Friday, February 21, 2014

WAENDESHA MASHITAKA WAONDOA HOJA MUHIMU KATIKA KESI YA MAUAJI YA PISTORIUS.

WAENDESHA mashitaka nchini Afrika Kusini ambao wanamshitaki mwanariadha nyota mlemavu Oscar Pistorius kwa mauaji wamekiri kuwa kuna uwezekano mshitakiwa huyo hakuwa na miguu yake ya bandia wakati akifyatua risasi zilizomuua mpenzi wake hivyo kuondoa hoja muhimu kuwa alifyatua risasi kwa makusudi. Pistorius ambaye anatarajiwa kupanda kizimbani Machi 3 mwaka huu, amekana shitaka la kuua na kudai kuwa alidhani amevamiwa na majambazi wakati akifyatua risasi kadhaa kuelekea mlango wa bafuni ambazo zilimuua mpenzi wake Reeva Steenkamp pale pale. Steenkamp ambaye alikuwa ni manamitindo na mtangazaji alikuwa na umri wa miaka 29 wakati wa tukio hilo mwaka jana. Wakati wa usikilizwaji wa kesi ya dhamana mwaka jana, waendesha mashitaka walidai kuwa Pistorius alichukua muda kuvaa miguu yake ya bandia kabla ya kufyatua risasi katika mlando wa bafu uliofungwa hali ambayo ilionyesha hakuwa katika mshituko kwa kile alichodai kuwa alidhani amevamiwa. Waendesha mashitaka wanaamini walinzi wanaolinda eneo hilo ilipo nyumba ya Pistorius walipiga simu baada ya kusikia mlio wa risasi ili kuona kama kila kitu kiko sawa ambapo walijibiwa kuwa alikuwa salama na hakuomba msaada wowote. Polisi pia walidai jirani anayeishi mita 100 kutoka ilipo nyumba ya Pistorius alisikia milio ya risasi katika usiku wa siku ya wapendanao ambapo Steenkamp aliuawa. Mwanariadha huyo ambaye aliweka historia mwaka 2012 ya kuwa mwanariadha mlemavu wa kwanza kushiriki mashindano ya olimpiki na paralimpiki, anaweza kufungwa kifungo cha maisha kama akikutwa na hatia katika kesi hiyo.

No comments:

Post a Comment