Tuesday, December 31, 2013

WENGER MAJERUHI WAMUWEKA KATIKA HALI NGUMU.

KLABU ya Arsenal inakabiliwa na balaa la majeruhi wakati wakielekea katika mchezo wao wa mwaka mpya dhidi ya Cardiff City baada ya wachezaji wanne kuondolewa katika orodha ya kikosi kitakachoanza katika mchezo huo. Meneja wa klabu hiyo Arsene Wenger amethibitisha kuwa Olivier Giroud, Aaron Ramsey, Mesut Ozil na Kieran Gibbs hawatakuwepo katika mchezo huo wakati Theo Walcott, Tomas Rosicky, Thomas Vermaelen na Jack Wilshere nao wakiwa katika hati hati ya kucheza. Kwa upande mwingine Wenger amethibitisha kuwa wanatafuta mchezaji muhimu katika kipindi cha usajili wa dirisha dogo huku safu ya ushambuliaji ikipewa nafasi kubwa. Giroud ambaye amekuwa mshambuliaji tegemeo katika kipindi kirefu msimu huu alikaririwa karibuni akidai kuwa klabu hiyo haitaji mshambuliaji mwingine pamoja na yeye kushindwa kufunga mabao mengi.

MESSI AHOFIA MAJERUHI.

MSHAMBULIAJI nyota wa Barcelona, Lionel Messi amesema kuwa mwaka ujao anategemea kuepuka majeruhi tofauti ilivyokuwa kwa mwaka huu. Mwaka huu umekuwa sio mzuri kwa Messi baada ya kusumbuliwa na mejeruhi ya mara kwa mara huku akiwa amekaa nje toka mwezi Novemba kwa majeraha ya msuli. Barcelona imekuwa ikihaha kutokana na kumkoa nyota huyo kwa kufungwa na Ajax Amsterdam katika Ligi ya Mabingwa barani Ulaya na Athletic Bilbao katika La Liga lakini sasa inaweza kupumua baada ya Messi kutegemewa kurudi baada ya mapumziko ya majira ya baridi. Akihojiwa na mtandao wa timu hiyo, Messi amesema baada ya kusheherekea sikukuu za mwisho wa mwaka na familia yake atasafiri kuelekea jijini Barcelona kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kabla ya kurejea uwanjani.

HALI YA SCHUMACHER BADO TETE.

FAMILIA ya dereva nguli wa mashindano ya langalanga, Michael Schumacher imeendelea kuwa pembeni ya kitanda cha wakati akipigania maisha yake kufuatia ajali aliyopata wakati akiteleza katika barafu katika milima ya Ufaransa. Meneja wa dereva huyo Sabine Kehm amesema mke Corinna, binti yake Gina Maria na kijana wake wa kiume Mick bado wameendelea kubakia katika hospitali ya Grenoble ili kujua hatma ya mpendwa wao. Schumacher ambaye ambaye ni bingwa wa dunia mara saba wa mashindano ya langalanga alipata majeraha ya kichwani wakati alipoanguka kwenye tukio hilo. Mkuu wa hospitali hiyo profesa Jean-Francois Payen amesema nyota huyo bado ameendelea kubakia katika wodi ya watu wanaohitaji uangalizi maalumu huku akiwa amepewa dozi nzito za usingizi ili ubongo wake uweze kujitibu taratibu baada ya upasuaji.

MPUTU AACHWA KIKOSI CHA CHAN.

KOCHA wa timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC, Mutumbile Santos ametaja kikosi chake kitakachoshiriki michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani mwakani huku akimuacha Tresor Mputu ambaye amejiunga na klabu ya Kabuscorp ya Angola akitokea TP Mazembe. Hakuna sababu yoyote iliyotolewa ya kuachwa kwa mshambuliaji huyo ingawa hata hivyo amekuwa akitishia kutojumuika na kikosi hicho kama baadhi ya mambo ya kimaslahi hayatarekebishwa. Mputu ndio aliteuliwa kuwa mchezaji bora wa mashindano hayo mwaka 2009 ambapo nchi yake ilinyakuw ataji hilo. Ni wachezaji wawili pekee waliokuwepo katika kikosi cha mwaka 2009 ndio watashiriki michuano hiyo itakayofanyika Januari nchini Afrika Kusini.

RAIS WA IOC AMTUMIA SALAMU ZA RAMBIRAMBI RAIS PUTIN.

RAIS wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki-IOC, Thomas Bach amesema ana uhakika kuwa Urusi itaandaa michuano ya olimpiki ya majira ya baridi jijini Sochi iliyokuwa salama. Bach alimtumia salamu za rambirambi Rais Vladimir Putin kufuatia mashambulio ya mabomu ya kujitoa muhanga katika treni na basi matukio ambayo yamepelekea vifo vya watu 31. Matukio hayo yametokea ukiwa umebaki mwezi mmoja pekee kabla ya kuanza michuano hiyo. Bach amesema matukio hayo hayakubaliki na hayawezi kurudisha nyuma dhamira ya nchi hiyo kuwa mwenyeji wa michuano hiyo ambapo kwa pamoja wanaweza kumshinda adui.

BAYERN INAWEZA KUTAWALA SOKA LA ULAYA KWA MIAKA 10 ZAIDI - HEYNCKES.

MENEJA wa zamani wa klabu ya Bayern Munich ya Ujerumani Jupp Heynckes amedai kuwa timu hiyo inaweza kutawala soka barani Ulaya kwa miaka 10 mingine. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 68 ambaye aliiongoza Bayern kushinda mataji msimu uliopita amesema kikosi hicho ambacho hivi sasa kinanolewa na Pep Guardiola kinaweza kuendelea kutawala soka la Ulaya kwa muongo mmoja zaidi. Heynckes amesema kwa jinsi kikosi hicho kilivyokuwa na wachezaji chipukizi hakuna shaka kwamba wataendelea kutamba kwa kipindi kirefu huko mbele. Kocha huyo alichagua kustaafu kufundisha soka baada ya kuinoa Bayern pamoja na kupata ofa kutoka timu mbalimbali barani Ulaya.

Monday, December 30, 2013

WILLIAMS NDIO ANAYENIFANYA NI BORA - AZARENKA.

MWANADADA nyota katika tenisi Victoria Azarenka wa Belarus anafikiri hasimu wake Serena Williams wa Marekani ndio anamfanya awe mchezaji bora ambapo wanatarajia kukutana tena katika michuano ya kimataifa ya Brisbane na baadae michuano ya wazi ya Australia. Azarenka anayeshika nafasi ya pili katika orodha za ubora duniani atakutana na Williams anayeshika nafasi ya kwanza kama wachezaji hao wakifanikiwa kufika fainali ya michuano hiyo inayotarajiwa kuchezwa mwishoni mwa wiki ijayo katika uwanja wa Pat Rafter jijini Abu Dhabi. Akihojiwa Azarenka mwenye umri wa miaka 24 amesema ni jambo jema kuwa na hasimu kama Williams kwasababu inamjenga kama mchezaji kutokana na mazoezi ya nguvu anayofanya ili aweze kumudu kupambana na yoyote. Azarenka na Williams wamekuwa mahasimu kwa muda lakini ni Williams ndio mwenye rekodi nzuri zaidi baada ya kushinda mechi 13 dhidi ya tatu za Azarenka walizokutana.

MOYES AIKUMBUKA KOMBINESHENI YA VAN PERSIE NA ROONEY.

MENEJA wa klabu ya Manchester United, David Moyes anategemea washambuliaji wake Robin van Persie na Wayne Rooney kuwa fiti mwaka mpya baada ya nyota huyo wa kimataifa wa Uholanzi kuanza mazoezi mepesi. Van Persie amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya paja, kidole gumba na kiuno msimu huu na majeraha yake ya hivi karibuni aliyapata wakati akipiga mpira wa kona katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya dhidi ya Shakhtar Donetski. Moyes ambaye ameshuhudia kikosi chake kikipata ushindi wa sita mfululizo katika mashindano yote amesema Van Persie tayari ameanza mazoezi mepesi hivyo anaweza kurejea uwanjani hivi karibuni. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa siku nyingi hawajashuhudia Van Parsie na Rooney wakicheza pamoja hivyo itakuwa vyema wakikutana tena ili kuongeza nguvu katika safu yake ya ushambuliaji.

BOATENG ALAZWA BAADA YA KUSHAMBULIWA CHRISTMAS.

KIUNGO wa klabu ya Schalke 04, Kevin-Prince Boateng amelazwa hospitalini baada ya kushambuliwa siku ya Christmas. Nyota huyo wa kimataifa wa Ghana mwenye umri wa miaka 26 aliumia mbavu, mgongo na shingo wakati wa tukio hilo lililotokea katika mji wa Kaarst ulio karibu na jiji la Dusseldorf. Taarifa ya polisi ilidai kuwa Boateng alishambuliwa na mtu ambaye hakujulikana mara moja wakati akikatiza katika mitaa ya mji huo. Boateng alijiunga na Schalke kutoka AC Milan kwa ada ya euro milioni 12 Agosti mwaka huu.

SCHUMACHER TAABANI BAADA YA KUPATA AJALI AKITELEZA KATIKA BARAFU.

DEREVA nyota wa zamani wa mashindano ya langalanga kutoka Ujerumani, Michael Schumacher yuko katika hali mbaya baada ya kupata ajali wakati akiteleza katika barafu huko Ufaransa. Schumacher mwenye umri wa miaka 44 ambaye ni bingwa wa dunia mara saba wa langalanga alijibamiza kichwa katika jiwe alipoanguka wakati akiteleza ambapo sasa anatumia mashine maalumu akiwa hajitambui baada ya kufanyiwa upasuaji wa ubongo. Meneja wake, Sabine Kehm amesema Schumacher ambaye alikuwa na mwanae wa kiume wakati wa tukio hilo alikuwa amevaa kofia ngumu wakati alipojibamiza kichwa katika jiwe. Schumacher alichukuliwa na helikopta kutoka katika milima ya Ufaransa alipopata ajali hiyo na kuwahishwa katika kituo cha afya cha karibu lakini baadae alihamishwa katika hospitali ya Chuo Kikuu cha Grenoble ambayo ina vifaa vingi na kisasa zaidi.

MAN CITY NDIO WENYE NAFASI YA KUNYAKUWA TAJI LA LIGI KUU - MOURINHO.

MENEJA wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho anafikiri kuwa Manchester City bado ndio wenye nafasi ya kunyakuwa taji la Ligi Kuu nchini Uingereza pamoja na ushindi wa timu yake dhidi ya Liverpool. Kikosi cha Mourinho kilifanikiwa kutoka nyuma na kufanikiwa kuibuka na ushindi muhimu wa mabao 2-1 yaliyofungwa na Eden Hazard na Samuel Eto’o huku bao la Liverpool likifungwa na Martin Skrtel. Chelsea sasa wamefanikiwa kupata ushindi wao wan ne mfululizo katika Ligi Kuu huku wakiingia mwaka 2014 wakiwa nyuma kwa alama mbili mbele ya vinara Arsenal lakini Mourinho anaamini kuwa City wanaoshika nafasi ya pili ndio tishio zaidi katika mbio hizo. Mourinho amesema kuna tofauti kubwa kati ya City na timu zingine na sio ubora kwasababu timu zingine zina ubora pia lakini ni ukomavu, nguvu na uzoefu wa wachezaji ndio unawatofautisha na timu zingine.

Friday, December 27, 2013

BOATENG ASHAMBULIWA MTAANI HUKO UJERUMANI.

POLISI nchini Ujerumani wanachunguza madai ya kushambuliwa kwa kiungo wa kimataifa wa Ghana Kevin-Prince Boateng siku ya Christmass baada ya mabishano humo Kaarst. Polisi wa mji wa Dusseldorf wamethibitishia wana habari kuwa mtu huyo mwenye umri wa miaka 26 aliyehusika katika tukio hilo ni Boateng ambaye anacheza katika klabu ya Schalke 04. Taarifa hiyo ya polisi ilidai kuwa Boateng ambaye ni mkazi wa Meerbusch alishambuliwa na mtu asiyejulikana wakati akikatiza mtaani. Nyota huyo ambaye anaripotiwa kuumia kidogo, alirejea nyumbani baada ya tukio hilo na kisha kupiga simu polisi.

UTEAUZI WANGU NI KAMA KAMARI - SHERWOOD.

TIM Sherwood amekiri kuwa uteuzi wake kama kocha mkuu wa Tottenham Hotspurs ni uamuzi wa hatari uliochukuliwa na mwenyekiti Daniel Levy. Akizungumza mara baada ya timu hiyo kutoka sare ya bao 1-1 na West Bromwich ukiwa ni mchezo wake wa kwanza toka apate kibarua hicho, Sherwood amesema uteuzi wake ni kama kamari kwasababu hajawahi kufanya kazi kama kocha mkuu. Pamoja na hayo lakini Sherwood anaamini kuwa anaweza kupata mafanikio kwasababu wako wengi walioanza kama yeye na baadae kufanikiwa. Sherwood alipewa kibarua hicho Jumatatu akichukua nafasi ya Andres Villas-Boas aliyetimuliwa wiki iliyopita.

MOYES ATAMBA UNITED KUTETEA TAJI LAKE.

MENEJA wa klabu ya Manchester United, David Moyes ametamba kuwa kikosi chake kinaweza kutetea taji lao la Ligi Kuu nchini Uingereza baada ya kushinda mchezo wao dhidi ya Hull City kwa mabao 3-1. United walijikuta wakiwa nyuma kwa mabao 2-0 ndani ya dakika 15 za kwanza mchezo huo uliochezwa katika Uwanja wa KC lakini walipambana na kuhakikisha wanasawazisha na baadae kuongeza lingine na kuondoka na alama zote tatu. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo Moyes amesema kuwa nyuma na baadae kupata matokeo ya ushindi ni jambo hakulitegemea lakini wachezaji wake wameshawahi kufanya hivyo huko nyuma. Moyes amesema watajitahidi kadri ya uwezo wao kujaribu kupunguza pengo la alama katika msimamo wa ligi kwasababu anaamini bado wana nafasi ya kutetea taji lao.

RAMSEY KUSUGUA BENCHI MPAKA MWAKANI KUTOKANA NA MAJERUHI.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amebainisha kuwa kiungo wake mahiri Aaron Ramsey atakosa mechi zote za kipindi hiki cha sikukuu baada ya kupata majeruhi katika mchezo walioshinda kwa mabao 3-1 dhidi ya West Ham United jana. Nyota huyo wa kimataifa wa Wales atakosa mchezo wa ugenini dhidi ya Newcastle United Jumapili na pia mchezo mwingine utakaochezwa katika Uwanja wa Emirates dhidi ya Cardiff City mwaka mpya. Wenger aliwaambia waandishi wa habari kuwa Ramsey ameumia msuli wa paja na hajui ni kipindi gani atakaa nje ila anafahamu hataweza kucheza tena katika kipindi cha sikukuu kilichobakia. Kocha huyo pia alikisifu kikosi chake kwa mchezo mzuri ambao uliwawezesha kutoka nyuma na kushinda mchezo huo muhimu na kuwafanya kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu nchini Uingereza.

MURRAY ALA KICHAPO ABU DHABI.

MCHEZAJI nyota wa tenisi kutoka Uingereza Andy Murray amejikuta akikubali kipigo kutoka kwa Jo-Wilfried Tsonga wa Ufaransa katika michuano ya ya dunia ya tenisi inayofanyika jijini Abu Dhabi. Hiyo ni mara ya kwanza kwa Murray kurejea tena uwanjani toka alipofanyiwa upasuaji wa mgongo miezi mitatu iliyopita. Murray anayeshika nafasi ya nne katika orodha za ubora dunia na bingwa wa michuano ya Wimbledon alijikuta akifungwa seti 2-0 zenye alama za 7-5 6-3 na Tsonga nayeshika nafasi ya 10 katika orodha katika michuano hiyo ya maonyesho. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo Murray alijitetea kuwa uwanja ulikuwa unafanya mpira kwenda kasi sana na kukiri kuwa Tsonga alikuwa katika kiwango kizuri kuliko yeye katika mchezo huo. Michuano inayofahamika kwa jina la Mubabala inatarajiwa kuendelea tena leo ambapo Rafael Nadal anayeshika namba moja atachuana na Mhispania mwenzake David Ferrer.

Tuesday, December 24, 2013

UFARANSA KUJIPIMA NGUVU MECHI TATU KABLA YA KWENDA BRAZIL.

TIMU ya taifa ya Ufaransa inatarajiwa kuchezwa mechi tatu za kimataifa za kirafiki kabla hawajaondoka kuelekea nchini Brazil kushiriki michuano ya Kombe la Dunia. Shirikisho la Soka la nchi hiyo limedai kuwa timu hiyo itacheza mchezao wake wa kwanza wa kirafiki huko Stade de France mei 27 huku michezo mingine ikichezwa katika miji ya Nice Juni mosi na Lille Juni 8. Majina ya timu watakazopimana nazo nguvu yanatarajiwa kutolewa mapema mwakani. Ufaransa imepangwa kundi F sambamba na timu za Switzerland, Ecuador na Honduras.

PETROVA AJITOA AUSTRALIA OPEN.

MCHEZAJI nyota wa tenisi, Nadia Petrova wa Urusi amejitoa katika michuano ya wazi ya Australia inayotarajiwa kuchezwa mapema mwakani kufuatia kifo cha mama yake kilichotokana na ajali ya gari. Mama yake Petrova aitwaye Nadezhda Illyina alikuwa mwanariadha ambaye aliwahi kushinda medali ya shaba katika mbio za mita 400 kupokezana vijiti katika michuano ya olimpiki iliyofanyika jijini Montreal mwaka 1976. Mrusi mwenzake Maria Kirilenko ambaye anashika namba 19 katika orodha za ubora duniani naye amjitoa kutokana na majeruhi. Kujitoa kwa Petrova kunamaanisha kuwa Tsevetana Pironkova mwenye umri wa miaka 26 raia wa Bulgaria atachukua nafasi hiyo katika droo kubwa ya michuano hiyo.

MWAKANI NITATISHA ZAIDI - RONALDO.

MSHAMBUIAJI nyota wa klabu ya Real Madrid, Cristiano Ronaldo amefunga mabao 69 katika kipindi cha miezi 12 iliyopita lakini nyota huyo anafikiri kuwa kuna vitu vizuri zaidi vinakuja. Ronaldo mwenye umri wa miaka 28 amevunja rekodi kadhaa mwaka huu lakini mwenyewe amedai kuwa anaweza kucheza kwa kiwango cha juu zaidi mwakani. Mbali na rekodi pamoja na tuzo mbalimbali alizoshinda mwaka huu nyota huyo pia amejumuishwa katika orodha ya mwisho ya wachezaji watakaogombea tuzo ya Ballon d’Or mwakani. Ronaldo pia aliibeba timu yake ya taifa ya Ureno kufuzu hatua ya mtoano ya michuano ya Kombe la Dunia kwa kufunga mabao yote kwenye ushindi wa mabao 4-2 waliopata dhidi ya Sweden Novemba. Lakini pamoja na hayo yote nyota huyo aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa facebook kuwa mwaka 2013 ulikuwa mzuri kwake lakini mwaka ujao utakuwa mzuri zaidi.

WENGER ALIA KUNYIMWA PENATI.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger anaamini kuwa timu yake ilistahili kupewa penati kwa asilimia 100 baada ya kupata sare ya bila ya kufungana na Chelsea katika Uwanja wa Emirates jana usiku. Kauli hiyo ya Wenger imekuja kufuatia winga wake Theo Walcott kuangushwa na Willian katika eneo la hatari dakika ya 36 lakini mwamuzi wa mchezo huo Mike Dean alikataa kuwa adhabu. Wenger anaamini kama mwamuzi angewapa penati hiyo hakuna shaka hali ya mchezo ingebadilika na kuweza kuibuka na alama zote tatu. Akihojiwa Wenger amesem hana shaka katika mawazo yake kwamba ile ilikuwa ni penati ya wazi lakini hajui kwanini mwamuzi aliwakatalia. Wakati huohuo meneja wa Chelsea Jose Mourinho alimnanga Wenger kuwa aache kulalamika sana kwani mchezo wa soka lazima watu wagusane hivyo haoni tatizo kama mwamuzi hakuona kosa lililofanywa na Willian.

Monday, December 23, 2013

MECHI YA MTANI JEMBE YAINGIZA MIL 422/-.

MECHI ya Nani Mtani Jembe kati ya Yanga na Simba iliyochezwa juzi (Desemba 21 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 imeingiza sh. 422,611,000. Mapato hayo ni kutokana na washabiki 52,589 waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 40,000. Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo walikuwa 19,044. Asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa kutokana na mapato hayo ni sh. 64,466,084.75 wakati gharama za kuchapa tiketi ni sh. 7,488,000. Mgawo mwingine ilikuwa kama ifuatavyo; kila klabu imepata sh. 117,470,066.61, asilimia 15 ya uwanja ni sh. 52,598,537.29, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 35,065,691.53 wakati gharama za mchezo zilikuwa sh. 28,052,553.22.

MPUTU AONDOKA TP MAZEMBE.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC, Tresor Mputu ameikacha klabu yake ya TP Mazembe na kuhamia kwa mabingwa wa soka nchini Angola timu ya Kabuscorp. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 28 alitangazwa mbele ya waandishi wa habari jijini Luanda kuwa amesaini mkataba wa mwaka mmoja wenye thamani ya euro milioni mbili ambao utamuwezesha kukunja kitita cha euro 40,000 kwa mwezi. Mashabiki wa Mazembe wamekuwa wakipinga kuondoka kwa nyota huyo hatua ambayo imepelekea uongozi wa Mazembe kutoa taarifa ya kuwa kuondoka kwake hakutaathiri kiwango cha timu hiyo. Mputu ameitumikia Mazembe kwa miaka 10 akiisaidia timu hiyo kushinda taji la Klabu Bingwa barani Afrika mwaka 2009 na 2010 pamoja na kuweka historia ya kufika fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Duniani ambapo walifungwa na Inter Milan kwa mabao 3-0 mwaka 2010. Timu ya Kabuscorp ilitengeneza vichwa vya habari Januari mwaka jana wakati walipomsajili mshambuliaji nyota wa zamani wa Brazil Rivaldo aliyecheza soka nchini humo kwa msimu mmoja pekee.

VAN GAAL AITAMANI TOTTENHAM HOTSPURS.

KOCHA wa timu ya taifa ya Uholanzi, Louis van Gaal amedokeza nia yake ya kuinoa klabu ya Tottenham Hotspurs lakini mpaka baada ya michuano ya Kombe la Dunia 2014. Tim Sherwood ndio amepewa mikoba ya kuinoa kwa muda Tottenham akichukua mikoba ya Andres Villas-Boas lakini kocha huyo amesisitiza kuwa anataka kibarua cha moja kwa moja baada ya kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Southampton. Van Gaal ambaye amewahi kuzinoa Barcelona na Bayerm Munich kwasasa ana mkataba na Uholanzi unaomalizika Julai mwakani lakini amekataa kukubali kunoa timu mbili kwa wakati mmoja. Kocha huyo amesema ni kweli anapenda kufanya kazi katika Ligi Kuu nchini Uingereza lakini hawezi kufanya kazi mbili kwa wakati mmoja hivyo muda wake wa kuondoka Uholanzi utakapofika na bado nafasi ikiwa wazi hakuna shaka kwamba lazima ataomba.

RONALDO SASA WATATU KWA KUPACHIKA MABAO MADRID.

MSHAMBULIAJI wa klabu ya Real Madrid, Cristiano Ronaldo sasa kuna wachezaji watatu pekee mbele yake katika orodha ya wachezaji waliofunga mabao mengi zaidi baada ya kufunga bao katika mchezo dhidi ya Valencia jana. Nyota huyo wa kimataifa wa Ureno amefunga mabao 164 katika mechi 151 na kufikia rekodi ya mshambuliaji wa kimataifa wa Mexico Hugo Sanchez ambaye alifunga mabao 164 katika mechi 207 alizochezea Madrid. Ronaldo sasa amezidiwa na Santillana aliyefunga mabao 186, Alfredo de Stephano aliyefunga mabao 216 na Raul anayeongoza orodha hiyo kwa kufunga mabao 228. Katika mchezo wa jana Madrid walifanikiwa kuinga Valencia kwa mabao 3-2.

BLANC AWAHIMIZA WACHEZAJI WAKE KUTOMTEGEMEA MOJA KWA MOJA IBRAHIMOVIC.

MENEJA wa klabu ya Paris Saint-Germain, Laurent Blanc ameonya kikosi chake kuwa kinatakiwa kuwa makini wanapokuwa mwa adui baada ya kutoka sare ya kufungana mabao 2-2 na Lille. Blanc pia amedai kuwa wahezaji wake hawapaswi kumtegemea moja kwa moja mshambuliaji nyota wa klabu hiyo Zlatan Ibrahimovic. Ibrahimovic alifunga bao la kuongoza kwa timu yake dakika ya 27 lakini Lille walikuja juu na kurudisha bao hilo kupitia kwa Rio Mavuba kabla ya Salomon Kalou hajaongeza lingine huku PSG wakisawazisha kupitia bao la kujifunga la Marko Basa na kupelekea timu hizo kugawana alama moja kila mmoja. Mara baada ya mchezo huo Blanc alikitaka kikosi chake kutowategemea sana Ibrahimovic na Edinson Cavani ambaye alikosa mchezo huo kwasababu binafsi. Blanc amesema pamoja na kufurahishwa na kiwango bora walichokionyesha lakini matokeo hayakumridhisha kwasababu kuna nafasi nyingi walizokosa ambazo kama wangezitumia vyema wangeweza kuibuka na ushindi katika mchezo huo. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa wachezaji wote wanatakiwa kuwa makini pindi wafikapo langoni mwa adui na sio kuwategemea moja kwa moja Ibrahimovic na Cavani.

RIBERY APEWA TUZO NYINGINE NCHINI UJERUMANI.

IKIWA ni chini ya saa 24 baada ya kutajwa kama mchezaji bora wa michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia, Franck Ribery kwa mara nyingine ametajwa kama mchezaji bora wa mwaka nchini Ujerumani. Baada ya pia kushinda tuzo hiyo mwaka 2008, gazeti maarufu la michezo la Ujarumani, Kicker lilimpigia nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa kuwa mchezaji bora wa mwaka kutokana na kiwango alichokionyesha kiwa na Bayern Munich. Ribery anaungana na washindi wengine waliowahi kunyakuwa tuzo hiyo akiwemo kocha wa Borussia Dortmund Jurgen Klopp mwaka 2012 na kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Loew mwaka 2011. Jmamosi iliyopita Ribery mwenye umri wa miaka 30 alichukua tuzo ya mchezaji bora wa michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia baada ya Bayern kuwagaragaza wenyeji kwa Raja Casablanca kwa mabao 2-0 jijini Marrakech na kufanyiwa kunyakuwa taji la nne kwa mwaka huu. Ribery amekuwa mchezaji munimu kwa Bayern kuwa timu ya kwanza ya Ujerumani kushinda mataji matatu likiwemo la Ligi ya Mabingwa, Bundesliga, Kombe la Ujerumani sambamba na UEFA Super Cup.

Sunday, December 22, 2013

TUNAHITAJI MAPUMZIKO - KLOPP.

MENEJA wa klabu ya Borussia Dortmund, Jurgen Klopp amekiri kuwa kikosi chake kinahitaji mapumziko ya majira ya baridi baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka Hertha Barlin jana. Dortmund wamekuwa wakisumbuliwa na majeruhi katika mzunguko wa kwanza wa ligi msimu huu ambapo sasa wako nyuma ya vinara wa Bundesliga Bayerm Munich kwa alama 12. Kipigo hicho cha jana walichopata nyumbani kinakuwa cha tatu mfululizo na Klopp sasa anajipanga kurejesha makali ya timu yake ambayo yamepotea kutokana na majeruhi ya wachezaji yaliyomwandama. Klopp amekiri kuwa wanahitaji mapumziko ili kujipanga na kuangalia mapungufu yao ili waweze kurejea katika kiwango chao.


HAKUNA WA KUIFUNGA ARGENTINA KATIKA MAKUNDI YA KOMBE LA DUNIA - MARADONA.

NGULI wa soka wa Argentina, Diego Armando Maradona ametamba kuwa hakuna nchi yoyote katika kundi lao itakayoweza kuizuia timu ya taifa ya nchi hiyo kusonga mbele katika michuano ya Kombe la Dunia nchini Brazil mwakani. Argentina imepangwa katika kundi F sambamba na nchi za Nigeria, Iran na Bosnia-Herzegovina ambapo nchi hiyo itacheza mechi yake ya ufunguzi dhidi ya Nigeria Juni 25. Maradona amesema sio Nigeria ambao ni mabingwa wa soka barani Afrika wala nchi nyingine yoyote waliopangwa nayo inayoweza kuwazuia kusonga mbele. Nguli huyo aliendelea kudai kuwa Argentina itafanikiwa kunyakuwa taji lake la tatu nchini Brazil ingawa amesema itakabiliwa na vikwazo kutoka kwa nchi za Ujerumani, Uholanzi na wenyeji wa michuano hiyo.

PELLEGRINI AMUOGOPA SUAREZ.

MENEJA wa klabu ya Manchester City, Manuel Pellegrini amekiri kuwa kikosi chake kitakabiliwa na wakati mgumu kumdhibiti Luis Suarez wakati watakapocheza na Liverpool Alhamisi. City wamekwea mpaka katika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu wakiwa nyuma ya Liverpool kwa alama moja baada ya ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Fulham ambao umewafanya kufikisha ushindi mechi nane kati ya tisa walizocheza katika mashindano yote. Hata hivyo safari ya City kuelekea Anfield itawakutanisha na Suarez ambaye yuko katika kiwango cha juu katika upachikaji mabao akiwa ameshafunga mabao 10 katika mechi nne zilizopita na kumfanya kufikisha jumla ya mabao 19 katika mechi 12 za ligi alizocheza. Pellegrini amesema mchezo wao dhidi Liverpool utakuwa mgumu haswa ukizingatia Suarez yko katika kiwango cha juu kabisa hivi sasa.

LIVERPOOL INAWEZA KUTISHA ZAIDI - RODGERS.

MENEJA wa klabu ya Liverpool, Brendan Rodgers anafikiri kikosi chake kinaweza kucheza kwa kiwango cha juu zaidi baada ya kuigaragaza Cardiff City kwa mabao 3-1 na kuweka hai matumaini yao ya kunyakuwa taji la Ligi Kuu nchini Uingereza. Mabao mawili yaliyofungwa na Luis Suarez na kumfanya kufikisha mabao 19 katika ligi msimu huu umeifanya Liverpool kupata ushindi wake wa nne na kuwapeleka kileleni mwa msimamo wa ligi. Rodgers anaamini kikosi chake kinaweza kunyakuwa taji la kwanza la ligi toka mwaka 1990. Kocha huyo amesema kikosi chake kilionyesha kiwango bora katika mchezo dhidi ya Cardiff lakini akatamba bado kuna nafasi ya kuboresha kiwango chao zaidi ya hapo.

MOURINHO AMGWAYA OZIL.

MENEJA wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho amesifu kiwango cha Mesut Ozil toka atue katika Ligi Kuu nchini Uingereza na kudai kuwa ndio kitu klabu ya Arsenal ilikuwa inakikosa ili inyakue taji la ligi. Nyota huyo wa kimataifa wa Ujerumani alitua Arsenal kwa ada ya euro milioni 50 na mpaka sasa ameshafunga mabao manne na kutoa pasi za mwisho saba. Mourinho ambaye amefanya kazi na Ozil kwa miaka mitatu akiwa Real Madrid anafikiri kiungo huyo akiwa sambamba na Aaron Ramsey na Theo Walcott wanaweza kuingoza Arsenal kuwanyakuwa taji. Kocha huyo amesema Ozil ni mmoja wa wachezaji ambaye unamnunua ili aje kuziba pengo katika timu yako na haitaji muda wa kuzoea mazingira kwasababu ni mchezaji aliyekamilika.

Saturday, December 21, 2013

SINA MATUMAINI YA KUITWA KOMBE LA DUNIA - TEVEZ.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Argentina amedai kuwa hana matumaini ya kuitwa katika kikosi cha nchi hiyo kitakachoshiriki michuano ya Kombe la Dunia mwakani. Tevez mwenye umri wa miaka 29 ambae amekuwa katika kiwango kizuri msimu huu ambapo ameifungiwa timu yake ya Juventus mabao 10, amekuwa akiachwa katika kikosi cha nchi yake toka Alejandro Sabella alipotwaa mikoba ya kuinoa Argentina Agosti mwaka 2011. Akihojiwa Tevez amesema kama Sabella hatamwita katika kikosi chake, hana mpango wa kumpigia simu na kumhoji kwanini hajamwita kwasababu anataka aifanye kazi yake kwa weledi. Nyota huyo wa zamani wa vilabu vya Manchester City, Manchester United na West Ham United amesema ana mahusiano mazuri na wachezaji wote wa Argentina pamoja na nahodha wao Lionel Messi, hivyo suala la yeye kuitwa au kutokuitwa ni juu ya kocha mwenyewe. Argentina ambao ni mabingwa wa Kombe la Dunia mwaka 1978 na 1986 wamepangwa kundi F sambamba na timu za Bosnia, Iran na Nigeria.

SEEDORF ATAKUWA KOCHA MZURI KWA MILAN - KAKA.

KIUNGO wa klabu ya AC Milan, Kaka anafikiri kuwa Clarence Seedorf anaweza kuwa kocha mzuri mara atakapoamua kutundika daruga. Kauli hiyo ya Kaka imekuja kufuatia tetesi kuwa Milan imepanga kumchukua Seedorf ili kuziba nafasi ya Massimiliano Allegri mwishoni mwa msimu huu. Kaka ambaye amecheza sambamba na Seedorf kwa miaka sita wakati akiwa Milan anaamini kuwa kiungo huyo abaye kwasasa anacheza klabu ya Botafogo atakuwa mmoja wa makocha bora kabisa duniani siku zijazo. Kaka amesema kila kitu anachofanya Seedorf anafanya kwa uwezo wake na wekedi wa hali ya juu hivyo anadhani atakuwa kocha mzuri ingawa kuna vitu vingi inabidi ajifunze.

HAPATOSHI BUNDESLIGA.

WAKATI vinara wa Bundesliga, Bayern Munich wakikabiliwa na mchezo wa fainali ya Klabu Bingwa ya Dunia baadae leo, mahasimu wao katika ligi Borussia Dortmund na Bayer Leverkusen wataingia uwanjani ili kujaribu kupunguza pengo la alama baina yao. Bayern wanaongoza kwa tofauti ya alama saba katika msimamo wa ligi na wamekuwa tishio kunywakuwa taji hilo tena kama mahasimu wao hao hawatavuna alama wakati wakiwa nchini Morocco. Bayer Leverkusen ambao wanashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi watakuwa wageni wa Werder Bremen baadae leo huku wenyeji wakiwa wana kiu ya ushindi baada ya kuukosa katika mechi tano zilizopita. Kocha wa Bayer ambaye ni nyota wa zamani wa Liverpool, Sami Hyypia amesema hautakuwa mchezo rahisi kwao lakini wanataka kumaliza vyema kwa kuchukua alama zote tatu kabla ya mapumziko ya majira ya baridi. Borussia Dortmund wanaoshika nafasi ya tatu ambao wako nyuma ya Bayern kwa alama 12 na tano kwa Leverkusen, watakuwa wenyeji wa Hertha Berlin wakitafuta ushindi wao wa pili katika mechi tano za ligi walizocheza.

SUAREZ AICHA SOLEMBA ARSENAL BAADA YA KUKUBALI MKATABA MPYA LIVERPOOL.

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Liverpool, Luis Suarez amesaini mkataba mpya wa miaka minne kuitumikia klabu hiyo. Suarez mwenye umri wa miaka 26 ambaye alijiunga na Liverpool Januari 2011 amefunga mabao 17 katika 11 za ligi alizocheza msimu huu. Nyota huyo ambaye mkataba wake wa sasa unaishia mwaka 2016 atakunja kitita cha paudi 160,000 mpaka mkataba utakapoisha na baadae kukunja kitita cha paundi 200,000 kwa miaka minne iliyobakia. Suarez amekiri kuwa ukaribu aliokuwa nao na mashabiki wa klabu hiyo ndiyo uliopelekea kufanya uamuzi huo na ni mategemeo yake hatawaangusha katika kipindi atakachokuwepo hapo.

Friday, December 20, 2013

SITAJALI KAMA RONALDO HATAHUDHURIA SHEREHE ZA UTOAJI TUZO ZA BALLON D'OR - RIBERY.

WINGA mahiri wa klabu ya Bayern Munich, Franck Ribery amesisitiza kuwa hatajali kama mshambuliaji nyota wa Real Madrid Cristiano Ronaldo atahudhuria au kutohudhuria sherehe za utoaji tuzo ya Ballon d’Or zitakazofanyika jijini Zurich. Kumekuwa na tetsi kuwa nyota huyo wa kimataifa wa Ureno hatahudhuria sherehe hizo kutokana na mahusiano mabovu na rais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Sepp Blatter lakini Ribery amesema uamuzi wowote utakaochukuliwa na nyota huyo hautamuhusu. Ribery amesema hajawasiliana na Ronaldo na hawajadili naye wala mtu yoyote hivyo hajali kama hatahudhuria sherehe za utoaji tuzo hizo. Baadae Ribery alikiri kuwa uamuzi wa FIFA na Shirikisho la Soka la Ufaransa kusogeza mbele muda wa kupiga kura kwa ajili ya tuzo hiyo unaweza kumnyima nafasi ya kuitwaa kwa mara ya kwanza. Tuzo ya Ballon d’Or ambayo zamani ilikuwa ikijulikana kama tuzo ya mchezaji bora wa dunia wa mwaka inatarajiwa kutolewa Januari 13 mwakani.

ITAKUWA HESHIMA KUBWA KWANGU KAMA TOTTENHAM WAKINIHITAJI - DE BOER.

MENEJA wa klabu ya Ajax Amsterdam ya Uholanzi, Frank de Boer amesema itakuwa ni jambo la heshima kwake kuhusishwa na nafasi ya umeneja iliyokuwa wazi katika klabu ya Tottenham Hotspurs. Spurs imekuwa bila kocha toka imtimue Andres Villas-Boas Jumatatu iliyopita na nafasi yake kuachiwa kocha wa muda Tim Sherwood ambaye alishindwa kukiongoza kikosi hicho ipasavyo na kujikuta wakitolewa katika Kombe la Ligi kwa kufungwa na West Ham United kwa mabao 2-1. De Boer amesema kama Spurs wanamhitaji ni heshima kwake lakini kwasasa anaelekeza nguvu zake katika klabu yake ya Ajax. Mapema Alhamisi wakati wa kocha huyo, Guido Albers alibainihsa kuwa De Boer ambaye ni mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi amekuwa akiitaka nafasi ya Villas-Boas ingawa Spurs wenye wenye hawajamfuata rasmi.

INIESTA AKUBALI KUSAINI MKATABA MPYA BARCELONA.

KIUNGO mahiri wa klabu ya Barcelona, Andres Iniesta anatarajiwa kuwa mchezaji anaelipwa zaidi katika timu hiyo baada ya Lionel Messi wakati atakapotia saini makubaliano ya mkataba mpya wiki ijayo. Habari hizi zitakuwa sio nzuri kwa klabu ya Real Madrid ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa wakimuwinda winga huyo wa kimataifa wa Hispania. Rais wa Barcelona, Sandro Rosell alitangaza Alhamisi kuwa Iniesta tayari amefikia makubaliano ya mdomo kuongeza mkataba wake mpaka 2018 ambapo anatarajiwa kukunja kitita cha paundi milioni 14 kwa msimu katika miaka minne ijayo ikiwa ni mara mbili ya kiasi anachopata sasa. Mpaka kufikia kipindi hicho nyota huyo atakuwa ametimiza miaka 34 na Rosell amebainisha kuwa anaweza kuongezwa mkataba zaidi kutokana na uwezo wake utakavyokuwa. Iniesta alianza kukitumikia kikosi cha kwanza cha Barcelona mwaka 2002 chini ya kocha Louis van Gaal ambapo mpaka sasa amecheza mechi 479 na kufunga mabao 48.

RIBERY AWAFAGILIA WAKWE ZAKE ALGERIA KUFANYA VYEMA KOMBE LA DUNIA.


WINGA mahiri wa kimataifa wa Ufaransa, Franck Ribery amedai kuwa Algeria wana uwezo wa kuvuka hatua ya makundi katika michuano ya Kombe la Dunia ncini Brazil mwakani pamoja na kupangwa katika kundi lisilotabirika. Ribery mwenye umri wa miaka 30 amemuoa Wahiba Belhami ambaye ni raia wa Algeria na siku zote amekuwa akiziunga mkono timu za taifa za wakubwa na wadogo katika nchi hiyo. Nyota huyo amesema kwakuwa mke wake ni raia wa Algeria siku zote amekuwa akiiunga mkono timu ya taifa ya nchi hiyo na anafikiri wana kila sababu ya kuvuka hatua ya makundi katika michuano hiyo. Algeria imepangwa katika kundi H sambamba na timu za Urusi, Ubelgiji na Korea Kusini ambapo wachambuzi wa soka wamedai kuwa ni mojawapo kati makundi magumu kabisa katika michuano hiyo. Algeria watacheza mechi yao ya ufunguzi dhidi ya Ubelgiji Juni 17 mwakani katika Uwanja wa Mineirao huko Belo Horizonte.

RUFANI YA WILSHERE YAGONGA MWAMBA.

CHAMA cha Soka nchini Uingereza-FA kimemfungia kucheza mechi mbili kiungo wa klabu ya Arsenal, Jack Wilshere baada ya kukutwa na hatia ya kuonyesha ishara ya matusi kwa mashabiki wa Manchester City. Tukio hilo lilitokea wakati Arsenal walipopata kipigo cha mabao 6-3 kutoka kwa City kwenye Uwanja wa Etihad Jumamosi iliyopita. Mwamuzi wa mchezo huo hakuliona tukio hilo lakini picha za video zilimuonyesha kiungo huyo akionyesha ishara hiyo ambapo pamoja na kukiri kosa hilo lakini Wilshere alidai kuwa adhabu aliyopewa ilikuwa kubwa. Wilshere atakosa mechi mbili za muhimu kutoka kwa mahasimu wao wa jiji la London timu ya Chelsea ambayo watacheza nayo Jumatatu na West Ham United Desemba 26 mwaka huu.

Thursday, December 19, 2013

HATIMAYE OKWI AWASILI KUITUMIKIA YANGA.

HATIMAYE mshambuliaji Emmanuel Okwi amewasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere -JNIA, Dar es Salaam jioni hii tayari kuanza kuutumikia Mkataba wake wa miaka miwili katika klabu ya Yanga. Okwi alitua kwa ndege ya RwandaAir Saa 9:55 jioni na kulakiwa na viongozi na mamia ya wapenzi kadhaa wa timu hiyo JNIA kabla ya kupakiwa kwenye gari ndogo alilokuwa akiendesha Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Kimataifa ya Yanga, Seif Ahmed na kuondoka. Mbali na Ahmed aliyekuwa akiendesha gari Okwi alikaa kiti cha nyuma sambamba na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Mussa Katabaro. Okwi alitokea geti la wageni maalum la JNIA na kusindikizwa na Polisi huku, umati wa mashabiki wa Yanga ukimshangilia na kumfanya atoke kwa taabu hadi kupanda gari.

TANZANIA YAMALIZA MWAKA KATIKA NAFASI YA 120 VIWANGO VYA FIFA.

TANZANIA itamaliza mwaka 2013 ikiwa katika nafasi ya 120 katika viwango vipya vilivyotolewa na Shrikisho la Soka Duniani-FIFA mwezi huu. Katika miezi yote 12 Tanzania imekuwa ikipanda na kushuka mara kadhaa huku nafasi ya juu kabisa iliyofikiwa kwa mwaka huu ikiwa ni nafasi ya 109 walioshika Juni. Hispania imaliza mwaka kama vinara katika orodha hizo kwa mwaka wa sita mfululizo toka mwaka 2008 waliponyakuwa taji la michuano ya Ulaya wakizipiku nchi za Ujerumani waliopo nafasi ya pili, Argentina nafasi ya tatu, Colombia waliopo nafasi ya nne na Ureno wanaofunga orodha ya tano bora. Kwa upande wa Afrika, Ivory Coast wameendelea kuongoza kwa kushika nafasi ya 17 wakifuatiwa na Ghana wanaoshika nafasi ya 24, huku Algeria wakiwa nafasi ya 26, wakati mabingwa wa Afrika Nigeria wao wako katika nafasi ya 37 na tano bora kwa upande wa Afrika inafungwa na Misri waliopo nafasi ya 41.

UNITED, CITY ZATENGANISHWA KOMBE LA LIGI.

KLABU ya Manchester United na Manchester City zimetenganishwa katika ratiba ya michuano ya Kombe la Ligi hatua ya nusu fainali. United ambao walifanikiwa kuibamiza Stoke City kwa mabao 2-0 jana usiku inatarajiwa kuchuana na Sunderland ambao waliiondosha Chelsea katika mchezo wa robo fainali. Kwa upande wa City ambao walitinga hatua hiyo baada ya kuifunga kirahisi Leicester, wanatarajiwa kuivaa West ham United ambayo iliondosha Tottenham Hotspurs kwa mabao 2-1. Mkondo wa kwanza mechi hizo unatarajiwa kuchezwa Januari 6 mwakani wakati mhi za mkondo wa pili zikitarajiwa kuchezwa wiki moja baadae.

MMILIKI WA QPR AMNG'ANG'ANIA REDKNAPP.

MMILIKI wa klabu ya Queens Park Rangers, Tony Fernandes anataka kumuona Harry Redknapp akibakia kuwa meneja wa klabu hiyo kwa miaka mingi na ana uhakika wa kumbakisha pamoja na vilabu mbalimbali kumhitaji. Mashabiki wa klabu ya Tottenham Hotspurs wanaonekana kumtaka Redknapp kurejea kuinoa timu hiyo baada ya kutimuliwa kwa Andres Villas-Boas. Lakini Fernandes ana uhakika kuwa kocha huyo atabakia hapo kwa kipindi kirefu kijacho kwasababu anadhani ni mmoja wa makocha bora kabisa duniani. Fernandes amesema hakuna haja ya kuwa profesa ili uweze kutambua kuwa timu nyingo zilizopata mafanikio nchini Uingereza zimekuwa zikiongozwa na makocha waliokaa kwa kipindi kirefu kama Arsene Wenger wa Arsenal, Sir Alex Ferguson wa Manchester United na David Moyes aliyekuwa akiinoa Everton. Bilionea huyo aliendela kudai kuwa Redknapp ni mmoja wa makocha wa kiwangu cha juu na watu wengi wanamhitaji lakini anadhani ana furaha kufanya kazi naye.

RIBERY ATEULIWA MCHEZAJI BORA BUNDESLIGA.

MSHAMBULIAJI wa klabu ya Bayern Munich, Franck Ribery ametajwa kuwa mchezaji bora wa mwaka wa Ligi Kuu nchini Ujerumani maarufu kama Bundesliga kufuatiwa kiwango bora alichokionyesha katika miezi 12 iliyopita. Nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa ambaye pia yuko katika orodha ya kugombea tuzo ya Ballon d’Or sambamba na Lionel Messi na Cristiano Ronaldo, imekuwa ni tuzo yake ya tatu baada ya kushinda tuzo ya mchezaji bora wa Ligi ya Mabingwa Ulaya pamoja na ile ya mchezaji bora wa Ulaya alizoshinda mapema mwaka huu. Ribery mwenye umri wa miaka 30 alishinda tuzo hiyo mbele ya mshambuliaji wa Borussia Dortmund Robert Lewandowski ambaye kuna tetesi naye akahamia Bayern katika kipindi cha usajili majira ya kiangazi. Toka mwaka huu uanze Ribery amefunga mabao 18 na kutoa pasi za mwisho zilizozaa mabao 20 katika mechi 44 alizocheza katika mashindano yote na kuisaidia Bayern kushinda mataji matatu kwa pamoja.

MPUTU ATISHIA KUTOSHIRIKI CHAN.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC, Tresor Mputu ametishia kujitoa katika timu ya taifa ya nchi hiyo itakayoshiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani itakayofanyika nchini Afrika Kusini mwez ujao. Nyota mwenye umri wa miaka 28 anayekipiga katika klabu ya TP Mazembe amesema hatashiriki michuano hiyo kama mamlaka husika na maofisa wa soka wa nchi hiyo hawatachukua hatua za makusudi ili kuimarisha hali ya kazi kwa wachezaji wanaocheza soka nyumbani. Akihojiwa Mputu amesema anadhani hawezi kwenda Afrika Kusini kwasababu wachezaji wanaocheza nyumbani hawaheshimiwi na kuna hakuna maelewano ndani ya timu hivyo hali hiyo inaathiri kazi yao. Kama wahusika wakiweka mambo sawa kabla ya michuano hiyo hakuna shaka kwamba ataliwakilisha taifa lake kwa mara nyingine.

WILSHERE AKUBALI ADHABU YA FA.

KIUNGO mahiri wa klabu ya Arsenal, Jack Wilshere amekubali adhabu aliyopewa na Chama cha Soka cha Uingereza-FA lakini atapinga adhabu ya kufungiwa mechi mbili aliyopewa. Nyota huyo wa kimataifa wa Uingereza alikuwa akituhumiwa kuonyesha ishara ya matusi kwa mashabiki wa Manchester City katika uwanja wa Etihad baada ya timu yake kupewa kipigo cha mabao 6-3 katika mchezo wa Ligi Kuu uliofanyika wiki iliyopita. Tukio hilo halikuonwa na mwamuzi wa mchezo huo lakini picha za video zilimuonyesha Wilshere akitoa ishara hiyo na FA kumpatia adhabu kwa sheria mpya ambayo huwaruhusu kufanya hivyo kama tukio halikuonekana na mwamuzi. Kesi yake inatarajiwa kusikilizwa Alhamisi na kama adhabu ikibaki hivyo nyota huyo anatarajiwa kukosa mechi mbili za Ligi Kuu ukiwem mchezo dhidi ya Chelsea Desemba 23 na mchezo dhidi ya West Ham United siku tatu baadae.

UWANJA WA BILBAO NA ATLETICO KUGOMBEA UENYEJI WA EURO 2020.

SHIRIKISHO la Soka nchini Hispania, RFEF limethibitisha kuwa Uwanja mpya wa San Mames uliopo Bilbao na Uwanja wa la Peineta wa Atletico Madrid ndio viwanja vitakavyotumika kuwania kuandaa mechi za michuano ya Ulaya 2020. Katika taarifa yake RFEF imedai kuwa baada ya kupitia viwanja vyote vinne vilivyotuma maombi vikiwemo viwanja vya Cornella El Prat wa Espanyol na ule mpya wa Mestalla wa Valencia, wameumua kuchukua viwanja hivyo viwili vya Bilbao na Atletico. Viwanja vyote vilivyochaguliwa ba RFEF bado havijakamilika kutokana na kuwa katika matengenezo. Uwanja mpya wa San Mames ulifunguliwa Septemba mwaka huu lakini jukwaa moja bado lipo katika matengenezo ili uweze kufukia uwezo wake wa kuchukua mashabiki 53,000. Kwa upande wa Uwanja wa La Peineta wenyewe hautakuwa tayari mpaka 2016 ambapo ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuingiza mashabiki 70,000.hi ya mechi.

RAJA YATINGA FAINALI KLABU BINGWA YA DUNIA, RONALDINHO AGEUKA LULU.

WENYEJI wa michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia, Raja Casablanca ya Morocco imefanikiwa kutinga fainali ya michuano hiyo baada ya kuwagaragaza mabingwa wa soka wa Amerika Kusini timu ya Atletico Mineiro ya Brazil kwa mabao 3-1. Wenyeji Casablanca ndio walioanza kupata bao la kuongoza kabla ya Mineiro kupitia kwa nyota wao Ronaldinho kusawazisha bao hilo lakini wenyeji walikuja juu na kuongeza bao lingine katika dakika ya 84 kwa njia penati huku Vivien Madibe akihitimisha ushindi huo kwa kufunga bao la tatu dakika za majeruhi. Mara baada ya mchezo huo wachezaji wa Raja walimvamia Ronaldinho aliyekuwa akirejea katika vyumba vya kubadilishia nguo, kumsalimia na kumuomba viatu vyake alivyokuwa akitumia katika mchezo huo pamoja na fulana aliyovaa. Wenyeji hao sasa watakwaana na mabingwa wa soka barani Ulaya, Bayern Munich katika mchezo wa fainali ya michuano hiyo utakaochezwa Jumamosi jijini Marakech.

Wednesday, December 18, 2013

REUS ATAKA KUSHINDANA AUBAMEYANG ILI KUHAKIKISHA KAMA ANA KASI KULIKO USAIN BOLT.

MWANARIADHA nyota wa mbio fupi wa Ujerumani, Julian Reus amempa changamoto winga mahiri wa Borussia Dortmund Pierre-Emerick Aubemeyang kushindana naye katika mbio za mita 100 ili kuhakiki kama nyota huyo wa soka ana kasi kuliko Usain Bolt. Aubameyang ambaye amefunga mabao mabao tisa msimu huu katika Bundesliga alitumia muda wa sekunde 3.7 katika mita 30 alizokimbia mazoezini, muda ambao unaonekana ni wa kasi zaidi na alioutumia Bolt wakati akiweka rekodi ya dunia yam bio za mita 100 kwa sekunde 9.58 mwaka 2009. Jumamosi iliyopita nyota huyo wa kimataifa wa Gabon alitamba katika mazungumzo ya luninga huko Ujerumani kwamba ana kasi zaidi ya Bolt madai ambayo Reus anataka kuhakikisha kwa kushindana naye. Reus amesema alichozungumza Aubameyang katika luninga kinamkera ndio maana anataka kushindana naye ili kulinda heshima ya riadha.