Friday, May 31, 2013

VALDES KUBAKIA BARCELONA MPAKA 2014.

GOLIKIPA wa klabu ya Barcelona, Victor Valdes amesisitiza kuwa hataki kuondoka klabuni hapo katika kipindi cha usajili na badala yake ameamua kukaa mpaka mkataba wake utakapomalizika Juni mwaka kesho. Mapema msimu huu Valdes aliiambia klabu hiyo kwamba hahitaji kuongeza mkataba wake hivyo kuzusha tetesi kuwa anaweza kuondoka mwishoni mwa msimu huu. Klabu iliyopanda daraja msimu huu ya AS Monaco ndiyo iliyoaminika kuwa inataka kusajili nyota huyo lakini mwenyewe sasa ameweka wazi nia yake ya kumaliza mkataba wake akiwa Camp Nou. Valdes amesema nafasi anayocheza imekuwa na changamoto nyingi na anahisi kama amechoka kiakili ndio maana amemua kumaliza mkataba wake 2014 bila kuongeza mwingine ili aweze kupumzika.

FIFA YAPITISHA SHERIA KALI KWA WABAGUZI.

SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA limepigia kura adhabu mpya kwa ajili ya vitendo vya kibaguzi ambapo timu zinaweza kushushwa daraja au kutolewa katika mashindano kama wakikutwa na hatia ya kufanya vitendo hivyo. Adhabu ya kwanza kwa matukio hayo itakuwa ni onyo, kutozwa faini au kuchezeshwa kaika uwanja mtupu wakati adhabu ya pili kama tukio hilo likijirudia itakuwa ni kukatwa alama, kuenguliwa katika mashindano au kushushwa daraja. Rais wa FIFA Sepp Blatter anaamini kuwa hatua inatuma ujumbe madhubuti kwa watu wenye tabia za kibaguzi kwamba muda wao umeisha. Azimio la kupambana na vitendo vya kibaguzi lilipigiwa kura ya kupitishwa kwa asilimia 99 katika mkutano mkuu wa FIFA unaofanyika huko Mauritius.

GUTI AMPONDA MOURINHO.

KIUNGO wa zamani wa klabu ya Real Madrid, Guti amemshambulia Jose Mourinho kwa kudai kuwa Mreno huyo alitakiwa kuonyesha unyenyekevu zaidi kufuatia timu yake kushindwa kunyakuwa taji lolote msimu wa 2012-2013. Madrid walishuhudia mahasimu wa Barcelona wakinyakuwa taji la Ligi Kuu wakati wao wakipata kipigo kutoka kwa majirani zao Atletico Madrid kwenye fainali ya Kombe la Mfalme hatua ambayo imepelekea Mourinho kuondoka mwishoni mwa msimu. Guti amesema walikuwa wakitegemea vitu vingi kutoka kwake na sio mataji pekee, lakini wakati unapomaliza msimu vibaya inabidi uonyeshe unyenyekevu kidogo ili kuwapoza mashabiki. Nyota huyo amesema hakuwepo kujua ni kitu gani gani kinaendelea katika vyumba vya kubadilishia nguo kila siku lakini kama una mkataba wa miaka minne halafu unaondoka kabla ya kumaliza mkataba huo lazima kutakuwa na tatizo. Pamoja na kumaliza msimu huu vibaya Mourinho amefanikiwa kuingoza Madrid kunyakuwa taji moja la ligi, Kombe la Mfalme na Kombe la Ligi katika kipindi cha miaka mitatu ambayo ameinoa klabu hiyo.

LEONARDO AFUNGIWA MIEZI TISA.

MKURUGENZI wa Michezo wa klabu ya Paris Saint-Germain-PSG, Leonardo amefungiwa miezi tisa kujishughulisha na masuala ya michezo kwa kosa la kumsukuma mwamuzi. Leonardo alionekana katika picha za video akimsukuma mwamuzi Alexandre Castro kwa bega lake baada ya kukasirishwa na kitendo cha Thiago Silva kupewa kati nyekundu katika mchezo ambao PSg ilitoa sare ya bao 1-1 na Valenciennes. Nyota huyo wa zamani wa kimataifa wa Brazil mwenye umri wa miaka 43 alikana kufanya tukio hilo huku PSG ikithibitisha kumkatia rufani kupinga adhabu hiyo. Mbali na adhabu hiyo ya Leonardo, PSG nao pia wamekatwa alama tatu adhabu ambayo wataitumikia msimu ujao wa Ligi Kuu nchini Ufaransa.

PLATINI AWAPASHA FIFA.

RAIS wa Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA, Michel Platini anaamini kuwa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA haliko tayari kuweka kikomo cha umri na muda wa uongozi kwa viongozi wa juu baada ya kutupilia ajenda hiyo kwenye mkutano wake mkuu. Rais wa FIFA Sepp Blatter alitupilia mbali ajenda hiyo kwa kudai kuwa inatengeneza ubaguzi miongoni mwa viongozi lakini Platini amedai kuwa suala hilo limewachukiza viongozi wengi wa kamati ya utendaji ya FIFA. Platini amesema miongozi mwa wajumbe 24 wa kamati ya utendaji saba kati yao ambao wanaiwakilisha UEFA hawakufurahishwa na hatu hiyo. Platini aliendelea kusema kuwa suala hilo limekuwa likijadiliwa kwa kipindi cha miaka miwili lakini FIFA wanaonekana kama hawakubaliani nalo ndio maana wanalipiga danadana.

Thursday, May 30, 2013

ABIDAL ATANGAZA KUONDOKA BARCELONA.

BEKI wa kushoto nyota wa kimataifa wa Ufaransa na klabu ya Barcelona, Eric Abidal ametangaza kuondoka katika klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu ikiwa ni miezi miwili imepita tangu arejee uwanjani baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuandikiza ini. Abidal aliwaambia waandishi wa habari kuwa pamoja na kuondoka klabuni hapo lakini atarejea tena katika nafasi tofauti, baada ya tetesi kuwa timu hiyo imempa kibarua kuendesha shule ya michezo. Huku akibubujikwa na machozi Abidal amesema angependa kuendelea kuichezea Barcelona lakini klabu hiyo inaangalia mambo tofauti na lazima aheshimu hilo. Abidal mwenye umri wa miaka 33 ambaye upasuaji wake wa kupandikiza ini ulifanikiwa kwa kiwango cha kushangaza na kurejea uwanjani mwezi uliopita, mkataba wake unaishia mwishoni mwa msimu huu. Pamoja na kuondoka Barcelona nyota huyo amesema ataendelea kucheza kwa kipindi kingine kifupi katika klabu yoyote itakayomsajili.

MAN UNITED, MAN CITY ZAMGOMBEA FABREGAS.

KLABU za Manchester United na Manchester City zinashindana kumrejesha katika Ligi Kuu kiungo nyota wa klabu ya Barcelona Cesc Fabregas msimu ujao. Meneja mpya wa United David Moyes amepanga kumtengea nyota huyo kitita cha paundi milioni 25 kiungo huyo baada ya Barcelona kuonyesha nia ya kumuuza nahodha huyo wa zamani Arsenal. Lakini mahasimu wa United, timu ya City nao walipata tetesi za kutaka kuuzwa kwa nyota huyo wa kimataifa wa Hispania na wao pia kuanza kumnyatia. Arsenal ndio wenye nafasi ya kwanza kwenye usajili wa nyota huyo ikiwa ni sehemu ya makubaliano na Barcelona, lakini Moyes kwa kipindi kirefu amekuwa akimhusudu kiungo huyo mwenye umri wa miaka 26 na kuna kipindi alitaka kumpeleka Everton kwa mkopo wakati akichipukia.

BALOZI BISWARO AWAPA CHANGAMOTO STARS.

Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Joram Biswaro amewataka wachezaji wa Taifa Stars kuhakikisha wanaipeleka timu hiyo kwenye fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazil. Ametoa changamoto hiyo wakati alipotembelea mazoezi ya timu hiyo jana (Mei 29 mwaka huu). Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imepiga kambi nchini Ethiopia na inafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Addis Ababa. “Watanzania tunafurahi kutokana na uwezo mnaouonyesha, hasa baada ya kuifunga Morocco mabao 3-1. Kama mliwafunga nyumbani hata kwao mnaweza kuwafunga. Tunataka kuwaona Maracana (Brazil) mwakani, mimi tayari ninayo tiketi mtanikuta kule,” amesema Balozi Biswaro ambaye enzi zake aliwahi kuichezea timu ya Yanga. Taifa Stars ambayo iko Addis Ababa tangu Jumatatu (Mei 27 mwaka huu) imeweka kambi katika hoteli ya Hilton ambapo Jumapili (Juni 2 mwaka huu) itacheza mechi ya kirafiki na Sudan (Nile Crocodile) kwenye Uwanja wa Addis Ababa. Balozi Biswaro ameikaribisha Taifa Stars ubalozini Addis Ababa mara baada ya mechi dhidi ya Sudan ambapo itakutana na baadhi ya Watanzania wanaoishi Ethiopia kabla ya kuondoka alfajiri kwenda Marrakech, Morocco kwa kupitia Cairo, Misri. Kocha Kim Poulsen amesema kikosi chake kinaendelea na mazoezi vizuri na kitaimarika zaidi baada ya wachezaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kujiunga nacho Juni 3 mwaka huu jijini Marrakech kwa ajili ya mechi dhidi ya Morocco itakayochezwa Juni 8 mwaka huu. Wachezaji walioko katika kikosi cha Stars jijini Addis Ababa ni Juma Kaseja, Aggrey Morris, Mwadini Ally, Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Erasto Nyoni, Haroub Nadir, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vicent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd, Haruni Chanongo na Zahoro Pazi.

FRENCH OPEN: SERENA NA VENUS WILLIAMS WAJITOA MASHINDANO YA WAWILI WAWILI.

WANADADA nyota katika mchezo wa tenisi, Serena na Venus Williams wamejitoa katika michuano ya wazi ya Ufaransa kwa wachezaji wawili wawili kabla ya kucheza hata mechi moja. Wanadada hao walitarajiwa kushiriki katika michuano hiyo kwa mara ya kwanza toka mwaka 2010 lakini walijitoa Jumatano na hakuna sababu yoyote iliyotolewa na waandaaji wa michuano hiyo. Mapema Venus alidai kusumbuliwa na matatizo ya mgongo wakati alipopoteza mchezo wake wa Jumapili iliyopita kwa kufungwa seti tatu wakati Serena yeye alifanikiwa kumlipizia kisasi dada yake na kutinga katika mzunguko wa tatu wa michuano hiyo. Nyota hao wawili wamefanikiwa kushinda jumla ya mataji 13 ya Grand Slam kwa michezo ya wawili wawili kwa wanawake yakiwemo mataji ya michuano ya wazi ya Ufaransa mwaka 1999 na 2010.

NEYMAR KUTAMBULISHWA RASMI JUMATATU.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Brazil na klabu ya Santos, Neymar ambaye amesaini mkataba wa miaka mitano na Barcelona ya Hispania, anatarajiwa kutambulishwa rasmi Jumatatu. Akiongea na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Ufundi wa Barcelona Alberto Parreira amesema kwa Neymar amepewa ruhusa kwenda Barcelona baada ya kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Uingereza Jumapili. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 21 ambaye jina lake kamili ni Neymar da Silva Santos Junior alibainisha Jumanne kuwa ana hamu kubwa ya kujiunga na Barcelona lakini kwasasa anataka kufikiria zaidi michuano ya Kombe la Shirikisho inayotarajiwa kuanza mwezi ujao. Kombe la Shirikisho ni michuano ambayo hufanyika mwaka mmoja kabla ya kuanza rasmi michuano ya Kombe la Dunia na itaanza kutimua vumbi rasmi kuanzia Juni 15 hadi 30 mwaka huu. Brazil wamewahi kunyakuwa Kombe la Dunia mara tani na Kombe la Shirikisho mara tatu.

PELLEGRINI, CITY WAKARIBIA KUFUNGA "NDOA".

MENEJA wa klabu ya Malaga aliyebwaga manyanga, Manuel Pellegrini amesema anamatumaini makubaliano ya awali waliyofikia na klabu ya Manchester City yatakamilika. Pellegrini ambaye ni raia wa Chile amesema ana majukumu ya kuipa kipaumbele Manchester City kwani wameshafanya mazungumzo ya awali na ni mategemeo yake yatakwenda vyema. Wiki iliyopita kocha huyo mwenye umri wa miaka 59 ambaye amewahi pia kuzinoa klabu za Villarreal na Real Madrid alitangaza kuondoka Malaga mwishoni mwa msimu huu baada ya kuinoa klabu hiyo kwa miaka miwili na nusu. Kocha huyo amekuwa akihusishwa na tetesi za kipindi kirefu za kuhamia City toka klabu hiyo ilipomtimua kocha wake Roberto Mancini mapema mwezi huu.

BALE AMEZALIWA KUITUMIKIA MADRID - PEREZ.

RAIS wa klabu ya Real Madrid, Florentino Perez ameongeza uvumi wa kutaka kumsajili mshambuliaji nyota wa klabu ya Tottenham Hotspurs Gareth Bale baada ya kusisitiza kuwa nyota amezaliwa kwa ajili ya kuichezea klabu hiyo. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 23 amefunga mabao 21 katika Ligi Kuu nchini Uingereza msimu huu mabao ambayo yameifanya Spurs kukosa kidogo nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa na anategemewa kusainishwa mkataba mpya ambao utamuwezesha kulipwa paundi 130,000 kwa wiki msimu ujao. Hatahivyo wakala wa mchezaji huyo Jonathan Barnett alikiri mapema jana kuwa mshambuliaji huyo anaweza kukubali ofa yoyote watakayotoa Madrid. Perez aliongeza uvumi huo kwa kauli yake ya kudai kuwa mchezaji huyo kawazaliwa kwa ajili ya kuichezea klabu yake huku mkurugenzi mpya wa michezo wa Zinedine Zidane naye akimtaka mchezaji huyo baada ya kumfananisha na Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.

STOKE CITY WAMPA KIBARUA HUGHES.

KLABU inayoshiriki Ligi Kuu nchini Uingereza, Stoke City imemteua Mark Hughes kuwa meneja mpya wa klabu hiyo baada ya kutimuliwa Queens Park Rangers-OPR. Hughes amechukua nafasi ya Tony Pulis ambaye aliondoka Stoke kwa maelewano wiki iliyopita baada ya kuifundisha klabu hiyo kwa kipindi cha miaka saba. Hughes mwenye umri wa miaka 49 ambaye pia amewahi kuifundisha Manchester City amekaa bila toka alipoondoka QPR Novemba mwaka jana. Kocha huyo raia wa Wales alishindwa kupata ushindi katika mechi 12 za ligi kwenye msimu wa 2012-2013 na kupelekea kutimuliwa QPR na nafasi ya kuchukuliwa na Harry Redknapp.

Wednesday, May 29, 2013

CRUYFF AMSHAURI VILANOVA KUJIUZULU UKOCHA KWA MUDA.

NGULI wa zamani wa soka wa Barcelona, Johan Cruyff amemshauri meneja wa klabu hiyo Tito Vilanova kujiuzulu wadhifa huo na kufikiria zaidi kuhusu mustakabali wa afya yake. Vilanova mwenye umri wa miaka 44 aliondolewa uvimbe wa saratani katika koo lake mwaka 2011 lakini Desemba mwaka jana hali hiyo ilijirudia tena hivyo kumfanya kukosa miezi kadhaa katika msimu wa 2012-2013 wakati akipata matibabu. Kocha huyo alirejea katika benchi la ufundi la Barcelona Aprili mwaka huu lakini Cruyff anafikiri ingekuwa vyema kwa manufaa yake kama angeachana na masuala ya ukocha kwasasa. Cruyff amesema hasemi hayo kwa kumkosea heshima ila ni kwa manufaa yake kwani huwezi kufundisha katika kiwango cha juu kama afya yako haiku vizuri.

BALE NI GHALI ZAIDI YA NEYMAR - WAKALA.

WAKALA wa mshambuliaji nyota wa klabu ya Tottenham Hotspurs, Gareth Bale amedai kuwa itawagharibu Real Madrid zaidi ya fedha ambazo Barcelona imelipa kwa ajili ya Neymar kama wanataka kumsajili nyota huyo raia wa Wales. Wakala huyo Jonathan Barnett amesema inashangaza lakini gharama yoyote iliyogharimu Barcelona kumsajili, Bale ana thamani zaidi ya hiyo. Rais wa Madrid Florentino Perez anahisiwa kumhitaji nyota huyo mwenye umri wa miaka 23 ikiwa ni hatua ya kwanza ya kukibadilisha kikosi cha timu hiyo baada ya kumaliza masimu vibaya kwa kushindwa kunyakuwa taji lolote. Madrid walimkosa Neymar baada ya mahasimu wao Barcelona kuwazidi na kumnyakuwa nyota huyo kwa mkataba wa miaka mitano mwishoni mwa wiki iliyopita hivyo kuhamishia nguvu zao kwa Bale. Lakini Barnett amedai kuwa Bale ni mchezaji bora zaidi ya Neymar hivyo kama Madrid wanamhitaji hawana neno wanawasubiri ila itawagharimu kiasi kikubwa.

HENRY AITAKA ARSENAL KUWEKA MALENGO YA MBALI ZAIDI.

MSHAMBULIAJI wa zamani wa klabu ya Arsenal, Thierry Henry ameionya klabu hiyo kuwa lazima waongeze malengo yao kuliko kufikiria kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kila msimu. Kikosi cha Arsene Wenger kilishangilia baada ya kujihakikishia nafasi ya nne za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu nchini Uingereza kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Newcastle United katika mechi ya mwisho na kupelekea wadau mbalimbali kuiponda timu hiyo. Henry ambaye kwasasa anacheza katika klabu ya New York Red Bulls amesema kitu pekee ambachi kinaweza kushangiliwa katika msimu huu ni kitendo cha kuwa nyima nafasi mahasimu wao Tottenham Hotspurs nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa. Henry amesema kama ukiwa mshabiki wa kweli wa Arsenal lazima ufurahie kuwashinda mahasimu wenu lakini bado klabu hiyo ina changamoto ya kuhakikisha inarejesha heshima yake kwa kushinda vikombe.

TOURE AKAMILISHA USAJILI HURU KWENDA LIVERPOOL.

KLABU ya Liverpool imebainisha kuwa wamekubali kumsajili beki wa kimataifa wa Ivory Coast Kolo Toure wakati mkataba wake na Manchester City utakapomalizika Julai mosi mwaka huu. Beki huyo mwenye umri wa miaka 32 alijiunga na City akitokea Arsenal ada ya paundi milioni 16 mwaka 2009 ambapo mwaka mmoja baadae aliungana na mdogo wake Yaya aliyetokea Barcelona. Kolo Toure alikuwa amekabidhiwa mikoba ya unahodha wa City lakini alipoteza nafasi yake ya kikosi cha kwanza baada ya kufungiwa miezi sita kwa kosa la kukutwa na chembechembe za dawa zilizokatazwa michezoni Machi 2011. Mchezaji huyo alidai kuwa alitumia vidonge vya kupunguza uzito vua mke wake na alikuwa hajui kwamba vidonge hivyo vina dawa ndani yake zilizokatazwa. Pamoja na kufungiwa huko Toure anaondoka City akiwa na medali za Kombe la FA na Ligi Kuu ya Uingereza.

KAMATI YA BLATTER YATUPILIA MBALI AJENDA YA KIKOMO CHA UONGOZI NA UMRI.

KAMATI ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Duniani-FIFA iliyokuwa ikiongozwa na rais wake Sepp Blatter wametupilia mbali pendekezo la kikomo cha umri na muda wa uongozi kuwa ajenda ya kuzungumziwa katika mkutano wake Ijumaa. Uamuzi huo ambao umekuwa ukizua mjadala karibu kipindi cha mwaka mzima juu ya kikomo cha umri kwa viongozi wa juu ulikubaliwa na kamati hiyo iliyokutana katika kisiwa cha Bahari ya Hindi. Hatua imekuja ikiwa ni siku moja baada ya Blatter ambaye anaweza kugombea tena nafasi hiyo katika kipindi cha miaka miwili ijayo kwa sheria za sasa, kudai kuwa kuweka kikomo cha umri kutachukuliwa kama aina ya ubaguzi. Katika taarifa iliyotumwa katika mtandao wa FIFA imedai kuwa ajenda mbili za kikomo cha umri na muda wa kukaa madarakani zimeondolewa kwa ajili ya kujadiliwa zaidi ambapo zinaweza kuletwa tena katika mkutano mkuu wa shirikisho hilo 2014.

EURO MILIONI 60 ZAMPELEKEA FALCAO MONACO.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Colombia, Radamel Falcao yuko mbioni kukamilisha uhamisho wake unaogharimu kiasi cha euro milioni 60 kutoka Atletico Madrid kwenda klabu ya AS Monaco ya Ufaransa. Falcao mwenye umri wa miaka 27 amekuwa gumza katika kipindi hiki cha usajili huku vilabu mbalimbali vikubwa kama Real Madrid, Chelsea na Manchester City zikipigana vikumbo kutaka saini yake. Hata hivyo, badala ya kwenda huko nyota huyo sasa atatua Monaco baada ya kusaini mkataba wa miaka minne na klabu hiyo jana. Falcao tayari amekamilisha vipimo vya afya mapema wiki hii na kitu kilichobakia ni utambulisho rasmi kwa klabu hiyo ambao utafanyika muda wowote. Nyota huyo anakuwa mchezaji wan ne kusajiliwa na Monaco katika kipindi hiki cha majira kiangazi baada ya Joao Moutinho na James Rodriguez kutoka Porto ambao wameigharimu klabu hiyo jumla ya euro milioni 70 pamoja na Rocardo Carvalho wa Madrid.

COLE AKABIDHIWA UNAHODHA WA MUDA LEO.

BEKI wa kushoto wa klabu ya Chelsea, Ashley Cole atakabidhiwa unahodha wa timu ya taifa ya Uingereza katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Jamhuri ya Ireland kama heshima ya kufikisha mechi ya 100 akiitumikia nchi yake. Meneja wa Uingereza Roy Hodgson aliwaambia waandishi wa habari kuwa Cole ndiye atakayekiongoza kikosi chake lakini Frank Lampard anataendelea kuwa nahodha wakati Steven Gerrard hayupo. Hodgson amempongeza nyota huyo kwa kuwa mtumishi bora sio kwa klabu za Arsenal na Chelsea lakini pia kwa taifa lake. Cole atatimiza mechi ya 102 akiwa na timu ya taifa kwenye mchezo huo utakaochezwa Wembley baadae leo ambapo anakuwa mchezaji wa saba wan chi hiyo kufikisha idadi hiyo ya michezo.

Tuesday, May 28, 2013

ZIDANE MKURUGENZI MPYA WA MICHEZO MADRID - PEREZ.

RAIS wa klabu ya Real Madrid, Florentino Perez amedai kuwa Zinedine Zidane atakuwa mkurugenzi mpya wa michezo wa klabu hiyo. Akihojiwa na kituo kimoja cha redio nchini Hispania, Perez amesema hajui nani atakuwa kocha mpya wa klabu hiyo kuchukua mikoba ya Jose Mourinho waliositisha mkataba wake lakini anajua wazi kwamba Zidane ndiye atakuwa mkurugenzi wa michezo. Zidane mwenye umri wa miaka 40 ameichezea Madrid katika kipindi cha mwa mwaka 2001 na 2006 na kurejea tena miaka miwili iliopita kama mshauri wa Perez. Perez alikataa kuzungumzia juu ya makocha wawili Carlo Ancelotti na Jupp Heynckes wanaopewa nafasi kubwa kuchukua mikoba ya Mourinho akidai kuwa suala hilo litawekwa wazi wiki ijayo.
WAKATI HUOHUO
RAIS wa klabu ya Real Madrid, Florentino Perez anajiandaa kumfanya Cristiano Ronaldo kuwa mchezaji anayelipwa zaidi duniani ili kumbakisha katika klabu hiyo baada ya kuondoka kwa Jose Mourinho. Perez amesema angependa kumfanya Ronaldo kuwa ghali zaidi duniani na watafanya kila linalowezekana ili kuhakikisha anakuwa na furaha. Nyota huyo wa zamani wa Manchester United amekuwa akihusishwa na tetesi za kurejea Old Trafford katika kipindi cha majira ya kiangazi huku pia mabingwa wa Ufaransa, Paris Saint-Germain nao wakimmezea mate. Ronaldo amekuwa akiifungia mabao mengi Madrid toka alipotua kwa ada ya paundi milioni 80 mwaka 2009 akifunga mabao 146 katika mechi 135 alizochezea klabu hiyo.

NEYMAR ANGETUGHARIMU EURO MILIONI 150 - PEREZ.

RAIS wa klabu ya Real Madrid, Florentino Perez amebainisha kuwa Neymar angewagharimu kiasi cha euro milioni 150 kama wangefanikiwa kumsajili nyota huyo wa kimataifa wa Brazil. Madrid walikuwa na nia ya kumsajili Neymar mwenye umri wa miaka 21 katika kipindi cha msimu wa 2013-2014 lakini nyota huyo aliamua kukaa kwenda huko na badala yake kusaini kwa mahasimu wao Barcelona. Perez amesema walikuwa na nafasi kubwa ya kumsajili nyota huyo miaka mitatu iliyopita lakini kumekuwa na hali tofauti katika kipindi hiki na ingewagharimu kiasi hicho kama wangefanikiwa. Rais huyo wa Madrid alikwenda mbali zaidi na kutoa maoni yake kuwa mshambuliaji nyota wa klabu hiyo Cristiano Ronaldo ni mchezaji bora wa dunia ingawa alikiri kuwa asingesita kumsajili nyota wa Barcelona Lionel Messi kama angepata nafasi.

TAIFA STARS YAANZA KUJINOA ADDIS ABABA.

Taifa Stars imetua jijini Addis Ababa, Ethiopia leo (Mei 28 mwaka huu) alfajiri kwa ndege ya EgyptAir ambapo itaweka kambi ya wiki moja kujiandaa kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco (Lions of the Atlas) itakayochezwa Juni 8 mwaka huu jijini Marrakech. Stars iliyotua na kikosi cha wachezaji 21 imefikia hoteli ya Hilton, na imeanza mazoezi leo (Mei 28 mwaka huu) saa 12 jioni kwenye Uwanja wa Addis. Kwa mujibu wa Kocha Kim Poulsen, Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itakuwa na vipindi (sessions) vinne vya mazoezi kabla ya kucheza mechi ya kirafiki na Sudan (Nile Crocodile). Mechi dhidi yan Sudan itachezwa Jumapili kuanzia saa 11 jioni kwenye Uwanja wa Addis. Sudan ambayo pia imeweka kambi yake Addis Ababa kujiandaa kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia ilicheza mechi yake ya kwanza jana (Mei 27 mwaka huu) dhidi ya wenyeji Ethiopia na kulala mabao 2-0. Wachezaji wanaounda Stars ni nahodha Juma Kaseja, nahodha msaidizi Aggrey Morris, Mwadini Ally, Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Erasto Nyoni, Haroub Nadir, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vicent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd, Haruni Chanongo na Zahoro Pazi. Kikosi hicho kinatarajiwa kuondoka Addis Ababa kwenda Marrakech alfajiri ya Juni 3 mwaka huu kwa ndege ya EgyptAir. Stars itatua siku hiyo hiyo Casabalanca na kuunganisha moja kwa moja kwenda Marrakech.

NEYMAR AMWAGA WINO RASMI BARCELONA.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Brazil, Neymar ametanabaisha kuwa sasa yeye ni mchezaji rasmi wa klabu ya Barcelona ya Hispania. Neymar amesema amesaini mkataba wa miaka mitano na klabu hiyo jana, zikiwa zimepita siku mbili baada ya kutangaza kuwa ameamua kuchagua timu hiyo badala ya mahasimu wao Real Madrid. Nyota amesema anaondoka Santos huku akiwa na majonzi lakini pia ni heshima kwake kusajiliwa na klabu kama Barcelona na kupata nafasi ya kucheza na baadhi ya wachezaji bora kabisa duniani. Neymar mwenye umri wa miaka 21 atajiunga na nyota wenzake Barcelna akiwemo mshindi wan ne mfululizo wa tuzo ya mchezaji bora wa dunia Lionel Messi, Xavi Hernandez na Andres Iniesta. Sio Neymar wala Barcelona walioweka wazi ada halisi ya uhamisho huo lakini vyombo vya habari nchini Brazil vimedai kuwa Barcelona watalipa kiasi cha euro milioni 30 kwa nyota huyo.

CAXIROLA MARUFUKU CONFEDERATION CUP.

WARATIBU wa michuano ya Kombe la Shirikisho linalotarajiwa kuanza mwezi ujao wamepiga marufuku kutumika kwa vyombo vya plastiki mfano wa vuvuzela kwa sababu za kiusalama. Ofisa mmoja wa kamati ya maandalizi ya michuano hiyo Medeiros Hilario amesema mashabiki watakaohudhuria michuano hiyo hawataruhusiwa kuingia na kifaa chochote cha muziki ikiwemo vyombo hivyo vya plastiki ambavyo kwa huko huitwa caxirola. Kufungiwa kwa vyombo hivyo kutaanza rasmi Jumapili wakati wa mchezo wa kirafiki kati ya Brazil na Uingereza utakaochezwa katika Uwanja wa Maracana jijini Rio de Janeiro. Uamuzi wa kufungia vifaa hivyo umekuja kufuatia tukio la Aprili 28 mwaka huu ambapo mashabiki waliokuwa wamebeba caxirolas katika mchezo wa kati ya klabu ya Bahia na Vitoria kuanza kuzirusha uwanjani baada ya kukasirishwa na matokeo ya upande mmoja. Caxirola ndio kifaa rasmi kinachotambulika na kutumika katika michuano ya Kombe la Dunia 2014 ambapo Brazil watakuwa wenyeji na kilitambulishwa na rais wa nchi hiyo Dilma Rousseff mwezi uliopita.

BENITEZ KOCHA MPYA NAPOLI.

MENEJA wa zamani wa klabu za Inter Milan, Liverpool na Chelsea, Rafael Benitez anatarajia kurejea nchini Italia kuchukua mikoba ya kuinoa klabu ya Napoli. Rais wa Napoli, Aurelio De Laurentiis alithibitisha ujio wa kocha huyo kwenye ukurasa wake wa mtandao wa twitter kwamba Benitez ndio atakuwa mbadala wa aliyekuwa kocha wa klabu hiyo Walter Mazzarri. Mazzarri alitema kibarua cha kuinoa klabu hiyo baada ya kumaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Juventus katika msimamo wa Ligi Kuu nchini Italia maarufu kama Serie A na kukata tiketi ya moja kwa moja ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya msimu ujao. Mazzarri ameiongoza Napoli kwa kipindi cha miaka minne ambapo ameweza kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa mara mbili na kushinda Kombe la Italia mwaka jana ambapo katika barua yake ya kujiuzulu wadhifa huo alidai kuwa ameifikisha timu hiyo alipotaka. Benitez aliinoa Inter katika nusu ya kwanza ya msimu wa 2010-2011 baada ya kuchukua nafasi ya Mourinho lakini alimkasirisha mmiliki wa klabu hiyo baada ya kudai kuongezewa nguvu katika kikosi chake na kutimuliwa kabla ya kipindi cha Christmas mwaka 2011.

Monday, May 27, 2013

CASILLAS, TORRES WAJUMUISHWA KATIKA KIKOSI CHA HISPANIA.

KOCHA wa timu ya taifa ya Hispania, Vicente del Bosque amemuita golikipa Iker Casillas na mshambuliaji Fernando Torres katika kikosi cha wachezaji 26 ambacho kitaanza maandalizi ya Kombe la Shirikisho linalotarajiwa kuanza mwezi ujao nchini Brazil. Orodha hiyo ya wachezaji 26 itapunguzwa na kufikia 23 baada ya mzunguko wa mwisho wa mechi za Ligi Kuu nchini Hispania mwishoni mwa wiki ijayo. Hispania ambao ni mabingwa wa Dunia na Ulaya wana mechi mbili za kimataifa za kirafiki dhidi ya Haiti Juni 8 na Ireland siku tatu baadae kabla ya kuelekea nchini Brazil. Katika michuano ya Kombe la Shirikisho, Hispania imepangwa katika kundi B sambamba na Uruguay, Tahiti na Nigeria ambapo mchezo wa ufunguzi utachezwa Juni 16 dhidi ya Uruguay. Michuano hiyo ambayo inashirikisha timu nane inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Juni 15 mpaka 30. 
Goalkeepers: Iker Casillas (Real Madrid), Victor Valdes (Barcelona), Pepe Reina (Liverpool)

Defenders: Alvaro Arbeloa (Real Madrid), Sergio Ramos (Real Madrid), Gerard Pique (Barcelona), Cesar Azpilicueta (Chelsea), Jordi Alba (Barcelona), Ignacio Monreal (Arsenal), Raul Albiol (Real Madrid), Javi Garcia (Manchester City)

Midfielders: Javi Martinez (Bayern Munich), Xavi (Barcelona), Andres Iniesta (Barcelona), Sergio Busquets (Barcelona), Santi Cazorla (Arsenal), Xabi Alonso (Real Madrid), Benat Etxebarria (Real Betis)
Forwards: Cesc Fabregas (Barcelona), David Villa (Barcelona), David Silva (Manchester City), Roberto Soldado (Valencia), Pedro (Barcelona), Juan Mata (Chelsea), Jesus Navas (Sevilla), Fernando Torres (Chelsea). 

LEWANDOWSKI BAYERN INAMHUSU - WAKALA.

WAKALA wa mshambuliaji nyota wa klabu ya Borussia Dortmund, Robert Lewandowski amesema kuna uwezekano mkubwa wa mshambuliaji huyo kujiunga na mabingwa wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya Bayern Munich. Hata hivyo, wakala huyoaitwaye Cezary Kucharski aliiambia luninga moja nchini Ujerumani kwamba Bayern bado hawajafikia makubaliano ya mambo binafsi ya nyota huyo wa kimataifa wa Poland. Wakala huyo aliendelea kusema kuwa wao wako tayari lakini badi hawajasaini chochote kwasababu klabu nayo inatakiwa iafiki makubaliano hayo. Bayern ambao ni mabingwa wapya wa Ujerumani tayari wamemnyakuwa kiungo wa Dortmund Mario Gotze mwenye umri wa miaka 20 kwa ada ya euro milioni 37.

ZIDANE APEWA KIBARUA CHA KUHAKIKISHA BALE ANATUA MADRID.

MMOJA wa wachezaji bora kabisa kuwahi kuitumikia klabu ya Real Madrid, Zinedine Zidane amepewa kazi ya kuhakikisha anamshawishi mshambuliaji nyota wa klabu ya Tottenham Hotspurs, Gareth Bale ili aweze kusajili na klabu hiyo. Gazeti la Marca nchini Hispania limeripoti kuwa nyota huyo wa zamani ndio mshauri mkuu kuhusiana na suala la Bale ana anajaribu kumshawishi raia wa Madrid Florentino Perez kuwa lazima waipate saini ya nyota huyo. Kwa kuonyesha kwamba hawataki mchezo kwenye suala hilo Madrid wamepania hata kutoa kitita cha paundi milioni 65 kwa ajili ya kumchukua Bale kutoka Spurs. 
Zidane kwa kipindi kirefu amekuwa akimhusudu nyota huyo wa kimataifa wa Wales akidai kuwa amekuwa akiitazama Tottenham kwa ajili ya Bale ukiachilia mbali Ronaldo na Messi ambao ndio wachezaji anaowahusudu duniani kwa hivi sasa. Zidane ameendelea kufafanua kwa kummwagia sifa Bale kwamba ni mchezaji aliyekamilika na amekuwa akifunga mabao mazuri na muhimu ana kasi, mbunifu na anavutia kumtizama.

RIBERY AKIRI FURAHA ILIMFANYA KWENDA NALO KITANDANI KOMBE LA LIGI YA MABINGWA ULAYA.

WINGA machachari wa klabu ya Bayern Munich, Franck Ribery amebainisha kuwa alichukua Kombe la Ligi ya Mabingwa na kwenda nalo kitandani kufuatia ushindi wa timu yao wa mabao 2-1 dhidi ya Borussia Dortmund. Bayern wamefanikiwa kutinga fainali ya michuano hiyo mara tatu katika kipindi cha  miaka minne lakini walifanikiwa kushinda taji hilo kwa mara ya kwanza toka mwaka 2001 kwa ushindi waliopata katika Uwanja wa Wembley Jumamosi. Na Ribery alibainisha hilo katika sherehe za kulitembeza kombe hilo mtaani huko Ujerumani kwamba alichukua kombe hilo na kwenda nalo nyumbani. Nyota huyo raia wa Ufaransa amesema alikuwa macho mpaka alfajiri na baadae kwenda kulala akiwa na mke wake pamoja na kombe hilo. Bayern sasa wana nafasi ya kushinda matatu matatu kwa mkupuo kama wakifanikiwa kushinda taji la DFB Pokal Juni mosi mwaka huu.

BENITEZ ATAKA KUFUNDISHA TIMU INAYOSHIRIKI CHAMPIONS LEAGUE.

MENEJA wa muda wa klabu ya Chelsea, Rafael Benitez amekiri kuwa anataka kufundisha timu inayoshiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao baada ya kumaliza kazi yake katika klabu hiyo. Katika kipindi kifupi kijacho Benitez ataondoka Stamford Bridge akiwa ameisimamia klabu hiyo kwa mara ya mwisho Jumamosi iliyopita wakati walipochapwa na Manchester City katika mchezo wa kirafiki uliofanyika jijini New York Marekani. Kocha huyo raia wa Hispania aliiongoza Chelsea kushinda taji la Europa League na pia kuwasaidia kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwimu ujao baada ya kuajiriwa kwa muda mfupi kuziba nafasi ya Roberto Di Matteo Novemba mwaka jana. Banitez anaondoka Chelsea kumpisha Jose Mourinho na kocha huyo sasa anaweza kuangalia mstakabali wake huko mbele baada ya kuhusishwa na tetesi za kwenda Napoli na Paris Saint-Germain ambapo klabu zote hizo zinakidhi matakwa yake ya kushiriki Ligi ya Mabingwa.

MARCEDES KUFANYIWA UCHUNGUZI NA FIA WAKITUHUMIWA KUFANYA MAJARIBIO YA KIUFUNDI KINYUME CHA UTARATIBU.

TIMU ya Marcedes inakabiliwa na uchunguzi kutoka kwa chama kinachosimamia mbio za magari yaendayo kasi ya langalanga-FIA baada ya kutuhumiwa kujaribu matairi yao kinyume cha utaratibu. Timu za Red Bull na Ferrari zilipelekea malalamiko hayo katika michuano ya Monaco Grand Prix baada ya kugundua matairi yanayotengenezwa na kampuni ya Pirelli yanayotumiwa na Mercedes yalifanyiwa majaribio kwa siku tatu. Kwenye sheria za mashindano hayo msimu ukishaanza majaribio huwa hayaruhusiwi labda kwa madereva chipukizi au kwa kiwango kilichowekwa ambacho ni kilometa 1,000 lakini Pirelli wamedai kuwa wana mkataba na FIA unaowaruhusu kufanya majaribio kwa kiwango. Hata hivyo Red Bull na Ferrari wamedai kuwa sheria inasema kama utafanya majaribio kwa kiwango hicho kilichowekwa inabidi utumie aina ya gari ambalo limeshatumika kwa zaidi ya miaka miwili lakini Marcedes wao walitumia gari lao jipya lilitoka 2013 pamoja na madereva wao nyota Lewis Hamilton na Nico Rosberg. Timu pinzani na Marcedes zimefikia hatua kwasababu majaribio kama hayo ya ziada yanaweza kuwapa faida ya kiufundi hivyo kuwawezesha kufanya vizuri zaidi.

Sunday, May 26, 2013

MSIMU UJAO NITAKUJA IMARA ZAIDI - KLOPP.

MENEJA wa klabu ya Borussia Dortmund, Jurgen Klopp ameapa kuimarisha kikosi chake na kufikia fainali nyingine ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kipigo walichopata dhidi ya Bayern Munich. Dortmund walipoteza mchezo huo ulizikutanisha timu zote kutoka Ujerumani kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Wembley baada ya bao la dakika za mwisho lililofungw ana Arjen Robben. Lakini kocha huyo ametamba kuwa pamoja na kushindwa katika fainali hiyo ya Wembley lakini anaamini atafikia fainali nyingine katika kipindi kifupi kijacho. Klopp amesema kwasasa ana kazi kubwa ya kuimarisha kikosi chake baada ya wachezaji kadhaa tegemeo kutaka kuondoka mwishoni mwa msimu huu lakini anaamini mpaka kufikia msimu mpya tayari atakuwa na kikosi imara. Kiungo tegemeo wa klabu hiyo Mario Gotze tayari imeshathibitishwa kwenda Bayern Msimu ujao huku mshambuliaji wake nyota Robert Lewandowski naye akijipanga kuelekea huko. 


PICHA MBALIMBALI ZINAONYESHA WACHEZAJI WA BAYERN NA VIONGOZI WAKILA BATA KWA RAHA ZAO BAADA YA KUNYAKUWA TAJI LA LIGI YA MABINGWA ULAYA.







AGUERO AJITIA KITANZI CITY MPAKA 2017.

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Manchester City, Sergio Aguero ameongeza mkataba wa mwaka mmoja ambao utamuweka katika klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu nchini Uingereza mpaka mwaka 2017. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Argentina mwenye umri wa miaka 24 amefunga mabao 12 katika mechi 30 za ligi alizocheza msimu uliopita na kufunga bao la ushindi dhidi ya Queens Park Rangers lililowapa taji la ligi katika msimu wa 2011-2012. Mara baada ya kusaini mkataba huyo Aguero aliuambia mtandao wa klabu hiyo kwamba anajisikia furaha na kuhitajika hivyo atafanya kila awezalo ili aendelee kufanya kazi vyema na kuipa mataji klabu hiyo. Vyombo vya habari nchini Uingereza vilikuwa vikiripoti kuwa mchezaji huyo anaweza kutimkia Real Madrid lakini tetesi hizo zitakwisha baada ya kuwa mchezaji mwingine wa timu hiyo kuongeza mkataba baada ya Gael Clichy, Yaya Toure na David Silva kufanya hivyo.

SUALA LA KUONDOKA KWANGU HALIHUSIANI NA MASUALA YA FEDHA - ANCELOTTI.

MENEJA wa klabu ya Paris Saint-Germain-PSG, Carlo Ancelotti amesisitiza kuwa ombi lake la kuondoka klabuni hapo ni suala la binafsi na halihusiani na mambo ya kifedha. Akiongea kabla ya mechi ya mwisho ya Ligi Kuu nchini Ufaransa maarufu kama Ligue 1 dhidi ya Lorient, Ancelotti aliongeza kuwa hajazungumza na klabu yoyote toka aweke wazi kutaka kwake kuondoka mwishoni mwa wiki iliyopita. Kocha huyo aliendelea kusema kuwa uamuzi wa kutaka kuondoka ni wa binafsi zaidi na hauhusiani na mtu au kiongozi yoyote ndani ya klabu hiyo na pia siyo suala la fedha. Anceloti Jumapili iliyopita alibainisha kuwa kuna uwezekano akaelekea kuifundisha klabu ya Real Madrid baada ya Jose Mourinho kutangazwa kuondoka mwishoni mwa msimu lakini klabu hiyo imeonekana haitaki kumuachia kocha huyo. Hata hivyo Ancelotti amesisitiza kuwa hakuna chochote kilichoongelewa kwa wiki hii na mambo yote yapo kama yalivyozungumzwa wiki iliyopita.

TAIFA STARS KWENDA ADDIS ABABA LEO.

TIMU ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inatarajia kuondoka leo (Mei 26 mwaka huu) usiku kwenda Addis Ababa, Ethiopia ambapo itaweka kambi na kucheza mechi moja ya kirafiki kabla ya kwenda Morocco. Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itaondoka saa 5 usiku kwa ndege ya EgyptAir ikiwa na kikosi cha wachezaji 21 chini ya nahodha wake kipa Juma Kaseja. Timu hiyo ikiwa Ethiopia, Juni 2 mwaka huu itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Sudan ambapo siku inayofuata itaondoka kwenda Marrakech, Morocco kwa kupitia Cairo, Misri. Mechi hiyo ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya wenyeji Morocco itachezwa Juni 8 mwaka huu jijini Marrakech.
Mbali ya nahodha Kaseja, wachezaji wengine wanaoondoka katika kikosi hicho ambacho kina wiki sasa tangu kingie kambini jijini Dar es Salaam ni Mwadini Ally na Ally Mustafa ambao wote ni makipa. Wengine ni Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Aggrey Morris, Haroub Nadir, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vicent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd na Haruni Chanongo. Wachezaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu ambao wako na timu yao ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo watajiunga moja kwa moja na Stars jijini Marrakech, Juni 4 mwaka huu wakitokea Maputo, Msumbiji mara baada ya mechi yao ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Liga Muculumana ya huko. Katika msafara huo wa Ethiopia benchi la ufundi la Stars linaundwa na Kim Poulsen (Kocha Mkuu), Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi),Juma Pondamali (Kocha wa makipa), Leopold Tasso (Meneja wa timu), Dk. Mwanandi Mwankemwa (Daktari), Frank Mhonda (Mtaalamu wa tibamaungo) na Alfred Chimela (Mtunza vifaa).

WACHEZAJI WA TOTTENHAM HOTSPURS NA KOCHA WAO AVB WAKILA BATA KUPUNGUZA MACHUNGU YA KUKOSA LIGI YA MABINGWA BARANI ULAYA HUKO BAHAMAS.



SISI NI KIZAZI CHA DHAHABU CHA BAYERN - LAHM.

BEKI wa kati wa kimataifa wa Ujerumani na klabu ya Bayern Munich, Philipp Lahm anaamini kuwa ushindi wa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya unakifanya kikosi cha timu hiyo kuwa kizazi cha dhahabu. Bayern ambao wanajulikana pia kama The Bavarians walishindwa mara mbili katika hatua ya fainali ya michuano hiyo katika kipindi cha misimu mitatu iliyopita lakini bao la ushindi la dakika ya 89 lililofungwa na Arjen Robben liliwahakikishia ushindi mabao 2-1 dhidi ya wajerumani wenzake Borussia Dortmund. Lahm anaamini ushindi huo waliopata katika Uwanja wa Wembley utakuwa chachu ya kufanya vizuri zaidi katika mchezo wao mwingine wa fainali ya Kombe la Ujerumani itakayofanyika Juni mosi katika Uwanja wa Allianz Arena huku tayari wakiwa wameshanyakuwa taji la Bundesliga. 
Nyota huyo aliendelea kusema kuwa kama mchezaji unahitaji kuweno katika kizazi cha dhahabu unatakiwa kushinda mataji makubwa na anashukuru walifanya hilo jana.

NEYMAR KUSAINI MKATABA WA MIAKA MITANO BARCELONA.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Brazil, Neymar amesema kuwa anatarajia kusaini mkataba wa miaka mitano na klabu ya Barcelona ya Hispania Jumatatu. Neymar alichagua Barcelona na kuwatema mahasimu wao Real Madrid baada ya klabu yake ya Santos kumaliza utata wa kumng’ang’ania mchezaji huyo kwa kipindi cha miaka mitatu na kumwachia kuondoka kabla ya michuano ya Kombe la Dunia 2014. Nyota huyo alithibitisha hayo katika ukurasa wake wa mtandao wa Instagram na Twitter kwamba atasaini mkataba wa miaka mitano kesho huku klabu ya Santos kwenye ukurasa wake wa facebook na katika mtandao wa Barcelona wote wakithibitisha uamuzi huo wa Neymar. Neymar aliongeza kuwa familia na marafiki zake tayari wote wanajua kuhusiana na uamuzi wake huku akiwashukuru mashabiki wa Santos kwa kuwa pamoja naye katika kipindi cha miaka tisa ambayo amekuwepo hapo.

Saturday, May 25, 2013

ADEBAYOR AITWA TOGO.

KOCHA wa timu ya taifa ya Togo, Didier Six amemuita mshambualiaji nyota na nahodha wan chi hiyo Emmanuel Adebayor katika kikosi chake ambacho kinakabiliwa na mechi za kufuzu michuano ya Kombe la Dunia dhidi ya Cameroon Juni 9 na Libya Juni 16 mwaka huu. Mshambuliaji huyo anayecheza katika klabu ya Tottenham Hotspurs hakutokea mara ya mwisho alipoitwa na kocha huyo kwa ajili ya mchezo dhidi ya Cameroon uliochezwa Machi mwaka huu. Adebayor amekuwa katika mzozo na kocha huyo raia wa Ufaransa ambaye amedai kuwa ndio alikuwa chanzo cha nchi hiyo kung’olewa katika michuano ya Mataifa ya Afrika yaliyofanyika Afrika Kusini 2013. Six pia amemuita golikipa Kossi Agassi ambaye amekuwa katika mzozo na Shirikisho la Soka nchini humo kuhusiana na masuala ya posho. Togo kwasasa inashika nafasi ya pili katika kundi I wakipisha alama moja na Cameroon ambao wanaongoza kundi hilo wakifuatiwa na Libya alama tano na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo alama nne.