Friday, December 30, 2016

MAPINDUZI CUP YANG'OA NANGA.

Timu zitakazoshiriki kombe la Mapinduzi msimu huu zinatarajiwa kupata asilimia kumi ya mapato ya uwanjani baada ya kulipiwa gharama zote za siku ya mchezo. Kila klabu itapatiwa asilimia hizo 10 baada ya kulipiwa gharama zote ya siku ya mchezo na kinachobakia watapatiwa asilimia hizo. Akizungumza na Waandishi wa Habari Mwenyekiti wa kamati inayosimamia kombe la Mapinduzi Sharifa Khamis amesema msimu huu wanatarajia kuwapatia kila timu asilimia 10 ya mapato ya uwanjani baada ya kulimia gharama zote za mchezo. “Vilabu vimelalamika hasa vya Zanzibar hali zao ni mbaya sana, kwaiyo kwa pamoja tumekubaliana kwa kila timu tutaipatia asilimia 10 ya mapato ya uwanjani baada ya kulimia gharama zote za mchezo.” Aidha kamati ya kombe la Mapinduzi msimu huu imepanga kila timu kuwapatia nafasi 35 kwa wachezaji pamoja na viongozi kuingia bure uwanjani katika mashindano hayo. “Tumekubaliana na vilabu kila timu tutaipatia nafasi 35 za kuingia bure uwanjani kuangalia mashindano hayo.” Pazia la Mashindano ya Kombe la Mapinduzi linatarajiwa kuanza kutimua vumbi lake Disemba 30, 2016 katika uwanja wa Amaan saa 2:15 Usiku ambapo kutakuwa na mchezo wa Derby ya Jangombe kati ya Taifa ya Jangombe na Jangombe boys ambapo mashindano ya msimu huu yameshirikisha vilabu 9, vitano vikitokea Zanzibar, vitatu Tanzania bara na kimoja kutaka Uganda ambao ndio mabingwa watetezi timu ya URA.


KUNDI A: Simba, URA, KVZ, Taifa ya Jangombe na Jangombe Boys.
KUNDI B: Yanga, Azam, Zimamoto na Jamhuri.
RATIBA KAMILI YA MAPINDUZI CUP

30/12/2016 Taifa ya jang’ombe vs Jang’ombe boys saa 2:30 usiku.
1/1/2017 KVZ VS URA Saa 10:00 alasiri, Simba vs Taifa ya Jang’ombe saa 2:30 usiku.
2/1/2017 Azam vs Zimamoto saa 10:00 alasiri, Yanga vs Jamhuri saa 2:30 usiku.
3/1/2017 Jang’ombe boys vs URA saa 10:00 alasiri, KVZ vs Simba saa 2:30 usiku.
4/1/2017 Zimamoto vs Yanga saa 10:00 alasiri, Jamhuri vs Azam saa 2:30 usiku.
5/1/2017 KVZ vs Jang’ombe boys saa 10:00 alasiri, Simba vs URA saa 2:30 usiku.
6/1/2017 Taifa ya jang’ombe vs KVZ saa 2:30 usiku.
7/1/2017 Jamhuri vs Zimamoto saa 10:00 alasiri, Yanga vs Azam saa 2:30 usiku.
8/1/2017 Simba vs Jang’ombe boys saa 10:00 alasiri ,Taifa ya jang’ombe vs URA 2:30 usiku.
10/1/2017 Saa 10: 00 nusu fainal ya kwanza , Saa 2:30 nusu fainal ya pili.

13/1/2017 FAINAL saa 2: 30 usiku.

FEDHA ZA CHINA ZAMTOA UDENDA CLATTENBURG.

MWAMUZI maarufu kutoka Uingereza Mark Clattenburn amedai yuko tayari kwenda nchini China kwani anataka kujikuza zaidi kwenye kazi yake hiyo. Clattenburg mwenye umri wa miaka 41, alitwaa tuzo ya mwamuzi bora wa dunia wa mwaka ya Global Soccer Jumanne iliyopita baada ya kusimamia vyema mechi za fainali ya Kombe la FA, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Euro 2016 katika miezi 12 iliyopita. Wakati China ikijaribu kujijenga katika soka kufuatia kusajili wachezaji nyota hivi karibuni wakiwemo Oscar aliyetoka Chelsea na Carlos Tevez aliyetoka Boca Juniors, Clattenburg amedai atakuwa tayari kwenda kama ofa nzuri ikiwekwa mezani. Akihojiwa Clattenburg amesema China inataka kuendeleza soka lao na kama nafasi ikitokea pamoja na kwamba ana mkataba na Ligi Kuu lakini ataangalia mipango yake ya muda mrefu katika kibarua hicho.

NYOTA WA ZAMALEK AACHWA MISRI.

KOCHA wa timu ya taifa ya Misri, Hector Cuper ameita kikosi chake cha awali cha wachezaji 27 kwa ajili ya michuano ya Mataifa ya Afrika-Afcon inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Januari 14 mwaka huu huko nchini Gabon. Katika kikosi hicho, mshambuliaji wa Zamalek Basem Morsi ameachwa lakini mshambuliaji wa AS Roma Mohamed Salah ambaye amekuwa nje akisumbuliwa na majeruhi kifundo cha mgu ameitwa. Nyota wa Arsenal, Mohamed Elneny naye ni miongoni mwa wachezaji 11 wanaocheza soka nje ya nchi walioitwa. Wachezaji wanne pekee Essam El-Hadary, Ahmed Elmohamady, Mohamed Abdel-Shafy na Ahmed Fathi ndio wamewahi kuchiriki michuano hiyo kabla. Cuper ana kibarua cha kuchuja kikosi hicho kabla ya kubakiwa na wachezaji 23 wanaohitaji kwa ajili ya michuano hiyo. Misri wamepangwa kundi D sambamba na Ghana, Mali na Uganda na mchezo wao wa ufunguzi unatarajiwa kuwa dhidi ya Mali Januari 17 mwakani.

Egypt squad:

Goalkeepers: Essam El Hadary (Wadi Degla), Ahmed El Shenway (Zamalek), Sherif Ekramy (Al Ahly) , Mohamed Awad (Al Ismaily).

Defenders: Ahmed Elmohamady (Hull City) , Mohamed Abdel-Shafy (Al Ahly Jeddah, Saudi Arabia), Ahmed Fathi (Al Ahly),Karim Hafez (Nice, France) , Hamada Tolba (Al Masry) , Ahmed Hegazy (Al Ahly) , Saad Samir (Al Ahly) , Ahmed Dweidar (Zamalek), Omar Gaber (FC Basel, Switzerland) , Ali Gabr (Zamalek).

Midfielders: Abdallah El-Said (Al Ahly) , Amr Warda (Panetolikos, Greece) , Mohamed Elneny (Arsenal) , Tarek Hamed (Zamalek) , Ibrahim Salah (Zamalek) , Mahmoud Hassan 'Trezeguet' , Mohamed Ibrahim (Zamalek) , Ramadan Sobhi (Stoke City).

Forwards: Ahmed Gomaa (Al Masry) , Mahmoud Abdel-Moneim 'Kahraba' (Ittihad Jeddeh) , Mohamed Salah (AS Roma, Italy) , Ahmed Hassan 'Koka' (Braga, Portugal) , Marwan Mohsen (Al Ahly).

MUSTAFI FITI KUIVAA PALACE.

BEKI wa Arsenal, Shkodran Mustafi amepona majeruhi yake ya msuli wa paja na anatarajiwa kuwepo katika mchezo wa derby ya London dhidi ya Crystal Palace lakini winga Theo Walcott na beki wa kushoto Kieran Gibbs wanatarajiw akukosa mchezo huo wa Ligi Kuu utakaofanyika Emirates. Arsenal ilikuwa imemkosa beki wake huyo na kuwafanya kuyumba katika safu yao ya ulinzi baada ya kupoteza mechi mbili kati ya tatu walizocheza wakati hayupo. Akihojiwa Wenger amesema Mustafi mwenye umri wa miaka 24 amerejea mazoezini kama kawaida na atarejea katika kikosi chake. Kocha mbali na kudai kuwa atawakosa Gibbs anayejiuguza goti na Walcott, pia amedokeza habari njema kwa Danny Welbeck akidai kuwa ameshaanza mazoezi na wakati anaweza kurejea uwanjani.

MICHO AACHA WANNE THE CRANES.

KOCHA wa timu ya taifa ya Uganda, The Cranes Milutin Sredojevic Micho amewaacha wachezaji wanne akiwemo Ronald Mukiibi anayecheza soka la kulipwa nchini Ujerumani, kipa Ismail Watenga, Vitalis Tabu na Derrick Nsibambi. Micho amepunguza wachezaji kufuatia safari yao ya kuelekea nchini Tunisia leo kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Mataifa ya Afrika ambayo wanashiriki kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka 39. Kocha huyo anatarajia kuwachuja wachezaji wengine watatu katika kikosi chake cha sasa cha wachezaji 26 ili abaki na kikosi cha wachezaji 23 wanaohitajika katika michuano hiyo. Akihojiwa Micho amesema walishaanza mazoezi yao toka Desemba 19 na mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Tunisia Januari 4 ndio utampatia kikosi chake kamili cha wachezaji 23 kabla ya kwenda kwenye kambi yao ya mwisho huko Dubai. Uganda itaanza kupambana na Ghana katika mchezo wao wa ufunguzi Januari 17 huko Port Gentil kabla ya kuivaa Misri na baadaye Mali katika mchezo wao wa mwisho wa kundi D.

BAADA YA KUFANYA KUFURU KWA TEVEZ, CHINA SASA WAMTAKA RONALDO.

WAKALA Jorge Mendes amedai kuwa Real Madrid ilipewa ofa ya kitita cha paundi milioni 250 kutoka katika klabu moja ya China kwa ajili ya Cristiano Ronaldo. Mendes amesema nahodha huyo wa kimataifa wa Ureno mwenye umri wa miaka 31 hakuwa na mpango na dili hilo ambalo lingemuwezesha kulipwa kiasi cha zaidi ya paundi milioni 85 kwa mwaka. Novemba mwaka huu Ronaldo amesema anaweza kucheza kwa miaka mingine 10 baada ya kusaini mkataba mpya na Madrid ambao unamalizika Juni 2021. Akihojiwa Mendes amesema soko la China ni jipya na wanaweza kununua wachezaji wengine lakini haitawezekana kumnunua Ronaldo. Wakala huyo aliongeza kuwa Ronaldo ni mchezaji bora duniani hivyo ni kawaida kwa ofa kama hizo kuja mara kwa mara. Chini ya ofa hiyo anayodai Mendes, Ronaldo angeweza kulipwa kitita cha paundi milioni 1.6 kwa wiki.

Thursday, December 29, 2016

MARTIAL MGUU NDANI MGUU NJE UNITED.

WAKALA wa Anthony Martial amesema yeye pamoja na mteja wake wanafuatilia kwa karibu ofa kutoka Sevilla kipindi hiki ambacho chipukizi huyo wa Manchester United anapanda mustakabali wake. Martial mwenye umri wa miaka 21 alitokea katika benchi na kucheza dakika 16 pekee katika ushindi wa mabao 3-1 waliopata United dhidi ya Sunderland Desemba 26, huku akiwa ameanza katika mechi moja pekee kati ya nne zilizopita. Nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa amekuwa akipata tabu kupata nafasi katika kikosi cha Jose Mourinho msimu huu na kutakiwa na meneja huyo kujituma ili aweze kupata nafasi ya kuanza mara kwa mara. Pamoja na taarifa kuwa United bado wanataka kuendelea kubaki na Martial lakini wakala wake Philippe Lamboley amedai kuwa Sevilla wanataka kumsajili mshambuliaji huyo kwa mkopo. Lamboley amesema wanaifuatilia Sevilla kwa karibu kwani ni klabu nzuri, iliyopo nafasi ya nzuri katika La Liga na wapo katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Mapema wiki hii Mourinho alimtaka Martial kufuata nyayo za mchezaji mwenzake Henrikh Mkhitaryan kama anataka kurejea katika kikosi cha kwanza cha United.

OFA YA CHELSEA KWA KESSIE YAGONGA MWAMBA.

WAKALA wa Franck Kessie amedai kuwa ofa ya euro milioni 25 iliyotolewa na Chelsea kwa ajili ya kiungo huyo imekataliwa na Atalanta. Chelsea wanataka kutafuta mbadala wa Oscar ambaye wamemuuza China, katika kipindi cha usajili wa dirisha dogo Januari mwakani. Kessie amefunga mabao sita katika mechi 16 alizocheza msimu huu na kuisaidia Atalanta kukwea mpaka nafasi ya sita katika msimamo wa Serie A. Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 20 amekuwa katika kiwango kizuri msimu huu na kupelekea kufananishwa na nyota mwenzake wa kimataifa wa Ivory Coast Yaya Toure, na wakala wake George Atangana amesema Chelsea watakabiliwa na upinzani katika kuwania saini yake. Atangana amesema wamekuwa wakipata ofa nyingi kutoka Ligi Kuu kwa klabu kama Chelsea, Liverpool, Manchester City, Manchester United na Arsenal. Wakala huyo aliendelea kudai kuwa hawezi kusema thamani halisi ya mteja wake lakini wanazungumzia mmoja kati ya wachezaji bora kabisa chipukizi.

MESSI NI BORA KULIKO RONALDO - RAFINHA.

LIONEL Messi anaweza kuwa amemaliza wa pili mbele ya Cristiano Ronaldo katika tuzo za Ballon d’Or, lakini mchezaji mwenzake wa Barcelona Rafinha hana shaka kabisa kuwa nyota huyo wa kimataifa wa Argentina ndio bora duniani. Ronaldo alishinda tuzo hiyo akiwashinda Messi na nyota wa Atletico Madrid Antoine Griezmann. Lakini Rafinha mwenye umri wa miaka 23 anaamini Messi anastahili kupewa heshima ya kuwa bora kuliko wachezaji wote wa sasa. Akihojiwa Rafinha amesema kwa upande wake mchezaji bora duniani ni Messi.

TEVEZ AKAMILISHA USAJILI WAKE KWENDA CHINA.

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Manchester City na Manchester United, Carlos Tevez amekamilisha rasmi usajili wake kwenda klabu ya Shanghai Shenhua ya China. Kocha wa Shanghai Gus Poyet amemsajili mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Argentina mwenye umri wa miaka 32 kutoka Boca Junior lakini hakuna taarifa zaidi zilizotolewa kuhusu mkataba wake. Klabu ya Boca Junior ilimtumia salamu za heri Tevez katika klabu yake hiyo mpya huku wakiongeza kuwa siku zote atakuwa katika mioyo yao. Tevez alifanikiwa kushinda taji la Ligi Kuu akiwa na klabu hizo zote za Manchester. Pia alitwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na United mwaka 2008 kabla ya kujiunga na Juventus mwaka 2013 ambako nako alishinda mataji mawili ya Serie A.

CONCACAF YADOKEZA UWEZEKANO ZABUNI YA PAMOJA KOMBE LA DUNIA 2026.

RAIS wa Shirikisho la Soka la nchi za Amerika ya Kaskazini na kati-CONCACAF, Victor Montagliani amedokeza uwezekano wa kuwepo kwa maombi ya pamoja kati ya Marekani, Mexico na Canada kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2026. Baada ya Urusi na Qatar kuwa wenyeji wa michuano ya mwaka 2018 na 2022, CONCACAF inapewa nafasi kubwa ya kuwa mwenyeji wa michuano ya mwaka 2026. Ukanda huo haijaandaa michuano ya Kombe la Dunia toka Marekani walipofanya hivyo mwaka 1994. Wakati Marekani inaweza kugombea zabuni hiyo yenyewe kwa mara nyingine, Montagliani amedokeza kuwa kuna uwezekano wa kuandaa kwa pamoja. Hakuna Kombe la Dunia liliandaliwa na nchi zaidi moja toka Japan na Korea Kusini walipofanya hivyo mwaka 2002.

Tuesday, December 27, 2016

INTER YAMUWANIA LUCAS.

KLABU ya Inter Milan inataka kumsajili kiungo wa Liverpool Lucas Leiva kwa mkopo katika kipindi cha usajili wa dirisha dogo Januari mwakani. Hakuna makubaliano yeyote yaliafikiwa mpaka sasa lakini Inter wanataka kuimarisha kikosi chao kabla ya Serie A haijaanza tena Januari 8. Lucas mwenye umri wa miaka 29 alijiunga na Liverpool akitokea Gremio mwaka 2007 na ameichezea nchi yake ya Brazil mechi 24. Kiungo huyo ndio mchezaji aliyeitumikia Liverpool kwa kipindi kirefu kwasasa.

MAN CITY YATOA WAWILI KWA MKOPO.

KLABU ya Manchester City imethibitisha kuwa Pablo Maffeo na Angelino wamekamilisha uhamisho wao wa mkopo kwenda Girona. Maffeo mwenye umri wa miaka 19 alicheza mechi 13 kwa klabu hiyo inayoshiriki Ligi daraja la Pili nchini Hispania msimu uliopita na sasa anarejea tena Catalunya mpaka mwishoni mwa msimu huu. Beki wa kulia Angelino ambaye anafikisha umri wa miaka 20 Januari 4 mwakani, anataka kupata uzoefu wa kucheza katika kikosi cha kwanza, uzoefu ambao alipata kidogo katika klabu ya New York City FC msimu uliopita. Katika taarifa yake, City imedai kuwa chipukizi wake hao watakwenda Girona kuanzia Januari mosi na dili hilo la mkopo linatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.

BEKI WA BILBAO AFANYIWA UPASUAJI WA KORODANI.

KLABU ya Athletic Bilbao imethibitisha kuwa beki wake Yeray Alvarez amefanyiwa upasuaji kufuatia kugundulika kuwa na saratani ya korodani. Beki huyo chipukizi mwenye umri wa miaka 21 ambaye aliibuka La Liga mwaka jana, alifanyiwa upasuaji kuondoa korodani zilizoathirika katika hospitali ya Cruces mapema leo. Taarifa ya klabu hiyo imedai kuwa upasuaji umekwenda kama ulivyopangwa na Yeray anatarajiwa kuendelea kubakia hospitali kwa saa 24 ili kufuatilia maendeleo yake. Inategemewa kuwa beki huyo ataruhusiwa kurejea nyumbani kesho.

SUSO KUONGEZA MKATABA MILAN.

KIUNGO wa AC Milan, Suso ana uhakika kuwa hakutakuwa na tatizo la yeye kukubali kusaini mkataba mpya na klabu hiyo. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 23, ameanza kujiimarisha katika klabu hiyo msimu huu baada ya kupelekwa kwa mkopo Genoa katika msimu wa 2015-2016. Suso alifunga mabao mawili katika sare ya mabao 2-2 dhidi ya mahasimu wao Inter Milan mwezi uliopita na kuonyesha umuhimu wake katika kikosi cha Vincenzo Montella. Suso ameshaanza mazungumzo na makamu wa rais wa Milan Andriano Gallian juu ya kuongeza mkataba wake ambao unamalizika mwaka 2019 na anategemea watafikia makubaliano.

FUFA YATUMA RAMBIRAMBI KWA WACHEZAJI NA MASHABIKI WALIOKUFA MAJI.

SHIRIKISHO la Soka la Uganda-FUFA limetuma salamu zake za rambirambi baada ya mashabiki na wachezaji wa timu moja ya soka nchini humo kufariki dunia wakati boti waliyokuwa wakitumia kusafiri kupinduka katika Mto Albert. Polisi wamesema jana watu 30 walikufa maji wakati boti hiyo inayodaiwa kuwa ilibeba watu kupita kiasi kupinduka baada ya kukosa uwiano mzuri katika maji. Boti hiyo ilikuwa imebeba wachezaji na mashabiki wa timu ya kijiji cha Kaweibanda ambao walikuwa wakisafiri kwenda kucheza mechi ya kirafiki katika sikukuu za Christmas katika wilaya ya Hoima. Katika taarifa yake, FUFA ilielezea masikitiko yao kufuatia kupoteza maisha kwa wachezaji na mashabiki wa timu hiyo ya kijiji inayotoka wilaya ya Buliisa.

GUARDIOLA AINYOOSHEA MIKONO CHELSEA.

MENEJA wa Manchester City, Pep Guardiola amesema itakuwa vigumu kwa kikosi chake kuwafukuzia vinara wa Ligi Kuu Chelsea katika mbio za ubingwa. City wamekwea mpaka nafasi ya pili katika msimamo wa ligi baada ya kuichapa Hull City kwa mabao 3-0 jana na kuwafanya kuwa nyuma ya Chelsea kwa tofauti ya alama saba. Akihojiwa Guardiola amesema wamecheza mechi saba zaidi ya Chelsea hiyo ndio sababu haswa ni kwanini anaona itakuwa vigumu kuwakuta. Meneja huyo aliendelea kudai kuwa Liverpool ilikaribia kutwaa taji kipindi cha hivi karibuni kwasababu walikuwa wana mchezaji mmoja pekee kwa wiki na msimu uliopita ilikuwa hivyohivyo kwa Leicester City. Guardiola amesema kuwa msimu huu Chelsea na Liverpool ndio nafasi yao kwasababu hawana majukumu mengi. Liverpool na Chelsea zote zimeshindwa kufuzu kushiriki michuano ya Ulaya msimu huu baada ya kumaliza katika nafasi ya nane na 10 msimu uliopita.

Sunday, December 25, 2016

BEKI3 INAWATAKIWA WASOMAJI WAKE HERI YA KRISMASI.


VINCENT BOSSOU AITWA TOGO KWA AJILI YA AFCON.

BEKI mahiri wa klabu ya soka ya Yanga, Vincent Bossou ameitwa katika kikosi cha awali cha timu ya taifa ya Togo kwa ajili ya michuano ya Mataifa ya Afrika itakayofanyika huko nchini Gabon mapema mwezi ujao. Beki huyo amekuwa muhimili mkubwa katika safu ya ulinzi ya Yanga toka asajiliwe na kufanikiwa kuliziba vyema pengo la nahodha wa klabu hiyo Nadir Harub ambaye majeruhi ya mara kwa mara yamemfanya kupoteza nafasi yake katika kikosi cha kwanza. Wengine walioitwa katika kikosi hicho ni beki Yaovi Joseph Douhadji ambaye anacheza katika klabu ya Rivers United inayoshiriki Ligi Kuu ya Nigeria. Mshambuliaji mkongwe wa nchi hiyo Emmanuel Adebayor naye ameitwa na kocha Claude Leroy pamoja na kutokuwa na timu yeyote hivi sasa baada ya kuondoka West Ham.

MESSI NI BORA KULIKO RONALDO - GUARDIOLA.

MENEJA wa zamani wa Barcelona, Pep Guardiola amesisitiza kuwa hakuna mjadala wowote pindi unapokuja wakati wa kuamua nani zaidi kati ya Lionel Messi na Cristiano Ronaldo. Ronaldo alitwaa tuzo ya Ballon d’Or mwaka jana baada ya kuwa na mwaka mzuri ambao walitwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na Euro 2016, lakini Guardiola amedai kuwa Ronaldo bado ana safari ndefu ya kumfikia Messi. Hivi karibuni meneja wa Barcelona Luis Enrique alidai kuwa ni jambo la kijinga kumfananisha Messi na wachezaji wengine jambo ambalo linaungw amkono na Guardiola. Akihojiwa meneja huyo wa Manchester City amesema anakubaliana na Enrique kwamba Messi ndio bora, kwani anajua jinsi ya kucheza, kufunga na kuwachezesha wenzake pia jamboa ambalo ni nadra kupata kwa wachezaji wengine. Guardiola aliendelea kudai kuwa kwa heshima kubwa aliyonayo kwa wachezaji wote pamoja na Ronaldo, lakini anadhani Messi yuko katika kiwnago cha juu zaidi.

JUVENTUS YAPATA PIGO LINGINE KTK SAFU YAKE YA ULINZI.

KLABU ya Juventus, imethibitisha kuwa beki wake Alex Sandro alipata majeruhi ya msuli katika mchezo wa Supercoppa Italiana waliofungwa na AC Milan. Nyota huyo wa kimataifa wa Brazil alitolewa nje na nafasi yake kuchukuliwa na Patrice Evra baada ya dakika ya 33 kwenye mchezo huo uliofanyika jijini Doha, Qatar Ijumaa iliyopita ambapo Milan walishinda kwa changamoto ya mikwaju ya penati 4-3 baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika muda wa kawaida. Sandro anaongeza idadi ya majeruhi katika safu ya ulindi ya Juventus baada ya Leonardo Bonucci na Dani Alves, huku Andrea Barzagli akiwa ndio amerejea hivi karibuni baada ya kukaa nje kwa kipindi cha wiki sita. Mabingwa hao wa Italia hawajatoa muda kamili haswa wa atakaokaa nje beki huyo lakini taarifa kutoka nchini Italia zimedai kuwa atakaa nje kwa wiki sita.

DEFOE HAENDI KOKOTE - MOYES.

KLABU ya West Ham United imekuwa ikihusishwa na tetesi za kumuwania Jermain Defoe lakini meneja wa Sunderland David Moyes anadaiwa kutokuwa na mpango wowote wa kumuacha mshambuliaji huyo. Sunderland wanashika nafasi ya 18 katika msimamo wa Ligi Kuu huku Defoe ndio akiwa tegemeo la kuwaokoa washishuke daraja. Defoe amefunga mabao nane msimu huu hatua ambayo imefanya kuivutia klabu yake hiyo ya zamani. Akihojiwa kuhusiana na tetesi hizo, Moyes amesema Defoe hauziki kwani ni mchezaji muhimu sana katika kikosi chake. Sunderland watavaana na Manchester United kesho katika mchezo wa Ligi Kuu utakaofanyika katika Uwanja wa Old Trafford.

RAIS WA VALENCIA AWAOMBA RADHI MASHABIKI.

RAIS wa Valencia, Layhoon Chan ametuma video ya ujumbe wa Christmas akiwaomba radhi mashabiki wa klabu hiyo kufuatia kufanya vibaya kwa timu hiyo mwaka 2016. Valencia wanashika nafasi ya 17 katika msimamo wa La Liga hivi sasa huku Cesare Prandelli akiwa kocha wa tatu kubadilishwa kwa mwaka huu. Klabu hiyo ilianza mwaka na Gary Neville ambaye alitimuliwa Machi na nafasi yake kuchukuliwa na Pako Ayestaran aliyedumu mpaka Septemba na timu hiyo kuchukuliwa na kocha wa muda Voro kabla ya ujio wa Prandelli Octoba. Katika video hiyo Chan aliomba mashabiki kwa msimu mbaya na kuahidi kuwa watajifunza kutokana na makosa na kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha wanarejesha furaha tena katika klabu hiyo.

Saturday, December 24, 2016

DRAXLER RASMI PSG.

KLABU ya Wolfsburg imethibitisha kuondoka kwa Julian Draxler kwenda Paris Saint-Germain-PSG, huku nyota huyo wa kimataifa wa Ujerumani akisaini mkataba wa miaka minne na nusu na mabingwa hao wa Ligue 1. Taarifa zinadai kuwa PSG wamelipa kitita cha euro milioni 35 kwa ajili ya nyota huyo na wanaweza kulipa ziada ya euro milioni 10 kulingana na mafanikio ya nyota huyo. Wolfsburg imethibitisha katika taarifa yake kuwa tayari wameshafikia makubaliano na PSG na kinachosubiriwa vipimo vya afya. Draxler amejiunga na Wolfsburg kutoka Schalke Agosti waka 2015 lakini amekuwa akipata wakati mgumu kuzoea mazingira pale Volkswagen Arena.

FIFA KUJA NA SHERIA KALI KUDHIBITI TABIA ZA WACHEZAJI.

KOCHA na mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi, Marco van Basten amesema Shirikisho la Soka Duniani-FIFA linajadili kama waruhusu nahodha pekee kuzungumza na mwamuzi. Kama hatua hiyo ikiafikiwa itakuwa imelifanya soka kufanana na raga ambapo wana sheria kali kuhusiana na mawasiliano katika mchezo. Van Basten ambaye ni ofisa wa FIFA kitengo cha maendeleo ya kiufundi, amesema kumekuwa na mjadala wa jinsi gani ya kudhibiti tabia za wachezaji na heshima kwa waamuzi. Nguli huyo amesema kumekuwa na wachezaji wengi hivi sasa wanaolalamika wakati wa mchezo, jambo ambalo wanataka kulidhibiti.

SENEGAL KUWEKA KAMBI YA AFCON CONGO.

KIKOSI cha timu ya taifa ya Senegal kinatarajiwa kucheza mechi mbili za kirafiki kwa ajili ya kujiwinda na michuano ya Mataifa ya Afrika nchini Congo, ambapo ndio wamepanga kuweka kambi yao kabla ya kwenda Gabon. Mechi ya kwanza inatarajia kuwa dhidi ya Libya Januari 8 katika Uwanja wa Kinkele jijini Brazzaville kabla ya kuja kucheza na wenyeji wao katika uwanja huohuo siku tatu baadae. Senegal, ambao bado hawajataja kikosi chao watajiandaa kwa ajili ya michuano hiyo nchini Congo ambayo inapakana na gabon, kuanzia Januari 5. Baada ya kucheza mechi yao ya pili ya kirafiki wataondoka Brazzaville kwenda Franceville ambapo ndio kambi ya kundi B yenye timu za Algeria, Tunisia na Zimbabwe.

RANIERI APONDA UAMUZI WA FA KUHUSU KADI YA VARDY.

MENEJA wa Leicester City, Claudio Ranieri ameponda uamuzi wa kutupilia mbali rufani ya klabu hiyo kupinnga kadi nyekundu na anadhabu ya kufungiwa mechi tatu aliyopewa mshambuliaji Jamie Vardy. Vardy, mfungaji bora wa Leicester msimu uliopita, alilimwa kadi nyekundu y moja kwa moja katika sare ya mabao 2-2 waliyopata dhidi ya Stoke City na anatarajiwa kaunza kutumikia adhabu yake Jumatatu katika wakati timu hiyo itakapovaana na Everton. Akihojiwa Ranieri amesema kila mtu Uingereza na duniani kote aliangalia lile tukio lakini wote waliona hakuna kibaya kilichofanywa na vardy. Ranieri aliendelea kudai kuwa walikata rufani wakiamini walikuwa na haki na wamesikitishwa na matokeo waliyopata kwani wakati wakifanya makosa au awachezaji wakifanya makosa huwa hawakati rufani.

MAN UNITED IMEPOTEZA UTAMADUNI WAKE - MOYES.

MENEJA wa klabu ya Sunderland, David Moyes amedai kuwa utamaduni kwa kipindi kirefu uliokuwepo Manchester United sasa umetoweka. Meneja huyo raia wa Scotland alitimuliwa United mwaka 2014 kabla ya kumaliza msimu baada ya kuchaguliwa kuchukua nafasi ya Sir Alex Ferguson. Moyes amesema ilikuwa utamaduni wa klabu hiyo kuchagua mameneja raia wa Uingereza na kamwe hawakuona umuhimu wa kujiingiza katika usajili. Meneja huyo aliendelea kudai kuwa hivi sasa United imebadilika lakini ndio jinsi walivyoamua kwenda. United imetumia kiasi cha paundi milioni 480 toka Ferguson alistaafu mwaka 2013 baada ya kuiongoza timu hiyo kwa miaka 26.

NFF YAMUOMBA AMOKACHI USHAHIDI KUFUATIA TUHUMA ALIZOTOA.

NAHODHA wa zamani wa Nigeria, Daniel Amokachi amesema desturi ya makocha wazawa kuhongwa ili kuita wachezaji katika timu ya taifa ni jambo la kawaida. Pamoja na kuwa hakuna kocha yeyote alitekutwa na hatia kufuatia tuhuma hizo, kumekuwa na tetesi hizo kwa kipindi kirefu nchini Nigeria. Akihojiwa Amokachi amesema mawakala mara zote wamekuwa wakitoa fedha ili wachezaji wao waitwe katika kambi ya timu ya taifa. Shirikisho la Soka la Nigeria-NFF limemtaka Amokachi kutoa ushahidi kufuatia tuhuma hizo alizotoa. Amokachi mwenye umri wa miaka 43 ambaye alishinda taji la michuano ya Mataifa ya Afrika akiwa mchezaji mwaka 1994, amesema anadhani ni muda wa watu kuongea kuhusu suala hilo ambalo limekuwa likitafuna soka la Nigeria kwa muda.

Friday, December 23, 2016

MADRID WAPANGWA NA SEVILLA KOMBE LA MFALME.

KLABU ya Real Madrid imepangwa kucheza na Sevilla katika hatua ya timu 16 bora ya michuano ya Kombe la Mfalme. Mabingwa hao wa Ulaya na Dunia wanatarajiwa kuchuana na Sevilla iliyo chini ya Jorge Sampaoli ambao wanashikilia nafasi ya tatu katika La Liga, ikiwa kama marudiano baada ya kukutana katika Super Cup ya UEFA Agosti mwaka huu ambapo Madrid waliibuka kidedea. Ratiba hiyo inamaanisha Madrid na Sevilla watakutana katika mechi tatu katika kipindi kisichozidi siku 11 mwezi ujao, kufuatia mchezo wa ligi baina yao kuwa Januari 15. Mabingwa watetezi wa taji hilo Barcelona wao watakwaana na Athletic Bilbao ambao waliwafunga katika fainali ya msimu uliopita, wakati Atletico Madrid wao watapambana na Las Palmas. Valencia wao watapambana na Celta Vigo, Villarreal watacheza na Real Sociedad, Osasuna dhidi ya Eibar na Deportivo La Coruna watachuana na Alaves. Mechi za mkondo wa kwanza zinatarajiwa kuchezwa Januari 4 huku zile za marudiano zikichezwa Januari 11.

WEST BROM WATUMA OFA KWA SCHNEIDERLIN.

KLABU ya West Bromwich Albion imetenga ofa ya ya kiasi cha paundi milioni 13 kwa ajili ya Morgan Schneiderlin ambaye ataruhusiwa kuondoka Manchester United kama ikitolewa ofa sahihi. Meneja wa West Brom alithibitisha ofa hiyo, wakati meneja wa United Jose Mourinho akidai kuwa kama wakipata ofa nzuri hawezi kumzuia kiungo huyo kuondoka. Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 27, alijiunga na Southampton kwa kitita cha paundi milioni 25 Julai mwaka 2015 lakini amefanikiwa kucheza dakika 11 pekee msimu huu. Everton nao pia wanatajwa kumuwania kiungo huyo.

RAIS WA BOCA JUNIORS ATHIBITISHA SAFARI YA TEVEZ CHINA.

RAIS wa Boca Juniors, Daniel Angelici amedokeza kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kumpoteza mshambuliaji wao Carlos Tevez kufuatia taarifa za ofa kubwa aliyopewa kutoka China. Nyota huyo wa zamani wa Manchester United na Manchester City amepewa ofa inayokadiriwa kufikia kitita cha paundi 615,000 kwa wiki na klabu ya Shanghai Shenhua inayoshiriki Ligi Kuu ya China. Akihojiwa Angelici amesema amekuwa na mahusiano ya karibu na Tevez na kwa jinsi hali inavyokwenda anadhani itakuwa vigumu kwa mshambuliaji huyo kubaki klabuni hapo. Rais huyo aliendelea kudai kuwa akiwa kama kiongozi na mshabiki wa klabu hiyo anataka Tevez abaki lakini ukitizama ofa kubwa aliyopewa kutoka China anadhani itakuwa ngumu kwa mshambuliaji huyo kuikataa. Tevez mwenye umri wa miaka 32, ana mkataba na Boca utakaomalizika Juni mwaka 2018 na anatarajiwa kusafiri kwenda China kukamilisha uhamisho wake mwezi ujao kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi ya huko Februari.

DRAXLER NJIANI KWENDA PSG.

KLABU ya Paris Saint-Germain-PSG inadaiwa kufikia makubaliano na VfL Wolfsburg kwa ajili ya uhamisho wa Julian Draxler. Tetesi zimekuwa zikizagaa kwa wiki kadhaa kuwa PSG wanamtaka nyota huyo wa kimataifa wa Ujerumani na taarifa za mapema wiki hii kutoka Ufaransa zimedai mmiliki wa klabu hiyo anataka kutoa ofa huku mchezaji mwenyewe akiridhia kuondoka. Draxler mwenye umri wa miaka 23 anadaiwa kuwa tayari ameshazungumza na mkurugenzi wa michezo wa PSG Patrick Kluivert na kilichobakia ni hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho wake na kupewa mkataba unaokadiriwa utakuwa wa miaka mitatu au minne na nusu. Draxler alianza kucheza soka lake katika klabu ya Schalke akikaa hapo kwa kipindi cha miaka minne kabla ya kutimkia Wolfsburg.

CHELSEA INAWEZA KUPAMBANA NA SHINIKIZO - CONTE.

MENEJA wa Chelsea, Antonio Conte amesema klabu hiyo imevuka mategemeo msimu huu lakini ana uhakika kikosi chake kitatumia uzoefu wao ili kuepuka shinikizo la kuwepo kileleni mwa msimo wa Ligi Kuu. Baada ya kuanza kwa kusuasua, Chelsea ambao walimaliza nafasi ya 10 msimu uliopita, wamekwenda kushinda mechi 11 mfululizo za ligi ushindi ambao umewasaidia kutengeneza pengo la alama sita kileleni baada ya kucheza mechi 17. Akihojiwa Conte amesema hakuna mtu yeyote aliyefahamu kuwa Chelsea itakuwa kileleni mwa msimamo wa ligi. Meneja huyo aliendelea kudai kuwa anadhani wamepata uwiano sahihi na kipindi ambacho wamebakisha mechi mbili kabla ya kuingia duru la pili ni muhimu kwa wachezaji wake kuendelea kutumia uzoefu wao kuzuia shinikizo. Chelsea wanatarajiwa kukutana na Bournemouthkatika Uwanja wa Stamford Bridge Jumatatu ijayo.

AUBAMEYANGA, MAHREZ, MANE WAINGIZWA ORODHA YA MWISHO YA CAF.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Gabon na klabu ya Borussia Dortmund bado yuko katika nafasi ya kutetea taji lake la Mchezaji Bora wa Mwaka wa Afrika baada ya kuingia katika orodha ya mwisho ya wachezaji wa tatu iliyotolewa na Shirikisho la Soka la Afrika-CAF. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 atachuana na winga wa kimataifa wa Algeria na Leicester City Riyad Mahrez ambaye ni mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Afrika ya BBC kwa mwaka huu pamoja na winga wa kimataifa wa Senegal na Liverpool Sadio Mane. CAF imethibitisha kuwa mshindi anatarajiwa kutangazwa katika sherehe zitakazofanyika Alhamisi ya Januari 5 huko jijini Abuja, Nigeria. Aubameyang ndio aliyemaliza utawala wa kiungo wa Ivory Coasy na Manchester City Yaya Toure aliyetwaa tuzo hiyo kwa miaka minne mfululizo. Kiungo wa Zambia na klabu ya TP Mazembe, Rainford Kalaba, mshambuliaji wa Zimbabwe na Mamelodi Sundowns, Khama Billiat na kipa wa Uganda na Mamelodi Sundowns Denis Onyango wenyewe watagombea tuzo hiyo kwa wachezaji wanaocheza ndani ya bara hili.

ADHABU YA FIFA YAMTESA EBOUE.

BEKI wa kimataifa wa Ivory Coast, Emmanuel Eboue amekiri kuwa anapata tabu kuzoea adhabu ya kufungiwa kutocheza soka kwa mwaka mzima mpaka muda mwingine anafikiria kujiua. Nyota huyo alifungiwa mwaka mmoja na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA ikiwa kama sehemu ya adhabu kwa kushindwa kulipa deni alilokuwa akidaiwa na wakala wake wa zamani Sebastian Boisseau. Mkataba wa Eboue na Sunderland ulisitishwa baada ya FIFA kutoa adhabu hiyo, kufuatia madai ya Boisseau kudai kitita cha karibu paundi milioni moja ikiwa ni sehemu ya stahiki yake aliyotakiwa kupewa baada ya kufanikisha uhamisho wake kwenda Galatasaray kutoka Arsenal mwaka 2011. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 33 amekuwa akifanya mazoezi na timu za chini jijini London ili aendelee kuwa fiti lakini amebainisha kuwa adhabu hiyo inamtesa sana. Akihojiwa Eboue amesema kuna baadhi ya siku huwa hajisikii kabisa kutoka kitandani na kuna wakati alifikiria hata kujiua lakini anashukuru kwani familia inamtia moyo na kumpa nguvu za kuendelea.

OSCAR ATIMKIA CHINA RASMI.

KLABU ya Chelsea na Shanghai SIPG zimekubaliana uhamisho wa kiungo Oscar kwenda Ligi Kuu ya China katika kipindi cha usajili wa majira ya kiangazi Januari mwakani. Nyota huyo wa kimataifa wa Brazil mwenye umri wa miaka 25 mapema mwezi huu alibainisha kuwa uhamisho wake ulikuwa umekamilika kwa asilimia 90. Oscar alijiunga na Chelsea akitokea Internacional kwa kitita cha paundi milioni 25 mwaka 2012 na kufunga mabao 38 katika mechi 203 alizoichezea klabu hiyo. Katika taarifa yake ilitolewa mapema leo Chelsea walithibitisha taarifa hizo kuwa kiungo huyo atakwenda nchini China Januari mwakani. Oscar ambaye amekuwa akihangaika kupata nafasi chini ya meneja mpya Antonio Conte, anakwenda Shanghai kujiunga na meneja wa zamani wa Chelsea Andre Villas-Boas.

Wednesday, December 21, 2016

KOCHA CAMEROON ATAKA WACHEZAJI WALIOGOMA KUCHUKULIWA HATUA.

BEKI wa Liverpool Joel Matip ni mmoja kati ya wachezaji saba ambao wamesema hawataki kwenda kushiriki michuano ya Mataifa ya Afrika ambayo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Januari 14 mwakani. Kwa mujibu ya taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka la nchi hiyo-FECAFOOT imedai kuwa beki huyo ametoa kauli hiyo kupitia uzoefu wake aliopata katika benchi la ufundi lililopita. Beki wa West Browich Albion, Allan Nyom ni miongoni mwa orodha ya wachezaji saba waliogoma. FECAFOOT inaweza kuliagiza Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kuwasimamisha wachezaji hao kuzitumikia klabu zao kwa kipindi cha wiki tatu michuano hiyo itakapokuwa ikiendelea. Kocha wa Cameroon, Hugo Broos amesema wachezaji hao waliogoma wameweka maslahi yao mbele kuliko yale ya timu ya taifa na shirikisho lina haki ya kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria za FIFA. WEngine waliopo katika mgomo huo ni pamoja na Andre Onana wa Ajax Amsterdam, Guy N’dy Assembe wa Nancy, Maxime Poundeje wa Bordeaux, Andre-Frank Zambo Anguissa wa Marseille na Ibrahim Amadou wa Lille. Cameroon imepangwa kundi A sambamba na wenyeji Gabon, Burkina Faso na Guinea Bissau.

UNITED KUMUONGEZA MKATABA MOURINHO.

KLABU ya Manchester United inadaiwa kujipanga kumpa ofa ya kumuongeza mkataba meneja wake Jose Mourinho nyuma ya mkataba wake wa sasa wa miaka mitatu. Wamiliki wa United wanadaiwa kuridhishwa na kazi aliyofanya Mourinho toka alipotua Old Trafford ana wanaamini anaweza kufanikisha wakatwaa taji la 21 la Ligi Kuu kwa klabu hiyo. Pamoja na United kuanza msimu kwa kusuasua lakini meneja huyo amefanikiwa kuirejeshea makali yake kwa kushinda mechi tatu mfululizo ambazo kwa kiasi kikubwa zimewasaidia kupunguza pengo la alama baina yake na timu zilizokuwa katika orodha nne za juu. Inafahamika kuwa mustakabali wa Mourinho mwenye umri wa miaka 53 unategemea matokeo na aina ya uchezaji lakini familia ya Glazers imeonyesha kufurahishwa na anachokifanya meneja huyo mpaka sasa.

ARSENAL YAJIANDAA KUTUPIA NDOANO KWA KINDA LA VALENCIA.

KLABU ya Arsenal inadaiwa kujipanga kumuwania beki wa kushoto wa Valencia, Jose Gaya. Gaya anaonekana kama mmoja ya wachezaji wanaoibuka kwa kasi Ulaya na kuna kila dalili kuwa Valencia hataweza kumzuia chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 21 kuondoka. Manchester United na Chelsea nazo pia zimetajwa kumuwania chipukizi huyo lakini Arsenal ndio wanaoonekana kumuhitaji zaidi ili kuimarisha eneo lao la ulinzi la kushoto. Katika taarifa nyingine kutoka ndani ya klabu hiyo imedaiowa kuwa Wenger ameonyesha dalili kuwa ataendelea kuinoa klabu hiyo kupita mkataba wake wa sasa.

WEST HAM WAMNYATIA RASHFORD.

KLABU ya West Ham United inadaiwa kujiandaa kuwawania kwa mkopo nyota wa Manchester United Marcus Rashford na Anthony Martial katika kipindi cha usajili wa dirisha dogo. West Hama kwasasa wako juu kidogo la eneo la kushuka la kushuka daraja katika msimamo wa Ligi Kuu na wanataka kuongeza nguvu katika safu yao ya ushambuliaji na washambuliaji hao wa United wanaweza kuleta tofauti ili waweze kuepuka kushuka daraja. Mshambuliaji wa Chelsea Michy Batshuayi ndio alikuwa chaguo namba moja la West Ham lakini meneja Slaven Bilic ameamua kuangalia uwezekano mwingine kwasababu Chelsea inaweza ikashindwa kumruhusu kuondoka januari. Kutokana na Rashford na Martial kupoteza nafasi zao katika kikosi cha kwanza United msimu huu, West Ham wana matumaini kuwa wakiwaahidi muda zaidi wa kucheza inaweza kuwarahisishia kuwapata.

VARDY KUTUMIKI ADHABU YA MECHI TATU.MSHAMBULIAJI wa Leicester City, Jamie Vardy anatarajiwa kukosa mechi tatu baada ya rufani yake kupinga kadi nyekundu aliyopewa Jumamosi iliyopita katika mchezo dhidi ya Stoke City kukataliwa. Chama cha Soka cha Uingereza-FA kilitupilia mbali rufani hiyo, hivyo sasa Vardy anatarajiwa kukosa mechi dhidi ya Everton, West Ham United na Middlesbrough. Nyota huyo wa kimataifa wa Uingereza alitolewa nje na mwamuzi Graig Pawson katika dakika ya 28 kwa kumkwatua Mame Diouf wa Stoke. Baada ya mchezo huo meneja wa Leicester Claudio Ranieri alimtetea Vardy akidai alikuwa amefuata mpira na sio kucheza rafu hivyo alidhani pengine mwamuzi angempa kadi ya njano badala ya nyekundu kama alivyofanya. Baada ya kukosa mechi zote za msimu wa sikukuu, Vardy anatarajiwa kurejea uwanjani Januari 7 mwakani wakati Leicester itakapochuana na Everton tena katika mzunguko wa tatu wa michuano ya Kombe la FA.

LIVERPOOL ITAKUWA SHWARI BILA MIMI - MANE.

MSHAMBULIAJI wa Liverpool, Sadio Mane ana uhakika klabu hiyo inaweza kuendelea vyema bila uwepo wake wakati atakapoondoka kwa ajili ya michuano ya Mataifa ya Afrika mwezi ujao. Mane ambaye anaongoza orodha ya wafungaji katika klabu hiyo akiwa na mabao nane amebakisha mechi tatu pekee za Ligi Kuu dhidi ya Stoke City, Manchester City na Sunderland kabla ya hajakwenda kujiunga na timu yake ya taifa ya Senegal. Nyota huyo anatarajiwa kuwa na Senegal mpaka hatua ya mwisho ambayo nchi hiyo itafikia kabla ya kurejea tena Uingereza kuitumikia Liverpool. Akihojiwa Mane amesema sio jambo rahisi kuondoka na kuwaacha wachezaji wenzake wa Liverpool wakipigana peke yao lakini hana jinsi kwani lazima akalitumikie taifa lake kwani ni moja ya ndoto zake pia. Mane aliendelea kudai kuwa anaamini kikosi chao kiko vizuri na wanaweza kuendelea vyema hata bila uwepo wake.

Tuesday, December 20, 2016

MESSI HAENDI KOKOTE - BARTOMEU.

RAIS wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu amedai Lionel Messi ana uhakika wa kuendelea kubakia klabuni hapo, pamoja na kwamba mazungumzo ya mkataba mpya bado hayajafanyika. Mustakabali wa Messi umekuwa mjadala kipindi hiki kufuatia kuingia miezi 18 ya mwisho katika mkataba wake unaotarajiwa kuisha Juni mwaka 2018. Makamu wa rais wa klabu hiyo, Jordi Mestre alibainisha Jumapili iliyopita kuwa Barcelona bado hawajaanza mazungumzo na nyota huyo, ingawa bado wana matumaini yakuendelea kuwa naye. Akihojiwa mapema leo, Bartomeu alithibitisha kauli ya Mestre kuwa bado hawajaanza mazungumzo na Messi lakini wana uhakika mchezaji mwenyewe bado anapenda kuitumikia klabu hiyo.

ARSENAL KUMFUATA REUS KAMA SANCHEZ NA OZIL WAKIGOMA.

KLABU ya Arsenal inadaiwa bado kuendelea kumuweka katika rada zake Marco Reus kama Alexis Sanchez au Mesut Ozil mmoja wapo akliamua kuondoka Emirates. Nyota huyo wa kimataiaf wa Ujerumani kwa kipindi kirefu amekuwa akihusishwa na tetesi za kuhamia Ligi Kuu lakini bado ameendelea kuwa mwaminifu kwa klabu yake ya Borussia Dortmund. Reus ana mkataba na Dortmund unaomalizika mwaka 2019 lakini anaweza kupewa ofa ya fedha nyingi kama Arsene Wenger akishindwa kuwazuia wachezaji wake muhimu. Sanchez na Ozil wako katika mazungumzo ya kuongezwa mkataba Arsenal lakini hakuna yeyote ambaye mpaka sasa ameshakubali dili jipya hivyo kuzuka tetesi kuwa wanaweza kuondoka.

BOATENG NJE WIKI SITA.

BEKI wa Bayern Munich, Jerome Boateng anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa kipindi wiki sita baada ya kufanyiwa upasuaji wa bega. Nyota huyo wa kimataifa wa Ujerumani hakuwepo katika mchezo ambao Bayern walifungw amabao 3-2 na Rostov kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Novemba 23 na alifanyiwa upasuaji mapema leo. Katika taarifa iliyotolewa na klabu hiyo, upasuaji wa Boateng ulikwenda salama na sasa anatarajiwa kurejea uwanjani mapema mwezi Februari mwakani. Msimu huu Boateng umekuwa sio mzuri sana kwake kwnai amekuwa akiandamwa na majeruhi ya mara kwa mara.

MADRID WAPUNGUZIWA ADHABU.


KLABU ya Real Madrid imetangaza kuwa adhabu yao ya kufungiwa kusajili katika vipindi viwili imepunguzwa mpaka kipindi kimoja na Mahakama ya Kimataifa ya Michezo-CAS. Madrid sambamba na majirani zao Atletico Madrid walilimwa adhabu hiyo Januari mwaka huu baada ya Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kuwakuta na hatia ya kukiuka sheria za usajili kwa wachezaji wa kimataifa walio umri chini ya miaka 18. Mabingwa wa Hispania Barcelona nao pia walikutwa na adhabu kama hiyo mwaka 2014. Rufani yao FIFA ilitupiliwa mbali SEptemba mwaka huu hatua ambayo iliwafanya Madrid kwenda CAS. Kufuatia maamuzi hayo mapya sasa Madrid wataweza kuendelea kusajili wachezaji wapya msihoni mwa msimu huu pindi watakapomaliza kutumikia adhabu hiyo Januari mwakani.

SUPER FALCON WAMALIZA MGOMO BAADA YA KUPEWA CHAO.

TIMU ya taifa ya soka ya wanawake ya Nigeria, hatimaye wamemaliza maandamano yao ya kugoma kutoka hotelini jijini Abuja baada ya kulipwa fedha walizokuwa wakidai. Timu hiyo ilikuwa ikidai kiasi cha dola 23,650 kwa kila mchezaji kutoka Shirikisho la Soka la Nigeria kufuatia ushindi wao waliopata wa taji la Mataifa ya Afrika. Kikosi hicho kinachojulikana kama Super Falcon kimekuwa hotelini hapo toka Desemba 6 mwaka huu pindi walipotua kutoka katika michuano hiyo. Taarifa kutoka kwa msemaji wa timu imedai kuwa wachezaji wote wameshaondoka hotelini baada ya kupewa stahiki zao. Nigeria imetwaa taji hilo la wanawake mara nane kati ya 10 toka michuano hiyo ilipoanzishwa mwaka 1998.

GUARDIOLA NA MOURINHO KUKUTANA MAREKANI KIANGAZI.

MCHEZO wa kwanza wa derby ya Manchester kuchezwa nje ya Uingereza huenda ukafanyika nchini Marekani katika kipindi cha majira ya kiangazi. Manchester City inayonolewa na Pep Guardiola na Manchester United iliyokuwa chini ya Jose Mourinho ilikuwa wakutane jijini Beijing, China Julai mwaka huu. Hata hivyo, mvua kubwa iliyonyesha katika jiji hilo ilipelekea Uwanja wa Bird Nest kushindw akuchezeka hivyo mchezo baina timu hizo kuahirishwa saa sita kabla. Timu zote hizo zinatarajiwa kusafiri kwenda nchini Marekani Julai mwakani kwa ajili ya maandalizi ya msimu wa 2017-2018. Ingawa hakuna maelezo yeyote yaliyotolewa, timu hizo zinatarajiwa kushiriki katika michuano ya Ubingwa wa Kimataifa hatua ambayo inaweza kuwakutanisha.

AC MILAN YAMNYATIA FELLAINI.

KIUNGO Marouane Fellaini anaweza kupewa nafasi ya kuondoka Manchester United Januari wakani na AC Milan. Milan wamekuwa wakihusishwa na tetesi za kumsajili nyota huyo wa kimataifa wa Ubelgiji katika kipindi cha majira ya kiangazi lakini akaendelea kubakia Old Trafford na kuwa sehemu ya mipango ya meneja Jose Mourinho. Hata hivyo, hivi karibuni amekuwa akikosolewa vikali na mashabiki wa klabu hiyo haswa pale aliposababisha penati ambayo iliwapa nafasi Everton kutoa sare ya bao 1-1 kule Goodison park. Kutokana na hilo uhamisho wa Fellaini katika kipindi cha Januari unaonekana unaweza kufanyika na Milan wanataka kutumia mwanya huo kumnasa.