Tuesday, May 28, 2013

CAXIROLA MARUFUKU CONFEDERATION CUP.

WARATIBU wa michuano ya Kombe la Shirikisho linalotarajiwa kuanza mwezi ujao wamepiga marufuku kutumika kwa vyombo vya plastiki mfano wa vuvuzela kwa sababu za kiusalama. Ofisa mmoja wa kamati ya maandalizi ya michuano hiyo Medeiros Hilario amesema mashabiki watakaohudhuria michuano hiyo hawataruhusiwa kuingia na kifaa chochote cha muziki ikiwemo vyombo hivyo vya plastiki ambavyo kwa huko huitwa caxirola. Kufungiwa kwa vyombo hivyo kutaanza rasmi Jumapili wakati wa mchezo wa kirafiki kati ya Brazil na Uingereza utakaochezwa katika Uwanja wa Maracana jijini Rio de Janeiro. Uamuzi wa kufungia vifaa hivyo umekuja kufuatia tukio la Aprili 28 mwaka huu ambapo mashabiki waliokuwa wamebeba caxirolas katika mchezo wa kati ya klabu ya Bahia na Vitoria kuanza kuzirusha uwanjani baada ya kukasirishwa na matokeo ya upande mmoja. Caxirola ndio kifaa rasmi kinachotambulika na kutumika katika michuano ya Kombe la Dunia 2014 ambapo Brazil watakuwa wenyeji na kilitambulishwa na rais wa nchi hiyo Dilma Rousseff mwezi uliopita.

No comments:

Post a Comment