na mwingine kupigwa karibu na eneo la Taksim Square lililopo katikati ya mji huo ambapo mashabiki wawili wa Leeds United walishambuliwa na kuuawa mwaka 2000 kuelekea katika nusu fainali ya mchezo wa Kombe la UEFA. Taarifa hiyo haikusema kama majeruhi hao walilazwa hospitalini lakini klabu imeshaonywa kuhusiana na tukio hilo. Ofisa wa mambo ya nje alithibitisha kufanyia uchunguzi taarifa hiyo na watachukua hatua stahiki itakapothibitika kutokea kwa tukio hilo.

KESI YA PISTORIUS KUONYESHWA MOJA KWA MOJA KATIKA LUNINGA.

JAJI Dunstan Mlambo wa mahakama ya Pretoria nchini Afrika Kusini anayesikiliza kesi ya mwanariadha mlemavu Oscar Pistorius ameruhusu kesi hiyo kuonyesha moja kwa moja katika luninga pindi itakapoanza kusikilizwa. Pistorius anakabiliwa na kesi ya kumuua kwa kumpiga risasi mpenzi wake ambaye ni mwanamitindo na mtangazaji Reeva Steenkamp zaidi ya mwaka mmoja uliopita. Waendesha mashtaka wanamtuhumu Pistorius kufanya mauaji hayo kwa kukusudia lakini mwenyewe alikana akidai kuwa alifanya mauaji hayo kwa bahati mbaya akidhani kuwa alivamiwa na majambazi. Mwandishi wa BBC Pumza Fihlani amesema hiyo itakuwa mara ya kwanza kwa kesi nchini humo kusikilizwa huku ikirushwa moja kwa moja katika luninga.

TULISTAHILI KUFUNGWA - MOYES.

MENEJA wa klabu ya Manchester United, David Moyes amekiri kikosi chake kucheza kwa kiwango kibovu zaidi msimu huu katika michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Olympiakos. Mabao yaliyofungwa katika kila kipindi na Alejandro Dominguez na Joel Campbell yaliwahakikishia ushindi mabingwa hao wa Ugiriki na kuiacha United katika wakati mgumu wa kufuzu robo fainali ya michuano hiyo. Kikosi cha Moyes kilifanikiwa kupiga shuti moja pekee langoni mwa wapinzani wao kwenye mchezo huo na kocha huyo Mscotland anakiri wachezaji walistahili kufungwa mechi hiyo. Moyes amesema wachezaji wake walicheza kwa kiwango kibovu sana na kitu kizuri pekee ni kwasababu wana mchezo wa pili wa kujiuliza. Michuano hiyo inaendelea tena leo ambapo Chelsea watakuwa wageni wa Galatasaray jijini Istanbul, Uturuki huku Wajerumani Schalke 04 wakiwakaribisha Real Madrid.

Monday, February 24, 2014

MECHI YA TWIGA STARS, ZAMBIA BURE.

MASHABIKI wa mpira wa miguu nchini watashuhudia bure mechi ya timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya wanawake (Twiga Stars) dhidi ya Zambia (Shepolopolo). Mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya kwanza ya michuano ya Afrika kwa Wanawake (AWC) itachezwa Ijumaa (Februari 28 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili alasiri. Twiga Stars ambayo ilipoteza mechi ya kwanza iliyochezwa Lusaka, Februari 14 mwaka huu kwa mabao 2-1 iko kambini chini ya Kocha Rogasian Kaijage na msaidizi wake Nasra Juma ikijiwinda kuwakabili Wazambia wanaotarajiwa kutua nchini Alhamisi (Februari 26 mwaka huu). Waamuzi wa mechi hiyo Ines Niyonsaba, Jacqueline Ndimurukundo, Axelle Shikana na Suavis Iratunga kutoka Burundi kutoka Burundi wanatarajiwa kuwasili nchini keshokutwa (Februari 26 mwaka huu). Kamishna Fran Hilton Smith kutoka Afrika Kusini yeye atatua nchini Februari 27 mwaka huu kwa ndege ya South Africa Airways.



YANGA, SIMBA ZAINGIZA MIL 100/- VPL
Mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zilizohusisha timu za Yanga na Simba, na kuchezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki zimeingiza jumla ya sh. 101,165,000. Yanga ambayo iibugiza Ruvu Shooting mabao 7-0 mechi yake iliingiza sh. 68,450,000 kutokana na washabiki 11,972 kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 15,000 na sh. 20,000. Katika mechi hiyo kila klabu ilipata mgao wa sh. 15,687,488 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa kutokana na mapato hayo ni sh. 10,441,525.42. Gharama za tiketi ni sh. 3,813,600 na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ilipata sh. 4,877,538.71. Uwanja sh. 8,129,231.19. Gharama za mchezo zilikuwa sh. 4,877,538.71 wakati Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,438,769.36. Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) kila kimoja kilipata sh. 945,110. Nayo mechi ya Simba na JKT Ruvu ilishuhudia na watazamaji 5,850 na kuingiza sh. 32,715,00 kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 15,000 na sh. 20,000. Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 4,990,423.73. Kila klabu ilipata mgawo wa sh. 7,428,742 wakati tiketi ni sh. 2,542,400 huku gharama za mechi zikiwa 2,266,395.86. Uwanja ulipata sh. 3,777,326.44 wakati Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ni sh. 2,266,395.86. Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) ulipata mgawo wa sh. 1,133,167.93 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 881,376.17.



RWIZA KUSIMAMIA MECHI YA TP MAZEMBE
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua Alfred Rwiza Kishongole kuwa Kamishna wa mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya TP Mazembe na Asres De Douala ya Cameroon. Mechi hiyo ya hatua ya 16 itafanyika kati ya Machi 7, 8 au 9 mwaka huu jijini Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na kuchezeshwa na waamuzi kutoka Uganda. Mwamuzi wa kati atakuwa Denis Batte wakati wasaidizi wake ni Mark Ssonko, Samuel Kayondo na Mashood Ssali.

WAHUNI WA GALATASARAY NA BESIKTAS WACHAPANA KAVU KAVU MTAANI.

IKIWA imebaki siku chache kabla ya Galatasaray kuikaribisha Chelsea katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya, kumezuka vurugu za kupigana na kurushiana viti kati ya mashabiki wa Galatasaray na mahasimu wao Besiktas katika mitaa ya jiji la Istanbul. Kumekuwa na picha za video katika mtandao wa Youtube ukionyesha makundi makubwa ya wahuni wa Galatasaray na Besiktas wakichapana katika mitaa yenye maduka mengi kabla ya mchezo baina ya timu hizo katika Uwanja wa Turk Telekom. 
Vurugu hizo ziliendelea pia wakati wa mchezo huo ambao Galatasaray ilishinda kwa bao 1-0. Mashabiki wa Chelsea watakaosafiri kwenda jijini Istanbul kwa ajili ya kuishangilia timu yao wameonywa kuwa makini pindi watakapokuwa huko.


MOURINHO AMTAMANI FALCAO KWA UDI NA UVUMBA.

MENEJA wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho amedokeza kuwa anaweza kumsajili mshambuliaji wa Monaco, Radamel Falcao katika usajili wa majira kiangazi. Mourinho ameshindwa kuficha hisia zake za kumtamani nyota huyo ambaye kwasasa yuko benchi akiuguzi goti lake na kuna ripoti kuwa anafikiria kuondoka Ufaransa baada ya kucheza kwa mwaka mmoja kutokana na Ligi Kuu ya nchi hiyo kukosa ushindani. Akihojiwa Mourinho pia aliondoa uwezekano wa kuhitaji huduma ya washambuliaji wa timu ya Paris Saint-Germain Zlatan Ibrahimovic na Edinson Cavani. Mourinho amesema ana timu lakini hana mshambuliaji na Falcao ni kama hana timu kwasababu mchezaji wa kiwango kama chake hastahili kucheza mbeke ya mashabiki 3,000. Mourinho alienda mbali na kudai kuwa Monaco ni klabu ambayo mchezaji anaweza kumalizia soka lake wakati akiwa ameanza kuchuja. Falcao mwenye umri wa miaka 28 alijiunga na Monaco kwa paundi milioni 50 akitokea Atletico Madrid katika majira ya kiangazi mwaka jana.

RAMSEY AACHWA KIKOSI CHA WALES.

TIMU ya taifa ya Wales itamkosa kiungo wake mahiri Aaron Ramsey wakati watakapocheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Iceland Machi 5 mwaka huu. Kiungo huyo wa Arsenal mwenye umri wa miaka 23 bado anajiuguza baada ya kupata majeraha ya msuli Desemba mwaka jana. Wakati Ramsey akishindwa kujumishwa katika kikosi cha nchi hiyo kocha Chris Coleman amemuita winga wa Real Madrid Gareth Bale katika kikosi chake ambacho kitacheza mechi hiyo katika Uwanja wa Cardiff City. Coleman pia amemuita kinda wa Manchester City Emyr Huws ambaye kwasasa anacheza kwa mkopo katika timu ya Birmingham City na kuna uwezekano kinda huyo mwenye miaka 20 akapata nafasi ya kucheza mechi yake ya kwanza katika timu ya wakubwa ya nchi hiyo. Mchezo dhidi ya Iceland utakuwa muhimu kwa Wales kujenga kikosi chake tayari kwa mechi za kufuzu michuano ya Ulaya 2016 ambapo wamepangwa katika kundi B sambamba na Ubelgiji, Bosnia-Hercegovina, Israel, Cyprus na Andora.

PIRLO ASISITIZA KUBAKIA JUVENTUS.

KIUNGO mkongwe Andrea Pirlo amesisitiza kuwa hajafanya mawasiliano yoyote na Real Madrid kuhusu suala la uhamisho katika majira ya kiangazi na amepanga kuendelea kubakia Juventus. Nyota huyo wa kimataifa wa Italia mkataba wake na Juventus unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu na Madrid wanamfuatilia kwa karibu mkongwe huyo. Hata hivyo Pirlo amesema kwasasa akili yake iko vibibi hivyo vya Turin na anategemea kufikia makubaliano juu ya nyongeza ya mkataba wake mapema iwezekanavyo. Pirlo amesema hajawahi kuzungumza na Madrid kuhusu uhamisho lakini amekiri mara kadhaa amekuwa akizungumza na Carlo Ancelotti kuhusu mambo mengine. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 34 amesema anajisikia vyema kuendelea kuwepo Juventus hivyo hana mpango wa kwenda popote kwasasa.

VAN GAAL BADO AITAMANI SPURS.

KWA mara nyingine kocha wa timu ya taifa ya Uholanzi, Louis van Gaal amegusia uwezekano wake wa kuhamia Ligi Kuu nchini Uingereza kuifundisha Tottenham Hotspurs baada ya michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika nchini Brazil. Spurs wamejipanga kuanza mazungumzo mapya na Van Gaal kuhusu kuinoa klabu hiyo baada ya michuano hiyo itakayofanyika baadae mwaka huu. Mkataba wa Van Gaal na Uholanzi unatarajiwa kumalizika baada ya Kombe la Dunia na ameonekana hana mpango wa kuongeza mwingine. Akihojiwa Van Gaal mara baada ya droo ya ratiba ya kufuzu michuano ya Ulaya 2016, amesema hata kuwa kocha wa timu hiyo wakati wakianza kampeni zao na hajui ataelekea wapi baada ya hapo lakini kama akipata changamoto mpya hatasita kuichukua. Van Gaal amesema changamoto mpya atakayochukua ni kufundisha timu ya Ligi Kuu nchini Uingereza na inawezekana ikawa Spurs lakini kwasasa anaangalia safari yao ya Brazil.

NASRI AJISTUKIA KUWA NA GUNDU.

KIUNGO wa klabu ya Manchester City, Samir Nasri ana hofu kuwa wakifungwa katika mchezo wa fainali ya Kombe la Ligi wiki ijayo inaweza kuwaathiri katika kampeni zao wa kuwania taji la Ligi Kuu kama ilivyokuwa kwa Arsenal. Nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa alifika fainali ya michuano hiyo akiwa na Arsenal mwaka 2011 lakini walipata kipigo cha kushtusha kutoka Birmigham ambao walikuwa wanashuka daraja msimu huo. Kipigo hicho kiliichanganya Arsenal na kujikuta wakishinda mechi mbili kati ya 11 walizocheza za Ligi na kuporomoka kutoka nafasi ya pili mpaka ya nne mwishoni mwa msimu wakimaliza kwa tofauti ya alama 18 na mabingwa Manchester United msimu huo. Nasri pia alikuwa sehemu ya kikosi cha City kilichochapwa na Wigan katika mchezo wa fainali ya Kombe la FA msimu uliopita na nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 amepania kuhakikisha timu yake inaibuka kidedea ili yasije kuwakuta yalioikuta Arsenal. Akihojiwa Nasri alikiri kuwa hana kumbukumbu nzuri na vikombe baada ya kupoteza fainali akiwa na Arsenal na pia City msimu uliopita hivyo hataki suala hilo lijirudie tena.

DAVIDS AMVULIA KOFIA CONTE.

MCHEZAJI wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi, Edgar Davids ameeleza jinsi anavyomkubali kocha wa Juventus Antonio Conte na anaamini kuwa angepata wakati mgumu hata kuwepo katika mechi la wachezaji wa akiba kutokana na jinsi mabingwa hao wa Serie A walivyokuwa imara. Davids aliichezea Juventus kati ya mwaka 1997 na 2004 na kufanikiwa kushinda mataji matatu ya Serie A na timu hiyo huku pia akifanikiwa kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya msimu wa 2002-2003. Nguli huyo aliuambia mtandao wa klabu hiyo kuwa kiwango cha timu hiyo kwasasa kiko juu kiasi ambacho angekuwa bado anacheza hadhani kama angeweza kuwemo katika benchi la wachezaji wa akiba. Davids amesema kwasasa Juventus wana kikosi kizuri wakiwemo wachezaji kama Arturo Vidal na Paul Pogba ambao wametoa mchango mkubwa msimu huu. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 40 pia alimpongeza Carlos Tevez kwa kuongeza chachu ya ushindi katika safu ya ushambuliaji akiwa mefunga mabao 14 katika mechi 25 za Serie A alizocheza msimu huu.

NADAL ANYAKUWA TAJI LA RIO OPEN.

NYOTA wa tenisi kutoka Hispania, Rafael Nadal amefanikiwa kumgaragaza Alexandr Dolgopolov wa Ukraine kwa 6-3 7-6 na kunyakuwa taji la michuano ya wazi ya Rio de Janeiro nchini Brazil. Ushindi huo wa Nadal ambaye anashika nafasi ya kwanza katika orodha za ubora duniani umekuja ikiwa zimepita wiki nne baada ya kupoteza taji la michuano ya wazi ya Australia kwa Stanislas Wawrinka. Katika mchezo huo Nadal ambaye aliumia mgongo wakati wa mazoezi katika michuano ya Melbourne hakuonyesha kutetereshwa na mpinzani hivyo kuonyesha dalili kuwa amepona. Hilo linakuwa taji la 43 kwa Nadal katika viwanja vya udongo na pia hajawahi kupoteza mchezo katika viwanja hivyo toka alipochapwa na Novak Djokovic katika michuano ya Monte Carlo Masters miezi 10 iliyopita.

WENGER KUMPA MKATABA MPYA ROSICKY.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amedai kuwa klabu hiyo imefikia makubaliano ya mkataba mpya na Tomas Rosicky. Novemba mwaka jana kulizuka tetesi kuwa kiungo huyo atapewa mkataba mpya kama akifanikiwa kucheza mechi 25 za klabu hiyo msimu huu. Risicky alicheza mechi yake ya 26 wakati Arsenal ikiibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Sunderland JUmamosi iliyopita na Wenger hana kwamba anahitaji kumbakisha nyota huyo mwenye umri wa miaka 33. Akihojiwa Wenger amesema Rosicky atabakia na tayari wameshafanya mazungumzo ambayo yatawekwa wazi mapema iwezekanavyo. Rosicky alirejea katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo na kufunga bao wakati Mesut Ozil alipopumzishwa.

WENYEJI URUSI WAONGOZA KWA MEDALI MICHUANO YA OLIMPIKI YA BARIDI HUKO SOCHI.

MICHUANO ya 22 ya Olimpiki majira ya baridi imemalizika rasmi jana jijini Sochi baada ya siku 17 za mashindano hayo huku wenyeji Urusi wakiibuka kidedea kwa kuongoza kwa kuzoa medali. Zaidi ya wanariadha 2800 kutoka mataifa 88 walishiriki katika mashindano hayo yaliyojumuisha michezo 12 mpya ambapo Urusi walimaliza wakiwa wa kwanza katika jedwali la medali, wakiwa na medali 13 za dhahabu 11 za fedha na 9 za shaba. Norway ilimaliza katika nafasi ya pili baada ya kujizolea medali 11 za dhahabu 5 za fedha na 10 za shaba huku Canada wao wakiwa katika nafasi ya tatu kwa kuwa na medali 10 za dhahabu 10 za fedha na 5 za shaba. Akifunga mashindano hayo katika sherehe zilizochukua takribani dakika 130 rais wa Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa, IOC Thomas Bach aliitaka dunia kuitizama Urusi kwa mtazamo mpya kwani wamezidisha matarajio ya washiriki wengi walioshiriki mashindano hayo ya Sochi. Mara baada ya sherehe hizo wenyeji waliwakabidhi bendera ya olimpiki nchi ya Korea Kusini ambao ndio watakuwa wenyeji wa mashindano hayo 2018 katika mji wa Pyeongchang.

Friday, February 21, 2014

ITACHUKUA MUDA OZIL KUSAHAU PENATI ALIYOKOSA.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amesema kiungo wake Mesut Ozil bado anatafunwa na dhambi ya kukosa penati katika mchezo dhidi ya Bayern Munich. Kiungo aliyevunja rekodi katika usajili wake alipata penati ya mapema katika mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya lakini alikosa kwa kumpigia moja kwa moja kipa wa Bayern Manuel Neuer. Akihojiwa Wenger amesema kwasasa wanamuacha asahau yaliyotokea kwasababu yamepita masaa 48 toka akose penati hivyo ni muda mfupi sana. Wenger amesema ana mifano ya wachezaji waliopitia wakati kama wa Ozil akiwemo Dennis Bergkamp ambaye alikosa penati dhidi ya Manchester United mwaka 1999 katika nusu fainali ya Kombe la FA na hakutaka kupiga penati baada ya hapo lakini leo ana sanamu lake nje ya uwanja wao.

NEUER AMKUNA RAIS WA BAYERN.

RAIS wa klabu ya Bayern Munich, Uli Hoeness ameonyesha kumhusudu Manuel Neuer kutokana na kiwango bora alichoonyesha katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Arsenal katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya uliochezwa Jumatano. Golikipa huyo wa kimataifa wa Ujerumani alifanikiwa kupangua penati iliyopigwa na Mesut Ozil mapema katika mchezo huo pamoja na kuokoa michomo kadhaa kutoka kwa wapinzani wao iliyowezesha kuiweka timu hiyo sawa. Akihojiwa Hoeness amesema golikipa huyo amekuwa katika kiwango chake cha juu kabisa na haoni kama anaweza kuuzika kwa bei yoyote. Mbali ya kuokoa michomo hatari lakini pia Neuer amekuwa mazuri kwa kusaidia wachezaji wenzake kwa pasi zake za ufundi huku akiweza kutumia miguu yake yote miwili kwa ustadi. Neuer hajafungwa mechi 22 kati ya 35 alizocheza na Bayern msimu huu 2013-2014.

ROBBEN KUSAINI MKATABA MPYA UTAKAOMUWEKA ALLIANZ ARENA MPAKA 2017.

WINGA mahiri wa klabu ya Bayern Munich, Arjen Robben amefikia makubaliano juu ya mkataba mpya ambao utamuweka klabuni hapo mpaka 2017. Nyota huyo wa kimataifa wa Uholanzi mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika majira ya kiangazi mwaka 2015 na pande zote mbili zimekuwa katika mazungumzo katika wiki kadhaa. Hivi karibuni Robben alielezea uhakika wake wa kuendelea kubakia Bayern na kubainisha kuwa kilichobaki kufanya sasa ni kukamilisha taratibu za kusaini makaratasi. Robben amesema kuwa kilichobakia ni kutia saini mkataba wake mpya lakini kuna mambo yanayoendelea hivi sasa ikiwemo michezo mingi na kusafiri ndio maana anaweza kuchelewa kidogo kusaini mkataba huo. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 30 alijunga na Bayern akitokea Real Madrid mwaka 2009 na toka kipindi hicho amekuwa mchezaji muhimu wa mabingwa hao wa Ujerumani na Ulaya akiwa ametupia nyavuni mabao saba katika mechi 16 za Bundesliga alizocheza msimu huu.

WAENDESHA MASHITAKA WAONDOA HOJA MUHIMU KATIKA KESI YA MAUAJI YA PISTORIUS.

WAENDESHA mashitaka nchini Afrika Kusini ambao wanamshitaki mwanariadha nyota mlemavu Oscar Pistorius kwa mauaji wamekiri kuwa kuna uwezekano mshitakiwa huyo hakuwa na miguu yake ya bandia wakati akifyatua risasi zilizomuua mpenzi wake hivyo kuondoa hoja muhimu kuwa alifyatua risasi kwa makusudi. Pistorius ambaye anatarajiwa kupanda kizimbani Machi 3 mwaka huu, amekana shitaka la kuua na kudai kuwa alidhani amevamiwa na majambazi wakati akifyatua risasi kadhaa kuelekea mlango wa bafuni ambazo zilimuua mpenzi wake Reeva Steenkamp pale pale. Steenkamp ambaye alikuwa ni manamitindo na mtangazaji alikuwa na umri wa miaka 29 wakati wa tukio hilo mwaka jana. Wakati wa usikilizwaji wa kesi ya dhamana mwaka jana, waendesha mashitaka walidai kuwa Pistorius alichukua muda kuvaa miguu yake ya bandia kabla ya kufyatua risasi katika mlando wa bafu uliofungwa hali ambayo ilionyesha hakuwa katika mshituko kwa kile alichodai kuwa alidhani amevamiwa. Waendesha mashitaka wanaamini walinzi wanaolinda eneo hilo ilipo nyumba ya Pistorius walipiga simu baada ya kusikia mlio wa risasi ili kuona kama kila kitu kiko sawa ambapo walijibiwa kuwa alikuwa salama na hakuomba msaada wowote. Polisi pia walidai jirani anayeishi mita 100 kutoka ilipo nyumba ya Pistorius alisikia milio ya risasi katika usiku wa siku ya wapendanao ambapo Steenkamp aliuawa. Mwanariadha huyo ambaye aliweka historia mwaka 2012 ya kuwa mwanariadha mlemavu wa kwanza kushiriki mashindano ya olimpiki na paralimpiki, anaweza kufungwa kifungo cha maisha kama akikutwa na hatia katika kesi hiyo.

USHINDI DHIDI YA MAN CITY WAMPA JEURI XAVI, ATAMBA BARCELONA KUTOOGOPA TIMU YOYOTE.

KIUNGO mahiri wa klabu ya Barcelona Xavi Hernandez amesisitiza kuwa timu hiyo haimuogopi yoyote katika michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya lakini pia hawatawadharau wapinzani wanaokutana nao. Kauli hiyo ya Xavi imekuja kufuatia ushindi murua wa mabao 2-0 waliopata dhidi ya Manchester City katika mechi ya mkondo wa kwanza hatua ya mtoano ya michuano hiyo ushindi ambao kiungo huyo amesema umewajengea kujiamini zaidi. Xavi amesema hawaogopi timu yoyote lakini hiyo haimaanishi kuwa hawawaheshimu wapinzani wao kama Bayern Munich, Paris Saint-Germain na Atletico Madrid ambao wote wameanza vizuri katika hatua hiyo. Nyota huyo aliendela kusema kuwa kwasasa wako wanacheza katika kiwango kizuri na kila mtu anafurahia kwasababu wanaongoza La Liga, wako katika nafasi nzuri kwenye Ligi ya Mabingwa na pia wamefika fainali ya Kombe la Mfalme.

BAADA YA KUSHITAKIWA KWA UDANGANYIFU, RAIS WA BARCELONA ASEMA HAWANA CHA KUFICHA KUHUSIANA NA UHAMISHO WA NEYMAR.

RAIS wa klabu ya Barcelona, Josep Maria Bartomeu amesisitiza kuwa hatabadilisha chochote kuhusiana na uhamisho wa Neymar, licha ya utata na mambo ya kisheria yanayotokana na uhamisho huo. Barcelona wameshitakiwa kwa udanganyifu na mahakama ya juu nchini Hispania jana kwa madai ya kukwepa kulipa kodi ya euro milioni 9.1 katika uhamisho wa Neymar kwenda Camp Nou katika majira ya kiangazi mwaka jana. Bartomeu ambaye alichukua nafasi ya Sandro Rosell aliyejiuzulu Januari kufuatia sakata hilo amesema ana uhakika kuwa klabun hiyo itakutwa haina hatia juu ya tuhuma hizo za ukwepaji kodi. Rais huyo amesema mkataba waliosaini na Neymar na klabu ya Santos ulikuwa halali sambamba na mazungumzo, shughuli za kifedha na mengineyo yote yalifanyika kwa mujibu wa sheria hivyo hawana shaka yoyote. Bartomeu aliendelea kudai kuwa watafanya kama walivyofanya mwanzo kama watapewa nafasi ya kumsajili Neymar kwa mara nyingine.

TWIGA STARS, ZAMBIA SASA KUCHEZA FEB 28.

MECHI ya mkondo wa pili ya raundi ya kwanza kuwania kufuzu michuano ya Kombe la Afrika kwa Wanawake,AWC kati ya timu ya taifa ya Tanzania,Twiga Stars na Zambia inayojulikana kama Shepolopolo sasa itachezwa Februari 28 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam. Twiga Stars tayari ipo kambini kujiandaa kwa mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 10 kamili jioni chini ya kocha Rogasian Kaijage huku wakifanya mazoezi yao kwenye Uwanja wa Karume ambao ni wa nyasi za bandia kama ulivyo ule wa Azam Complex. Shepolopolo iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mechi ya kwanza iliyochezwa Februari 14 mwaka huu kwenye Uwanja wa Nkoloma jijini Lusaka na kama Twiga Stars wakifanikiwa kuiondoa Shepolopolo itacheza na mshindi wa mechi kati ya Botswana na Zimbabwe. Wakati huohuo Ligi Kuu ya Vodacom,VPL kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaingia raundi ya 19 kesho kwa mechi tano zitakazochezwa katika miji ya Dar es Salaam, Bukoba, Morogoro, Tanga na Arusha. Kwa upande wa Dar es Salaam, Yanga watakuwa wageni wa Ruvu Shooting ya mkoa wa Pwani katika Uwanja wa Taifa, wakati huko Bukoba Kagera Sugar wataikaribisha Rhino Rangers ya Tabora katika Uwanja wa Kaitaba. Huko Morogoro katika Uwanja wa Manungu uliopo Turiani Mtibwa Sugar watakuwa wenyeji wa Ashanti United huku Coastal Union wakiwa na kibarua kigumu dhidi ya Mbeya City katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga na maafande wa Oljoro JKT watakuwa nyumbani kupambana na Mgambo Shooting katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.


EUROPA LEAGUE YASHIKA KASI.

TIMU za Valencia ya Hispania, Juventus ya Italia na Benfica ya Ureno zimejiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele katika michuano ya Europa League baada ya kushinda mechi zao za mkondo wa kwanza zilizochezwa jana. Kwa upande wa Valencia wao walifanikiwa kuifunga Dynamo Kiev kwa mabao 2-0 katika mchezo ulihamishwa na kuchezwa jijini Nicosia, Cyprus kutokana na vurugu zinazoendelea mji mkuu wa Ukraine, Kiev. Kwa upande wa Juventus na walifanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Trabzonspor katika mchezo uliochezwa jijini Turin kuhu Benfica wao wakipaa ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya PAOK Salonika ya Ugiriki. Mechi zingine zilizochezwa jana na matokeo kushangaza ni Ajax Amtserdam ambao walipokea kichapo cha mabao 3-0 nyumbani kwao kutoka kwa FC Salzburg ya Austria huku Porto wao wakilazimishwa sare nyumbani ya mabao 2-2 na Eintracht Frankfurt ya Ujerumani. Kwa upande wa timu za Uingereza mambo hayakuwa mazuri kama ilivyokuwa katika matokeo ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya, ambapo Swansea City walilazimishwa sare ya bila kufungana na Napoli ya Italia huku Tottenham Hotspurs wakichapwa bao 1-0 ugenini na FC Dnipro ya Ukraine.

KLOPP AMTEGEMEA REUS UWANJANI WIKIENDI HII.

MENEJA wa klabu ya Borussia Dortmund, Jurgen Klopp anategemea nyota wake Marco Reus kurejea uwanjani wakati kikosi chake kitakaposafiri kwenda kupambana na Hamburg katika mchezo wa Bundesliga utakaochezwa kesho. Nyota huyo wa kimataifa wa Ujerumani alikosa michezo miwili iliyopita ya Dortmund baada ya kuchanika msuli katika mchezo dhidi ya Werder Bremen uliochezwa mapema mwezi huu lakini anaonekana kuwa fiti kwa ajili ya mchezo huo. Akihojiwa kuhusu afya ya mchezaji huyo Klopp amesema Reus alifanya mazoezi kwa asilimia 100 na alionekana kuwa vizuri hivyo anadhani atakakuwa fiti kwa ajili ya mchezo kesho. Klopp amesema watakwenda katika mchezo huo bila kuwadharau wenyeji wao ambao wanaonekana kusuasua baada ya kufungwa mechi saba mfululizo hatua iliyopelekea kocha wake Bert van Marwijk kutimuliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Mirko Slomka.

PUYOL HATIHATI KUCHEZA KOMBE LA DUNIA - GRANDE.

KOCHA msaidizi wa timu ya taifa ya Hispania, Toni Grande amedai kuwa kuna hatihati ya beki wa kati wa klabu ya Barcelona Carles Puyol kuitwa katika kikosi cha nchi hiyo kitakachoshiriki michuano ya Kombe la Dunia mwaka huu. Kikosi cha Hispania kinachonolewa na Vicente del Bosque kilinyakuwa taji la michuano hiyo miaka minne iliyopita huku kikiwa na safu ya ulinzi imara iliyoongozwa na mkongwe Puyol lakini nyota huyo atakuwa na miaka 36 wakati wa michuano hiyo itakayofanyika nchini Brazil. Kutokana na maswali juu ya afya yake huku akiwa amecheza mechi moja pekee ya La Liga kwa mwaka huu, Grande anafikiri wakati umefika kwa mkongwe huyo kustaafu rasmi soka la kimataifa baada ya kucheza mechi 100. Grande amesema siku zote Puyol amekuwa mchezaji muhimu kwa nchi yake hivyo hawezi kumuondoa moja kwa moja lakini ni suala lililo wazi kuwa anahitaji muda zaidi wa kucheza hususani mechi muhimu za Barcelona.

Thursday, February 20, 2014

FEDERER BADO YUKO FITI - SAMPRAS.

NYOTA wa zamani wa tenisi kw upande wa wanaume Pete Sampras wa Marekani anaamini kuwa Roger Federer wa Switzerland bado ana uwezo na kasi ya kuweka rekodi ya kunyakuwa taji la michuano ya Wimbledon kwa mara ya nane. Sampras na Federer wote kwa pamoja wamewahi kushinda taji hilo mara saba kila mmoja. Lakini taji la mwisho kubwa kwa Federer mwenye umri wa miaka 32 lilikuwa la Wimbledon alilonyakuwa mwaka 2012. Kutokana na kiwango kibovu alichoonyesha mwaka jana kumepelekea baadhi ya wadau wa mchezo huo kudai kuwa nyota huyo mwenye rekodi ya kunyakuwa mataji 17 kuwa amekwisha makali yake. Hata hivyo Sampras mwenye umri wa miaka 42 hivi sasa amesema bado ni mapema sana kumuondoa Federer kwani kama akiendelea kufurahia na kuwa na afya anaweza kucheza kwa miaka mingine miwili zaidi au minne.

STYLE YA UFUNDISHAJI WA MOYES NDIO INAYOMSHINDA VAN PERSIE - VAN GAAL.

KOCHA wa timu ya taifa ya Uholanzi, Louis van Gaal amedai kuwa mshambuliaji nyota wa klabu ya Manchester United anapata wakati mgumu kuzoea aina ya soka inayofundishwa na kocha David Moyes. Kuna taarifa kuwa Van Persie alikwaruzana na Moyes kutokana na aina ya mazoezi anayotoa msimu huu huku Shirikisho la Soka la Uholanzi likiwasiliana na United kuhusu majeruhi yanayomuandama nyota huyo kuelekea katika michuano ya Kombe la Dunia. Van Gaal anaamni kuwa mshambuliaji huyo wa zamani wa Arsenal atakuwa fiti kwa Kombe la Dunia kwasababu mechi za timu ya taifa ni rahisi ukilinganisha na za United. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa ana uhakika nyota huyo atang’aa akija katika timu ya taifa kama alivyofanya katika mechi zao za kufuzu kwasababu ni mahala ambapo anaweza kucheza kama alivyozoea kulinganisha na klabu yake.

NEYMAR AMTETEA BABA YAKE.

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Barcelona ameonyesha kukasirishwa kwake na rais wa zamani na sasa wa klabu ya Santos huku akimkingia kifua baba yake juu ya sakata la uhamisho wake kwenda Camp Nou. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 22 aliondoka nchini Brazil kwa ada rasmi ya euro milioni 57 ingawa mwezi uliopita Barcelona Barcelona ilitoa vielelezo vilivyoonyesha kuwa nyota huyo alisajiliwa kwa euro milioni 86.2. Rais wa sasa wa Santos Odilio Rodrigues ameishambulia kampuni ya baba yake Neymar kwa kulipwa bonasi ya kitita cha euro milioni 40 kama sehemu ya uhamisho ambapo klabu hiyo imechukua hatua za kisheria ili kuonya nyaraka zilizotumika katika makubaliano kati ya Barcelona na baba wa nyota huyo. Rais wa zamani wa Santos, Luis Alvaro de Oliveira Ribeiro pia alimshambulia baba yake Neymar akidai kuwa ni haki kabisa kupelekwa mahakamani. Neymar amesema amekaa kimya kwa kipindi kirefu lakini ameshindwa kwa jinsi watu aliokuwa akiwaheshimu wanavyomnyanyapaa baba yake. Nyota huyo aliendelea kusema kuwa haoni kosa alilofanya baba yake mpaka ashambuliwe hivyo kwani hata kama aliipata hela hiyo wanayosema hakuipata akiwa amekaa bali aliifanyia kazi kwa kipindi kirefu.